Ndugu yangu msomaji wa safu yetu hii, kwa uwezo wa Allah Aliyetukuka, leo tujifunze kumhusu konokono, kiumbe ambaye maumbile yake yanatupatia mazingatio makubwa kutokana na alivyoumbwa kipekee. Kwanza, ijulikane kwamba konokono ni kiumbe hai asiye na uti wa mgongo.
Kama ilivyo kwa kobe, konokono pia ana gamba mgongoni ambalo huuficha mwili wake anapohisi mazingira ya hatari. Konokono ana minara minne, tunaweza kuita antenna, ambapo mbili za juu huwa ndefu kuliko za chini. Antena za juu hubeba macho na za chini ni kwa ajili ya kuhisi.
Kwa maana hiyo, macho hutangulizwa mbele zaidi kuliko mwili, na hivyo basi nafasi ambayo hubakia antena za chini ndiyo hufanya kazi ya kuepusha mwili kuingia katika tatizo. Licha ya kuwa na macho, uoni wa konokono ni dhaifu.
Konokono ni viumbe wanaomiliki jinsia mbili, yaani huyo huyo ni jike na huyo huyo ni dume. Utajiuliza sasa inakuwaje kwenye kupandana!? Iko hivi si kwamba kwa umiliki wa jinsia hizo basi ndiyo hujitosheleza mwenyewe kimahaba! Hapana. Konokono nao hukutana wawili kwa kuviziana. Atakayewahiwa, ndiye atakayepandwa; na mara nyingi yule mwili wake utakaokuwa na joto ndiye atakayepandwa.
Kwa kawaida, konokono huwa na uzito wa gramu zipatazo tano na kuendelea, na urefu wao hufikia hadi sentimita 18 na kuendelea. Allah Aliyetukuka amejaalia umri wa wastani wa kuishi konokono ni miaka 10.
Kimwendo, konokono hutembea taratibu sana kwa sababu mwili wake ni laini na hivyo huhofia asiumie. Anapotembea, konokono hutanguliza uteute chini, ili pindi anapouvuta mwili wake asiumie. Uteute huo hutengeneza alama ya njia aliyopita.
Kimsingi, konokono wapo wa aina tatu: wa nchi kavu, maji baridi na maji ya chumvi. Viumbe kadhaa huathiri maisha ya konokono kwa kuwatumia kama chakula, wakiwemo ndege, panya, kobe, binadamu na mijusi.
Mwendo wa konokono ni taratibu mno kiasi kwamba mpaka sasa hakuna ushahidi wa kutosha kuonesha kwamba, amewahi kuwepo konokono aliyevuka salama barabara. Yaani, mwendo wao ni wa kusuasua mno. Utafiti unaonesha kwamba, konokono anahitaji wiki moja na siku kadhaa ili kumaliza kutembea umbali wa kilometa moja.
Uzazi na chakula:
Katika uzazi, konokono hutaga hadi mayai 70 au zaidi. Kumbuka yule aliyewahiwa ndiye atakayefanya shughuli hiyo ya kutaga. Chakula kikuu cha konokono ni majani, hususani mboga mboga na matunda, ikiwa ni pamoja na mimea iliyooza.
Mambo kumi usiyoyajua kuhusu konokono
- Ni ngumu sana kujua jike ni yupi na dume ni yupi kwa sababu konokono ana jinsia zote.
- Anapototoa mayai yake, konokono hula magamba ya mayai hayo. Pia, mayai ambayo hayajatotolewa hiliwa na watoto wake.
- Pengine konokono ndiye kiumbe mwenye meno mengi kuliko wengine. Watafiti hudai ana meno zaidi ya elfu moja.
- Konokono ni kiumbe asiyekula nyama kabisa. Hivyo, akikupanda mwilini kwa bahati mbaya mtoe kistaarabu kwani hawezi kukuuma.
- Konokono hupendelea mazingira machafu, yenye giza na unyevunyevu.
- Konokono wanaona vema usiku kuliko mchana.
- Konokono hawasikii kabisa, hivyo hujiongoza kwa kunusa.
- Konokono huweza kutembea hali ya kuwa gamba lake ameliweka juu au chini.
- Katika hali zote anaweza kutembea pasina tatizo lolote.
- Konokono huweza kuufupisha mwili wake ili kujificha katika gamba lake anapohisi hatari. Baada ya hatari kutoweka, hutoa tena mwili wake.
- Baadhi ya watafiti wanasema, ukimmwagia chumvi konokono huwa anayeyuka kabisa na kupotea. Kwa maana hiyo, kama wamevamia eneo lako, mwaga maji ya chumvi tu. Hata hivyo, chumvi huua konokono wa nchi kavu na maji baridi tu. Wale wa baharini hawadhuriki na chumvi na pia gamba lao ni gumu sana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni