Ufafanuzi wa Thawabu za Sita kama Kufunga Mwaka Mzima
Naam,Hayo ni kutokana na Hadithi ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
(( من صام رمضان ثم أتبعه ستًّا من شوال كان كصيام الدهر)) أرجه مسلم في صحيحه
((Atakayefunga Ramadhaan kisha akafuatiliza na siku sita za mwezi wa Shawwaal' itakuwa kama ni funga ya mwaka)) [Muslim]
Inavyompasa Muislamu ni kwamba anatakiwa kwanza alipe deni lake la Ramadhaan kisha ndio afunge 'sitatu Shawwaal' ili aweze kupata thawabu za kama kafunga mwaka mzima. Na maulamaa wameona hivyo ni kutokana na dalili zifuatazo katika Qur-aan na Sunnah:
Katika Qur-aan:
Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((مَن جَاء بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا وَمَن جَاء بِالسَّيِّئَةِ فَلاَ يُجْزَى إِلاَّ مِثْلَهَا وَهُمْ لاَ يُظْلَمُون))
((Afanyae wema atalipwa mfano wake mara kumi. na afanyae ubaya hatalipwa ila sawa nao tu. Na wao hawatadhulumiwa)) [Al-An'aam:160]
Katika Sunnah:
Kuna Hadiyth mbali mbali zinazothibitisha kauli hiyo ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala), tutazitaja hapa mbili:
Ya kwanza ambayo kutokana na Imaam At-Tirmidhiy kuwa ni sababu ya kuteremshwa Aayah hiyo:
((من صام ثلاث أيام من كل شهر فقد صام الدهر كله))
((Atakayefunga siku tatu katika mwezi atakuwa amefunga mwaka mzima)) [Ahmad, An-Nasaaiy, Ibn Maajah, At-Tirmidhiy]
Hadiyth ya pili:
عن أبي العبَّاسِ عبدِ اللهِ بنِ عباسِ بنِ عبد المطلب رضِيَ اللهُ عنهما، عن رَسُول الله صلى الله عليه وسلم فيما يروي عن ربهِ تباركَ وتعالى قَالَ: ((إنَّ اللهَ كَتَبَ الحَسَنَاتِ والسَّيِّئَاتِ ثُمَّ بَيَّنَ ذلِكَ، فَمَنْ هَمَّ بحَسَنَةٍ فَلَمْ يَعْمَلْهَا كَتَبَها اللهُ تَبَارَكَ وتَعَالى عِنْدَهُ حَسَنَةً كامِلَةً، وَإنْ هَمَّ بهَا فَعَمِلَهَا كَتَبَهَا اللهُ عَشْرَ حَسَناتٍ إِلى سَبْعمائةِ ضِعْفٍ إِلى ضعَافٍ كَثيرةٍ، وإنْ هَمَّ بِسَيِّئَةٍ فَلَمْ يَعْمَلْهَا كَتَبَهَا اللهُ عِنْدَهُ حَسَنَةً كَامِلةً، وَإنْ هَمَّ بِهَا فَعَمِلَهَا كَتَبَهَا اللهُ سَيِّئَةً وَاحِدَةً)). مُتَّفَقٌ عليهِ.
‘Abul-‘Abbaas, ‘Abdillaah bin ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amepokea kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika aliyopokea kutoka kwa Rabb wake Tabaaraka wa Ta’aalaa: Amesema: ((Kwa hakika Allaah Ameandika mema na mabaya, kisha akabainisha hayo: Atakayefanya hamu ya kutenda jema kisha asitende, Allaah Aliyetukuka Atamuandikia Kwake jema moja kamili. Na akilifanyia hamu na akalitenda, Allaah Atamuandikia mema kumi hadi nyongeza mia saba, hadi nyongeza nyingi zaidi (zaidi ya hizo). Na akifanya hamu ya kutenda jambo baya kisha asilitende, Allaah Atamuandikia Kwake jema kamili. Na akifanya hamu ya kulitenda na akalitenda, Allaah Atamuandikia baya moja)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Kutokana na dalili hizo, kwamba kila jema mtu anapata mara kumi, hivyo Swawm ya Ramadhaan itakuwa ni hivi:
30 x 10 = 300
Na funga ya 'sitatu Shawwaal'itakuwa ni 6 x 10 = 60
300 + 60 = 360
Hivyo siku 360 ni sawa taqriban na mwaka mzima.
Na Allaah Anajua zaidi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni