Translate

Alhamisi, 13 Juni 2019

Maana ya Tawbah

Maana ya Tawbah


Maana ya tawbah ni kurejea. Na tawbah inaanza pale mtu anapokumbuka madhambi yake, akaingiwa na khofu ya kughadhibikiwa na Rabb wake, ikampelekea kurejea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kumuomba Amghufurie madhambi yake.

Tawbah ni aina ya ‘ibaadah, haghafiliki nayo Muumini. Hata Manabii walikuwa wakiomba tawbah na wakiwaamrisha watu wao pia waombe maghfirah na tawbah:

Nabiy Shu’ayb ('Alayhis-Salaam) aliwaamrisha watu wake:

وَاسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ ۚ إِنَّ رَبِّي رَحِيمٌ وَدُودٌ﴿٩٠﴾
 “Na ombeni maghfirah kwa Rabb wenu, kisha tubieni Kwake. Hakika Rabb wangu ni Mwenye kurehemu, Mwenye upendo khalisi.” [Huwd: 90]

Tawbah ni sababu mojawapo ya kufaulu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٣١﴾
Na tubuni kwa Allaah nyote, enyi Waumini mpate kufaulu. [An-Nuwr: 31]


Kuomba tawbah kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) isiwe kwa ajili ya  madhambi makubwa pekee, bali mtu anahitaji kuomba tawbah usiku na mchana kwani madhambi mangapi madogo madogo mtu anayafanya mengine bila ya kujijua. Atakuja kuyakuta katika daftari lake ikiwa ataipuuza tawbah.   

Muislam anapofanya maasi ni muhimu kurudi kwa Allaah ('Azza wa Jalla)  aombe maghfirah na tawbah ili airudishe nafsi yake katika kutakasika. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) yuko tayari kabisa kupokea tawbah zetu na kutughufuria madhambi yetu. Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 وَهُوَ الَّذِي يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَعْفُو عَنِ السَّيِّئَاتِ
Naye Ndiye Ambaye Anapokea tawbah kutoka kwa waja Wake, na Anasamehe maovu [Ash-Shuwraa: 25]


Nani aliyejidhulumu nafsi yake akawa hana raha kutokana na madhambi aliyoyatenda? Basi tambua  ee ndugu Muislamu kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Mwingi wa kughufuria na Mwenye kurehemu kama Anavyosema:

 وَمَن يَعْمَلْ سُوءًا أَوْ يَظْلِمْ نَفْسَهُ ثُمَّ يَسْتَغْفِرِ اللَّـهَ يَجِدِ اللَّـهَ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿١١٠﴾
Na atakayetenda ovu au akajidhulumu nafsi yake; kisha akamwomba Allaah maghfirah; atamkuta Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu[An-Nisaa: 110]

Na kwa Rahmah Yake Allaah ('Azza wa Jalla) Ametuamrisha pia kukimbilia Kwake kuomba tawbah. Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ
Na kimbilieni maghfirah kutoka kwa Rabb wenu [Aal-'Imraan: 133]

 Na  Allaah  anajua  zaidi


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...