Jumuiya ya Wanafunzi na Vijana wa Kiislamu nchini (TAMSYA) imepanga kuanzisha kituo maalumu cha mafunzo ya ujasiriamali na ujuzi mwingine kwa minajili ya kusaidia vijana waweze kujikwamua kimaisha.
Akiongea katika semina elekezi ya siku mbili iliyowakutanisha wanafunzi wa kike wanaotarajia kumalizia vyuo vikuu hapa nchini, Amirati Taifa wa TAMSYA, Neema Mandulanga ambaye amesema kuwa lengo lao ni kuona vijana wanapata elimu na ujuzi ili kuwa jenga kukabiliana na wimbi la ukosefu wa ajira na pia kusaidia jamii zao.
Katika semina hiyo iliyoandaliwa na Idara ya Wanawake wa jumuiya hiyo na kufanyika Dar es Salaam katika ukumbi wa Red Cross, Neema alisema TAMSYA imegundua kuwa vijana wengi wana changamoto ya ukosefu wa ujuzi katika maisha yao na hivyo kushindwa kuajirika au kujiajiri.
Kuhusu malengo ya semina hiyo iliyovutia washiriki zaidi ya 50, Neema alisema: lengo ni kuwajengea uwezo washiriki hao katika masuala ya ujasiriamali, hususani kuwapa elimu ya fedha, akiba na mikopo.“Warsha ya leo inalenga kuwapatia washiriki hawa elimu ya ujasiriamali, elimu ya fedha kama kujua jinsi ya ku–‘manage’ (kusimamia) mapato na matumizi ya fedha,” alisema Neema.
Naye Rais wa TAMSYA Taifa, Mohaja Kabadi, amesema wanatarajia kuwa washiriki wa semina hiyo watakwenda kuwa wakufunzi kwa wenzao wengine.
Mgeni rasmi Kwa upande wake mgeni rasmi, Katibu Mtendaji wa Baraza na Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi liliopo chini ya Ofisi ya waziri Mkuu, Beni Issa amesisitizia wananchi umuhimu kujiunga na VICOBA kwa ajili ya kujikwamua kimaisha. Katibu huyo aliongeza kuwa ili dini ya Uislamu iweze kusongambele ni muhimu Waumini wake wawe na nguvu za kiuchumi.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TAMSYA, Aklan Mohamed Majaliwa, amepongeza semina hiyo akisema ni muhimu kwa maendeleo ya vijana.“Siye kama bodi ya wadhamini, tunapata faraja kuona semina elekezi kama hizi zinafanyika, hizi zinasaidia sana vijana wetu kujitambua na kuwa watu muhimu katika jamii,” alisema Majaliwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni