Homa ya matumbo ni moja kati ya magonjwa ya kuambukiza yanayoathiri mfumo wa chakula. Kwa lugha ya kisayansi, ugonjwa huu hujulikana kama ‘enteric fever’ au ‘typhoid fever’ na husababishwa na bakteria hatari wanaoitwa ‘salmonella typhi.’ Bakteria hawa, wanaosambazwa na nzi, hupatikana hasa kwenye maji machafu. Mtu anaweza kuambukizwa mara baada ya kuyanywa maji yenye bakteria hawa.
Namna ugonjwa unavyosambaa
Kama ilivyo kwa kipindupindu, homa ya matumbo huambukizwa kwa kula choo kikubwa cha mgonjwa wa homa hii. Hii kitaalamu tunaitwa ‘fecal oral route’. Ili kuelewa ni vipi mtu anaweza kula choo kikubwa bila ya yeye kujua, angalia uhusiano uliopo kati ya kinyesi (chanzo), nzi (msambazaji) na chakula (maambukizi).
Mtu anapojisaidia hovyo, huvutia nzi ambao hutua kwenye kinyesi chenye bakteria wa homa ya matumbo. Nzi huyo hukibeba kinyesi chenye bakteria kupitia miguu na sehemu nyengine za mwili wake. Nzi huyo akitua tu kwenye chakula au maji, basi kiasi kidogo cha choo na bakteria kitabakia. Yoyote atakayekula au kunywa chakula au kinywaji hicho, huambukizwa mara.
Dalili zake
Dalili za homa ya matumbo huanza kujitokeza taratibu ndani ya wiki mbili. Wiki ya kwanza, wagonjwa huanza kupata homa kali na ikizidi kupanda kadri siku zinavyokwenda, maumivu ya kichwa, tumbo na misuli, kukosa choo (watu wazima), kuhara (kwa watoto), kichefuchefu, kikohozi kikavu, kuvimba tumbo pamoja na kutoka upele mgongoni na kifuani.
Katika wiki ya pili, ikiwa mgonjwa hatopatiwa matibabu, dalili nyengine za hatari zaidi huweza kufuata. Dalili hizi ni pamoja na kuchanganyikiwa na kupoteza fahamu na mwishowe kifo.
Athari za homa ya matumbo
Ingawa homa hii inaonekana si hatari, lakini inaweza kuleta athari kubwa ikiwa haitatibiwa mapema. Kama isipotibiwa, homa ya matumbo inaweza kusababisha kutoboka kwa utumbo na kusababisha kuvuja damu ndani ya mwili. Vilevile, bakteria hawa wanaweza kusambaa na kuambukiza maeneo mengine ya mwili kama vile moyo, figo, mapafu, wengu, ubongo na pia homa hii huweza kusababisha ukichaa.
Mambo ya kuzingatia
Ugonjwa wa homa ya matumbo unaweza kuepukwa kirahisi ikiwa tutazingatia kanuni mbalimbali za afya. Homa ya matumbo, kama tulivyotaja, inatokana na kula choo kikubwa cha mtu alieathirika. Hivyo, ili kujikinga na ugonjwa huu lazima tukate mnyororo wa mahusiano kati ya kinyesi (chanzo), nzi (msambazaji) na chakula, maji au matunda (maambukizi) kwa kufuata mambo mbalimbali.
Mambo hayo ni pamoja na kunawa mikono kwa maji safi na sabuni baada ya kutoka msalani, kuepuka kula chakula kilicho wazi, kuepuka kula chakula kiholela katika magenge ambayo hayazingatii usafi, kuhakikisha maji ya kunywa yamechemshwa, yamechujwa na kufunikwa vizuri, kuosha matunda na mbogamboga kwa maji yanayotiririka na kunawa mikono kwa maji yanayotiririka kabla ya chakula. Pia, hatua nyingine za kujikinga ni kuchoma moto au kuhifadhi takataka hasa mbichi katika chombo maalum chenye mfuniko, kuangamiza nzi wote kwa kutumia dawa za kupuliza za kuulia wadudu. Pia, ni muhimu kwa choo cha shimo kuwa na mfuniko, kuepuka kujisaidia ovyo hasa karibu na vyanzo vya maji. Watoto wadogo nao wapelekwe vyooni au watumie vyombo maalum kwa ajili ya haja kubwa na kisha kukitupa chooni au kukifukia ardhini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni