Kipindupindu ni moja ya maradhi ya mlipuko yanayoenea kwa kasi sana. Kipindupindu husababisha kuharisha na kutapika mfululizo hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa maji katika mwili.
Kabla ya kuendelea, ni vyema tukavijua vimelea vinavyosababisha kipindupindu. Ugonjwa huu hatari husababishwa na bakteria wanaoitwa Vibrio cholerae wanaopatikana kwenye maji machafu na ambao huenezwa na nzi. Hivyo, mtu anaweza kuambukizwa mara baada ya kuyanywa maji yenye bakteria hawa.
Hali ya sasa
Mpaka kufikia Mei 31, tayari visa vipatavyo 39 vya kipindupindu vimeripotiwa jijini Dar es Salaam na kusababisha kifo cha mgonjwa mmoja.
Vipi huambukiza?
Kipindupindu huambukiza kwa kula choo kikubwa cha mtu aliyeathirika na ugonjwa huu (fecal oral route). Ili kuelewa ni vipi mtu anaweza kula choo kikubwa bila ya yeye kujua, turejee uhusiano uliopo kati ya choo kikubwa (chanzo), nzi (msambazaji) na chakula (maambukizi).
Ndugu msomaji, ikiwa mtu atajisaidia ovyo choo kikubwa bila shaka atavutia nzi. Nzi huyu akitua kwenye kinyesi chenye kipindupindu hubeba kiasi kidogo cha choo kupitia miguu yake na sehemu nyingine za mwili. Kisha, nzi huyu hutua kwenye chakula na kubakisha kiasi kidogo cha choo na mlaji huambukizwa mara moja baada ya kula chakula hicho chenye kinyesi.
Dalili za kipindupindu
Kipindupindu ni ugonjwa unaoua haraka sana ikiwa mgonjwa hatopatiwa tiba sahihi kwa wakati unaostahili. Hivyo, ni muhimu kuzifahamu dalili za ugonjwa huu. Ugonjwa unaweza kuepukika ikiwa tu kanuni za usafi zitafuatwa.
Dalili za kipindupindu
Kwanza, ijulikane kuwa, kipindupindu kina dalili kuu mbili ambazo ni kuharisha na kutapika.
Mgonjwa huharisha maji ambayo yanafanana na maji yaliyooshewa mchele na harufu yake inafanana na shombo la samaki. Kuharisha huku, kwa kawaida, huanza ghafla bila ya kuumwa na tumbo.
Dalili ya pili ya kipindupindu ni kutapika mfululizo na hivyo kupelekea upotevu mkubwa wa maji mwilini. Kutapika huku hupelekea mshtuko wa mwili (hypovolemic shock) na mwishoe kifo.
Huduma ya kwanza
Ndugu msomaji, kama tulivyojionea hapo juu, kipindupindu ni ugonjwa unaoua kwa kukausha maji mwilini. Hivyo, huduma kuu ya kwanza kwa mgonjwa ni kuhakikisha anapata kiwango kikubwa cha maji safi na salama ambayo ndani yake kuna mchanganyiko wa chumvi na sukari.
Mchanganyiko huu unaweza kutengenezwa majumbani kwa kuchukua ujazo wa lita moja ya maji safi na salama kisha kuyachanganya na chumvi nusu kijiko cha chai na sukari vijiko sita vya chai. Mchanganyiko huu apewe mgonjwa lita nyingi iwezekanavyo wakati taratibu za kumpeleka kituo cha afya zikiwa zinafuatwa.
Namna ya kujikinga
Kama tulivyoona hapo mwanzo kua, kipindupindu kinatokana na kula choo kikubwa cha mtu aliyeathirika hivyo ili kujikinga na ugonjwa huu lazima tukate mnyororo wa mahusiano kati ya choo kikubwa (chanzo), nzi (msambazaji) na chakula au matunda (maambukizi) kwa kufuata mambo yafuatayo:
- Hakikisha unanawa mikono kwa maji safi na sabuni baada ya kutoka msalani.
- Epuka kula chakula kilichokua wazi.
- Epuka kula chakula kiholela katika magenge ambayo hayazingatii usafi.
- Hakikisha maji ya kunywa yamechemshwa, yamechujwa na kufunikwa vizuri.
- Osha matunda kwa maji yanayotiririka.
- Nawa mikono kwa maji yanayotiririka kabla ya chakula.
- Choma moto au hifadhi takataka hasa taka mbichi katika chombo maalum chenye mfuniko.
- Angamiza nzi wote kwa kutumia dawa za kupuliza za kuulia wadudu na pia ni muhimu kwa choo cha shimo kuwa na mfuniko.
- Epuka kujisaidia ovyo hasa karibu na vyanzo vya maji. Watoto wadogo wapelekwe vyooni au watumie vyombo maalum kwa ajili ya haja kubwa na kisha chombo hicho kitupwe chooni au kifunikwe ardhini.
Ndugu msomaji, ni muhimu sana kumuwahisha kituo cha afya mtu yeyote mwenye dalili za ugonjwa wa kipindupindu na pia kutoa taarifa katika mamlaka husika ikiwa unahisi ugonjwa huu umeingia katika maeneo unayoishi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni