Mwenyezi Mungu Aliyetukuka ndiye aliyeumba ulimwengu wote na viumbe vyote bila usaidizi wa mtu yoyote na Yeye ndiye anayeuendesha ulimwengu huu. Kwa hivyo basi, Yeye, Mwenyezi Mungu, ndiye anayestahiki ibada kwa sababu hakuna yoyote aliyemsaidia katika uumbaji.
Ndugu katika imani! Jueni ya kwamba viumbe vyote ambavyo vinapatikana ulimwenguni havijileti vyenyewe bali Mwenyezi Mungu Aliyetukuka ndiye aliyeviumba. Hivyo, tambua kuwa kila utakavyokuwa unajifunza kuhusu nyegere na namna alivyo hatari ukumbuke pia ukubwa wa huyo aliyemleta kwani ni wazi kuwa nyegere hajajileta mwenyewe duniani.
Nyegere ni miongoni mwa wanyama hatari zaidi duniani, anayeogofya hata wakali kama nyoka, chui na simba. Hawa wote huufyata kwa nyegere. Nyegere haogopi mnyama yoyote, humkabili simba au hata chui zaidi ya mmoja na kuwashinda na wala hategemei msaada wa wenzake kushinda maadui zake.
Nyegere ana ngozi ngumu zaidi kuliko mnyama yoyote wa mwituni na hivyo ni ngumu kumuua kwa mshale au hata panga. Upana (thickness) wa ngozi yake unapaelekea hata ile sindano ya nyuki kudunda. Allah Mbora wa uumbaji amemjaalia nyegere kuwa na kucha ndefu na ngumu zinazomsaidia kushambulia viumbe mbalimbali.
Mnyama mwenye wivu
Nyegere ni moja kati ya wanyama wenye wivu sana hapa duniani kwa jike lake. Nyegere hutembea nyuma ya jike huku akiwa ameziba sehemu za siri za jike hilo. Hata jani tu likiigusa sehemu ya siri ya jike litararuliwa. Wivu wa nyegere humfanya awachukie sana binadamu wanaume. Nyegere anaweza kununua ugomvi mpaka kijiji cha sita, na walina asali ndio waathirika wakubwa wa hasira za nyegere.
Nyegere anaweza kuuvamia mzinga na kuujambia, kisha hula kidogo asali na nyingine huipeleka kwa mke wake. Nyegere ana uwezo wa kufuatilia harufu ya mrina asali aliyeupakua mzinga ule mpaka nyumbani. Nyegere hufanya hivyo akiamini mrina asali ameiba asali yake. Nyegere akifika nyumbani kwa mrina asali, huvunja mlango, huingia ndani na kumvamia mwizi wa asali yake (ukizingatia milango ya vijijini si imara). Mara kadhaa imewahi kuripotiwa matukio ya watu vijijini kushambuliwa kwa namna hii.
Chakula
Mnyama huyu nyegere hula vitu vyote ikiwemo nyama na majani na hii imemfanya kustahamili shuruba za mazingira yote iwe nyikani ama mwituni. Chakula kikubwa cha nyegere ni asali. Nyegere hupanda juu ya mzinga wa asali na kuujambia. Baada ya mashuzi yake, nyuki wote hulewa na yeye kupakua asali na masega yake na kula.
Nyegere pia hula nyoka wa aina yoyote. Nyegere ana sumu kali ambayo akimng’ata nyoka wa aina yoyote haponi, ingawa wapo nyoka wenye sumu ambao nyegere akiwala anaweza kuzimia kwa masaa kadhaa kutokana na ukali wa sumu ambayo inamuua mwanadamu kwa dakika tu.
Mambo 10 Usiyoyajua Kuhusu Nyegere
- Nyegere ni mnyama mwenye asili ya Afrika, Mashariki ya Kati na Hindi.
- Nyegere ni mnyama mdogo kiumbo anayeweza kuleta balaa hata kwa wanyama wakubwa mithili ya tembo na kifaru.
- Nyegere ni mnyama wa aina yake sana. Wataalamu wa elimu ya viumbe wanasema yeye ni mnyama ambaye anapenda sana kujitungia safari zisizokuwa za lazima.
- Nyegere akiwa katika safari zake hasa zile zisizokuwa za lazima, popote anapochoka hufanya maskani hapohapo.
- Nyegere ni mnyama mwenye wivu kupindukia na mwenye mapenzi makubwa sana kwa jike lake.
- Mwili wa nyegere una kinga maalumu inayomsaidia kutodhurika na sumu ya nyoka wa aina yoyote. Hata hivyo, akigongwa na wale nyoka wakali na sumu ikamuingia, hulewa au kuzimia kwa dakika kadhaa kisha huamka na kuendelea na safari yake.
- Nyegere ni mchimbaji mzuri sana wa mashimo. Anaweza kuchimba shimo kwa dakika takriban kumi tu kwa kutumia kucha zake ngumu. Kwa mujibu wa wataalamu, nyegere ana meno makali na magumu kiasi kwamba anaweza kuvunja hata jumba la kobe.
“Nyegere ni wanyama ambao hawapendelei sana kutembea katika makundi. Mara kila mmoja huishi kivyake hadi kipindi cha kukutana kwa ajili ya uzazi. Na hata kipindi hicho cha kukutana, kila dume huwa na jike lake tu.Ni vigumu kumshambulia nyegere kwani ngozi yake inamfanya iwe rahisi kwake kujikaza na kujizungusha katika upande wowote anaotaka na kisha kukujeruhi wewe. Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mbora wa kuumba na anayeuendesha ulimwengu aliouumba anavyotaka na wala haulizwi kwa analofanya bali viumbe ndio watakaoulizwa kwa vitendo vyao”.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni