Kila sifa njema anastahiki Allah, Mmiliki wa ulimwengu huu. swala na amani zimfikie Mtume Muhammad pamoja na wale waliofuata mwenendo wake kwa wema. Kwa hakika, Allah ametuhabarisha kuhusu siku chache zenye kuhesabika ndani ya Ramadhan, tulizozishuhudia siku chache zilizopita.
Hakika, kila kitu katika ulimwengu huu kina mwanzo wake na mwisho wake, isipokuwa Mwenyezi Mungu, kama anavyotuhabarisha Mwenyewe katika Qur’an: “Yeye ndiye wa Mwanzo na ndiye wa Mwisho, naye ndiye wa Dhahiri na wa Siri, naye ndiye Mjuzi wa kila kitu.” [Qur’an, 57:3].
Hapa kuna funzo kubwa kwetu, kuwa, kadri siku zinavyoenda ndiyo tunapiga hatua kukaribia makaburi yetu. Allah amethibiti miaka yetu ya kuishi, kuwa ina mwanzo na mwisho wake. Hivyo, yatupasa tujichunguze ndani ya nafsi zetu, kipi tulichokitanguliza ndani ya miaka tuliyoishi.
Ni salio kiasi gani umeacha katika benki ya amali zako njema zitakazotusaidia kutokana na misukosuko ya siku ya Kiyama? Kama Ramadhan, inavyotuacha ipo siku na sisi tutauacha ulimwengu huu. Hivyo, kila mtu ajiandae. Tukiwa tumeuaga mwezi huu, tujaribu kukumbushana mambo muhimu ya kuyazingatia na kushikamana nayo nje ya Ramadhan.
Kama tulivyoeleza katika makala zilizopita, Allah anatuambia katika mwanzo wa Aya zinazoeleza kuhusu funga na akaiweka funga baina ya imani na taq’wa [Qur’an, 2:183]. Ukichunguza mwisho kabisa wa Aya inayofunga mazungumzo, kuhusiana na funga, Allah anasema: “Wala msiliane mali zenu kwa batili na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi, na hali mnajua.” [Qur’an, 2:188].
Katika Aya hii imetumika neno “ta’akul” lenye maana sawa na kufunga, kwani funga ni kujizuia kula na kunywa. Hivyo, tufahamu aina hii nyingine ya funga ambayo inatuwajibikia katika maisha yetu yote nako ni kujizuia kula mali za watu kwa dhuluma.
Jambo hili hutokeaje? Ni kwamba, mtu akijitahidi kufanya vema ibada, athari ya ibada hizo humpelekea kufikia lengo la uchamungu. Uchamungu ndiyo humfanya awe na nidhamu katika miamala na watu. Tufahamu kuwa, ndani ya mwezi huu ambao Allah ametuwafikisha kufanya ibada na kheri nyingi ambazo huenda hatukuwa tukizifanya nje ya mwezi huu.
Hekima za Allah kufanya uteuzi wa kuzifadhilisha baadhi ya siku ni kutaka kuenea kwa athari hiyo katika siku nyingine. Allah ametuafikisha katika kufunga, kutoa sadaka, na kusali hivyo mambo haya yasiishie hapa tu bali tuendelee nayo.
Hivyo basi, haina maana tufunge mwezi wa Ramadhan peke yake bali tuna siku sita za Shawwal, siku ya Jumatatu na Alhamisi na mfano wa hayo. Kadhalika kuna mambo mengi ya kheri ya kufanya katika ibada nyingine ikiwemo kuisoma Qur’an na kutoa sadaka.
Alama ya kufaulu Ramadhan
Katika fadhila za siku sita za Shawwal, imekuja Hadithi aliyeisimulia Muslim kuwa, Mtume wa Allah anasema: “Mwenye kufunga mwezi wa Ramadhan kisha akaufuatiliza na siku sita za Shawwal, ni sawa na kufunga mwaka mzima. “Miongoni mwa alama za kukujulisha kuwa umefaulu na kufuzu ndani ya Ramadhan ni kuona mabadiliko katika nafsi yako, namna ya uchaji, ibada, tabia na mfano wa hayo.
Ikiwa kuna mabadiliko makubwa elewa kuwa, Ramadhan imekufaidisha. Ama ukiona hakuna mabadiliko yoyote kabla na baada ya Ramadhan elewa kuwa umepata hasara. Ramadhan ni sawa na msimu wa soko kubwa ambalo ndani yake kuna kila aina ya kitu unachokihitaji ila baada ya muda soko hilo halitokuwepo tena, atapata faida mwenye kutaka faida na atapata hasara yule aliyetaka hasara.
Tuhitimishe ibada kwa uzuri na ubora
Allah amemfundisha Mtume wake (rehema za Allah na amani zimshukie) kuhitimisha kila amali iliyokuwa njema kwa kuleta toba na kuomba msamaha.
Tukiangalia maisha yote ya Mtume, Aya za mwazo wa sura ya 110 zinaonesha na kujulisha jukumu la Mtume wa Allah katika kueneza na kuwafundisha watu dini. Baada ya kumaliza jambo la muhimu alilotumwa kwalo, Allah anamuambia Mtume wake: “Zitakase sifa za Mola wako Mlezi, na umwombe msamaha; hakika Yeye ndiye anaye pokea toba.” [Qur’an, 110:3].
Kadhalika, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliamrishwa katika vita vya mwisho alivyopigana (Tabuuk) kuomba msamaha na kisha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka akateremsha Aya kuonesha amemsamehe Mtume wake na Waumini. Allah anasema: “Mwenyezi Mungu amekwisha pokea toba ya Nabii na Wahajiri na Ansari waliomfuata katika saa ya dhiki, pale baada ya kukaribia nyoyo za baadhi yao kugeuka. Basi akapokea toba yao, kwani hakika Yeye kwao wao ni Mpole na ni Mwenye kuwarehemu.” [Qur’an, 9:117]. Hivyo, vita ikahitimishwa kwa toba.
Kadhalika zimekuja Hadithi kuhusu jambo hili katika mafundisho ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ambapo tumeagizwa kuwa, tukimaliza ibada ya swala tulete istighfaar mara tatu, kama ilivyokuja katika Hadithi iliyoptajwa katika sahihi mbili.
Hivyohivyo, tukafundishwa tukiinuka katika vikao vyetu tuombe msamaha kama ilivyokuja katika Hadithi aliyoisimulia Tirmidh, ambapo Mtume wa Allah anasema: “Yeyote atakayekaa kwenye kikao yakakithiri ndani yake mazungumzo, akasema kabla ya kuamka katika kikao chake, ‘Sub- haanaka Allaahumma wabihamdika, Ash-hadu an Laa ilaaha illa Anta Astaghfiruka wa – atuubu Ilayka,’ atasamehewa katika kikao chake hicho.”
katika ushahidi mwingine wa umuhimu wa kuleta maghfira, Allah anawasifu wale wanaoamka usiku na kufanya ibada kwa kusema: “Walikuwa wakilala kidogo tu usiku.” [Quran, 51:17], na baada ya kumaliza visimamo vyao ni wenye kuomba msamaha. Allah anasema: “Na kabla ya Alfajiri wakiomba Maghfira.” [Qur’an, 51:18].
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni