Swali: Mimi nilioa na tahamaki mke wangu akaniomba talaka kwa hoja kwamba hakuishi maisha ya starehe vile alivyotarajia. Mimi ni kijana na mwanafunzi vilevile ambaye hali yangu ni ya kawaida. Kuniomba kwake talaka kulikuwa ni pasi na haki na mimi sikuwa na nia ya kumtaliki kwa kuwa alikuwa ni mjamzito. Je, akiniomba talaka ni haki kwangu kurudishiwa mahari? Isitoshe mahari yenyewe ilikuwa ni misaada kutoka kwa watu. Je, ikiwa atanipa mahari hayo nina haki ya kuzitumia au nitatakiwa kuzirudisha kule nilikozichukua pamoja na kuwa mimi ni mwenye madeni tele yasiyojua yeyote isipokuwa Allaah pekee.
Jibu: Katika hali hii mwanaume akiweza kuwa na subira na asimjibu ndio bora zaidi. Hili ni kwa sababu mbili:
Ya kwanza: Baadhi ya wanawake wanapokuwa na mimba wanawachukia waume zao. Wanawachukia waume zao hata kama ameishi naye miaka mingi. Kwa hivyo awe na subira juu yake mpaka yataisha. Huenda akarudi katika hali yake ya kawaida na yakamuondoka yaliyomkereta moyoni mwake.
Ya pili: Huenda baada ya kujifungua akaelewa kuwa anatakiwa kubaki kwa mume wake na hatimaye yakamwondoka yaliyomo moyoni mwake.
Mimi naona kwamba ikiwa amemridhia tabia na dini yake basi awe na subira juu yake na amfanyie wepesi mpaka migogoro iishe. Baada ya yeye kujifungua ataangaliwa kama kweli anaona hawezi kubaki basi ni sawa akaomba haki yake. Mwanamke wa Thaabit bin Qays (Radhiya Allaahu ´anhaa) alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumwambia:
“Ee Mtume wa Allaah! Sina cha kumtia dosari Thaabit bin Qays si katika tabia wala dini. Lakini mimi nachelea kufuru katika Uislamu.”
Kumesemwa tabia na dini. Isitoshe huyu ni miongoni mwa wale ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemshuhudilia Pepo.
Aliposema kuwa anachelea kufuru katika Uislamu bi maana kwamba hawezi. Hapo ndipo alipomwambia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
“Je, utaweza kumrudishia bustani yake?” Akajibu: “Ndio.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwita na kumwambia: “Chukua bustani yako na umtaliki.”
Akachukua bustani yake na kumtaliki. Kwa hivyo tunamshauri mwanaume huyu asubiri mpaka pale mwanamke huyu atapojifungua. Huenda vilevile akabadilika baada tu ya kujifungua midhali ameridhika na dini na tabia yake. Vinginevyo mambo yasipobadilika basi hakuna ubaya kwake akamuomba haki yake yote aliyompa kuanzia mahari, zawadi na vinginevyo.
Ikiwa baadaye atarudi kwake basi hivyo vitu ni vya mwanaume kwa kuwa alivichukua kwa haki. Ikiwa alivichukua kwa haki yake basi yeye ndiye mwenye kuvimiliki. Wakati mwanaume alipovichukua kwa ajili ya ndoa amekuwa ni mwenye kuvimiliki. Vikirudi kwake basi ni miliki yake. Katika hali hii sio wajibu kwake kuvirudisha kwa yule aliyevichukua kutoka kwake.
Rejea al-Liqaa' ash-Shahriy (31)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni