Damu ya nifasi na hukumu yake
Nifasi ni damu inayotoka ukeni kwa sababu ya kuzaa. Inakuja kwa kuzaa, baada ya kuzaa au siku mbili mpaka tatu kabla ya kuzaa sambamba na machungu. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:
“Damu inayotoka wakati machungu yanaanza ni nifasi na haikukomeka kwa siku mbili wala tatu. Katika hali hii machungu ya uzazi ni yale yanayofuatiwa na uzazi. Vinginevyo sio nifasi.”
Wanachuoni wametofautiana juu ya uchache na wingi wake. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:
“Nifasi haina muda maalum kwa uchache na wingi wake. Lau tutakadiria kuwa mwanamke atapata damu zaidi ya siku arubaini, sitini au sabini kisha ikakatika, hiyo ni nifasi. Lakini lau itakuja kwa kuendelea itazingatiwa kuwa ni damu isiyokuwa na maana na katika hali hiyo nifasi itakuwa ni yenye kukomeka kwa siku arubaini. Kikomo hichi ndicho kwa jumla kilichokuja katika mapokezi.”Majmuu´-ul-Fataawaa (19/37).
Damu yake ikizidi zaidi ya siku arubaini na amezowea kuwa inakata au akaona alama kuwa inakata karibuni, atasubiri mpaka ikatike. Vinginevyo ataoga baada ya siku arubaini kwa sababu ndivyo ilivyo kwa jumla. Nifasi ikigongana na hedhi atamili upande wa hedhi mpaka ikatike. Baada ya hapo namna hii ndivyo inatakiwa kuwa ada yake anayoitendea kazi katika mustaqbal. Na ikiwa damu itaendelea kutoka, itahesabika kuwa ni damu ya ugonjwa ambayo atatakiwa kutendea kazi hukumu zake baada ya hapo.
Damu ikikatika kabla ya siku arubaini atazingatiwa kuwa ni mtwaharifu. Hivyo atatakiwa kuoga, kuswali, kufunga na kufanya jimaa na mume wake. Lakini hili linahitajia kusitoke damu chini chini kwa muda wa siku moja. Vinginevyo ile damu yenye kukatika haina hukumu yoyote, hivyo ndivyo alivosema Ibn Qudaamah katika “al-Mughniy”.
Nifasi inaanza kuthibiti pale mwanamke anapozaa kitu kinachoashiria mwanaadamu. Lau mimba yake itaharibika na kusiwe na uashiriaji kuwa ni mwanaadamu basi damu yake sio nifasi. Katika hali hiyo ni mshipa uliyopasuka na hivyo anakuwa na hukumu moja kama mwanamke ambaye yuko na damu ya ugonjwa. Muda mdogo kabisa ambapo kipomoko [mtoto tumboni] anaweza kupata umbo la mwanaadamu ni siku thamanini kuanzia siku ujauzito ulipoanza. Muda wake mrefu kabisa ni siku tisini. al-Majd bin Taymiyyah amesema:
“Akipata damu na maumivu kabla ya muda huo, aipuuze. Na ikiwa atapata damu baada ya muda huo, aache kuswali na kufunga. Ikiwa baada ya kuzaa itamdhihirikia kuwa haikuwa kama alivyodhania, atafanya yale aliyoacha kuyafanya. Na itapomdhihirikia alivofanya ndivyo, atachukulia hivo na hatolipa chochote.”Sharh-ul-Iqnaa´.
Na Allaah anajua zaidi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni