Translate

Jumatano, 12 Juni 2019

'Ikrimah Bin Abi Jahl (Radhwiya Allaahu 'Anhu)

'Ikrimah Bin Abi Jahl (Radhwiya Allaahu 'Anhu)


Mtume Muhammad(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoanza Da’wah yake pale alipopatiwa Utume, ‘Ikrimah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa katika ujana akiwa na miaka baina ya ishirini na thelathini. Alikuwa anatukuzwa sana na kabila lake la Quraysh kwa ajili utajiri na nasaba nzuri. Wengine kama yeye, Sa’ad bin Abi Waqqaas, Musw’ab bin ‘Umayr na watoto wengine wa familia tukufu huko Makkah walikuwa tayari wamesilimu. Yeye pia angekuwa amesilimu haingekuwa kwa ushawishi wa baba yaake kwani baba yake alikuwa adui nambari moja dhidi ya ulinganizi wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mtesaji mkubwa hapo Makkah.

Kama baba yake alivyokuwa, naye aliwaadhibu sana Waumini ambao walibaki katika ukweli wa Uislamu na Iymaan. ‘Ikrimah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alijikuta akiutetea uongozi na mamlaka ya baba yake aliposimama kuwa dhidi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Uadui wake dhidi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), unyanyasaji wake kwa wafuasi wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na majaribio yake ya kuukwamisha Uislamu na Waislamu ulimfanya apendwe na baba yake.

Katika Vita vya Badr, Abu Jahl aliongoza jeshi la Mushrikina wa Makkah dhidi ya Waislamu. Aliapa kwa al-Laat na al-‘Uzza kuwa hatorudi Makkah mpaka amsagesage Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Abu Jahl mwenyewe alikuwa miongoni wa watu wa kwanza kuuliwa katika vita hivyo. Mtoto wake, ‘Ikrimah alimuona wakati mikuki ilikuwa ikiingia katika mwili wake na kumsikia akitoa ukulele wa mwisho wa uchungu. ‘Ikrimah alirudi Makkah akiwa ameacha maiti ya mtemi wa Quraysh, baba yake. Alikuwa anataka kumzika Makkah lakini kushindwa kukubwa kwao kulikwaza suala hilo, hivyo kutowezekana.

Kuanzia siku hiyo, moto wa uchungu uliwaka kwa nguvu sana katika moyo wa ‘Ikrimah. Wale wengine ambao baba zao waliuliwa katika Vita vya Badr, waliingiwa na uadui kwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wafuasi wake. Hilo lilipelekea Vita vya Uhud.

Katika Vita vya Uhud, ‘Ikrimah alifuatana na mkewe, Umm Hakiym. Mkewe pamoja na wanawake wengine walisimama nyuma ya safu ya vita wakipiga magoma, huku wakiwahimiza Quraysh wapigane kwa shime na hamasa zaidi na kuwasuta wapanda farasi wowote ambao walitaka kukimbia kwenye vita na kutoroka.

Aliyekuwa akiongoza jeshi la Mushrikina upande wa kuume alikuwa Khaalid bin Al-Waliyd ilhali upande wa kushoto alikuwa ni ‘Ikrimah bin Abi Jahl. Quraysh waliwatia hasara kubwa Waislamu na kudhania kuwa tayari wamelipiza kisasi kwa kushindwa kwao katika Vita vya Badr. Hata hivyo, hiyo haikuwa ni mwisho wa mzozano na mapigano.

Katika Vita vya Khandaq, Mushrikina wa Quraysh waliuzunguka mji wa Madiynah kwa muda mrefu. ‘Ikrimah, alihisi mbano wa kuuzunguka mji huo, akaona sehemu ambayo ni nyembamba. Kwa juhudi kubwa aliweza kuruka shimo hilo wakamfuata kikundi kidogo cha Quraysh. Hilo lilikuwa tendo la kijinga, na mmoja wao aliuliwa papo hapo naye aliweza kupona tu pale aliporudi mbio mbio.

Miaka minane baada Hijrah, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alirudi Makkah na Maswahaba elfu kumi. Quraysh waliwaona Waislamu wakija na wakaamua kuwaachilia njia kwani walijua kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametoa maagizo kwa majemadari wake wasianze vita. ‘Ikrimah na baadhi yao waliokuwa naye walikwenda kinyume na ijmai ya Quraysh na wakafanya hima ya kulizuilia jeshi la Waislamu. Khaalid ibn al-Waliyd, aliyekuwa Muislamu, alipambana nao na kuwashinda ambamo baadhi ya washiriki wa ‘Ikrimah waliuliwa na wengine kukimbia. Miongoni mwa waliokimbia ni ‘Ikrimah mwenyewe.

Ubwanyenye na utukufu aliokuwa nao ‘Ikrimah wote ukaanguka. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia Makkah na kuwasamehe Quraysh wote walioingia Msikiti Mtukufu, au waliokaa katika nyumba zao au walioingia katika nyumba ya Abu Sufyaan, mtemi wa Quraysh.
Hata hivyo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakutoa msamaha kwa baadhi ya watu aliowataja kwa majina. Alitoa maagizo kuwa hao watu wauliwe hata wakiwa kwenye kis-wa cha Ka‘bah. Juu ya orodha hiyo ya kuuliwa alikuwa ni ‘Ikrimah bin Abi Jahl. ‘Ikrimah alipojua hilo, alitoka Makkah akiwa anakimbia huku amejibadilisha akielekea Yemen.

Umm Hakiym, mke wa ‘Ikrimah, alikwenda katika kambi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hind bint ‘Utbah, mke wa Abu Sufyaan na mama wa Mu’aawiyah, alikuwa pamoja na Umm Hakiym wanawake wengine kumi waliotaka kumbayi’ Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kambini kulikuwa na wakeze wawili, binti yake Faatwimah na baadhi ya wanawake wa ukoo wa Abdul-Muttwalib. Hind ndiye aliyezungumza akiwa amejifunika huku akiwa amesikitishwa kwa yaliyompata Hamzah, ‘ami ya Mtume katika Vita vya Uhud. “Ewe Mtume wa Allaah! Sifa zote njema anastahiki Allaah Ambaye Ameibainisha Diyn Aliyoichagua. Nakuomba kwa uhusiano wa damu unitendee wema. Sasa nimesilimu pamoja na kuyakinisha ukweli wa ulinganizi wako”, alisema. Baada ya hapo akajifunua na kusema: “Mimi ni Hind, binti ya ‘Utbah, ewe Mtume wa Allaah”. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu kwa kumwambia: “Karibu sana”.

“Naapa kwa Allaah”, aliendelea Hind, “Hakukuwa na nyumba hapa duniani niliyotaka kuivunja kuliko yako. Sasa, hakuna nyumba duniani ninayoipenda sana kuienzi na kuinyanyua kuliko yako”.

Umm Hakiym naye alinyanyuka na kuingia katika Uislamu, akasema:“Ewe Mtume wa Allaah! ‘Ikrimah amekukimbia na kuelekea Yemen kwa hofu ya kwua utamuua. Naomba umpe amani na Allaah naye Atakupa amani”. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuahidi kwa kumwambia:“Amepata amani na usalama kutoka kwangu”. Umm Hakiym hapo hapo akatoka kumtafuta ‘Ikrimah. Aliyefuatana naye alikuwa ni mtumwa wake Myunani (Mgiriki). Walipofika mbali huyu mtumwa alitaka kumfanyia utovu wa adabu, hata hivyo alifanikiwa kumweka mbali naye mpaka alipofika katika makazi ya Waarabu. Aliomba usaidizi wao dhidi yake. Waarabu hao walimfunga mtumwa na kumweka kwao. Umm Hakiym aliendelea na safari yake mpaka mwishowe akampata ‘Ikrimah kwenye ufuo wa Bahari Nyekundu (Red Sea) katika eneo la Tihamah. Alikuwa akizungumza na baharia Muislamu ili amsafirishe, ambaye alimwambia:“Kuwa msafi na mwenye Niyah njema nami nitakusafirisha”. ‘Ikrimah akauliza: “Nawezaje kuwa msafi?”Huyo Muislamu akamwambia:“Sema, Ash-hadu an laa ilaaha illa Allaahu wa Ash-hadu anna Muhammadan Rasuulu Allaah”. ‘Ikrimah akamwambia: “Mimi nimekimbia jambo hilo.”

Hapo, Umm Hakiym alikuja kwa ‘Ikrimah na kumwambia: “Ewe ndugu yangu! Nimekuja kwako kutoka kwa mtu mkaribu kabisa, mwema miongoni mwa watu, mbora wa watu… Kutoka kwa Muhammad bin ‘Abdillaah. Nimemuomba akupe amani na usalama na hilo umepatiwa. Hivyo, usijiangamize”. Akauliza kwa mshangao: “Je, umezungumza naye?” “Ndio, nimezungumza naye, naye ametoa ahadi ya kukupatia amani”, alimuyakinishia, nao wakarudi pamoja. Hapo akamuelezea jaribio la yule mtumwa wa Kiyunani ya kutaka kumnajisi. ‘Ikrimah alikwenda moja kwa moja mpaka katika makazi ya Waarabu, akamshika yule mtumwa na kumuua.

Katika sehemu moja ya mapumziko yao, ‘Ikrimah alitaka kulala na mkewe, lakini mkewe alikataa katakata na kumwambia: “Mimi ni Muislamu nawe ni Mushrik, hivyo hatuwezi kufanya hilo ulitakalo”.‘Ikrimah alirudishwa kabisa, hivyo akamwambia, “Kuishi bila ya wewe na pasi na wewe kulala na mimi ni jambo lisilowezekana”. ‘Ikrimah alipokaribia Makkah, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaambia Maswahaba zake: “Ikrimah bin Abi Jahl atawajieni akiwa Muumini na Muhaajir. Hivyo, msimtusi baba yake, kwani kuwatusi waliokufa inaleta huzuni kwa walio hai na hilo haliwafikii waliokufa”.

‘Ikrimah na mkewe walifika mpaka alipokuwa amekaa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliinuka na kumsalimia kwa hima kubwa.“Muhammad”, alisema ‘Ikrimah,“Umm Hakiym amenieleza kuwa umenipatia amani”. “Ndio”, alisema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), “Wewe uko salama”.

“Unalingania nini?” aliuliza Ikrimah.“Nakulingania ushuhudie kuwa hapana mola apasaye kuabudiwa ila Allaah na kuwa mimi ni mtumwa na Mjumbe wa Allaah, kusimamisha Swalaah, kutoa Zakaah na kutekeleza majukumu yote ya Uislamu”.

“Naapa klwa Allaah”, alijibu ‘Ikrimah, “Umeita tu kwa kilicho cha kweli na haki na umeamrisha tu kilicho kizuri. Umeishi miongoni mwetu kabla ya kupatiwa risala na wakati huo ulikuwa mwaminifu wa kauli miongoni mwetu na mwema zaidi kati yetu”. Akanyosha mono wake, akasema: “Nashuhudia kuwa hakuna mungu wa kuabudiwa ila Allaah na kuwa Muhammad ni mtumishi na Mtume Wake”. Kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuagiza aseme: “Namuita Allaah na wote waliokuwa hapa kushuhudia kuwa mimi ni Muislamu ambaye ni Mujaahid na Muhaajir”. ‘Ikrimah aliirudia kauli hii, kisha akasema:“Nakuomba unitakie msamaha kwa Allaah kwa uadui wote niliouelekeza dhidi yako na kwa matusi yoyote niliyokutusi kwayo ukiwepo au kutokuwepo”. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuombea kwa kusema: “Ee Mola! Msamehe kwa uadui wote ulioelekezwa dhidi yangu na kwa vita vyote alivypigana kutaka kuizima nuru Yako. Msamehe kwa aliyoyasema au kufanya nikiwepo au nilipokuwa sipo ili kunitweza”.

Uso wa ‘Ikrimah uling’aa kwa furaha.“Naapa kwa Allaah, ewe Mtume wa Allaah! Naahidi kuwa vyote nilivyotumia kuipinga njia ya Allaah, nitatumia mara mbili katika njia Yake na vita vyovyote nilivyopigana dhidi ya njia ya Allaah na nitapigana mara mbili katika njia Yake”.

Kuaniza siku hiyo, ‘Ikrimah alisimama imara kabisa katika risala ya Uislamu kama mpandaji farasi mahiri na shujaa na mcha Mungu aliyekuwa akitumia muda wake mwingi katika ‘Ibaadah Msikitini huku akisoma Kitabu cha Allaah. Mara nyingi alikuwa akiushika Msahafu na kusema: “Kitabu cha Mola wangu Mlezi, maneno ya Mola wangu”. Na alikuwa analia sana kwa hofu ya Allaah Aliyetukuka.

‘Ikrimah alibaki na ahadi yake aliyoitoa kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Vita vyovyote walivyopigana Waislamu baada ya hapo, alishiriki pamoja nao kwa dhati kabisa. Katika Vita vya Yarmuk, aliingia katika uvamizi kama mtu mwenye kiu akihitajia maji baridi siku ya joto. Katika pambano moja ambalo Waislamu walivamiwa sana, ‘Ikrimah aliingia ndani sana katika safu ya Warumi. Khaalid bin al-Waliyd (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikimbia kumfuatia na kumwambia,“Usifanye hivyo, ‘Ikrimah. Kifo chako kitakuwa pigo kubwa kwa Waislamu”.

“Wacha tuendelee, Khaalid”, akasema ‘Ikrimah, akiwa katika kilele cha hamasa. “Wewe umepata hadhi ya kuwa pamoja na Mtume wa Allaah kabla ya leo. Ama kuhusu mimi na baba yangu, tukiwa adui yake mkubwa kwa hivyo niachilie sasa ili nifutiliwe madhambi kwa niliyoyafanya. Nilipigana dhidi ya Mtume wakati mwingi. Je, niwakimbie Warumi?”
Kisha akawaita Waislamu kwa ukulele, “Nani atatoa ahadi ya kuigana hadi kufa?” Waislamu mia nne wakiwemo al-Haarith bin Hishaam and Ayyaash bin Abi Rabi’ah waliitikia mwito wake. Walijivurumiza ndani ya vita na kupigana kwa ushujaa bila ya uongozi wa Khaalid bin al-Waliyd (Radhiya Allaahu ‘anhu). Ushujaa wao ulitoa mwanya kupatikana kwa ushindi wa Waislamu.

Vita vilipoisha, miili mitatu ya Mujaahidiyn waliojeruhiwa ilikuwa imelala kwenye uwanja wa vita, miongoni mwao wakiwemo Al-Haarith bin Hishaam, Ayyaash bin Abi Rabi’ah na ‘Ikrimah bin Abi Jahl (Radhiya Allaahu ‘anhum). Al-Haarith aliitisha maji ya kunywa. Yalipoletwa kwake, Ayyaash alimtizama na al-Haarith akasema:“Mpatie Ayyaash”. Walipomfikia Ayyaash, akawa tayari ameaga dunia. Waliporudi kwa al-Haarith na ‘Ikrimah, wakawakuta pia nao wameaga dunia. Maswahaba wakawaombea kwa Allaah Aliyetukuka awe radhi nao wote na Awape kinywaji kutoka katika chemchemi ya Kawthar, Peponi, kinywaji ambacho wenye kukinywa hawatokuwa na kiu baada ya hapo abadan.

Huyo ndiye ‘Ikrimah bin Abi Jahl (Radhwiya Allaahu ‘anhu).


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...