Haki za mume na mke
Haki za mume na mke zimedhihirishwa katika Qur-aan na Sunnah. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:
وَلَهُنَّ مِثْلُ الَّذِي عَلَيْهِنَّ بِالْمَعْرُوفِ وَلِلرِّجَالِ عَلَيْهِنَّ دَرَجَةٌ وَاللّهُ عَزِيزٌ حَكُيمٌ
Na hao wanawake wana kama ile (haki) iliyo juu yao kwa ma’aruwf (mujibu wa shariy’ah). Na kwa wanaume juu ya hao wanawake wana daraja. (Al-Baqara 2: 228)
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akasema katika Hijjah ya kuaga aliposimama kuwahutubia Maswahaaba:
((يآ أيُّهَا النَّاسُ إِنَّ لِنِسَائِكُمْ عَلَيْكُمْ حَقاً وَلَكُمْ عَلَيْهِنَّ حَقّ)) أبو داود
((Ee nyie watu, hakika nyinyi mna haki juu ya wake zenu na wake zenu wana haki juu yenu)) Abu Daawuud
Zifuatazo ni haki zinazowahusu wote wawili; mke na mume katika kuamiliana:
1-Ukweli
Mke na mume wawe ni wakweli baina yao kwa kauli na vitendo. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَكُونُوا مَعَ الصَّادِقِينَ
Enyi mlioamini! Mcheni Allaah na kuweni pamoja na wakweli. (At-Tawbah: 11)
2-Mapenzi, huruma na utulivu.
Kila mmoja amdhihirishie mwenziwe mapenzi, na wawe na huruma baina yao katika shida na matatizo mpaka iwe kila mmoja awe ni kutulizo cha mwenziwe wakati wa dhiki. Allaah (Subhanaahu wa Ta’ala) Anasema:
وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَة ًإِنَّ فِي ذَلِكَ لَآ يَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ
“Na katika Aayaat Zake ni kwamba Amekuumbieni kutokana na nafsi zenu (jinsi moja) wake ili mpate utulivu kwao; na Amekujaalieni baina yenu mapenzi na Rahmah. Hakika katika hayo bila shaka (kuna) Aayah kwa watu wanaotafakari.” (Ar-Ruwm 30: 21)
3-Amana, Uaminifu na kutumiza ahadi:
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amewasifu na kuwaahidi Jannah wanaotimiza amana na ahadi zao:
وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ
|
Na ambao amana zao na ahadi zao wanazichunga (wanazitimiza). [Al-Muuminuwn 8] (Al-Ma’aarij: 32)
|
Kuweko uaminifu kutazuia dhana mbaya au kutiliana shaka:
فَإِنْ أَمِنَ بَعْضُكُم بَعْضًا فَلْيُؤَدِّ الَّذِي اؤْتُمِنَ أَمَانَتَهُ وَلْيَتَّقِ اللّهَ رَبَّهُ
Na ikiwa mmoja wenu amewekewa amana na mwengine, basi airudishe yule ambaye ameaminiwa amana ya mwenzake; na amche Allaah Mola wake (Al-Baqarah: 283)
4-Tabia njema
Wawe na tabia njema katika kauli na matendo ili iwepo heshima baina yao:
وَعَاشِرُوهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ
Na kaeni nao kwa wema ((An-Nisaa 4: 19))
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akausia:
((Nakuusieni kuwafanyia wema wanawake)) Al-Bukhaariy na Muslim
5-Kuhifadhiana siri
Haiwapasi wote kutoleana siri zao au kutoa aibu zao nje:
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Watu watakaokuwa katika hali mbaya kabisa mbele ya Allaah Siku ya Qiyaamah ni mwanamme anaekwenda kwa mke wake na mke kwenda kwa mume wake kisha (mmojawao) akapita kutoa siri yake)) Muslim
Haki hizo zitakapotimizwa kwa mume na mke, itakuwa ni kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
وَلاَ تَنسَوُاْ الْفَضْلَ بَيْنَكُمْ إِنَّ اللّهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ
Na wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Allaah kwa myatendayo ni Baswiyr (Mwenye kuona). (Al-Baqarah 2: 237)
NA ALLAAH ANAJUA ZAIDI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni