Naam! Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa makala zetu hizi za kuwasoma na kujifunza viumbe mbalimbali wa Allah Aliyetukuka.
Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Muumba wa kila kitu ndiye peke anayestahiki kuabudiwa katika dunia hii. Yeye ameumba mbingu na ardhi, Jua na Mwezi na wanyama wa bara na baharini, naye ndiye anayewaruzuku. Katika viumbe wote ambao Mwenyezi Mungu amewaumba, zipo dalili na ishara ya kuwa Allah Aliyetukuka peke yake ndie anayestahiki kuabudiwa.
Katika dalili na alama za kumjua Mungu kupitia viumbe vyake, leo nataka ujifunze jambo kumuhusu samaki wa ajabu anayefahamika kwa Jina la pomboo.
Pomboo ni wanyama wa majini wanaofanana sana na nyangumi. Inatajwa kuwa, kuna pomboo takribani aina 40. Pomboo wana ukubwa tofauti, kuanzia urefu wa mita 1.2 – 9.5 na uzito wa kilogramu 40 mpaka tani 10. Viumbe hawa wanapatikana duniani kote, hasa kwenye bahari za kina kifupi.
Pomboo huchangamana sana wao kwa wao, na huweza hata kufikia kundi moja dogo. Makundi hayo yanaweza kuongezeka, hata kufikia pomboo 1,000. Pomboo hutumia milio mbalimbali katika mawasiliano yao, huku wakisaidiana sana hasa pale miongoni mwao wanapokuwemo wagonjwa. Pomboo huweza hata kuwasaidia wenzao kupumua kwa kuwasogeza kwenye usawa wa maji. Huko New Zealand, pomboo waliwahi kuonekana wakilinda jike na ndama wao.
Pomboo wameonekana pia wakiwalinda waogeleaji kwa kuwazunguka katika duara ili wasishambuliwe. Pia wameonekana wakiwakasirisha papa ili kuwafukuza.
Pomboo, mara nyingi, huwa Mara katika makundi. Mara kadhaa, pomboo, hasa dume, wame kuwa wakigombana na hivyo kusababisha kuwa na makovu mengi mwilini mwao. Aghalabu sababu ya kupigana ni kugombania nafasi ya kuwa na jike. Wale wanaoshindwa huenda zao mbali.
Pomboo ni samaki msafi. Hapendi usafi asilani. Ukirusha kitu majini, pomboo yeye hukirudisha nje kwa kukipiga na mkia wake, Midomo ya pomboo imechongoka na vijimeno vyake ni vidogo vidogo sana lakini hatari. Umaarufu wa samaki huyu pengine umechagizwa pia na mahusiano yake na binadamu.
Wataalamu wa elimu ya viumbe wa baharini wanasema, ni vigumu kufa maji kama pomboo yupo eneo hilo kwani samaki huyu anaweza kuja kukuokoa. Akiwepo samaki huyu jirani pia huwezi kudhuriwa na samaki wakali kama papa. Pomboo atakulinda kwa hali na mali.
Inapotokea umedumbukia majini na akakuona, haraka pomboo hukujia sana, kisha atakukumbatia na kwa spidi kubwa atakuwa anakupeleka nchi kavu. Atakapofika jirani atakurusha huko na msaada wake huishia hapo. Ukitua kwenye jiwe, mwamba, michongoma au kwenye mti hiyo ni shauri yako yeye kazi yake kashamaliza
UZAZI
Pomboo hujamiiana kwa vipindi vifupi lakini hufanya mara nyingi nyingi katika muda mfupi. Pomboo hubeba mimba kwa muda wa miezi 11-12, kutegemeana na aina husika. Pomboo huanza kujamiiana katika umri mdogo. Pia, umri hasa wa kukomaa kijinsia hutofautiana kutoka aina moja mpaka nyingine.
Pomboo huzaa mtoto mmoja au wawili, na huyu ni samaki mwenye kasi kubwa ya kusafiri majini. Pomboo hatagi bali anazaa. Pia, pomboo hunyonyesha. Samaki huyu anafanana na mwanadamu katika mambo mengi, ikiwemo kuzaa na kunyonyesha na vilevile kuishi kifamilia.
CHAKULA
Pamoja na kwamba samaki ndiyo chakula chake kikuu, pomboo pia hupendelea zaidi kula pweza na fisi maji. Pomboo hula kwa namna mbalimbali na pia ana mbinu mbalimbali za kushambulia samaki. Namna mojawapo ni ile ya kuwatenga samaki kadhaa kwa kuwazunguka, na kisha kuanza kuwashambulia taratibu. Namna nyingine ni pale pomboo wanapowafukuzia samaki kwenye maji yenye kina kifupi na kisha kuwakamata kwa urahisi.
MAMBO USIYOYAJUA KUHUSU POMBOO
- Pomboo ni kiumbe mpole na mwenye akili sana. Inatajwa pia na baadhi ya wataalamu kuwa, baada ya binadamu, viumbe wanaofuata kwa akili ni pomboo pamoja na kunguru.
- Licha ya upole wake, pomboo ana kasi kubwa sana majini.
- Kwa kawaida, pomboo hulala upande mmoja tu wa ubongo, huku mwingine ukiendelea kufanya kazi ya kuratibu masuala mengine kama vile kupumua na kujihami na hatari za mazingira yao. Hata hivyo, usingizi wa hatua za mwanzo hutokea katika sehemu zote za ubongo.
- Pomboo ni samaki anayelindwa na umoja wa mataifa hivyo chunga sana matamanio yako ya kutaka kumla.
- Pomboo huwasaidia wavuvi katika shughuli zao za uvuaji wa samaki. Kwa mfano, ili wavuvi wapate samaki, pomboo hutumia mkia wake kuwapiga samaki wakubwa. Pomboo hufanya yote haya kwa mapenzi aliyonayo kwa mwanadamu.
- Inaelezwa na wataalamu wa elimu wa viumbe wa baharini kuwa pomboo ana takriban meno yapatayo 100 mdomoni.
- Pomboo wana namna yao ya kuwasiliana kwa lugha, tena kwa sauti.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni