Ufafanuzi kuhusiana na Eda ya Talaka
BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa ba’ad.
✅Eda ni kipindi anachokaa mwanamke aliyeachika au aliyefiwa na mumewe, na baada ya kipindi hicho ndoa yake huwa halali. Na imeitwa eda kwa jina hili kutokana na jina la kiarabu ‘iddah’ kwa kukusanya kwake (idadi) ya miezi au ‘quruu’ au hedhi au vipindi vya tohara ya hedhi.
➡Kwahiyo leo nitazungumzia kuhusiana na Eda ya Talaka tu.
✅Ifahamike kwamba Eda ya Mwanamke aliyepewa Talaka inaanza Siku ile ile aliyopewa Talaka.
✅Kwa ujumla inafahamika kwamba Eda ya Mwanamke aliyepewa Talaka ni kukamilika kwa Twahara 3.
➡Yaani ni ‘quruu’ (vipindi vya hedhi/tohara) tatu, endapo atakuwa keshaingiliwa na mumewe na hakuwa ni mwenye mimba, au aliyekoma hedhi, au mdogo asiyepata hedhi bado. Na haya yamefafanuliwa na Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) Aliposema⤵
↪Surat Al-Baqarah Aya ya 228
✅Kwahiyo Ndugu zangu katika Imaani,Eda ya talaka imefungamana na hedhi. Mume akimtaliki mke wake baada ya kufanya naye jimaa au baada ya kuwa faragha naye basi ni wajibu kwake kukaa eda kwa kupata hedhi mara tatu ikiwa kama anapata hedhi na hana ujauzito.
➡Allaah (Subhaana wa Ta´ala) amesema kwamba⤵
وَالْمُطَلَّقَاتُ يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ ثَلَاثَةَ قُرُوءٍ
“Na wanawake waliotalakiwa wabakie kungojea [wasiolewe] quruu´ [twahara au hedhi] tatu.”
↪Surat Al-Baqarah Aya ya 228.
⏩Ama huyo mwanamke ikiwa kama ana ujauzito atakaa eda mpaka pale atapojifungua.
➡Allaah (Subhaana wa Ta´ala) amesema kwamba⤵
وَأُولَاتُ الْأَحْمَالِ أَجَلُهُنَّ أَن يَضَعْنَ حَمْلَهُنَّ
“Na wenye mimba muda wao [wa eda] watakapozaa mimba zao.”
↪Surat At-Talaak Aya ya 4
⏩Ama ikiwa huyo mwanamke ikiwa bado ni kijana sana au ni mzee au alifanya operesheni ukeni na mengineyo na si mwenye kupati hedhi, eda yake ni miezi mitatu.
➡Allaah (Subaana wa Ta´ala) amesema kwamba⤵
وَاللَّائِي يَئِسْنَ مِنَ الْمَحِيضِ مِن نِّسَائِكُمْ إِنِ ارْتَبْتُمْ فَعِدَّتُهُنَّ ثَلَاثَةُ أَشْهُرٍ وَاللَّائِي لَمْ يَحِضْنَ
“Na wale wanawake wanaokata tamaa [wanaokoma] hedhi miongoni mwa wanawake wenu, mkiwa na shaka [katika muda wao wa eda], basi eda yao ni miezi mitatu, na [hiyo pia ni eda ya] wale wanawake wasiopata hedhi.”
↪Surat At-Talaak Aya ya 4
⏩Na ikiwa kawaida ni mwenye kupata hedhi lakini kwa sababu fulani hedhi yake ikakatika kwa sababu ya ugonjwa, kunyonyesha au sababu nyengineyo, ni mwenye kubaki katika eda mpaka pale hedhi yake itaporudi hata kama itakawia.
➡Na ikiwa sababu hiyo itaondoka katika maradhi au kunyonyesha na hedhi isirudi, basi atasubiri/kukaa eda mwaka mmoja tangu pale sababu ilipoondoka. Haya ndio maoni sahihi yenye kuafikiana na kanuni za Kishari´ah.
➡Mwanamke ambaye sababu imeondoka na hedhi yake isiwe ni yenye kurudi ni kama mwanamke ambaye hedhi yake imesita bila ya sababu yenye kujulikana.
➡Kwahiyo Mwanamke kama huyu atasubiri mwaka mmoja kikamilifu; miezi tisa kwa ajili ya mimba kwa sababu ya usalama na miezi tatu kwa ajili ya eda.
✅Naam,Kwahiyo Ndugu zangu katika Imaani, ikiwa talaka itatokea baada ya kufunga ndoa lakini kabla ya jimaa na kabla ya kuwa faragha, basi hana eda ya talaka huyo mwanamke.
➡Yaani hapo haijalishi kitu sawa akiwa ni mwanamke mwenye kupata hedhi au mwengineo.
➡Allaah (Subhaana wa Ta´ala) amesema kwamba⤵
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا
“Enyi mlioamini! Mnapofunga nikaah [kuwaoa] Waumini wa kike, kisha mkawataliki kabla ya kuwagusa [jimai], basi hamna juu yao eda yoyote mtakayohesabu.”
↪Suraat Al-Ahzab Aya ya 49.
✅Kwahiyo sasa Ikiwa Mwanamke amepewa Talaka leo na baada ya saa chache au baada ya siku chache au baada ya wiki chache mwanamke huyo akaingia katika Siku zake basi hapo Mwanamke atakuwa tayari amemaliza Quruu ya kwanza(Tohara ya kwanza).
➡Kwahiyo si kweli kwamba Mwanamke akipewa Talaka alafu baada ya saa chache mwanamke akaingia katika siku zake ukasema kwamba Talaka haijapita,hapo talaka imepita na mwanamke ataanza kukaa Eda.
✅Naam ni haramu kwa mume kumtaliki mke wake wakati yuko na hedhi.(Yaani mwanamke akiwa katika siku zake).
➡Allaah (Subhaana wa Ta´ala) amesema kwamba⤵
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ وَأَحْصُوا الْعِدَّةَ
“Ee Nabii! Mtakapowataliki wanawake, basi watalikini katika wakati wa eda [twahara na si katika hedhi au katika twahara mliyowaingilia].”
↪Suraat At-Talaaq Aya ya 01.
➡Kwahiyo Ndugu zangu pale wanawake wanapoenda katika eda inayojulikana. Hali kama hiyo inakuwa wakati mume anapomtaliki wakati yuko na mimba au katika twahara ambayo hakumwingilia. Hakwenda katika eda ikiwa ataachika wakati yuko na hedhi kwa sababu eda haianzi kuhesabika katika hedhi aliyoachika.
➡Hali kadhalika si mwenye kwenda katika eda akiachika katika twahara aliyomwingilia kwa sababu anakuwa si mwenye kujua kama amepata ujauzito katika jimaa hiyo ili aweze kukaa eda ya mjamzito au hakupata ujauzito ili aweze kukaa eda ya mwenye hedhi. Pale ilipokuwa hakuna yakini ni eda aina ipi itayotumika, ndipo ikawa ni haramu kumtaliki mpaka mambo yabainike.
➡Kwahiyo Kutokana na Aayah niliyoiweka hapo juu ni jambo la haramu kumtaliki mwanamke mwenye hedhi. Vilevile imethibiti katika al-Bukhaariy, Muslim na wengine kutoka kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye alimtaliki mke wake wakati yuko na hedhi. Wakati ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alipomweleza hilo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakasirika na kusema⤵
“Muamrishe amrudishe na abaki naye mpaka atwaharike. Kisha apate hedhi na kutwaharika tena. Halafu akitaka abaki naye au amtaliki kabla ya kumwingilia. Hiyo ndio eda ambayo Allaah ameamrisha kuwataliki wanawake kwayo.”
↪Imepokelewa na Imaam Al-Bukhaariy (5251) na Muslim (1471).
✅Mwanaume akimtaliki mke wake ilihali yuko na hedhi ni mwenye kupata dhambi. Ni juu yake kutubu kwa Allaah (Ta´ala) na kumrejesha mke wake ili amtaliki talaka ya Kishari´ah na yenye kuafikiana na maamrisho ya Allaah na Mtume Muhammad(Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).
✅Baada ya hapo amwache mpaka atwaharike na hedhi ambapo alimtaliki ndani yake halafu apate hedhi tena na kutwaharika. Baada ya hapo akitaka atabaki naye au atamtaliki kabla ya kumwingilia.
Rejea Kitaab Ad-Dimaa' at-Twabiy´iyyah lin-Nisaa'
Tutaishia hapa kwa Muda huu
سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ وَبِحَمْدِكَ، أشهد أن لاَ إِلَهَ إِلاَّ أَنْتَ، أَسْتَغْفِرُكَ وَأَتُوبُ إِلَيْك
“Subhaanaka Allaahumma wa Bihamdika, Ash-hadu Allaa ilaaha illa Anta, Astaghfiruka wa Atuwbu ilayka.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni