Haki za Wazazi Kuwatendea Ihsaan
Allaah Aliyetukuka Anatuambia yafuatayo:
“Na Mola wako Ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima. Na tuwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyonilea utotoni”. (17: 23 – 24).
Allaah Aliyetukuka Amekariri katika surah saba tofauti kuhusu haki za wazazi kwa aina tofauti. Hata hivyo, kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa Qur-aan huwezi kupata maelezo yoyote kuhusu majukumu ya mzazi kwa watoto wake. Je, kuna hekima gani kwa Allaah Aliyetukuka kuwahimiza watoto kuwatendea wema wazazi na kutowahimiza wazazi juu ya majukumu yao kwa watoto wao? Ni jambo linalojulikana kuwa hata kwa wanyama, wanakuwa ni wenye kuwalinda na kutekeleza majukumu yao kwa watoto wao. Kwa ajili hiyo kuku anakuwa karibu na vijifaranga vyake ili kuvilinda wakati wa hatari.
Ni maumbile ya mwanadamu anapokuwa ni mzazi kutekeleza majukumu kwa watoto wake – majukumu ya msingi. Hata hivyo, watoto mara nyingi hujitazama wao wenyewe bila kujali kama mzazi anacho au hana. Mwanaadamu kimaumbile anapopata watoto hamu yake kubwa ni watoto wake na sio wazazi ambao ndio sababu ya kuja kwao. Kwa ajili hii Allaah Aliyetukuka Akatoa ufafanuzi mrefu kuhusu majukumu ya watoto kwa wazazi wao. Ukumbusho huu umekaririwa mara kadhaa ili kumpatia hisia mtoto atekeleza majukumu yake kwa mzazi wake.
Aayah ambayo imefafanua kwa kina suala hilo ni Aayah ya Suratul 'Israa' ambayo tumeitaja hapo juu. Amri ya kwanza iliyokuja katika Aayah hizo mbili zilizofuatana ni kumuabudu Allaah pekee bila ya kumshirikisha na yeyote wala chochote. Baada ya agizo hilo ni amri ya kuwatendea wema wazazi wawili. Kwa ile bahati ambayo anapata mtoto ni pindi wazazi wanapokuwa ni wakongwe na wako kwako wakiwa wanakutegemea wewe peke yako. Wakati huo utiifu wa kweli unajitokeza kwa kiasi kikubwa sana. Je, utawatazama kwa njia gani? Hakika huo ni mtihani mkubwa sana kwa mtoto au watoto wenye kulea wazazi wakongwe, ndio Allaah Aliyetukuka Akatoa maagizo Yake kuhusu wema na ihsani wanaofaa kufanyiwa. Katika walio kwako anaweza kuwa ni mzazi mmoja au wawili. Katika hali hiyo yao ya uzee wakiwa wanakutegemea wewe sio kinyume chake ndio utiifu wa kihakika unajulikana na ndio hapo pia hufai kuwaambia hata Ah au Uff au Uh na kadhalika.
Ibara iliyotumika hapa inamaanisha kuwa wewe pia si mtoto hivyo japokuwa mzazi wako bila shaka atakuwa ni mkubwa kuliko wewe. Ikiwa mzazi wako ni miaka themanini wewe huenda ukawa arobaini. Katika hali ya kuwa wapo kwako Allaah Aliyetukuka Anasema: "Usiwaambie Ah!" Wanazuoni wasema kuwa lau kuna neno dogo zaidi kuliko Uff basi Allaah Angelitumia lakini hakuna dogo zaidi. Katika Kiswahili chetu husema kuwapigia kitunu (kuguna). Hii ni alama ya kuonyesha kutoridhika kwako, hali hiyo isiwe ni yenye kutokea kabisa kwani sio sifa nzuri.
Pia usiwatolee ukali wala kuwakemea. Hii ni tabia ya utoto ambaye anakuwa hana hisia na jambo lolote linaweza kumkasirisha na hayo ndio maumbile ya mwanadamu anapozeeka. Wazazi wako walikuwa hawakukaripii ulipokuwa mdogo, nawe pia inatakiwa ufanye hivyo. Mbali na hayo unatakiwa useme nao maneno yaliyo mazuri, kauli za kuwafurahisha na sio kinyume chake. Bado Allaah Anaendelea kutupatia maagizo kuhusu kuwatendea wema wazazi wakati huo. Na baada kuwafanyia yote hayo basi pia kuwa mnyenyekevu kwao kwa kiwango cha juu. Bado hata baada ya kuwafanyia yote hayo utakuwa hujalipa ihsani na wema waliokufanyia. Ulipokuwa mdogo walisumbuka, walikopa, walikosa kula na mengineyo kwa ajili yako. Ihsani usiyoifahamu utailipa namna gani?
Hivyo ndio Allaah Aliyetukuka bado Anatuusia tuwe ni wenye kuwaombea du’aa kwa kusema: "Ee Mola wangu! Warehemu wao kama walivyonilea nikiwa mdogo". Hii ina maana kuwa Ee Allaah! kwa kuwa mimi siwezi kuwalipa kwa waliyonifanyia basi warehemu wazazi wangu. Hii ni Aayah moja miongoni mwa Aayah nyingi inayotufundisha kuwaamili wazazi wanapokuwa wazee wakiwa kwetu
Suala ni kuwa wengi wetu tuna wazazi, je muamala wetu kwao ni vipi? Utakuta kuwa wengi wetu huondosha kero (udhia na usumbufu) nyumbani huwa tunawapeleka wazazi wetu katika nyumba za wazee. Kufanya hivyo sio kwa sababu ya kuwa hakuna nafasi nyumbani wala hakuna cha kuwapa bali sababu kuu ni kuwa mke haridhiki kwa hilo. Huo sio ubinadamu kabisa. Allaah Anauliza: "Je, malipo ya wema yapo mengine ila wema?" Gari mara nyingi huwa tunalitazama likiwa ni jipya, lipo kazini na laleta pesa kwa mwenyewe lakini pindi linapozeeka anakwenda kulitupa mahali likimalizika kidogo kidogo. Hivyo ndivyo tunavyowafanya wazazi wetu wakati huu wetu wa leo.
Hakika ni kuwa haifai kuwepo majumba ya wazee katika jamii ya Kiislamu ikiwa tutakuwa tunafuata Uislamu inavyotakiwa. Lakini ni sikitiko kubwa sana kuona kuwa majumba hayo yanakithiri kila uchao. Huu si Uislamu. Kiislamu familia ni pana zikiwajumlisha wazazi wako, wazazi wa mke, mkeo, watoto wako na wajukuu na kadhalika. Lakini kwa kuwa fikra za kimagharibi zimetuvaa na kututawala tumejaalia kuwa familia ni wewe, mkeo na watoto wako basi. Leo katika nchi za kimagharibi wazee wamekuwa ni kero na kuna njia inayoitwa kuua kwa huruma inayotumika kuwamaliza na hivyo kuwapumzisha na mateso na udhia kwako.
Kiislamu sio hivyo bali kila wazazi wanapokuwa wazee ni nafuu kwetu kwa kiasi kikubwa. Imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema:“Mwana pua yake kusuguliwa na mchanga (amekhasirika), kisha mwana pua yake kusuguliwa na mchanga, kisha mwana pua yake kusuguliwa na mchanga yule ambaye atawakuta wazazi wake wawili wakiwa wazee, mmoja au wote kisha asiingie Peponi?” [Muslim].
Hakika kwetu sisi wazazi kuwa wazee ni neema na ni mlango wa mtu kuingia Peponi. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema: "Pindi mtu anapokuwa na wazazi wake wakiwa kwake basi milango miwili ya Peponi yanafunguliwa kwake". Uamuzi wa kuingia au kutoingia ni wake. Na kinyume chake pia ni sahihi, hivyo ukiwafanyia ubaya milango miwili ya Motoni itafunguliwa kwa ajili yake.
Wazazi tulipokuwa wadogo walikuwa wakitutazama kwa hali na mali mbali na kutufurahikia lakini wanapokuwa wazee huwa tunawakodishia wafanyakazi wa kuwatazama. Wewe uliyetoka katika tumbo lake huona huwezi kushika uchafu wa mzee wako. Je, unadhania kuwa hisia zako na za mfanyakazi itakuwa sawa? Tunadhania kuwa kumuwekea mtumishi inatosha lakini hilo halitoshi kabisa na ipo haja ya sisi kuzingatia hilo na kujirekebisha kwa njia iliyo nzuri. Kwa ajili ya umuhimu wa suala hili kwa kukaririwa mara nyingi na Allaah Aliyetukuka ipo haja kwetu kukumbushana kila mara tunapopata nafasi na fursa.
Utiifu kwa wazazi unakuja baada ya utiifu kwa Allaah Aliyetukuka lakini utiifu kwa wazazi una mipaka. Ipo hali moja ambayo mtoto hafai kumtii mzazi wake nayo tumefahamishwa na Allaah katika Qur-aan. Allaah Anasema:
"Na wazazi wako wakikushurutisha kunishirikisha na yale ambayo huna elimu nayo usiwatii; lakini kaa nao kwa wema hapa duniani" (31: 15).
Hii ni hali ambayo hufai kuwatii kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: "Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba".Hata hivyo, katika hali yoyote ile ni lazima uwatii na hata wakikuamrisha mabaya wewe hufai kuwatii tu lakini unatakiwa usuhubiane nao kwa wema hapa duniani. Sababu ni kuwa haki yao ya uzazi haipomoki (haiondoki) kwa wao kufanya ubaya au kuamrisha mabaya.
Kila mmoja wetu ana wazazi wawili na huenda tukawa tunauliza ni nani katika wao mwenye haki zaidi kuliko mwengine. Jawabu la hilo tunapatiwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Imepokewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu.) ambaye amesema:Alikuja mtu kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema: “Ewe Mjumbe wa Allah! Ni nani mwenye haki zaidi miongoni mwa watu kwa mimi kusuhubiana naye kwa wema?” Akasema: “Mamako”. Akasema: “Kisha nani?” Akasema: “Mamako”. Akasema: “Kisha nani?” Akasema: “Mamako”. Akasema: “Kisha nani?” Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): “Babako”(al-Bukhaariy na Muslim).
Na katika riwaya nyengine: “Ewe Mjumbe wa Allah! Nani ana haki zaidi kwa mimi kusuhubiana naye kwa wema?” Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): “Mamako, kisha mamako, kisha mamako, kisha babako, kisha wale waliokaribu, wale walio karibu nawe kijamaa”.
Hadithi hii inatuonyesha kuwa mama ana sehemu tatu ziada za kufanyia wema na watoto kuliko baba. Na hii ni sababu ya shida na uzito anaopata wa kubeba mimba, kisha kuzaa na baadaye kunyonyesha.
Al-Qurtubiy amesema: “Mama anastahiki wema na ihsani zaidi kuliko baba, na amemtangulia baba katika mashindano hayo”.
Haya yalizungumzwa wakati ulimwengu hauna masuala ya gender (jinsia). Bila shaka, masuala hayo ni katika nadharia za kimagharibi lakini katika Uislamu kila mmoja anapatiwa haki yake anayostahiki na Allaah Aliyetukuka. Hapa mama hakupendelewa kabisa bali alipatiwa haki yake anayostahiki kulingana na wajibu wake aliopewa. Majukumu ya mama ni makubwa zaidi. Yeye ndiye aliyekubeba wewe kwa udhaifu juu ya udhaifu na mimba hiyo ikamletea matatizo na pia akaonja mauti akiwa hai. Na kuna msemo kwetu unaosema: "Kuzaa ni kuonja mauti". Mbali na maendeleo katika utabibu bado wapo wanawake wengi wanaoaga dunia wakati wa kuzaa. Na mama kwa kumpenda mtoto wake lau ataulizwa achukuliwe nani baina yake na mwanae basi atajibu achukuliwe naye, abaki mwanae katika uhai. Hii ni ruhuma (huruma) ya mwisho aliyonayo mama kwa mtoto wake. Baba akiwa na ruhuma nyingi atakuwa na wasiwasi wakati mkewe anajifungua lakini si zaidi ya hapo. Hata hivyo, ni masikitiko makubwa sana kuona leo vijana wanawachukulia akina mama kama kitambaa cha mkono, hatuwajali kabisa.
Tumenyonya maziwa ya mama kwa miaka miwili, hiyo ni kunyonya nguvu zake. Maziwa hayo hayakutoka katika mfereji. Allaah Aliyetukuka Anasema: "Na wanawake waliozaa wawanyonyesha watoto wao miaka miwili kamili kwa anayetaka kukamilisha kunyonyesha" (2: 233).
Baba hata akitaka vipi hawezi kukunyonyesha labda akusaidie kukushikia chupa ya maziwa.
Allaah Aliyetukuka Anasema: "Na Tumemuusia mwanadamu afanye wema kwa wazazi wake. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu na akamzaa kwa taabu. Na kubeba mimba yake na hata kumwachisha ziwa ni miezi thelathini" (46: 15).
Hapa Allaah Anataja haki za wazazi wawili na kisha anabainisha uzito Aliopata mama hivyo kustahiki haki zaidi. Hakika shida na unyonge wa mama katika kubeba mimba yako ni mkubwa na kila miezi ilipokuwa inapita ndio udhaifu zaidi aliokuwa akipata. Si hayo tu bali mtoto si kama kifaranga ambapo anapoanguliwa tu anaanza kula bali mwanadamu ananyonya kwa miaka miwili kutoka kwa mamake.
Ama kuhusu fadhila nyengine za haki kwa wazazi ni Hadithi zifuatazo:
Imepokewa kwa Ibn Mas‘uud (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema:Nilimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): “Ni amali gani inampendeza Allah Aliyetukuka?” Akasema: “Ni Swalah kwa wakati wake”. Nikasema: “Kisha ni ipi?” Akasema: “Kuwatendea wema wazazi wawili”. Nikasema: “Kisha ipi?” Akasema: “Jihadi katika Njia ya Allah”(al-Bukhaariy na Muslim).
Na imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume wa Allah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: “Mtoto hawezi kumlipa babake (kwa yale aliyomfanyia) isipokuwa anapomkuta kuwa ni mtumwa, akamnunua kisha kumwacha huru” (Muslim, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy).
Pia kama ilivyo haki za wazazi na hasa ya mama, kuna kuwaasi wazazi. Kufanya hivyo ni katika madhambi makubwa kama alivyotuelezea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), yaani kumshirikisha Allaah Aliyetukuka na kuwaasi wazazi. Kumuasi mzazi si lazima umtusi au kumweka na njaa kama tulivyoona hata kuwaambia Uff.
Khasara ngapi mtu anapata kwa kukasirikiwa na mzazi wake. Hakika hii ni hasara kubwa ambayo Muislamu atapata ikiwa hataweza au atashindwa kuwajibika ipasavyo kwa kuwapatia wazazi wake. Allaah Aliyetukuka Atuepushe mbali na hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni