Alipowasili mji wa Basra, baada ya kuteuliwa na ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa gavana wa mji huo, Abu Muusa Al-Ash’ariy (Radhwiya Allaahu ‘anhu), aliwakusanya watu wa mji huo na kuwahutubia akiwaambia:
"Khalifa wa Waislam ‘Umar bin Al-Khattwaab amenileta kwenu ili nikufundisheni Kitabu cha Mola wenu na mafundisho ya Nabiy wenu na ili nikusafishieni barabara".
Watu walipigwa na mshangano kwa sababu wao wanajuwa kuwa kuwafundisha watu Kitabu cha Allaah na mafundisho ya Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni katika jukumu la gavana, lakini lililowashangaza ni pale aliposema kuwa amekuja pia ili awasafishie barabara.
Huyu ndiye ‘Abdullaah bin Qays (Radhwiya Allaahu ‘anhu) maarufu kwa jina la Abu Muusa Al-Ash’ariy.
Huyu ndiye Abu Muusa Al-Ash’ariy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye Hasan Al-Baswriy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alisema juu yake:
"Hajapata kuja katika mji huu wa Basra mtu mwema kwa watu wake kuliko huyu."
Mara baada ya kusikia kuwa Rasuli mpya aliyekuwa akisubiriwa kwa hamu kubwa sana amekwishakuja, Abu Muusa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliifunga safari ndefu kutoka katika nchi yake ya Yemen na kuelekea Makkah kwa ajili ya kuutafuta ukweli na ili ajiunge na Rasuli huyo katika dini hii mpya inayohubiri juu ya kumuabudu mwabudiwa wa haki Mmoja Pekee Asiye na mshirika.
Alipoonana na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuzitamka shahada mbili, Abu Muusa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alirudi nchini kwake Yemen, na haukupita muda mrefu akarudi tena Makkah, lakini safari hii akiwa na watu wa kabila lake wapatao hamsini waliosilimu mkononi mwake wakiwemo ndugu zake wawili, Abu Ruhmu na Abu Burdah (Radhiya Llaahu ‘anhum).
Kuwasili kwake Makkah kulisadifu kuwasili kwa Ja’afar bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyerudi kutoka nchi ya Uhabeshi, na ilipotolewa amri ya kuhama kwenda Madiynah, Abu Muusa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mionogni mwa wa mwanzo kuhajir.
Tokea siku hizo, Abu Muusa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa msitari wa mbele katika kuipigania dini hii kwa hali na mali.
Abu Muusa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni mchanganyiko wa ajabu; alikuwa mpiganaji vita hodari sana anapolazimika, jambo lililomfanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aseme juu yake:
"Bwana wa mashujaa ni Abu Muusa".
Abu Muusa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa pia mtu anayependa amani zaidi kuliko vita. Alikuwa akijulikana kuwa ni mtu mwema sana na mwenye taqwa, na alikuwa mwingi wa hekima na hodari wa kutoa uamuzi wenye kusibu.
Alipigana vita vingi chini ya uongozi wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na baada ya kufa kwake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipigana chini ya Makhalifa wake watukufu (Radhiya Llaahu ‘anhum).
Hebu tumsikilize Abu Muusa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akituhadithia juu ya mojawapo ya siku alizoishi na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"Tulikuwa safarini katika vita pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘('Alayhis-Salaam) wa aalihi wa sallam), na ulipoingia usiku tukasimamisha msafara kwa ajili ya mapumziko, na ghafla Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akatoweka.
Nikatoka kumtafuta kwa kuhofia asije akadhuriwa, maana tulikuwa vitani. Nikamuona mmoja katika Maswahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye pia akitafuta kile mimi nilichokuwa nikitafuta. Tulipokuwa tumesimama, ghafla akatokea mbele yetu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), tukamuambia:
"Ee Rasuli wa Allaah, sisi tumo vitani, na hatuaminishi kukuacha peke yako wasije wakakudhuru maadui. Ukiwa na haja yoyote ile, mwambie mmoja wetu afuatane nawe.
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akatuambia:
"Nilisikia sauti kama sauti ya nyuki, akanijia aliyenijia kutoka kwa Mola wangu Mtukufu, akanitaka nichaguwe moja kati ya mawili; ama waingie nusu ya umma wangu Peponi au nipewe uwezo wa kuwaombea shifaa. Nikachagua kuwaombea Shifaa kwani nilijuwa kuwa kwa kuwaombea shifaa wataingia wengi zaidi Peponi.
Akanitaka tena nichaguwe baina ya kuingia theluthi ya umma wangu Peponi na baina ya kuwaombea shifaa. Nikachagua kuwaombea shifaa, kwa sababu nilijuwa kuwa wataingia wengi zaidi".
Anasema Abu Muusa (Radhwiya Allaahu ‘anhu):
"Tukamuambia:
"Ee Rasuli wa Allaah; muombe Allaah Atujaalie tuwe miongoni mwa wanaostahiki shifaa yako".
Anasema Abu Muusa (Radhwiya Allaahu ‘anhu):
"Akatuombea du’aa."
Abu Muusa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa miongoni mwa Maswahaba waliokataa kujiingiza katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya majeshi ya ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na ya Mu’aawiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na katika mazungumzo ya amani baina yao, watu wa upande wa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) walipendekeza achaguliwe Abu Muusa kuuwakilisha upande wao.
Abu Muusa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikufa katika mwaka wa arubaini baada ya Hijra akiwa na umri wa miaka sitini na mitatu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni