Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa ya kufunga mwezi huu mtukufu. Licha ya kupata utakaso wa roho, funga hutupatia faida mbalimbali za kiafya ambazo baadhi tumeziona katika makala zilizopita. Ndugu msomaji, ungana nami katika makala hii ili kujionea miongoni mwa faida ambazo mwili huzipata kutokana na kitendo cha kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Kupungua uzito
Pengine hii inaweza kuwa ni faida iliyopatikana kwa wengi miongoni mwa waliomaliza mfungo. Katika siku za kawaida, mwili huhifadhi chakula cha ziada katika mfumo wa mafuta. Kama tunavyojua, mafuta ndiyo kisababishi kikubwa cha kuongezeka kwa uzito wa mwili. Hivyo, kitendo cha kufunga huufanya mwili kutumia sehemu kubwa ya akiba hii ya mafuta ili kujipatia nishati ya kuendesha shughuli mbalimbali za mwili. Pia, wakati wa kufunga matumizi ya mwili huwa makubwa kiasi kwamba mwili hunyimwa fursa ya kuhifadhi chakula katika mfumo wa mafuta.
Kupungua kwa sukari katika damu
Ndugu yangu uliyemaliza mfungo hivi karibuni, elewa ya kuwa, vyakula vyote vyenye asili ya wanga huvunjwavunjwa na mwili ili iwe sukari (glucose). Sukari hii huzunguka katika mfumo wa damu na kusambazwa katika sehemu zote za mwili. Katika hali ya kawaida, mtu anapokuwa hajafunga, sukari huwa katika kiwango cha juu kiasi, jambo ambalo si zuri kwa wagonjwa wa kisukari. Hivyo, sukari hii hutumiwa wakati mtu akiwa na njaa na mwisho kabisa zaidi ya asilimia 30 ya sukari ya ziada iliyokuwepo katika damu itakuwa imetumika. Kwa mtu wa kawaida, jambo hili linaweza lisiwe na faida za papo kwa papo lakini ukweli wa mambo ni kuwa jambo hili ni faida kubwa sana hasa kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari.
Kuwezesha uzalishwaji wa seli mpya katika mwili
Kwa kawaida, katika mwili wa binadamu kuna seli nyingi ambazo zimezeeka na nyingine gonjwa. Ingawa uwepo wa seli hizi haumpelekei mtu kupata dalili yoyote ya maradhi, seli hizi zisizo na faida husababisha matumizi yasiyo ya lazima ya nishati ya mwili. Hivyo, mtu akifunga huufanya mwili kuzalisha seli mpya na pia kuchukua hatua dhidi ya seli hizi ambazo pengine zikiachwa zingeweza kuleta madhara hapo baadae.
Kupungua kwa shinikizo la damu
Imebainika ya kuwa, kitendo cha kufunga kina uhusiano wa karibu na shinikizo la damu la mwili. Ingawa uhusiano huu si wa moja kwa moja; imebainika ya kuwa, utumiaji wa chumvi huwa ni mdogo kwa sababu njaa humpunguzia mtu tamaa ya kula chumvi na kumfanya atamani vyakula vyenye sukari. Upungufu huu wa matumizi ya chumvi umekua mchango mkubwa wa kupunguza shinikizo la damu.
Funga kichocheo cha kuacha vileo
Wakati wa kufunga si vyakula na vinywaji tu viliachwa kutumiwa, bali pia vileo mbalimbali huachwa kama vile pombe, sigara, tumbaku na vingine mfano wa hivyo. Hii imekua fursa nzuri ya kukabiliana na uteja huu kwani kuweza kuvumilia mwezi mzima bila ya kutumia vitu hivi kunaashiria ya kwamba mtu anaweza kuishi muda wote bila ya kutumia vitu hivi.
Kupunguza sumu
Kwa hali ya kawaida, mwili huhifadhi vitu vingi vinavyotokana na vyakula tunavyokula kila siku. Hifadhi ya vitu hivi mara nyingi huwa katika seli za mafuta hivyo sumu hizi huondolewa mwilini ikiwa mafuta yataunguzwa wakati mtu akiwa na njaa muda wa mchana.
Afya ya ubongo
Inaaminika ya kwamba, kitendo cha kufunga kinaufanya ubongo kuzalisha kemikali maalum (neurotrophic factors) ambazo huufanya ubongo kuzalisha seli mpya. Uzalishaji huu wa kemikali huufanya ubongo kufanya kazi kwa ufanisi zaidi tofauti na kabla ya kufunga.
Kubwa zaidi
Ndugu yangu Muislamu, funga ya Ramadhan imetuachia faida kubwa sana katika miili yetu lakini kubwa zaidi tunalopaswa kushukuru kwa funga hii ni kutufanya “tuwe wachamungu”, [Qur’an, 2.183]. Hivyo, ni muhimu sana kuyaendeleza yale.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni