Haki za mke kutoka kwa mume
1-Ni wajibu wa mume kumlisha mkewe kumvisha na kumtimizia mahitaji yake.
2-Mume ana haki kumfunza adabu mke anapohisi mke anamuasi. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
وَاللاَّتِي تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَاهْجُرُوهُنَّ فِي الْمَضَاجِعِ وَاضْرِبُوهُنَّ فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلاَ تَبْغُواْ عَلَيْهِنَّ سَبِيلاً إِنَّ اللّهَ كَانَ عَلِيًّا كَبِيرًا
Na wale (wanawake) ambao mnakhofu uasi wao, basi waonyeni na (wakiendelea uasi) wahameni katika malazi (vitanda) na (mwishowe wakishikilia uasi) wapigeni. Wakikutiini, basi msitafute dhidi yao njia (ya kuwaudhi bure). Hakika Allaah ni ‘Aliyyan Kabiyraa (Mwenye Uluwa – Mkubwa wa dhati, vitendo na sifa). (An-Nisaa 4: 34)
Aayah hiyo inataka maelezo kidogo kwani baadhi wa wanaume wameifahamu sivyo kuhusu: ((wahameni katika malazi (vitanda) na (mwishowe wakishikilia uasi) wapigeni)).
Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhumaa) na wengineo wamesema: “Aayah imemaanisha kupiga mpigo usio mkali” (yaani mpigo hafifu) Al-Hasan Al-Baswriy kasema: “Ina maana mpigo usio wa nguvu”.
Wanavyuoni wamefafanua kuhusu kauli hiyo ifautavyo:
i) Kwanza mume amnasihi mkewe bila ya kumshutumu au kumuonea au kumtia aibu kwa watu. Mke atakapomtii mumewe, itosheleze kuwa matatizo yamekwisha.
ii) Atakapoendelea mke kutokumtii mume wake, basi mume ajitenge naye kitandani, yaani asiwe analala nae kwa muda wala asiseme nae mpaka mke ahisi vibaya na atambue kuwa mumewe amamekasirikia. Pindi mke akikubali makosa yake, yaishe matatizo na warudiane katika hali yao ya kawaida.
iii) Ikiwa bado mke hana utiifu, hapo mume anaweza kufuata amri hiyo ya kipigo. Lakini sio kumpiga kwa nguvu bali kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) katika Hadiyth ifuatayo:
عن جابر (رضي الله عنه) عن النبي صلى الله عليه وسلم: أنه قال في حجة الوداع: ((واتَّقُوا اللهَ في النِّساءِ، فإنهن عندكم عَوَانٌ، ولكم عليهن ألا يُوطِئْنَ فُرُشكم أحدا تكرهونه، فإن فَعَلْن فاضربوهن ضَرْبا غير مُبَرِّح، ولهن رزْقُهنَّ وكِسْوتهن بالمعروف))
Kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema katika Hijja ya kuaga: ((Mcheni Allaah kuhusu wanawake kwani wao ni wasaidizi wenu. Mnayo haki juu yao kuwa wasimuruhusu mtu msiyempenda kukanyaga zulia lenu. (kuingia katika nyumba) Lakini wakifanya hivyo, mnaruhusiwa kuwatia adabu ndogo. Wao wana haki kwenu kwamba muwatimizie matumizi yao na nguo kwa njia ya kuridhisha)) Muslim
3-Ni wajib wa mume kumpatia mafunzo ya Dini mke wake ikiwa mke hakujaaliwa kupata elimu ya Dini yake. Mume amfundishe mwenyewe, na pindi asipoweza, amruhusu mke kuhudhuria darasa kwa sababu ni muhimu kwake apate kujifunza yanayopasa kama ‘Aqiydah na Tawhiyd na ajiepushe na shirki. Pia ajifunze Fiqhi na yote yanayohusiana na Dini yake, aweze kutekeleza ibaada zake sawasawa na pia apate kuitakasa nafsi yake na aweze kujiepusha na maasi na aweze kulea watoto wake. Kwa ujumla aihami familia yake na Moto wa Jahannam. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anaamrisha hivyo:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ ﴿٦﴾
Enyi mlioamini! Jikingeni nafsi zenu na ahli zenu na Moto (ambao) mafuta (kuni) yake ni watu na mawe; juu yake wako Malaika washupavu, shadidi hawamuasi Allaah kwa yale Anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa. (At Tahriym 66: 6)
4-Ni wajibu wa mume kumrekebisha mkewe anapokosea kufuata Shariy’ah za Dini; mfano mke asipotimiza hijaab. Vile vile asimwachie kuchanganyika na wanaume isipokuwa ambao kaharimishwa nao kuolewa.
5-Ni wajibu wa mume kumhifadhi mke kwa kila njia. Mume awe ndio mlinzi na msimamizi wa mambo yake na ndiye mwenye majukumu ya kumhudumia:
الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ ۚ
Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake kwa kuwa Allaah Amefadhilisha baadhi yao kuliko wengine na kwa sababu ya (matumizi) wanayotoa katika mali zao. (An-Nisaa 4: 34)
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Mwanamme ni mchunga (msimamizi) wa nyumbani kwake na ataulizwa kuhusu uchungaji (usimamizi) wake))Al-Bukhaariy na Muslim
6-Ikiwa mume ana mke zaidi ya mmoja, inampasa afanye uadilifu baina ya hao wake. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anakataza kutokufanya uadillifu:
وَلَن تَسْتَطِيعُوا أَن تَعْدِلُوا بَيْنَ النِّسَاءِ وَلَوْ حَرَصْتُمْ ۖفَلَا تَمِيلُوا كُلَّ الْمَيْلِ فَتَذَرُوهَا كَالْمُعَلَّقَةِ ۚ
Na wala hamtaweza kuadilisha baina ya wake japokuwa mkipania. Basi msielemee muelemeo wote (kwa mke mmoja) mkamuacha (mke mwengine (msiyempenda) kama kining’inio (aliyetundikwa). (An-Nisaa 4: 129)
Na Anasema:
فَإِنْ خِف ْتُمْ أَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوَاحِدَةً أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ ذَلِكَ أَدْنَى أَلاَّ تَعُولُواْ
Mkikhofu kuwa hamtoweza kufanya uadilifu, basi (oeni) mmoja au ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki (masuriya). Hivyo ni karibu zaidi kwamba hamtoelemea (kudhulumu).(An-Nisaa 4: 3)
Juu ya hivyo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) ameusia wanawake watendewe mema:
((Mbora wenu ni yule aliye mbora kwa familia yake na mimi ni mbora kabisa kwa familia yangu)) At-Twabaraaniy
NA ALLAAH ANAJUA ZAIDI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni