Tunakaribia kumaliza mwezi mtukufu wa Ramadhwaan na mambo matatu yafuatayo ya muhimu yanayotukabili yanapasa kuzingatiwa ili tukamilishe Swawm zetu ipasavyo na tupate fadhila zake.
1. Zakaatul-Fitwr
Inaitwa Zakaatul-Fitwr (Zakaah ya Kufuturu au Kufutari) kutokana na kumalizika Swiyaam za Ramadhwaan. Imefaridhiwa mwaka wa pili wa Hijrah katika mwezi wa Ramadhwaan.
i. Hikmah Ya Zakaatul-Fitwr:
Zakaatul-Fitwr ni kwa ajili ya kutakasa Swiyaam za Muislamu kutokana na maneno machafu na ya upuuzi wakati alipokuwa katika Swawm kwa kulisha maskini chakula ili nao wapate chakula kizuri siku ya ‘Iyd. Ndio maana kutolewa kwake kunakuwa kabla ya kuswali Swalaah ya ‘Iydul-Fitwr kwa dalili:
عَنْ ابْنِ عَبَّاس قَالَ فَرَضَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ زَكَاةَ الْفِطْرِ طُهْرَةً لِلصَّائِمِ مِنْ اللَّغْوِ وَالرَّفَثِ وَطُعْمَةً لِلْمَسَاكِينِ مَنْ أَدَّاهَا قَبْلَ الصَّلاةِ فَهِيَ زَكَاةٌ مَقْبُولَةٌ وَمَنْ أَدَّاهَا بَعْدَ الصَّلاةِ فَهِيَ صَدَقَةٌ مِنْ الصَّدَقَاتِ . " رواه أبو داود بِإِسْنَادٍ حَسَنٍ .
Kutoka Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amefaridhisha Zakaatul-Fitwr kuwa ni takaso kwa mwenye kufunga kutokana na maneno ya upuuzi na machafu, na kulisha masikini. Atakayeitoa kabla ya Swalaah basi hiyo ni Zakaah iliyotakabaliwa, na atakayeitoa baada ya Swalaah basi hiyo ni miongoni mwa swadaqag” [Abuu Daawuwd kwa isnaad iliyo nzuri].
Na ndio kusudio ya kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
قَدْ أَفْلَحَ مَن تَزَكَّىٰ ﴿١٤﴾
Hakika amefaulu ambaye amejitakasa.
وَذَكَرَ اسْمَ رَبِّهِ فَصَلَّىٰ ﴿١٥﴾
Na akadhukuru Jina la Rabb wake na akaswali. [Al-A’laa: 14-15]
‘Umar bin ‘Abdil-Aziyz alikuwa akiamrisha watu kutoa Zakatul-Fitwr na huku akisoma Aayah hizo tukufu.
ii. Wakati Unaowajibika Kutoa Zakaatul-Fitwr
Kuanzia Magharibi ya siku ya mwisho ya Ramadhwaan hadi asubuhi kabla ya Swalaah ya ‘Iydul-Fitwr. Inaweza pia kutolewa siku mbili tatu kabla. Mtoto atakayezaliwa siku hiyo kabla ya kuzama jua imewajibika kumtolea Zakaatul-Fitwr.
iii. Anayewajibika Kutoa Zakaatul-Fitwr Na Kitu Gani Cha Kutoa:
عَنْ ابْنِ عُمَرَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَال فَرَضَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ زَكَاةَ الْفِطْرِ صَاعًا مِنْ تَمْرٍ أَوْ صَاعًا مِنْ شَعِيرٍ عَلَى الْعَبْدِ وَالْحُرِّ وَالذَّكَرِ وَالأُنْثَى وَالصَّغِيرِ وَالْكَبِيرِ مِنْ الْمُسْلِمِينَ وَأَمَرَ بِهَا أَنْ تُؤَدَّى قَبْلَ خُرُوجِ النَّاسِ إِلَى الصَّلاةِ . صحيح البخاري
Kutoka kwa Ibn 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhumaa): "Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameifanya Zakaatul-Fitwr ni fardhi kwa mtumwa na aliye huru, mwanamume na mwanamke, mdogo na mkubwa miongoni mwa Waislamu kwa kutoa swaa' moja ya tende kavu au swaa’ moja ya shayiri, na akaamrisha kwamba itolewe kabla ya watu kwenda kuswali (Swalaatul-'Iyd)" [Al-Bukhaariy]
Swaa’ moja = Kilo mbili na nusu (mteko) viganja viwili vya mkono vya mtu wa wastani vilivyojaa mara nne.
iv. Kinachotolewa Ni Chakula Kinachotumika Na Watu Katika Nchi:
عن أبي سَعِيدٍ الْخُدْرِيَّ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ "ُكُنَّا نُعْطِيهَا فِي زَمَانِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ صَاعًا مِنْ طَعَامٍ أو صَاعاً من الشعير أو صاعاً من تَمر أو صاعاً من زَبيب، أو صاعاً من أقِط البخاري
Abuu Sa'iydil-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: "Tulikuwa tukitoa zama za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) swaa’ moja ya chakula, au swaa’ ya shayiri au swaa’ ya tende au swaa’ ya zabibu au swaa’ ya aqitw" (mtindi mkavu) (ambacho ndicho kilichokuwa chakula chao zama za hizo) [Al-Bukhaariy Na Muslim]
2. ‘Iyd Al-Fitwr
Yaliyo Sunnah - Yanayotakiwa Kutendwa Siku Ya 'Iyd
Yaliyo Bid'ah Na Maasi Yanayopaswa Kuepukwa Siku Ya 'Iyd
Inaitwa ‘Iydul-Fitwr (‘Iyd ya kufuturu au kufutari) kutokana na Waislamu kumaliza swiyaam ya Ramadhwaan.
Nayo ndio sikukuu mojawapo ya Waislamu.
Hivyo haifai kufunga siku ya ‘Iyd, bali ni siku ya kula na kunywa na kufurahi na kusherehekea kwa namna inayovuruhusika katika shariy’ah ya Dini ya Kiislamu.
a. Yaliyo Ya Sunnah Katika ‘Iyd Al-Fitwr:
i. Kuoga Kabla Ya Kutoka Kwenda Kuswali:
فقد صح في الموطأ وغيره أَنَّ عَبْدَ اللَّهِ بْنَ عُمَرَ كَانَ يَغْتَسِلُ يَوْمَ الْفِطْرِ قَبْلَ أَنْ يَغْدُوَ إِلَى الْمُصَلَّى
Imethibitika katika Muwattwaa na vitabu vinginevyo kwamba ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) alikuwa akioga siku ya ‘Iydul-Fitwr kabla ya kwenda Muswallaa.
ii. Kujipamba Na Kuvaa Nguo Nzuri:
وعن جابر رضي الله عنه قال : كان للنبي صلى الله عليه وسلم جبة يلبسها للعيدين ويوم الجمعة. صحيح ابن خزيمة
Kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ana jubbah akilivaa siku za ‘Iyd mbili na siku ya Ijumaa.” [Swahiyh Ibn Khuzaymah]
Na Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) alikuwa akivaa nguo zake nzuri kabisa siku ya ‘Iyd.
Kwa hiyo inapasa kujipamba kwa nguo nzuri, na manukato mazuri.
Ama wanawake hawapasi kudhihirisha mapambo yao ya mavazi au kujipaka vipodozi na pia hawapaswi kujitia manukato ikiwa watatoka nje.
Ama wakiwa majumbani mwao mbele ya Mahaarim zao, basi wanaruhusiwa.
iii. Kula Tende Kabla Ya Kutoka Kwenda Kuswali
عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ قَالَ كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ لا يَغْدُو يَوْمَ الْفِطْرِ حَتَّى يَأْكُلَ تَمَرَاتٍ .. وَيَأْكُلُهُنَّ وِتْرًا. البخاري
Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hatoki kwenda kuswali Swalaah ya ‘Iyd ila baada ya kula tende… na akila kwa hesabu ya witr. [Al-Bukhaariy]
Witr: ni moja, tatu, tano, saba n.k
Hii ni kwa sababu haifai kufunga siku hii ya ‘Iyd.
Asiyepata tende anaweza kula kitu chochote.
Ama katika 'Iydul-Adhwhaa ni Sunnah kutokula kabla ya kwenda Msikitini, na anaposhuka baada ya Swalaah ni bora kitu cha kwanza kula ni ile nyama ya Udhwhiyah (mnyama aliyechinjwa) ikiwa itapatikana.
iv. Kuleta Takbiyrah Kwa Sauti
Ni Sunnah kuu katika ‘Iyd kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿١٨٥﴾
na ili mkamilishe idadi na ili mumkabbir Allaah kwa kuwa Amekuongozeni na ili mpate kushukuru. [Al-Baqarah: 185]
Pia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akileta Takbirah mpaka anamaliza Swalaah. [Silsilat Al-Ahadiyth As-Swahiyhah - Shaykh Al-Albaaniy]
Matamshi Ya Takbiyrah
الله أكبر الله أكبر لا إله إلا الله والله أكبر الله أكبر ولله الحمد
Allaahu Akbar Allaahu Akbar, Laa Ilaaha Illa Allaah, Wa-Allaahu Akbar Allaahu Akbar wa Lillaahil Hamdu
Wakati wa Takbiyrah
Unaanza usiku wa ‘Iyd mpaka anapoingia Imaam kuswalisha Swalaah ya ‘Iyd
v. Kupongezana
Ni vizuri kwa Waislamu kupongezana siku ya ‘Iyd kwa ajili ya kudhihirisha mapenzi na undugu baina yao. Na ilivyo katika Sunnah ni kusema kama walivyokuwa wakiambiana Maswahaba wanapokutana siku ya ‘Iyd:
'Tuqubbila Minnaa wa Minka’
au
‘Taqabbala Allaahu Minnaa wa Minkum’
vi. Kwenda Muswallaa Kwa Kutembea Kwa Miguu Na Kurudi Kupitia Njia Nyingine:
عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ كَانَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا كَانَ يَوْمُ عِيدٍ خَالَفَ الطَّرِيقَ. رواه البخاري
Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) ambaye amesema: “Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akibadilisha njia siku ya ‘Iyd.” [Al-Bukhaariy]
Hikmah yake ni kwamba njia hiyo itashuhudia siku ya Qiyaamah na ardhi itataja yale yote ya kheri na shari anayotembelea mja juu yake.
Pia nii kudhihirsiha Uislamu na sikukuu yake katika njia mbili, na hali kadhaalika ni kukutana na watu tofauti na wakaweza kuitambua sikukuu hiyo.
vii. Kuswali Swalaah ya ‘Iyd Katika Muswallaa
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliamrisha watu wote watoke kwenda kuswali:
عَنْ أُمِّ عَطِيَّةَ رضي الله عنها قَالَتْ "أَمَرَنَا تَعْنِي النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ نُخْرِجَ فِي الْعِيدَيْنِ الْعَوَاتِقَ وَذَوَاتِ الْخُدُورِ وَأَمَرَ الْحُيَّضَ أَنْ يَعْتَزِلْنَ مُصَلَّى الْمُسْلِمِينَ." مسلم
Kutoka kwa Ummu ‘Atwiyyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba: “Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alituamrisha tutoke katika ‘Iyd mbili; vijana na vikongwe na kaamrisha wanawake wenye hedhi wajitenge katika Muswallaa.” [Muslim]
b. Bid’ah Zinazotendwa Katika ‘Iyd
i. Kuleta Takbiyrah Kwa Pamoja Katika Misikiti Na Muswallaa
Inavyopasa ni kila mtu kuleta Takbiyrah pekee.
ii. Kutembelea Makaburi
Baadhi ya watu wamefanya kuwa ni ada kutembelea makaburi siku za ‘Iyd. Jambo hili halikufanywa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala Maswahaba zake. Mtu anaweza kuzuru makaburi siku yoyote na si kutenga siku ya ‘Iyd kwa ni mahsusi kwa jambo hilo.
iii. Maamkizi Kama Maamkizi Ya Kikafiri
Kupelekeana kadi na zawadi kama wafanyavyo makafiri, haipasi kuwaiga kwani ni jambo tulilokatazwa katika Dini bali tubakie kuwa katika desturi zetu za Kiislamu na kufakharika nazo.
c. Maasi Yanayotendwa Katika ‘Iyd
i. Kunyoa Ndevu
Kunyoa ndevu haipasi hasa kwa kukusudia ‘Iyd kwa kudhani mtu anapendeza akifanya hivyo ilihali anavunja shariy'ah na kupingana na Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
ii. Wanawake Kutokutimiza Hijaab zao za kishariy'ah na kudhihirisha mapambo yao mbele ya wasio Maharimu wao.
d. Sherehe Za Maasi Zinazotendwa Katika ‘Iyd:
i. Kuchanganyika wanawake na wanaume na kuwekwa muziki, vyakula na vinywaji vya haraam na kupeana mikono wanawake na wanaume.
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
لأَنْ يُطْعَنَ فِي رَأْسِ أَحَدِكُمْ بِمِخْيَطٍ مِنْ حَدِيدٍ خَيْرٌ لَهُ مِنْ أَنْ يَمَسَّ امْرَأَةً لا تَحِلُّ لَه
“Ni bora kwa mwanaume kudungwa sindano katika kichwa chake kuliko kuushika mkono wa mwanamke ambaye si halali yake.” [Silsilat Al-Ahadiyth As-Swahiyhah - Shaykh Al-Albaaniy]
Wanawake wanaruhusiwa kupiga dufu na kuimba nyimbo zenye maadili siku za ‘Iyd wakiwa peke yao.
ii. Kufanya Israaf ya chakula na mali badala ya kuwasaidia masikini na mafakiri.
Tarbiyatul WhatsApp Group na Bustani ya Pepo Group inawaombea Waislamu wote 'Iyd njema yenye furaha.
3. Swiyaam Za Sittatu Ash-Shawwaal
http://bit.ly/2IO3u7w
Swawm hii inafuatia moja kwa moja baada ya mwezi wa Ramadhwaan na anaweza mtu kuanza siku ya pili baada ya ‘Idyul-Fitwr.
Swawm za Sittatu Ash-Shawwaal ni Sunnah yenye fadhila kuu kwani thawabu zake ni sawa na thawabu za Swawm ya mwaka mzima kwa dalili kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
(( من صام رمضان ثم أتبعه ستًّا من شوال كان كصيام الدهر)) أرجه مسلم في صحيحه،
((Atakayefunga Ramadhwaan kisha akafuatiliza na siku sita za mwezi wa Shawwaal itakuwa kama ni swiyaam ya mwaka)) [Muslim]
Ilivyohesabiwa kuwa ni mwaka mzima ni kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا ۖ
Atakayekuja kwa ‘amali nzuri basi atapata (thawabu) kumi mfano wa hiyo. [Al-An'aam:160]
Na pia:
عن أبي العبَّاسِ عبدِ اللهِ بنِ عباسِ بنِ عبد المطلب رضِيَ اللهُ عنهما، عن رَسُول الله صلى الله عليه وسلم فيما يروي عن ربهِ تباركَ وتعالى قَالَ: ((إنَّ اللهَ كَتَبَ الحَسَنَاتِ والسَّيِّئَاتِ ثُمَّ بَيَّنَ ذلِكَ، فَمَنْ هَمَّ بحَسَنَةٍ فَلَمْ يَعْمَلْهَا كَتَبَها اللهُ تَبَارَكَ وتَعَالى عِنْدَهُ حَسَنَةً كامِلَةً، وَإنْ هَمَّ بهَا فَعَمِلَهَا كَتَبَهَا اللهُ عَشْرَ حَسَناتٍ إِلى سَبْعمائةِ ضِعْفٍ إِلى ضعَافٍ كَثيرةٍ، وإنْ هَمَّ بِسَيِّئَةٍ فَلَمْ يَعْمَلْهَا كَتَبَهَا اللهُ عِنْدَهُ حَسَنَةً كَامِلةً، وَإنْ هَمَّ بِهَا فَعَمِلَهَا كَتَبَهَا اللهُ سَيِّئَةً وَاحِدَةً)). مُتَّفَقٌ عليهِ.
‘Abul-‘Abbaas, ‘Abdillaah bin ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amepokea kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika aliyopokea kutoka kwa Rabb wake Tabaaraka wa Ta’aalaa: Amesema: ((Kwa hakika Allaah Ameandika mema na mabaya, kisha akabainisha hayo: Atakayefanya hamu ya kutenda jema kisha asitende, Allaah Aliyetukuka Atamuandikia Kwake jema moja kamili. Na akilifanyia hamu na akalitenda, Allaah Atamuandikia mema kumi hadi nyongeza mia saba, hadi nyongeza nyingi zaidi (zaidi ya hizo). Na akifanya hamu ya kutenda jambo baya kisha asilitende, Allaah Atamuandikia Kwake jema kamili. Na akifanya hamu ya kulitenda na akalitenda, Allaah Atamuandikia baya moja)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
‘Ulamaa wameelezea sababu ya mtu kulipwa thawabu za mwaka mzima kwa atakayefunga Ramadhwaan na siku sita hizo za Shawwaal kwamba: Jambo zuri hulipwa ujira mara kumi, kwa hiyo mtu akifunga siku 30 za Ramadhwaan atapata ujira mara kumi; nazo zitakuwa 300, ukijumlisha na siku sita za Shawwaal ambazo zikilipwa mara kumi, huwa 60. Kwa hivyo 300 + 60 = 360, mtu atapata hesabu ya mwaka mzima.
Kwa mantiki hii, tunaona kuna umuhimu na ubora mkubwa wa kuifunga Swawm hii ya Sitta Shawaal.
Blog ya FisabililLaah na Bustani ya Pepo Group na Tarbiyatul Group inawaombea Waislamu wote wajaaliwe kumaliza mwezi Mtukufu wa Ramadhwaan kwa khayr na mafanikio, watakabaliwe Swawm zao, na madhambi kughufuriwa, waweze kutoa Zakaatul-Fitwr za kutakasa Swawm, Wawe na ‘Iyd ya furaha na uwezo wa kufunga Sittatu Ash-Shawwaal.
Taqabballa Allaahu Minnaa wa Minkum
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni