Translate

Jumatano, 26 Juni 2019

Tafsiyr ya Aayah “Na Arshi Yake Ikawa Katika Maji”

SWALI



Naomba maelezo na mafundisho kutoka katika aya "wakaana arshuhuu ala-lmaai" 



MAJIBU



Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Arshi ya Allaah Aliyetukuka.

Aayah hiyo inapatikana katika Surah Huud (11). Aayah yenyewe inasema hivi:

وَهُوَ الَّذِي خَلَق السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَكَانَ عَرْشُهُ عَلَى الْمَاء لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلاً وَلَئِن قُلْتَ إِنَّكُم مَّبْعُوثُونَ مِن بَعْدِ الْمَوْتِ لَيَقُولَنَّ الَّذِينَ كَفَرُواْ إِنْ هَذَا إِلاَّ سِحْرٌ مُّبِين

Maana ya Aayah hiyo ni:
“Na Yeye Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita; na ikawa ‘Arshi Yake juu ya maji; (kakuumbeni) ili Akujaribuni nani kati yenu mwenye ‘amali nzuri zaidi. Na kama ukisema: “Nyinyi mtafufuliwa baada ya mauti”; bila shaka watasema wale waliokufuru: “Hakika haya si chochote isipokuwa ni sihiri bayana."[11: 7].

Hebu tutazame hii ibara imefasiriwa vipi na Wanachuoni wetu wa tafsiyr.

Ibn Kathiyr naye amesema yafuatayo: “Allaah Aliyetukuka, Anatueleza kuhusu uwezo Wake na nguvu Zake, kuwa Ameumba mbingu na ardhi kwa siku sita. Ametaja kuwa 'Arsh Yake ilikuwa juu ya maji kabla ya hapo kama alivyonukuu Ahmad kutoka kwa ‘Imran Huswayn (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ‘Kubalini bishara, enyi Bani Tamiym!’ Wakasema: ‘Hakika umetuletea bishara njema na tayari umetupatia’. Kisha akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ‘Kubalini bishara, enyi watu wa Yemen!’ Wakasema: ‘Tumekubali. Hivyo tujulishe kuhusu mwanzo wa mambo na ilivyokuwa’. Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ‘Allaah Alikuwepo kabla ya chochote na kiti Chake cha enzi kilikuwa juu ya maji. Aliandika kwenye ubao uliohifadhiwa kila jambo’ …”

Muslim naye amenukuu kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allaah Alikuduria riziki za viumbe wote kabla ya kuumba mbingu na ardhi kwa miaka elfu khamsini na 'Arsh Yake ilikuwa juu ya maji”.


Na Al-Bukhaariy amemkuu Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Je mumeona kilichotumiwa kuanzia kuumbwa mbingu na ardhi? Hakiko hicho (kilichotumiwa) hakipunguzi kwa kilichomo Mkononi Mwake wa kuume (hata chembe) na 'Arsh Yake ilikuwa juu ya maji. Mkononi Mwake kulikuwa na mizani, Aliyokuwa Akiishusha na kuinyanyua” [juzuu ya pili].


Al-Qurtwubiy amesema: “Allaah Amebainisha kuwa kuumbwa kwa 'Arsh na maji kulikuwa kabla ya kuumbwa kwa mbingu na ardhi” [juzuu 5, uk. 8]

Na Allaah Anajua zaidi


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...