إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم
Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!
20 - Isti’aadhah (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah
Isti’aadhah maana yake ni kuomba kujikinga kuepukana na shari. Na Isti’aadhah kwa Allaah ni kuomba kujikinga Kwake (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kuitakidi kuwa unabakia katika hifdhi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na inapasa kujidhalilisha Kwake na kumtegemea Yeye Pekee kuwa Ndiye Atakayekukinga na shari zinazokusudiwa kujikinga nazo.
Ibnul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:
“Tambua kwamba tamshi la عاذ na yanayohusiana katika Swarf (sarufi) inamaanisha kujihifadhi na kinga na kuokoka. Na hakika maana yake ni kukimbia kitu unachokiogopa kwa ambaye atakayekuepusha nacho. Na ndio maana ikaitwa Isti’aadhah kwake kama ilivyo maana ya kimbilio.” [Badaa’i Al-Fawaaid (2426)].
Isti’aadhah inaweza kuwa kwa kutaja Jina Lake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama Anavyosema:
وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ﴿٣٦﴾
Na utakapokuchochea uchochezi kutoka kwa shaytwaan, basi omba kinga kwa Allaah. Hakika Yeye Ndiye Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote. [Fusw-Swilat: 36]
Kujikinga na shaytwaan ni kwa sababu shaytwaan ni adui mkubwa kabisa kwa bin-Aadam, inahitajika kujikinga naye katika kila hali kwa sababu ya ahadi yake ya kuazimia kuwapotosha wanaadamu. Ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaamrisha kujikinga naye pale anapoanza kuchochea.
Na katika hali ya kusoma Qur-aan pia inahitajika zaidi kujikinga naye. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameamrisha:
فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ﴿٩٨﴾
Unaposoma kusoma Qur-aan basi (kwanza) omba kinga kwa Allaah dhidi ya shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa. [An-Nahl: 98]
Na katika Swalaah inatakiwa kuomba kinga kutokana na shaytwaan kwa pindi anaposhawishi katika Swalaah kwa kusema:
أَعُوذُ بِاللَّه مِنْ شَرِّ خَنْزَبْ
A’uwudhu biLLaahi min sharri khanzab
kama maelezo yalivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:
عن عُثْمَانَ بْن أَبِي الْعَاصِ رضي الله عنه أنه أَتَى النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنَّ الشَّيْطَانَ قَدْ حَالَ بَيْنِي وَبَيْنَ صَلَاتِي وَقِرَاءَتِي يَلْبِسُهَا عَلَيَّ: فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((ذَاكَ شَيْطَانٌ يُقَالُ لَهُ خَنْزَبٌ، فَإِذَا أَحْسَسْتَهُ فَتَعَوَّذْ بِاللَّهِ مِنْهُ وَاتْفِلْ عَلَى يَسَارِكَ ثَلَاثًا)) قَالَ: فَفَعَلْتُ ذَلِكَ فَأَذْهَبَهُ اللَّهُ عَنِّي .
‘Uthmaan bin Abiy Al-‘Aasw (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba alikwenda kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika shaytwaan kanijia baina yangu na Swalaah yangu na kisomo changu akinivaa. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema ((Huyo ni shaytwaan anayeitwa Khanzab, basi ukimhisi jikinge naye kwa Allaah, na tema mate upande wa kushoto kwako mara tatu)). Akasema: Nikafanya hivyo basi akaniondoka shaytwaan. [Muslim]
Isti’aadhah pia inawezekana kwa kutaja ‘Rabb’ kwa dalili ya Suwrah mbili katika Qur-aan zinajulikana kama ni Al-Mu‘awwidhataan (mbili za kujikinga)
قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ ﴿١﴾
Sema: “Najikinga na Rabb wa mapambazuko. [Al-Falaq: 1] mpaka mwisho wake na
قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ ﴿١﴾
Sema: “Najikinga na Rabb wa watu. [An-Naas: 1] mpaka mwisho wake.
Na isti’aadhah inafaa pia kwa kutumia Sifa Zake na Utukufu Wake. Ilipoteremka Aayah:
قُلْ هُوَ الْقَادِرُ عَلَىٰ أَن يَبْعَثَ عَلَيْكُمْ عَذَابًا مِّن فَوْقِكُمْ أَوْ مِن تَحْتِ أَرْجُلِكُمْ
Sema: “Yeye ni Muweza wa kukuleteeni adhabu kutoka juu yenu, au kutoka chini ya miguu yenu, [Al-An’aam: 65]
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliomba kinga akasema:
أَعُوذُ بِوَجْهِكُ
Najikinga kwa Wajihi Wako [Hadiyth kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesimulia Al-Bukhaariy]
Na pia kwa kuunganisha Jina Lake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pamoja Sifa Zake kama ilivyothibiti katika kinga ya pale mtu anapopata maumivu akashika sehemu inayopatikana maumivu akasema:
أَعُوذُ بِاللَّهِ وَقُدْرَتِهِ مِنْ شَرِّ مَا أَجِدُ وَأُحَاذِرُ
A’uwdhu biLLaahi wa-Qudratihi min sharri maa ajidu wa uhaadhiru
Najikinga kwa Allaah na kwa Uwezo Wake kutokana na shari ya ninachokisikia na ninachokiogopa)) [Muslim, Ibn Maajah na wengineo kwa usimulizi tofauti kidogo]
Pia Isti’aadhah kwa kutumia Maneno Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa dalili:
أَعُوْذُ بِكَلِماتِ اللَّهِ التَّامَّتِ مِنْ شَرِّ مَا خَلَقَ
A’uwdhu bi-Kalimaati-LLaahit-ttaammati min sharri maa khalaq (mara 3 jioni na asubuhi)
Najikinga kwa Maneno ya Allaah yaliyotimia kutokana na shari Aliyoiumba [Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ameisimulia Ahmad (2/290), An-Nasaaiy katika ‘Amal Al-Yawm wal-Laylah [590], Ibn As-Sunniy [68]. Taz. Swahiyh At-Tirmidhiy (3/187), Swahiyh Ibn Maajah (92/266), Tuhfat Al-Akhyaar (Uk. 45) katika Swahiyh Al-Jaami’ [6427] (Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Atakayesema mara tatu jioni hatodhuriwa na mdudu wa sumu usiku huo”]
Pia; Dalili nyingi zipo katika Sunnah kuhusu kuomba kinga za kila aina;
-Kuomba kinga kutokana na adhabu za Allaah za duniani na Aakhirah.
-Kuomba kinga kutokana na adhabu za kaburi, fitnah za Masiyh Ad-Dajjaal na fitna za uhai na fitnah za mauti.
-Kuomba kinga kutokana na Moto wa Jahannam.
-Kuomba kinga kutokana na shari za mashaytwaan na majini.
-Kuomba kinga kutokana na shari za adui.
-Kuomba kinga kutokana na maradhi.
-Kuomba kinga kutokana na upotofu.
-Kuomba kinga kutokana na ufakiri na kufru,.
-Kuomba kinga kutokana na shari za viungo vya mwili, na vitu vinginevyo kadhaa.
-Pia kuomba kinga kutokana na hali kadhaa wa kadhaa. [Rejea Du’aa za Sunnah ya Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam]
Kujikinga kupitia kwa bin-Aadam inaruhusika pale inapokuwa jambo ambalo analoombwa kukinga ni katika uwezo wake kwa dalili:
عَنْ جَابِرٍ أَنَّ امْرَأَةً مِنْ بَنِي مَخْزُومٍ سَرَقَتْ فَأُتِيَ بِهَا النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَعَاذَتْ بِأُمِّ سَلَمَةَ زَوْجِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((وَاللَّهِ لَوْ كَانَتْ فَاطِمَةُ لَقَطَعْتُ)) يَدَهَا فَقُطِعَتْ
Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba mwanamke mmoja katika Baniy Makhzuwm aliiba akaletwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akajikinga kwa Ummu Salamah ambaye ni mke wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Wa-Allaahi angekuwa ni Faatwimah (aliyeiba) ningelimkata mkono wake)) Ukakatwa mkono wake. [Muslim]
Pia kujikinga katika mahali kadhaa:
عَنْ أبي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه، قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((سَتَكُونُ فِتَنٌ الْقَاعِدُ فِيهَا خَيْرٌ مِنَ الْقَائِمِ، وَالْقَائِمُ خَيْرٌ مِنَ الْمَاشِي، وَالْمَاشِي فِيهَا خَيْرٌ مِنَ السَّاعِي، مَنْ تَشَرَّفَ لَهَا تَسْتَشْرِفْهُ، فَمَنْ وَجَدَ مَلْجَأً أَوْ مَعَاذًا فَلْيَعُذْ بِهِ)).
Abuu Huraryah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kutatokea fitnah ambayo mtu aliyekaa kitako atakuwa bora kuliko yule aliyesimama, na aliyesimama atakuwa bora kuliko yule anayetembea, na anayetembea humo atakuwa bora kuliko anayekimbia. Atakayajitokeza kuingia katika fitnah hizi basi zitamuangamiza. Kwa hiyo yeyote atakayepata mahali pa kujikinga au kimbilio basi ajikinge kwayo)) [Al-Bukhaariy]
Na pia:
عَنْ عُبَيْدِ اللَّهِ ابْنِ الْقِبْطِيَّةِ، قَالَ دَخَلَ الْحَارِثُ بْنُ أَبِي رَبِيعَةَ وَعَبْدُ اللَّهِ بْنُ صَفْوَانَ وَأَنَا مَعَهُمَا، عَلَى أُمِّ سَلَمَةَ أُمِّ الْمُؤْمِنِينَ فَسَأَلاَهَا عَنِ الْجَيْشِ الَّذِي يُخْسَفُ بِهِ وَكَانَ ذَلِكَ فِي أَيَّامِ ابْنِ الزُّبَيْرِ فَقَالَتْ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((يَعُوذُ عَائِذٌ بِالْبَيْتِ فَيُبْعَثُ إِلَيْهِ بَعْثٌ فَإِذَا كَانُوا بِبَيْدَاءَ مِنَ الأَرْضِ خُسِفَ بِهِمْ)) فَقُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ فَكَيْفَ بِمَنْ كَانَ كَارِهًا؟ قَالَ: ((يُخْسَفُ بِهِ مَعَهُمْ وَلَكِنَّهُ يُبْعَثُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عَلَى نِيَّتِهِ)) وَقَالَ أَبُو جَعْفَرٍ هِيَ بَيْدَاءُ الْمَدِينَةِ
‘Ubaydu-Allaah bin Al-Qitwbiyyah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba: Haarith bin Abiy Rabiy’ah na ‘Abdullaah bin Abiy Swafwaan pamoja nami tulikwenda kwa Mama wa Waumini Ummu Salamah wakamuuliza kuhusu jeshi ambalo litadidimizwa ardhini, na hii ni pale wakati ambapo Ibn Zubayr (alipokuwa gavana wa Makkah). Akahadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((Atatafuta mtu kinga katika Nyumba Tukufu kisha jeshi litatumwa kwake (ili wamuue) basi litakapoingia ardhi kame iliyohamwa (jangwa) litadidimizwa)) Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Je itakuwaje kwa ambaye amelazimishwa hayo? Akasema: ((Atatadimizwa nao lakini atafufuliwa Siku ya Qiyaamah katika hali ya niyyah yake)) Abu Ja’far amesema: Ardhi kame ni Madiynah. [Muslim]
Ama kujikinga kinyume na vile ilivyothibiti katika shariy’ah kwa kuomba kinga kwa mambo ambayo hakuna mwenye uwezo nayo isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) huwa ni shirki, kama vile walivyofanya washirikina walipokuwa wakijikinga kwa majini Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَأَنَّهُ كَانَ رِجَالٌ مِّنَ الْإِنسِ يَعُوذُونَ بِرِجَالٍ مِّنَ الْجِنِّ فَزَادُوهُمْ رَهَقًا﴿٦﴾
“Na kwamba walikuwa wanaume miongoni mwa wana Aadam wanajikinga na wanaume miongoni mwa majini, basi wakawazidishia madhambi, uvukaji mipaka ya kuasi na khofu.” [Al-Jinn: 6]
Makosa yafanywayo na Waislamu wa sasa katika kujikinga kwa asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kufuata mila mfano;
-Baadhi ya watu wanaojikinga katika kufunga ndoa kwa kumwaga damu ya mbuzi na kuikanyaga.
-Kuna wanaojikinga dhidi ya jicho baya au husda kwa kuvunja mayai kwenye hicho kitu alichonunua mtu kama vile gari mpya.
-Kuna wanaojikinga kwa mayatima kwa kuwafadhili kwa chakula kuitakidi kuwa du’aa yao inawatosheleza kujikinga.
-Kuna wanaojikinga na mashaytwaan wanapohamia nyumba mpya kwa kuchinja mbuzi au mialiko ya watu kusoma kisomo.
Kinga hizo zote hazijuzu bali mtu Muislamu anapaswa kutumia kinga zilizothibiti katika mafundisho Swahiyh aliyokuja nayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Mfano katika kuhamia nyumba mafunzo Swahiyh ni:
عن خَوْلَةَ بِنْت الحَكِيمِ قالت: سمعت رَسُولِ الله -صلى الله عليه وسلم -يقَولَ: ((مَنْ نَزَلَ مَنْزِلاً فقَالَ أَعُوذُ بِكلِمَاتِ الله التّامّاتِ مِن شَرّ مَا خَلَقَ لَمْ يَضُرّهُ شيءٌ حَتّى يَرْحَلَ مِنْ مَنْزِلِهِ ذَلِكَ))
Khawlat bint Hakiym amehadithia kwamba kamsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Atakayeteremka katika kituo (au makazi) kisha akasema: “A’uwdhu bi-Kalimaatil-LLaahit-taammati min sharri maa Khalaq - Najilinda kwa Maneno ya Allaah yaliyotimia na shari Alichokiumba” hakuna kitakachomdhuru hadi atakapoondoka katika kituo (au makazi) hicho)) [Muslim]
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni