Imeandikwa Na: Imaam Muhammad Bin Swaalih Al-'Uthaymiyn
Imetarjumiwa Na: Muhammad Faraj Saalim As-Sa'y
Na Kupitiwa Na: Abu 'Abdillaah
بسم الله الرحمن الرحيم
Utangulizi
Itikadi Yetu
Sifa Ya Kusema
Sifa Ya Kuwepo Kwake Juu 'Al-'Uluw
Allaah Anayo 'Arsh
Sifa Ya Kushuka
Sifa Ya Iraada (Atakavyo Allaah)
Sifa Ya Kupenda
Wajihi Wa Allaah
Mikono
Macho
Tanbihi
Malaika
Vitabu
Mitume
Dini Ya Allaah
Makhalifa Waongofu
Siku Ya Mwisho
Shafa’ah
Hodhi Na Swiraat
Pepo Na Moto
Masuali Ya Kaburini
Adhabu Ya Kaburini
Qadar
Kutaka Kwa Allaah
Baadhi Ya Faida
Matunda Ya Kuamini Malaika
Matunda Ya Kuviamini Vitabu
Matunda Ya Kuamini Mitume
Matunda Ya Kuiamini Siku Ya Qiyaamah
Matunda Ya Kuamini Qadar
Utangulizi
Shukrani zote ni zake Mola wa uliwengu wote, na mwisho mwema ni wa wamchao Allaah, na hapana uadui isipokuwa kwa madhalimu.
Nashuhudia kuwa hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allah Peke yake Asiye na mshirika mwenye Ufalme na haki iliyo wazi. Na nashuhudia kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni mjumbe wake na Mtume wake na mwisho wa wajumbe wake na ni kiongozi wa wacha Mungu. Mola wetu mswalie na msalimie Mtume wako huyu pamoja na Masahaba wake na kila atakayemfuata kwa wema na uongofu mpaka Siku ya Qiyaamah.
Amma baad,
Hakika Allaah amemtuma Mtume wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) awe dalili iliyo wazi juu ya waja wake, na awabainishie yale aliyoteremshiwa katika Kitabu, na awe mfano mwema wa kuigwa na walimwengu wote, na ili watu wapate kuwa na muongozo mwema katika dini yao na dunia yao.
Ametumwa kutufundisha itikadi sahihi pamoja na hekima kwa ajili ya kutengenea hali ya umati wake, na pia kuwaweka juu ya njia safi na sahihi, ili watu wawe juu ya kitanga cheupe, mchana wake sawa na usiku wake, na asiende kinyume na njia hiyo isipokuwa mpotofu.
Wakaifuata njia hiyo Maswahaba wake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na wale waliokuja baada yao na waliowafuatilia kwa wema. Wakaisimamisha shari’ah ya Allaah na kuyakamata vizuri mafundisho hayo kwa magego yao kwa kuifuata itikadi hii iliyo sahihi, na ibada na mwenendo na tabia. Na sisi Alhamdulillah tunaendelea kuufuata mwenendo wao huo kwa kufuata dalili zilizomo ndani ya Qur-aan na zilizomo ndani ya mafundisho yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na tunamuomba Allaah Atuthibitishe juu ya njia hiyo sisi na ndugu zetu wote wa Kiislamu kwa kauli iliyo thabit katika maisha ya duniani na ya Aakhirah na atumiminie rehma Zake kwani yeye ni Mwenye kutoa kwa wingi.
Kutokana na umuhimu wa maudhui haya, na kutokana na tofauti iliyokuja baadaye, baada ya kuingizwa matamanio ya watu ndani ya itikadi hii, nilipenda kuiandika iwe kama ndiyo itikadi yetu. Itikadi ya Ahlus Sunnah wal Jama’ah, nayo ni imani ya kuwepo kwa Allaah na Malaika Wake na vitabu Vyake na Mitume Yake na Siku ya Qiyaamah na Qadar (qudra) kheri yake na shari yake.
Namuomba Allaah Aijaalie kazi hii iwe halisi kwa ajili yake, Aridhike nayo na iwe funzo kwa waja Wake.
Itikadi Yetu
Itikadi yetu ni kumuamini Allaah na Malaika Wake na Mitume Yake na Vitabu Vyake na Siku ya Mwisho na kila kinachotokea au kutusibu (Qadar) kheri na shari, vyote vinatoka kwa Allaah.
Kwa hivyo sisi tunaamini kuwa Yeye Subhaanahu wa Ta’ala ndiye Aliyeumba na ndiye Mfalme Mwenye kukiendesha kila kitu, na ni Yeye peke yake anayestahiki kuabudiwa, na kila kinachoabudiwa kisichokuwa Yeye ni batil.
Tunaamini pia kuwa Allaah Anayo majina mazuri mazuri na sifa nzuri nzuri na njema, sifa za ukamilifu, na tunaamini kuwa Yeye ni mmoja Asiye na mshirika katika kuumba Kwake na katika kuabudiwa Kwake na katika majina Yake mazuri na katika sifa Zake njema.
Allaah Anasema:
رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا فَاعْبُدْهُ وَاصْطَبِرْ لِعِبَادَتِهِ هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا
"Mola wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake. Basi muabudu Yeye tu, na udumu katika ibada yake. Je, mnamjua mwenye jina kama lake?"
Maryam – 65
Na tunaamini kuwa Yeye ndiye:
اللّهُ لاَ إِلَـهَ إِلاَّ هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ لاَ تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلاَ نَوْمٌ لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِنْدَهُ إِلاَّ بِإِذْنِهِ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلاَ يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلاَّ بِمَا شَاء وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ وَلاَ يَؤُودُهُ حِفْظُهُمَا وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ
"Allaah - hapana mungu ila Yeye, Aliye hai, Msimamiaji wa mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni Vyake pekee vyote viliomo mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake bila ya idhini Yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui chochote katika vilio katika ujuzi Wake, ila kwa atakalo mwenyewe. Kiti Chake Cha Enzi kimetanda mbinguni na duniani; na wala haemewi na kuvilinda hivyo. Na Yeye ndiye Aliye juu, na ndiye Mkuu."
Al-Baqarah – 255
Na tunaamini kuwa:
هُوَ اللَّهُ الْخَالِقُ الْبَارِئُ الْمُصَوِّرُ لَهُ الْأَسْمَاء الْحُسْنَى يُسَبِّحُ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالأرْضِ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ
"Yeye ndiye Allaah, Muumbaji, Mtengenezaji, Mtia sura, Mwenye majina mazuri kabisa. Kila kilioko katika mbingu na ardhi kinamtakasa, naye ni Mwenye kushinda, Mwenye hekima."
Al-Hashr - 24
Na tunaamini kuwa:
لِلَّهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ يَخْلُقُ مَا يَشَاء يَهَبُ لِمَنْ يَشَاء إِنَاثًا وَيَهَبُ لِمَن يَشَاء الذُّكُورَ. أَوْ يُزَوِّجُهُمْ ذُكْرَانًا وَإِنَاثًا وَيَجْعَلُ مَن يَشَاء عَقِيمًا إِنَّهُ عَلِيمٌ قَدِيرٌ
"Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Allaah; Anaumba Apendavyo, Anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na Anamtunukia amtakaye watoto wa kiume.
Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza."
Ash-Shuuraa – 49-50
Na tunaamini kuwa:
فَاطِرُ السَّمَاوَاتِ وَالأرْضِ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَمِنَ الْأَنْعَامِ أَزْوَاجًا يَذْرَؤُكُمْ فِيهِ لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ وَهُوَ السَّمِيعُ البَصِيرُ. لَهُ مَقَالِيدُ السَّمَاوَاتِ وَالأرْضِ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاء وَيَقْدِرُ إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ
"Yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi, Amekujaalieni mke na mume katika nafsi zenu, na katika wanyama nao (Akawaumba) dume na jike, Anakuzidishieni namna hii. Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.
Yeye ndiye Mwenye funguo za mbingu na ardhi. Humkunjulia riziki Amtakaye, na humpimia Amtakaye. Hakika Yeye ni Mjuzi wa kila kitu."
Ash-Shuuraa – 11-12
Na tunaamini kuwa:
وَمَا مِن دَآبَّةٍ فِي الأَرْضِ إِلاَّ عَلَى اللّهِ رِزْقُهَا وَيَعْلَمُ مُسْتَقَرَّهَا وَمُسْتَوْدَعَهَا كُلٌّ فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ
"Na hakuna mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Allaah. Naye Anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika Kitabu chenye kubainisha."
Huud - 6
Na tunaamini kuwa:
وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لاَ يَعْلَمُهَا إِلاَّ هُوَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَمَا تَسْقُطُ مِن وَرَقَةٍ إِلاَّ يَعْلَمُهَا وَلاَ حَبَّةٍ فِي ظُلُمَاتِ الأَرْضِ وَلاَ رَطْبٍ وَلاَ يَابِسٍ إِلاَّ فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ
"Na ziko kwake funguo za ghayb; hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Yeye Anajua kilioko nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila Analijua. Wala punje katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika Kitabu kinachobainisha."
Al-An’aam – 59
Na tunaamini kuwa:
إِنَّ اللَّهَ عِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَيُنَزِّلُ الْغَيْثَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الأَرْحَامِ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ
"Hakika kuijua Saa (ya Qiyaamah) kuko kwa Allaah. Na Yeye ndiye Anayeiteremsha mvua. Na Anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi. Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika Allaah ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari".
Luqmaan – 34
Sifa Ya Kusema
Tunaamini kuwa Allaah Anasema wakati wowote Anapotaka na kwa njia yoyote Anayotaka.
Allaah Anasema:
وَكَلَّمَ اللّهُ مُوسَى تَكْلِيمًا
"Na Allaah Akamsemeza Muwsaa."
An-Nisaa – 164
Na Akasema:
وَلَمَّا جَاء مُوسَى لِمِيقَاتِنَا وَكَلَّمَهُ رَبُّهُ
"Na alipokuja Muwsaa kwenye miadi yetu, na Mola wake Akamsemeza."
Al-A’araf – 143
Na Akasema:
وَنَادَيْنَاهُ مِن جَانِبِ الطُّورِ الأيْمَنِ وَقَرَّبْنَاهُ نَجِيًّا
"Na Tulimwita upande wa kulia wa mlima na tukamsogeza kunong'ona naye."
Maryam – 52
Na tunaamini kuwa:
قُل لَّوْ كَانَ الْبَحْرُ مِدَادًا لِّكَلِمَاتِ رَبِّي لَنَفِدَ الْبَحْرُ قَبْلَ أَن تَنفَدَ كَلِمَاتُ رَبِّي وَلَوْ جِئْنَا بِمِثْلِهِ مَدَدًا
"Lau kama bahari ndio wino kwa maneno ya Mola wangu, basi bahari ingelimalizika kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu, hata tungeliileta mfano wa hiyo kuongezea."
Al-Kahf – 109
Na tunaamini kuwa:
وَلَوْ أَنَّمَا فِي الأرْضِ مِن شَجَرَةٍ أَقْلَامٌ وَالْبَحْرُ يَمُدُّهُ مِن بَعْدِهِ سَبْعَةُ أَبْحُرٍ مَّا نَفِدَتْ كَلِمَاتُ اللَّهِ إِنَّ اللَّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ
"Na lau kuwa miti yote iliyomo duniani ikawa ni kalamu, na bahari (ikawa wino), na ikaongezewa juu yake bahari nyengine saba, maneno ya Allaah yasingelikwisha. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima."
Luqmaan – 27
Na tunaamini kuwa maneno Yake ni ya ukamilifu uliokamilika na ya ukweli uliokamilika na yenye uadilifu uliokamilika.
Allaah Anasema:
وَتَمَّتْ كَلِمَتُ رَبِّكَ صِدْقًا وَعَدْلاً لاَّ مُبَدِّلِ لِكَلِمَاتِهِ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ
"Yametimia maneno ya Mola wako kwa kweli na uadilifu. Hapana awezaye kuyabadilisha maneno Yake. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua."
Al-An’aam - 115
Na Akasema:
وَمَنْ أَصْدَقُ مِنَ اللّهِ حَدِيثًا
"Na ni nani msema kweli kuliko Allaah?"
An-Nisaa – 87
Na tunaamini kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah, Aliyeyatamka kwa uhakika kabisa kwa kumfundisha Jibriyl aliyeiteremsha ndani ya kifua cha Mtume wa Allaah Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Allaah Anasema:
قُلْ نَزَّلَهُ رُوحُ الْقُدُسِ مِن رَّبِّكَ بِالْحَقِّ
"Sema: Ameiteremsha hii (Qur-aan) Roho takatifu kutokana na Mola wako kwa haki."
An-Nahl – 102
Na Akasema:
وَإِنَّهُ لَتَنزِيلُ رَبِّ الْعَالَمِينَ. نَزَلَ بِهِ الرُّوحُ الأمِينُ. عَلَى قَلْبِكَ لِتَكُونَ مِنَ الْمُنذِرِينَ. بِلِسَانٍ عَرَبِيٍّ مُّبِينٍ.
"Na bila ya shaka hii ni Uteremsho wa Mola wa walimwengu wote.
Ameuteremsha Roho muaminifu, Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji. Kwa ulimi wa Kiarabu ulio wazi."
Ash-Shu’araa – 192 – 195
Sifa Ya Kuwepo Kwake Juu ‘Al-Uluw’
Tunaamini kuwa Allaah yupo juu kabisa mbali na viumbe vyake kwa dhati Yake na kwa sifa Zake, na hii inatokana na kauli Yake Subhaanahu wa Ta’ala Aliposema:
وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ
"Na Yeye ndiye Aliye juu, na ndiye Mkuu."
Al-Baqarah – 255
Na Akasema:
تَعْرُجُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ إِلَيْهِ فِي يَوْمٍ كَانَ مِقْدَارُهُ خَمْسِينَ أَلْفَ سَنَةٍ
"Malaika na roho hupanda Kwake katika siku ambayo muda wake ni miaka elfu hamsini."
Al-Ma’aarij – 4
Na Akasema:
أَأَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاء أَن يَخْسِفَ بِكُمُ الأَرْضَ فَإِذَا هِيَ تَمُورُ
"Je! Mnadhani muko salama kwa (Allaah) Ambaye Yuko mbinguni ya kuwa Yeye hatokudidimizeni ardhini tahamaki hiyo inataharaki?"
Al-Mulk - 16
Na Akasema:
وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ
"Naye Ndiye Mwenye nguvu (Yuko) juu ya waja Wake."
Al-An’aam -18
Na imekuja katika Sunnah (Mafundisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):
"Mrehemu aliye ardhini Atakurehemu aliye mbinguni."
Abu Ya’ala na Atw-Twabaraaniy na Al-Haakim
Na kuwepo mbinguni hakuna maana kuwa yupo katika mojawapo ya sayari zilizopo juu kama baadhi ya watu wanavyoweza kudhania, bali dunia yetu ukiilinganisha na mbingu ni mfano wa doa dogo sana, bali hata haionekani. Kwani huko juu kuna nyota na sayari zilizoenea hata kama mtu atasafiri kwa kasi ya kupita kiasi (speed of light) basi atachukuwa mamilioni ya miaka na hatoweza kufika mwisho wake, na hata kama ataufikia mwisho wake, basi atakuta kuwa bado ipo anga isiyo na mwisho. Kwa hivyo ni Allaah Peke Yake ndiye Mwenye kuelewa mfano ya kuwa juu Kwake Subhaanahu wa Ta’ala.
Allaah Anayo 'Arsh
Allaah Anasema:
إِنَّ رَبَّكُمُ اللّهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَى عَلَى الْعَرْشِ
"Hakika Mola wenu ni Allaah, Ambaye Ameziumba mbingu na ardhi kwa siku sita, kisha Akawa juu ya ‘Arshi Yake."
Yuunus – 3
Na kuwa juu ya ‘Arshi Yake ni kuwakunakonasibiana na utukufu wake Subhaanahu wa Ta’ala, hapana anayejua mfano wake isipokuwa Yeye.
Na tunaamini kuwa Allaah Akiwa juu ya ‘Arshi Yake, Yupo pamoja na viumbe Vyake kwa elimu Yake. Anasikia kauli zao na kuona vitendo vyao, huku Akiyaendesha mambo yao. Anamruzuku fakiri na Anampa ufalme Amtakaye na Anamuondolea ufalme amtakaye, Anamnyanyua amtakaye na Anamuangusha amtakaye, na tunaamini kwamba kheri yote imo mikononi Mwake Subhaanahu wa Ta’ala, na kwamba Yeye ni muweza wa kila jambo.
Na Yeyote mwenye uwezo huo, basi bila shaka yupo pamoja na viumbe vyake kikweli huku akiwa juu ya Arshi yake kikweli, na ni Yeye Peke yake ndiye mwenye kuujuwa uhakika wake.
Allaah Anasema:
لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ وَهُوَ السَّمِيعُ البَصِيرُ
"Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona."
Ash-Shuuraa – 11
Na Anasema:
وَالْمَلَكُ عَلَى أَرْجَائِهَا وَيَحْمِلُ عَرْشَ رَبِّكَ فَوْقَهُمْ يَوْمَئِذٍ ثَمَانِيَةٌ
"Na Malaika watakuwa kandoni mwake (hizo mbingu) na Malaika wa namna nane watachukua 'Arshi ya Mola wako juu yao."
Al-Haaqqah – 17
Sisi hatusema kama wanavyosema wengine kuwa eti Allaah yupo ardhini pamoja na viumbe Vyake, kwani tunaona kuwa kusema hivyo ni kukufuru au ni upotofu, kwa sababu kumpa Allaah wasfu usiolingana naye ni kupunguza katika sifa Zake.
Sifa Ya Kushuka
Tunaamini pia yale aliyotujulisha Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa Allaah Anashuka katika mbingu za dunia kila usiku katika thuluthi ya mwisho na kusema:
"Nani mwenye kuniomba nimkubalie, nani mwenye kuniomba nimpe, nani mwenye kuniomba maghfira nimghufirie."
Alipoulizwa Imaam Ash-Shaafi’iy:
'Vipi Allaah Anashuka?'
Akajibu:
'Kwani vipi Alipanda?'
Na tunaamini kuwa Allaah Atakuja Siku ya Qiyaamah kuwahukumu viumbe vyake.
Allaah Anasema:
كَلَّا إِذَا دُكَّتِ الأَرْضُ دَكًّا دَكًّا. وَجَاء رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا
"Sivyo hivyo! Itakapovunjwa ardhi vipande vipande. Na Akaja Mola wako na Malaika safu safu. Na ikaletwa Jahannamu siku hiyo, siku hiyo mtu atakumbuka! Lakini kukumbuka huko kutamfaa nini?".
Al-Fajr – 21 – 22
Sifa Ya Iraadah (Atakavyo Allaah)
Tunaamini kuwa Allaah Anatenda Atakavyo.
Allaah Anasema:
فَعَّالٌ لِّمَا يُرِيدُ
"Atendaye Ayatakayo."
Al-Buruuj – 16
Na tunaamini kuwa zipo Irada namna mbili.
Ya kwanza Anatujulisha katika kauli Yake:
وَلَوْ شَاء اللّهُ مَا اقْتَتَلُواْ وَلَـكِنَّ اللّهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ
"Na lau kuwa Allaah Alipenda wasingelipigana (Lau shaa'a Alaahu). Lakini Allaah Hutenda Atakavyo."
Al-Baqarah – 253
Na hapa maana yake ni ‘kutaka’, kama ilivyo katika kauli Yake:
وَلاَ يَنفَعُكُمْ نُصْحِي إِنْ أَرَدتُّ أَنْ أَنصَحَ لَكُمْ إِن كَانَ اللّهُ يُرِيدُ أَن يُغْوِيَكُمْ هُوَ رَبُّكُمْ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ
"Wala nasaha yangu haikufaini kitu nikitaka kukunasihini, ikiwa Allaah Anataka (In Kaana Allaahu Yuriydu) kukuachieni mpotee."
Huud – 34
Na uwezo mwingine ni wa kishari’ah, na Hamtakii isipokuwa Anayempenda, kama ilivyo katika kauli Yake Subhaanahu wa Ta’ala:
وَاللّهُ يُرِيدُ أَن يَتُوبَ عَلَيْكُمْ وَيُرِيدُ الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الشَّهَوَاتِ أَن تَمِيلُواْ مَيْلاً عَظِيمًا
"Na Allaah Anataka (Wa Allaahu Yuriydu) kukurejezeni kwenye utiifu wake, na wanaotaka kufuata matamanio wanataka mkengeuke makengeuko makubwa."
(Na maana yake hapa ni kuwa 'Hivi Ndivyo Anavyotaka Allaah' lakini kakupeni uhuru wa kuchagua wenyewe mnakotaka kwenda.)
An-Nisaa – 27
Na tunaamini kuwa Atakacho Allaah katika mambo ya kilimwengu na ya kishari’ah yote ni katika hekima Yake, na hafanyi kitu bila ya kuwa na hekima kubwa ndani yake, na sisi huenda tukaijua hekima hiyo au tusiijuwe kutokana na upungufu wa akili zetu.
Allaah Anasema:
أَلَيْسَ اللَّهُ بِأَحْكَمِ الْحَاكِمِينَ
"Kwani Allaah si muadilifu kuliko mahakimu wote?"
Atw-Twiyn - 8
Na Akasema:
وَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللّهِ حُكْمًا لِّقَوْمٍ يُوقِنُونَ
"Na nani aliye mwema zaidi katika kuhukumu kuliko Allaah kwa watu wenye yakini?"
Al-Maaidah - 50
Sifa Ya Kupenda
Na tunaamini kuwa Allaah Subhaanahu wa Ta’ala Anawapenda wacha Mungu wake wanaompenda.
Allaah Anasema:
قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللّهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ
"Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Allaah basi nifuateni mimi, Allaah Atakupendeni na Atakufutieni madhambi yenu."
Al-‘Imraan – 31
Na Akasema:
فَسَوْفَ يَأْتِي اللّهُ بِقَوْمٍ يُحِبُّهُمْ وَيُحِبُّونَهُ
"Basi Allaah atakuja leta watu anao wapenda nao wanampenda."
Al-Maaidah – 54
Na Akasema:
وَاللّهُ يُحِبُّ الصَّابِرِينَ
"Hakika Allaah Anawapenda wanaosubiri."
Al-‘Imraan – 146
Na tunaamini kuwa Allaah Huridhika zinapofuatwa shari’ah Zake na huchukizwa zisipofuatwa.
Allaah Anasema:
إِن تَكْفُرُوا فَإِنَّ اللَّهَ غَنِيٌّ عَنكُمْ وَلا يَرْضَى لِعِبَادِهِ الْكُفْر
"Mkikufuru basi Allaah si mwenye haja nanyi, lakini hafurahii kufuru kwa waja Wake."
Az-Zumar – 7
Na Akasema:
وَلَـكِن كَرِهَ اللّهُ انبِعَاثَهُمْ فَثَبَّطَهُمْ وَقِيلَ اقْعُدُواْ مَعَ الْقَاعِدِينَ
"Lakini Allaah Kachukia kutoka kwao, na kwa hivyo Akawazuia na ikasemwa: Kaeni pamoja na wanao kaa!"
Na tunaamini kuwa Allaah Huridhika na wale wanaoamini na kufanya mema.
Allaah Anasema:
رَّضِيَ اللَّهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ ذَلِكَ لِمَنْ خَشِيَ رَبَّهُ
"Allaah Yu radhi nao, na wao waradhi naye. Hayo ni kwa anayemwogopa Mola wake."
Al-Bayyinah-6
Na tunaamini kuwa Allaah Anamkasirikia kila mwenye kustahiki kukasirikiwa katika makafiri na wasiokuwa makafiri.
Allaah Anasema:
الظَّانِّينَ بِاللَّهِ ظَنَّ السَّوْءِ عَلَيْهِمْ دَائِرَةُ السَّوْءِ وَغَضِبَ اللَّهُ عَلَيْهِمْ
"Wanaomdhania Allaah dhana mbaya. Utawafikia mgeuko mbaya, na Allaah Awakasirikie."
Al-Fat-h – 6
Na Akasema:
وَلَـكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللّهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ
"Lakini aliyekifungulia kifua chake kukataa - basi hao ghadhabu ya Allaah ipo juu yao, na wao watapata adhabu kubwa."
An-Nahl – 106
Wajihi Wa Allaah
Na tunaamini kuwa Allaah Anao wajihi wenye utukufu na ukarimu.
Allaah Anasema:
وَيَبْقَى وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلألِ وَالاكْرَامِ
"Unabaki Wajihi wa Mola wako wenye utukufu na ukarimu."
Ar-Rahmaan – 27
Mikono
Tunaamini kuwa Allaah Anayo mikono miwili mitukufu.
Allaah Anasema:
بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ يُنفِقُ كَيْفَ يَشَاء
"Bali mikono yake (miwili - yadaahu) iwazi. Hutoa Apendavyo."
Al-Maaidah – 64
Na Akasema:
وَمَا قَدَرُوا اللَّهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالأرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّماوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَى عَمَّا يُشْرِكُونَ
"Na wala hawakumhishimu Allaah kama Anavyostahiki kadiri Yake. Na Siku ya Qiyaamah ardhi yote itakuwa mkononi Mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono Wake wa kuume. Subhaanahu wa Ta’ala Ametakasika na Ametukuka na hayo wanayomshirikisha nayo."
Az-Zumar – 67
(Siku ya Ridhwaan Waislamu walipofungamana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) chini ya mti kwa kumpa mkono wote kwa pamoja, mmoja baada ya mwengine, na Allaah Akateremsha kauli Yake:
إِنَّ الَّذِينَ يُبَايِعُونَكَ إِنَّمَا يُبَايِعُونَ اللَّهَ يَدُ اللَّهِ فَوْقَ أَيْدِيهِمْ
"Bila Shaka wale wanaofungamana nawe, kwa hakika wanafungamana na Allaah. Mkono wa Allaah uko juu ya mikono yao."
Al-Fat-h – 10
Ieleweke kuwa Allaah Anaposema Anayo mikono au macho, haina maana kuwa mikono Yake ni sawa na mikono yetu, au macho Yake ni sawa na macho yetu - AstaghfiruLlaah. Meza inayo miguu na viti vina miguu, lakini miguu ya viti na ya meza ni tofauti na miguu ya mwanaadamu aloitengeneza meza ile, kwani sifa ya mtengenezaji lazima iwe tofauti na sifa ya kilichotengenezwa, ama sivyo mtengenezaji na kilichotengenezwa watakuwa kitu kimoja. Na Allaah Ndiye mwenye kupigiwa mifano bora, sifa Zake Subhaanahu wa Ta’ala haziwezi kufananishwa na sifa zetu. Lakini wakati huo huo lazima tukikubali kila Alichojinasibisha nacho Subhaanahu wa Ta’ala.)
Macho
Na tunaamini kuwa Allaah Anayo macho mawili kikweli, na hii inatokana na kauli Yake Subhaanahu wa Ta’ala Aliposema kumwambia Nuuh (‘Alayhis-Salaam):
وَاصْنَعِ الْفُلْكَ بِأَعْيُنِنَا وَوَحْيِنَا
"Na unda jahazi mbele ya macho yetu na kwa mujibu wa ufunuo wetu."
Huud – 37
Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Pazia yake ni nuru, na lau kama Ataiondoa basi nuru ya Wajihi Wake ingeunguza kila kilichokifikia."
Na alipokuwa akihadithia juu ya Ad-Dajjaal alisema:
"Dajjaal ana chongo na Mola wenu Hana chongo."
Na tunaamini kuwa macho yetu hayamfikii kumuona Allaah.
Allaah Anasema:
لاَّ تُدْرِكُهُ الأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الأَبْصَارَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ
"Macho hayamfikilii, bali Yeye anayafikilia macho. Naye ni Mjuzi, Mwenye khabari."
Al-An’aam – 103
Waislamu Watamuona Allaah Qiyaamah
Na tunaamini kuwa Waislamu watamuona Mola wao Siku ya Qiyaamah.
Allaah Anasema:
وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ. إِلَى رَبِّهَا نَاظِرَةٌ
"Zipo nyuso siku hiyo zitang'ara. Zinamwangallia Mola wao."
Al-Qiyaamah – 22-23
Na tunaamini kuwa Allaah Subhaanahu wa Ta’ala hana mfano wake katika ukamilifu wa sifa Zake.
Allaah Anasema:
لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ وَهُوَ السَّمِيعُ البَصِيرُ
"Hapana kitu kama mfano Wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona."
Ash-Shuuraa – 11
Na tunaamini kuwa Allaah Hashikwi na usingizi wala halali.
Allaah Anasema:
لاَ تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلاَ نَوْمٌ
"Hashikwi na usingizi wala kulala."
Al-Baqarah – 255
Na tunaamini kuwa Allaah Hamdhulumu mtu, na hii inatokana na ukamilifu wa uadilifu Wake Subhaanahu wa Ta’ala, na kwamba hapana Asichokijua katika matendo ya waja Wake, na kwamba Hashindiwi na chochote, kwani Anapotaka chochote kiwe hukiambia tu; 'Kuwa' na kikawa.
Allaah Anasema:
إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَنْ يَقُولَ لَهُ كُنْ فَيَكُونُ
"Hakika amri Yake Anapotaka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa."
Yaasiyn – 82
Na tunaamini kuwa Allaah Haguswi na machofu wala tabu ya aina yoyote ile.
Allaah Anasema:
وَلَقَدْ خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَمَا مَسَّنَا مِن لُّغُوبٍ
"Na bila ya shaka Sisi tumeziumba mbingu na ardhi na vilio baina yao mnamo siku sita; na wala hayakutugusa machofu."
Qaaf – 38
Na tunakiamini kila Alichojithibitishia nafsi Yake, Akasema kuwa Anacho, basi sisi tunaamini kuwa Anacho kwa uhakika, na tunaamini pia kila alichotujulisha Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) juu ya Mola wake, katika Majina Yake mazuri mazuri na Sifa Zake njema.
Lakini tunakataa mambo mawili, nayo ni:
1. Kufananisha (kushabihisha). Nako ni kutamka kwa ulimi au kwa moyo kuwa wasfu wa Allaah unafanana na wasfu wa viumbe Vyake.
2. Na pia tunakataa kukisia. Nako ni kujisemeza moyoni au kutamka kwa ulimi kuzikisia sifa za Allaah kuwa labda ni hivi au vile.
Na tunakanusha kila Allaah Alichojikanushia nafsi Yake, au kile alichokikanusha Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na tunakinyamazia kila Alichokinyamazia, na tunaamini kuwa hii ndiyo njia sahihi, kwani kila Alichojikanushia nafsi Yake ni habari kutoka Kwake, na Yeye Subhaanahu wa Ta’ala ndiye mwenye kuijua nafsi Yake na ndiye Msema kweli kupita wote, Mwenye mazungumzo bora kupita wote, waja Wake hawana uwezo wa kujua chochote juu Yake bila Yeye kuwajulisha.
Tanbihi:
Kila tulichokitaja katika sifa za Allaah, iwe kwa urefu au kwa ujumla, katika kuthibitisha au katika kukanusha, yote tumeyanukuu kutoka katika kitabu cha Allaah (Qur-aan) au mafundisho ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) (Sunnah) iliyo sahihi nayo pia ni itikadi waliyokuwa nayo Maimamu wetu wema waliotangulia.
Tunaona kuwa inawajibika kuzifasiri nassw (dalili) zilizomo ndani ya Qur-aan kwa uhakika wake kama Anavyozistahiki Allaah, na tunajitenga mbali na njia ya wageuzaji wa maana wale waliozigeuza maana na kuzifasiri kwa njia Asiyoitaka Allaah Subhaanahu wa Ta’ala, na tunajitenga mbali na njia ya wabadilishaji waliobadilisha, mbali na maana iliyokusudiwa, na pia tunajitenga mbali na wazidishaji waliozidisha na kuzifanya sifa zake kuwa ni za kumfananisha.
Tuna hakika kuwa yale yaliyomo ndani ya Kitabu cha Allaah na ndani ya mafundisho ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni haki isiyopingana, na hii inatokana na kauli Yake Subhaanahu wa Ta’ala Aliposema:
أَفَلاَ يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ وَلَوْ كَانَ مِنْ عِندِ غَيْرِ اللّهِ لَوَجَدُواْ فِيهِ اخْتِلاَفًا كَثِيرًا
"Hebu hawaizingatii hii Qur-aan? Na lau kuwa imetoka kwa asiye kuwa Allaah bila ya shaka wangeli kuta ndani yake khitilafu nyingi."
An-Nisaa – 82
Na kwa vile kauli zinazopingana huwa zinasutana, na hili ni jambo lisiliowezekana katika habari Anazotupa Allaah Subhaanahu wa Ta’ala na anazotupa Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Na yeyote anayedai kuwa ndani ya Kitabu cha Allaah au ndani ya mafundisho ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) yamo maneno yanayopingana, akasema hayo kwa kukusudia au kwa vile moyo wake umekwenda upande, basi huyo anatakaiwa atubu kwa Mola wake na atoke ndani ya upotofu wake.
Na yeyote anayedhani kuwa mna upungufu wowote ndani ya Kitabu cha Allaah au ndani ya mafundisho ya Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au baina yao, basi huyo ima ana upungufu wa elimu au uchache wa fahamu au ana upungufu katika kuzingatia kwake, kwa hivyo aitafute elimu na ajitahidi katika kuzingatia mpaka ukweli utakapombainikia. Na kama haukumbainikia, basi amtafute mwenye elimu kupita yeye na aachane na upotofu wake, na aseme kama wanavyosema wale waliobobea katika elimu:
آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا
"Tumeamini, zote zimetoka kwa Mola wetu."
Aali-‘ImraAn – 7
Na ajue ya kuwa Qur-aan na Sunnah haviwezi kugongana wala kupingana wala hapana hitilafu baina yake.
Malaika
Na tunaamini juu Malaika wa Allaah kama ulivyokuja wasfu wao ndani ya Qur-aan kwamba wao ni:
بَلْ عِبَادٌ مُّكْرَمُونَ. لا يَسْبِقُونَهُ بِالْقَوْلِ وَهُم بِأَمْرِهِ يَعْمَلُونَ
"Bali hao ni watumwa walio tukuzwa.Hawamtangulii kwa neno, nao wanafanya amri Zake."
Allaah Amewaumba ili wamuabudu na kumtii.
Allaah Anasema:
لا يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِهِ ولا يَسْتَحْسِرُونَ. يُسَبِّحُونَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ لا يَفْتُرُونَ
"Hawafanyi kiburi wakaacha kumuabudu, wala hawachoki.
Wanamtakasa usiku na mchana, wala hawanyong'onyei."
Al-Anbiyaa – 19 – 20
Allaah Akatujaalia tusiweze kuwaona, na Aliwafanya wengine kati ya waja Wake kuweza kuwaona, kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimuona Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) akiwa katika umbile lake la kweli ana mbawa mia sita, akiwa ameizinga anga yote juu yake.
Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) aliwahi pia kuonekana na Bibi Maryam akiwa katika umbile la binaadamu aliyekamilika, akazungumza naye, na aliwahi pia kumjia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akiwa pamoja na Maswahaba wake (Radhiya Allaahu anhum) akiwa katika umbile la mwanamume asiyejulikana wala hapakuwa na ishara yoyote usoni mwake kama ni mtu aliyetoka safari ndefu, akaliegemeza goti lake juu ya goti la Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kuuweka mkono wake juu ya paja la Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), kisha akazungumza naye huku Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akimjibu, na baada ya kuondoka ndipo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akawaambia Maswahaba wake (Radhiya Allaahu anhum) kuwa yule alikuwa Jibriyl (‘Alayhis-Salaam).
Na tunaamini kuwa Malaika wana kazi zao maalum walizopewa na Mola wao. Jibriyl (‘Alayhis-Salaam)ni mletaji wahyi kwa Mitume. Anawateremshia kutoka kwa Allaah na kuwafikishia anaotumwa kuwafikishia katika Mitume yake Subhaanahu wa Ta’ala. Na yupo Mikaaiyl aliyepewa kazi ya kuteremsha mvua na ya mazao anapopewa amri na Allaah. Na yupo Israafiyl mwenye kazi ya kupuliza parapanda (baragumu) siku ya Qiyaamah. Na yupo Malaika wa kifo aliyepewa kazi ya kutoa roho wakati wa kufa, na yupo Malaika wa majabali, na yupo Malik mlinzi wa mlango wa Motoni, na wapo Malaika wanaowashughulikia watoto wachanga matumboni mwa mama zao, na wengine waliopewa kazi ya kuwahifadhi wanaadamu na wengine wenye kuandika ‘amali zao, na kila mtu ana Malaika wawili.
Allaah Anasema:
إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ. مَا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ
"Wanapopokea wapokeaji wawili, wanaokaa kuliani na kushotoni
Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari (kuandika)."
Qaaf – 17 – 18
Na wengine wana kazi za kuwauliza maiti baada ya kufikishwa kaburini, wanajiwa na Malaika wawili na kumuuliza Nani Mola wake, nini dini yake, nani mtume wake?
Allaah Anasema:
يُثَبِّتُ اللّهُ الَّذِينَ آمَنُواْ بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الآخِرَةِ وَيُضِلُّ اللّهُ الظَّالِمِينَ وَيَفْعَلُ اللّهُ مَا يَشَاء
"Allaah Huwatia imara wenye kuamini kwa kauli imara katika maisha ya dunia na katika Aakhirah. Na Allaah huwaacha kupotea hao wenye kudhulumu. Na Allaah Hufanya apendavyo."
Ibraahiym – 27
Na wapo Malaika waliopewa kazi ya kuwashughulikia watu wa Peponi.
Allaah Anasema:
وَالمَلاَئِكَةُ يَدْخُلُونَ عَلَيْهِم مِّن كُلِّ بَابٍ. سَلاَمٌ عَلَيْكُم بِمَا صَبَرْتُمْ فَنِعْمَ عُقْبَى الدَّارِ
"Na Malaika wanawaingilia katika kila mlango.(Wakiwaambia) Assalaamu ‘Alaykum! Amani iwe juu yenu, kwa sababu ya mlivyosubiri! Basi ni mema mno malipo ya Nyumba ya Aakhirah."
Ar-Ra’ad – 23 – 34
Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alitujulisha kuwa ndani ya 'Baytul Ma’amuur', iliyopo mbinguni wanaingia na kuswali ndani yake kila siku Malaika elfu sabini wakishamaliza hawaipati fursa ya kurudi humo tena.
Vitabu
Na tunaamini kuwa Allaah Amewateremshia Mitume Vitabu ili viwe hoja na mwangaza kwa walimwengu kwa ajili ya kuwafundisha hekima na kwa ajili ya kuwatakasa.
Na tunaamini kuwa Allaah Amemteremshia kila Mtume Kitabu.
Allaah Anasema:
لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَيِّنَاتِ وَأَنزَلْنَا مَعَهُمُ الْكِتَابَ وَالْمِيزَانَ لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ
"Kwa hakika tuliwatuma Mitume Wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu."
Al-Hadiyd – 25
Na katika vitabu hivyo tunavyovijua ni:
1. Taurati; Allaah Alimteremsia Nabii Muusa (‘Alayhis-Salaam), na hiki ni Kitabu kitukufu kupita vyote vya Bani Israaiyl.
Allaah Anasema:
إِنَّا أَنزَلْنَا التَّوْرَاةَ فِيهَا هُدًى وَنُورٌ يَحْكُمُ بِهَا النَّبِيُّونَ الَّذِينَ أَسْلَمُواْ لِلَّذِينَ هَادُواْ وَالرَّبَّانِيُّونَ وَالأَحْبَارُ بِمَا اسْتُحْفِظُواْ مِن كِتَابِ اللّهِ وَكَانُواْ عَلَيْهِ شُهَدَاء
"Hakika Sisi Tuliteremsha Taurati yenye uongofu na nuru, ambayo kwayo Manabii walionyenyekea Kiislamu, na wacha Mungu, na Wanachuoni, waliwahukumu Mayahudi; kwani walikabidhiwa kukihifadhi Kitabu cha Allaah. Nao wakawa ni mashahidi juu yake."
Al-Maaidah – 44
2. Injili; Allaah alimteremshia Nabii ‘Iysa (‘Alayhis-Salaam), na hiki kinakisadikisha Taurati na kukikamilisha.
Allaah Anasema:
وَآتَيْنَاهُ الإِنجِيلَ فِيهِ هُدًى وَنُورٌ وَمُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ التَّوْرَاةِ وَهُدًى وَمَوْعِظَةً لِّلْمُتَّقِينَ
"Na tukampa Injili iliyomo ndani yake uongofu, na nuru na inayosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na uongofu na mawaidha kwa wacha Mungu."
Al-Maaidah – 46
3. Zaburi; Aliyopewa Nabii Daawuud (‘Alayhis-Salaam).
4. Sahifa (Suhuf); Walizoteremshiwa Nabii Ibraahiym na Muusa (‘Alayhimas-Salaam).
5. Qur-aan tukufu; Aliyoteremshiwa Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) mwisho wa ma Nabii.
Allaah Anasema:
هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ
"Ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi."
Al-Baqarah – 185
Na Akasema:
مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ الْكِتَابِ وَمُهَيْمِنًا عَلَيْهِ
"Kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda."
Al-Maaidah – 48
Kwa Kitabu hiki Allaah Akavifuta vilivyotangulia na Akachukua Yeye mwenyewe jukumu la kukilinda ili kibaki kuwa hoja kwa viumbe wote mpaka siku ya Qiyaamah.
Allaah Anasema:
إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ
"Hakika Sisi ndio Tulioteremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio Tutaoulinda."
Al-Hijr – 9
Ama Vitabu vilivyotangulia, vilikuwa vikiletwa kwa ajili ya wakati maalum, na ukishamalizika wakati wake vinaletwa vingine kuchukua nafasi yake, na hii ndiyo maana havikuwa na uwezo wa kujilinda kutokana na ubadilishaji.
Allaah Anasema:
مِّنَ الَّذِينَ هَادُواْ يُحَرِّفُونَ الْكَلِمَ عَن مَّوَاضِعِهِ
"Miongoni mwa Mayahudi wamo ambao hubadilisha maneno na kuyatoa mahala pake."
An-Nisaa -46
Na Akasema:
فَوَيْلٌ لِّلَّذِينَ يَكْتُبُونَ الْكِتَابَ بِأَيْدِيهِمْ ثُمَّ يَقُولُونَ هَـذَا مِنْ عِندِ اللّهِ لِيَشْتَرُواْ بِهِ ثَمَناً قَلِيلاً فَوَيْلٌ لَّهُم مِّمَّا كَتَبَتْ أَيْدِيهِمْ وَوَيْلٌ لَّهُمْ مِّمَّا يَكْسِبُونَ
"Basi ole wao wanaoandika kitabu kwa mikono yao, kisha wakasema: Hiki kimetoka kwa Allaah, ili wachumie kwacho pato dogo. Basi ole wao kwa yale iliyoandika mikono yao, na ole wao kwa yale wanayoyachuma."
Al-Baqarah – 79
Na Akasema:
قُلْ مَنْ أَنزَلَ الْكِتَابَ الَّذِي جَاء بِهِ مُوسَى نُورًا وَهُدًى لِّلنَّاسِ تَجْعَلُونَهُ قَرَاطِيسَ تُبْدُونَهَا وَتُخْفُونَ كَثِيرًا
"Sema: Nani aliyeteremsha Kitabu alichokuja nacho Muwsaa, chenye nuru na uongofu kwa watu, mlichokifanya kurasa kurasa mkizionyesha, na mengi mkiyaficha."
Al-An’aam – 91
Na Akasema:
وَإِنَّ مِنْهُمْ لَفَرِيقًا يَلْوُونَ أَلْسِنَتَهُم بِالْكِتَابِ لِتَحْسَبُوهُ مِنَ الْكِتَابِ وَمَا هُوَ مِنَ الْكِتَابِ وَيَقُولُونَ هُوَ مِنْ عِندِ اللّهِ وَمَا هُوَ مِنْ عِندِ اللّهِ وَيَقُولُونَ عَلَى اللّهِ الْكَذِبَ وَهُمْ يَعْلَمُونَ. مَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُؤْتِيَهُ اللّهُ الْكِتَابَ وَالْحُكْمَ وَالنُّبُوَّةَ ثُمَّ يَقُولَ لِلنَّاسِ كُونُواْ عِبَادًا لِّي مِن دُونِ اللّهِ وَلَـكِن كُونُواْ رَبَّانِيِّينَ بِمَا كُنتُمْ تُعَلِّمُونَ الْكِتَابَ وَبِمَا كُنتُمْ تَدْرُسُونَ
"Na wapo baadhi yao wanaopindua ndimi zao katika kusoma Kitabu ili mdhanie kuwa hayo yanatoka Kitabuni, na wala hayatoki Kitabuni. Na husema: Haya yametoka kwa Allaah. Na wala hayatoki kwa Allaah. Na wanamsingizia Allaah uongo na wao wanajua.
Haiwezi kuwa mtu aliyepewa na Allaah Kitabu na hikima na Unabii kisha awaambie watu: Kuweni wa kuniabudu mimi badala ya Allaah. Bali atawaambia: Kuweni wenye kumuabudu Mola wa viumbe vyote, kwa kuwa nyinyi mnafundisha Kitabu na kwa kuwa mnakisoma."
Aali-‘Imraan – 78 – 79
Na Akasema:
يَا أَهْلَ الْكِتَابِ قَدْ جَاءكُمْ رَسُولُنَا يُبَيِّنُ لَكُمْ كَثِيرًا مِّمَّا كُنتُمْ تُخْفُونَ مِنَ الْكِتَابِ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ قَدْ جَاءكُم مِّنَ اللّهِ نُورٌ وَكِتَابٌ مُّبِينٌ
"Enyi Watu wa Kitabu! Amekwishakujieni Mtume wetu anayekufichulieni mengi mliyokuwa mkiyaficha katika Kitabu, na anayesamehe mengi. Bila shaka imekujieni kutoka kwa Allaah nuru na Kitabu kinachobainisha."
Al-Maaidah – 15
Mitume
Na tunaamini kuwa Allaah Amewatuma kwa waja Wake Mitume ili wawe wabashiri na waonyaji.
Allaah Anasema:
رُّسُلاً مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلاَّ يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللّهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ وَكَانَ اللّهُ عَزِيزًا حَكِيمًا
"Mitume hao ni wabashiri na waonyaji, ili watu wasiwe na hoja juu ya Allaah baada ya kuletewa Mitume. Na Allaah ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima."
An-Nisaa – 165
Na tunaamini kuwa Muhammad ni mbora wa Mitume yote, kisha Ibrahim kisha Musa kisha Nuh kisha Issa mwana wa Maryam, na hawa ndio waliohuswa katika aya ifuatayo.
Allaah Anasema:
وَإِذْ أَخَذْنَا مِنَ النَّبِيِّينَ مِيثَاقَهُمْ وَمِنكَ وَمِن نُّوحٍ وَإِبْرَاهِيمَ وَمُوسَى وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ وَأَخَذْنَا مِنْهُم مِّيثَاقًا غَلِيظًا
"Na tulipochukua ahadi kwa Manabii na kwako wewe (Muhammad), na Nuuh na Ibraahiym na ‘Iysaa mwana wa Mariamu, na tulichukua kwao ahadi ngumu."
Al-Ahzaab – 7
Na tunaamini kuwa shari’ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) imekusanya fadhila zote walizokuja nazo Mitume iliyotangulia.
Allaah Anasema:
شَرَعَ لَكُم مِّنَ الدِّينِ مَا وَصَّى بِهِ نُوحًا وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَمَا وَصَّيْنَا بِهِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَى وَعِيسَى أَنْ أَقِيمُوا الدِّينَ وَلَا تَتَفَرَّقُوا فِيهِ
"Amekuamrisheni Dini ile ile aliyomuusia Nuwh na tuliyokufunulia wewe, na tuliyowausia Ibraahiym na Muwsaa na ‘Iysaa, kwamba shikeni Dini wala msifarikiane kwayo."
Ash-Shuuraa – 13
Na tunaamini kuwa Mitume yote ni watu, viumbe na hawana uwezo wowote wa kuumba au kugawa rizki wala hawajui ghaibu nk.
Allaah Anasema:
وَلاَ أَقُولُ لَكُمْ عِندِي خَزَآئِنُ اللّهِ وَلاَ أَعْلَمُ الْغَيْبَ وَلاَ أَقُولُ إِنِّي مَلَكٌ
"Wala sikwambiini kuwa nina khazina za Allaah; wala kuwa mimi najua mambo ya ghayb; wala sisemi: Mimi ni Malaika."
Huud – 31
Allaah Alimuamrisha Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) atamke maneno yafuatayo:
قُل لاَّ أَقُولُ لَكُمْ عِندِي خَزَآئِنُ اللّهِ وَلا أَعْلَمُ الْغَيْبَ وَلا أَقُولُ لَكُمْ إِنِّي مَلَكٌ
“Sema: Mimi sikwambiini kuwa ninazo khazina za Allaah. Wala sijui mambo yaliyofichikana. Wala sikwambiini kuwa mimi ni Malaika”
Al-An’aam – 50
Na akaamrishwa pia atamke:
قُل لاَّ أَمْلِكُ لِنَفْسِي نَفْعًا وَلاَ ضَرًّا إِلاَّ مَا شَاء اللّهُ
"Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara, ila apendavyo Allaah."
Al-A’araaf – 188
Na atamke:
قُلْ إِنِّي لا أَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا ولا رَشَدًا. قُلْ إِنِّي لَن يُجِيرَنِي مِنَ اللَّهِ أَحَدٌ وَلَنْ أَجِدَ مِن دُونِهِ مُلْتَحَدًا
"Sema: Mimi sina mamlaka ya kukudhuruni wala kukuongozeni."
Sema: Hakika hapana yeyote awezaye kunilinda na Allaah, wala sitapata pa kukimbilia isipokuwa kwake Yeye tu."
Al-Jinn – 21-22
Na tunaamini kuwa wao ni waja wa Allaah Aliowakirimu kwa kuwapa ujumbe.
Allaah Anasema:
ذُرِّيَّةَ مَنْ حَمَلْنَا مَعَ نُوحٍ إِنَّهُ كَانَ عَبْدًا شَكُورًا
"Enyi kizazi tuliyowachukua pamoja na Nuwh! Hakika yeye alikuwa mja mwenye shukrani."
Al-Israa – 3
Na Akasema:
تَبَارَكَ الَّذِي نَزَّلَ الْفُرْقَانَ عَلَى عَبْدِهِ لِيَكُونَ لِلْعَالَمِينَ نَذِيرًا
"Ametukuka Aliyeteremsha Furqaan kwa mja Wake, ili awe mwonyaji kwa walimwengu wote."
Al-Furqaan – 1
Na juu ya Mitume mingine Akasema:
وَاذْكُرْ عِبَادَنَا إبْرَاهِيمَ وَإِسْحَقَ وَيَعْقُوبَ أُوْلِي الأَيْدِي وَالأبْصَارِ
"Wakumbuke waja wetu, Ibraahiym na Is-haaq na Yaa'quwb waliokuwa na nguvu na busara."
Swaad – 45
Na Akasema:
وَوَهَبْنَا لِدَاوُودَ سُلَيْمَانَ نِعْمَ الْعَبْدُ إِنَّهُ أَوَّابٌ
"Na Daawuwd Tukamtunukia Sulaymaan. Alikuwa mja mwema. Na hakika alikuwa mwingi wa kutubia."
Swaad – 30
Na juu ya ‘Iysa mwana wa Maryam Allaah Anasema:
"Hakuwa yeye (‘Iysaa) ila ni Mtumwa Tuliyemneemesha na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili."
Az-Zukhruf – 59
Tunaamini pia kuwa Allaah Subhaanahu wa Ta’ala Amekamilisha ujumbe wake kwa kumleta Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kama ni Mtume kwa watu wote.
Allaah Anasema:
قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللّهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ لا إِلَـهَ إِلاَّ هُوَ يُحْيِـي وَيُمِيتُ فَآمِنُواْ بِاللّهِ وَرَسُولِهِ النَّبِيِّ الأُمِّيِّ الَّذِي يُؤْمِنُ بِاللّهِ وَكَلِمَاتِهِ وَاتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ
"Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume kwenu nyinyi nyote, niliyetumwa na Allaah Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Hapana mungu ila Yeye Anayehuisha na Anayefisha. Basi muaminini Allaah na Mtume Wake asiyejua kusoma na kuandika, ambaye anamuamini Allaah na maneno Yake. Na mfuateni yeye ili mpate kuongoka."
Al-A’araf – 158
Dini Ya Allaah
Na tunaamini kuwa dini alokuja nayo ni Islam aliyoridhika nayo Allaah kwa waja Wake. Na kwamba Allaah Haikubali dini nyingine isipokuwa hii.
Allaah Anasema:
إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللّهِ الإِسْلاَمُ
"Bila ya shaka Dini mbele ya Allaah ni Uislamu."
Aali-‘Imraan – 19
Na Akasema:
الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الإِسْلاَمَ دِينًا
"Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini."
Al-Maaidah – 3
Na Akasema:
وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الإِسْلاَمِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ
"Na anayetafuta dini isiyokuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Aakhirah atakuwa katika wenye khasara."
Aali-‘Imraan – 85
Na tunaamini kuwa yeyote atakayedai kuwa ipo dini nyengine inayokubaliwa na Allaah isiyokuwa Islamu, kama vile dini ya Kiyahudi au ya Kinasara au dini nyengine yoyote, huyo anakuwa amekufuru, na lazima atubu kwa kufru yake hiyo. Akitubu anasamehewa, ama asipotubu huyo anauliwa kama ni Murtaddi, kwa sababu anakuwa ameikadhibisha Qur-aan tukufu.
Na tunaamini kuwa hapana tena Mtume baada ya Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na yeyote atakayejidai utume baada yake au akamsadiki mwenye kujidai utume anakuwa kafir, kwa sababu anakuwa amemkadhibisha Allaah na Mtume Wake na Waislamu wote.
Makhalifa Waongofu
Na tunaamini kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) anao Makhalifa waongofu waliouongoza ummah baada ya kufa kwake kwa kueneza elimu na da’awah na uongozi, na kwamba mbora wao ni Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu) akifuatiwa na ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) kisha ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘anhu), kisha ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu), na huu ndio mpangilio wao katika kufadhilishwa kwao.
Na tunaamini kuwa ummah ule ndio umma bora kupita zote, na hii inatokana na kauli yake Allaah Alipowaambia:
كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللّهِ
"Nyinyi ndio ummah bora kuliko umma zote waliodhihirishiwa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Allaah."
Aali-‘Imran – 110
Na tunaamini kuwa walio bora kupita wote ni Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum), kisha waliokuja baada yao, kisha waliokuja baada yao, na kwamba wangali wapo watu wenye kuidhihirisha haki bila kujali lawama za wanaowalaumu, mpaka siku Allaah atakapoleta amri Yake.
Na tunaitakidi kuwa yaliyotokea baina ya Maswahaba (Radhiya Allaahu anhum) katika fitna na mapambano, yanatokana na jitihada zao katika uamuzi. Wapo waliosibu na wapo waliokosea, na kama alivyosema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):
"Mwenye kujitahidi na kusibu anapata ujira mara mbili, na mwenye kukosea anapata ujira mara moja."
Na kwamba Allaah Atawasamehe makosa yao, na tunaamini kuwa lazima tuache kuwasema vibaya, na badala yake tuwaseme kwa wema, na tusiwataje isipokuwa kwa kuzitaja sifa wanazozistahiki, na tuziondoe chuki zetu juu yao.
Allaah Anasema:
لا يَسْتَوِي مِنكُم مَّنْ أَنفَقَ مِن قَبْلِ الْفَتْحِ وَقَاتَلَ أُوْلَئِكَ أَعْظَمُ دَرَجَةً مِّنَ الَّذِينَ أَنفَقُوا مِن بَعْدُ وَقَاتَلُوا وَكُلا وَعَدَ اللَّهُ الْحُسْنَى
"Hawawi sawa miongoni mwenu wenye kutoa kabla ya Ushindi na wakapigana vita. Hao wana daraja kubwa zaidi kuliko wale ambao waliotoa baadae na wakapigana. Na wote hao Allaah Amewaahidia wema."
Al-Hadiyd – 10
Na Akasema:
وَالَّذِينَ جَاؤُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلاخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالايمَانِ وَلا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَؤُوفٌ رَّحِيمٌ
"Na waliokuja baada yao (wakawa wanawapenda Waislamu waliotangulia wanawaombea du’aa) wanasema: Mola wetu! Tughufirie sisi na ndugu zetu waliotutangulia (kufa) katika Uislamu, wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani kuwafanyia Waislamu (wenzetu). Mola wetu! Hakika Wewe ni Mpole na Mwenye kurehemu."
Al-Hashr – 10
Siku Ya Mwisho
Tunaamini kuwa Siku ya Mwisho ndiyo Siku ya Qiyaamah, ambapo hapana tena siku nyingine baada yake, na siku hiyo Allaah Atawafufua waja wake kwa ajili ya kuwaingiza katika nyumba ya neema 'Peponi', au katika nyumba ya adhabu iumizayo 'Motoni'.
Tunaamini kuwa watu watafufuliwa baada ya baragumu kupigwa, kama Allaah Alivyosema:
وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَصَعِقَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الأرْضِ إِلا مَن شَاء اللَّهُ ثُمَّ نُفِخَ فِيهِ أُخْرَى فَإِذَا هُم قِيَامٌ يَنظُرُونَ
"Na litapulizwa barugumu, wazimie waliomo mbinguni na waliomo katika ardhi, isipokuwa Aliyemtaka Allaah. Kisha litapulizwa mara nyengine. Hapo watainuka wawe wanangojea."
Az-Zumar – 68
Kisha watu watasimamishwa mbele ya Allaah wakiwa kama siku waliyozaliwa bila viatu wala nguo (kama ilivyoelezwa katika Swahiyh Al-Bukhaariy na Muslim – Imepokelewa kuwa Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):
"Watu watafufuliwa wakiwa uchi kila mmoja anamtizama mwenzake?" Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia: "Ewe Aisha! mambo siku hiyo yatakuwa magumu kuliko hivyo."
Watu hawatakuwa na wakati wa kutazamana - mambo yatakuwa magumu sana - Ya rabbi sallim.)
Allaah Anasema:
يَوْمَ نَطْوِي السَّمَاء كَطَيِّ السِّجِلِّ لِلْكُتُبِ كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ وَعْدًا عَلَيْنَا إِنَّا كُنَّا فَاعِلِينَ
"Siku Tutakapozikunja mbingu kama mkunjo wa karatasi za vitabu. Kama tulivyoanza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika Sisi ni watendao."
Al-Anbiyaa – 104
Na tunaamini kuwa watu watapewa madaftari yao kwa mkono wa kulia au nyuma ya migongo yao au kushotoni mwao.
Allaah Anasema:
فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ. فَسَوْفَ يُحَاسَبُ حِسَابًا يَسِيرًا. وَيَنقَلِبُ إِلَى أَهْلِهِ مَسْرُورًا. وَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ وَرَاء ظَهْرِهِ. فَسَوْفَ يَدْعُو ثُبُورًا. وَيَصْلَى سَعِيرًا
"Ama atakayepewa daftari lake kwa mkono wa kulia. Basi huyo atahesabiwa hisabu nyepesi. Na arudi kwa ahli zake na furaha.
Na ama atakayepewa daftari lake kwa nyuma ya mgongo wake. Basi huyo ataomba kuteketea. Na ataingia Motoni."
Al-Inshiqaaq – 7 – 12
Na Akasema:
وَكُلَّ إِنسَانٍ أَلْزَمْنَاهُ طَآئِرَهُ فِي عُنُقِهِ وَنُخْرِجُ لَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كِتَابًا يَلْقَاهُ مَنشُورًا . اقْرَأْ كَتَابَكَ كَفَى بِنَفْسِكَ الْيَوْمَ عَلَيْكَ حَسِيبًا
"Na kila mtu tumemfungia ‘amali yake shingoni mwake. Na Siku ya Qiyaamah tutamtolea kitabu atakachokikuta kiwazi kimekunjuliwa.
Ataambiwa: Soma kitabu chako! Nafsi yako inakutosha leo kukuhesabu."
Al-Israa- 13 – 14
Na tunaamini kuwa mezani zitawekwa Siku ya Qiyaamah na kwamba hapana atakayedhulumiwa.
Allaah Anasema:
فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ. وَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ
"Basi anayetenda chembe ya wema, atauona! Na anayetenda chembe ya uovu atauona!."
Zilzaal – 7 – 8
Na Akasema:
فَمَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ. وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُوْلَئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ فِي جَهَنَّمَ خَالِدُونَ. تَلْفَحُ وُجُوهَهُمُ النَّارُ وَهُمْ فِيهَا كَالِحُونَ
"Ama wale ambao mizani zao zitakuwa nzito, hao ndio wenye kufanikiwa. Na wale ambao mizani zao zitakuwa nyepesi, hao ndio walio zitia khasarani nafsi zao, na katika Jahannamu watadumu. Moto utababua nyuso zao, nao watakuwa na nyuso zilizokunjana."
Al-Muuminuun – 102-104
Shafa’ah
Na tunaamini kuwa ipo Shafa’ah (msamaha) kubwa ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) atakapowaombea umma wake baada ya kupewa idhini hiyo na Mola wake Subhaanahu wa Ta’ala, na baada ya watu kuona dhiki na kuanza kuwaendea Manabii Nuuh kisha Ibraahiym kisha Muusa kisha ‘Iysa (Alayhimus-Salaam) mpaka watakapoishia kwake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Na tunaamini pia kuwa wale watakaoingia Motoni katika Waislamu (tu) nao pia wataombewa Shafa’ah watolewe humo, na Shafa’ah hii ni kwa ajili ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Mitume mingine na watu wema na Malaika, na tunaamini kwamba Allaah Atawatoa Motoni pia makundi kwa makundi ya Waislamu kwa fadhila Zake tu na rehma Yake, bila hata kuombewa Shafa’ah.
Hodhi na Swiraat
Na tunaamini kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ana hodhi lake, na maji yake ni meupe kuliko maziwa na matamu kuliko asali, na yenye harufu nzuri kuliko hal miski. Urefu wake hodhi hilo ni mwendo wa mwezi mzima, na upana wake mwendo wa mwezi mzima.na vyombo vyake vinang'aa kama nyota za mbinguni.
Waislamu watakunywa humo, na atakayekunywa hatopata kiu tena.
Tuaamini kuwa ipo 'Swiraat' itakayowekwa juu ya Jahannam, na watu watapita juu yake, na kasi zao zitakuwa kiasi cha ‘amali zao. Wapo watakaopita kama umeme, na wengine kama upepo, na wengine kama ndege, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) atakuwa juu yake huku akisema: "Ya rabbi Sallim sallim" (Allaah Salimisha Salimisha)
Na tunaamini kila kilichokuja katika mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuhusu Siku hiyo pamoja na vitisho vyake - Tunamuomba Allaah Atusaidie.
Pepo Na Moto
Na tunaamini juu ya Pepo na Moto, na kwamba Pepo ni nyumba ya neema Aliyowaandalia Allaah waja wake wema wamchao. Ndani yake mna yale ambayo macho hayajapata kuyaona, wala masikio kuyasikia wala halijapata kumpitikia mtu yeyote nafsini mwake.
Allaah Anasema:
فَلا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاء بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ
"Nafsi yoyote haijui waliyofichiwa katika hayo yanayofurahisha macho - ni malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda."
As-Sajdah – 17
Na Moto ni nyumba ya adhabu Aliyoitayarisha Allaah Subhaanahu wa Ta’ala kwa ajili ya makafiri madhalimu. Ndani yake mna kila aina ya adhabu ambazo hazijapata kumpitikia mtu yeyote nafsini mwake.
Allaah Anasema:
وَإِن يَسْتَغِيثُوا يُغَاثُوا بِمَاء كَالْمُهْلِ يَشْوِي الْوُجُوهَ بِئْسَ الشَّرَابُ وَسَاءتْ مُرْتَفَقًا
"Na wakiomba msaada watasaidiwa kwa kupewa maji kama mafuta yaliyotibuka. Yatayowababua nyuso zao. Kinywaji hicho ni kiovu mno!"
Al-Kahf – 29
Na Akasema:
إِنَّ اللَّهَ لَعَنَ الْكَافِرِينَ وَأَعَدَّ لَهُمْ سَعِيرًا. خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا لا يَجِدُونَ وَلِيًّا وَلا نَصِيرًا. يَوْمَ تُقَلَّبُ وُجُوهُهُمْ فِي النَّارِ يَقُولُونَ يَا لَيْتَنَا أَطَعْنَا اللَّهَ وَأَطَعْنَا الرَّسُولا
"Hakika Allaah Amewalaani makafiri na Amewaandalia Moto unaowaka kwa nguvu.Watadumu humo milele. Hawampati mlinzi wala wa kuwanusuru. Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa katika Moto. Watasema: Laiti tungelimtii Allaah, na tungelimtii Mtume!"
Al-Ahzaab – 64 – 66
Maswali Ya Kaburini
Na tunaamini juu ya mtihani wa kaburini, wakati mtu atakapoulizwa nani Mola wake na ipi dini yake na yupi Mtume wake.
Allaah Anasema:
يُثَبِّتُ اللّهُ الَّذِينَ آمَنُواْ بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الآخِرَةِ
"Allaah Huwatia imara wenye kuamini kwa kauli imara katika maisha ya dunia na katika Aakhirah."
Ibraahiym – 27
Na tunaamini juu ya neema za kaburini.
Allaah Anasema:
الَّذِينَ تَتَوَفَّاهُمُ الْمَلآئِكَةُ طَيِّبِينَ يَقُولُونَ سَلامٌ عَلَيْكُمُ ادْخُلُواْ الْجَنَّةَ بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ
"Wale ambao Malaika huwafisha katika hali njema, wanawaambia: Amani iwe juu yenu! Ingieni Peponi kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyatenda."
An-Nahl – 32
Adhabu Ya Kaburini
Na tunaamini juu ya adhabu ya kaburini kwa madhalimu na makafiri.
Allaah Anasema:
وَلَوْ تَرَى إِذِ الظَّالِمُونَ فِي غَمَرَاتِ الْمَوْتِ وَالْمَلآئِكَةُ بَاسِطُواْ أَيْدِيهِمْ أَخْرِجُواْ أَنفُسَكُمُ الْيَوْمَ تُجْزَوْنَ عَذَابَ الْهُونِ بِمَا كُنتُمْ تَقُولُونَ عَلَى اللّهِ غَيْرَ الْحَقِّ وَكُنتُمْ عَنْ آيَاتِهِ تَسْتَكْبِرُونَ
"Na lau ungeliwaona madhaalimu wanavyokuwa katika mahangaiko ya mauti, na Malaika wamewanyooshea mikono wakiwambia: Zitoeni roho zenu! Leo mtalipwa adhabu ya fedheha kwa sababu ya mliyokuwa mkiyasema juu ya Allaah yasiyo ya haki, na mlivyokuwa mkizifanyia kiburi Ishara Zake."
Al-An’aam – 93
Katika mlango huu zipo Hadiyth nyingi zilizo sahihi, na kila Muislamu anatakiwa aamini yote yaliyomo ndani ya Qur-aan na ndani ya Sunnah (Mafundisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) yanayohusu mambo ya ghaibu na wala asiyakatae kwa sababu hayalingani na mambo yanayotendeka duniani, kwani ya Aakhirah hayakisiwi na haya ya duniani kutokana na hitilafu kubwa sana iliyopo baina ya mawili hayo – WaAllaahu l Musta’aan.
Qadar
Tunaamini juu ya Qadar (kudra – majaliwa - yale yaliyokwisha andikwa) kheri yake na shari yake kuwa yote yamekwisha andikwa na yote yanatokana na Allaah na kwamba kisha waqadiria waja wake kwa elimu yake iliyokienea kila kitu.
Na Qadar imegawika sehemu nne.
1. Ujuzi: Tunaamini kuwa Allaah ni Mjuzi wa kila kitu, Anajua kilichotokea na kitakachotokea na namna inavyotokea, na hii inatokana na elimu yake isiyo na mwanzo wala mwisho ilichokienea kila kitu. Hakitokei kipya ikawa Allaah Hakuwa na elimu nacho, na tunaamini kuwa Allaah hasahau.
2. Maandishi: Tunaamini kuwa AllaahAmeandika katika ubao wa Lawh al-Mahfuudh yote yaliyotokea na yatakayotokea mpaka siku ya Qiyaamah.
Allaah Anasema:
أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللَّهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاء وَالاَرْضِ إِنَّ ذَلِكَ فِي كِتَابٍ إِنَّ ذَلِكَ عَلَى اللَّهِ يَسِيرٌ
"Je! Hujui kwamba Allaah Anayajua yaliyomo mbinguni na katika ardhi? Hakika hayo yamo Kitabuni. Hakika (kuyadhibiti) hayo kwa Allaah ni mepesi."
Al-Hajj – 70
3. Kutaka: Tunaamini kuwa Allaah Ametakakiwepo kila kilicho mbinguni na ardhini, kwani hakiwezi kuwepo kitu chochote bila Yeye kutaka kiwepo. Anachokitaka kinakuwa na Asichokitaka hakiwi.
4. Kuumba: Tunaamini kuwa Allaah ndiye Aliyeumba kila kitu.
Allaah Anasema:
لَهُ مَقَالِيدُ السَّمَاوَاتِ وَالأرْضِ وَالَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ اللَّهِ أُوْلَئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ
"Allaah ndiye Muumba wa kila kitu, na Yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu. Yeye Anazo funguo za mbingu na ardhi."
Az-Zumar – 63
Kutaka kwa Allaah
Na sehemu hii ya tatu imekusanya kutaka kwa Allaah Subhaanahu wa Ta’ala na kutaka kwa viumbe Vyake, kwa sababu Allaah Anakijuwa kila kinachotendwa na waja Wake, na kwamba Yeye mwenyewe Ametaka kiwepo, ama sivyo kisingewezekana kutendeka.
Allaah Anasema:
لِمَن شَاء مِنكُمْ أَن يَسْتَقِيمَ. وَمَا تَشَاؤُونَ إِلا أَن يَشَاء اللَّهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ
"Kwa yule miongoni mwenu anayetaka kwenda sawa. Wala nyinyi hamtataka isipokuwa Atake Allaah Mola wa walimwengu wote."
At-Takwiyr – 28 – 29
Na Akasema:
وَلَوْ شَاء اللّهُ مَا اقْتَتَلُواْ وَلَـكِنَّ اللّهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ
"Na lau kuwa Allaah Alipenda wasingelipigana. Lakini Allaah Hutenda atakavyo."
Al Baqarah – 253
Na Akasema:
وَلَوْ شَاء رَبُّكَ مَا فَعَلُوهُ فَذَرْهُمْ وَمَا يَفْتَرُونَ
"Na lau kuwa Allaah Angelipenda wasingefanya hayo. Basi waache na hayo wanayoyazua."
Al-An’aam – 112
Lakini juu ya yote hayo, tunaamini pia kuwa Allaah Amempa mwanaadamu uhuru wa kuamua na Akampa uwezo wa kutenda. Na ufuatao ni ushahidi kuwa mwanaadamu amepewa uwezo huo.
Allaah Anasema:
فَأْتُواْ حَرْثَكُمْ أَنَّى شِئْتُمْ
"Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo.'
Al-Baqarah – 223
Na Akasema:
وَلَوْ أَرَادُواْ الْخُرُوجَ لأَعَدُّواْ لَهُ عُدَّةً
"Na ingelikuwa kweli walitaka kutoka bila ya shaka wangelijiandalia maandalio."
At-Tawbah – 46
Kwa hivyo Allaah Amempa mwanaadamu uwezo wa kutaka, kuamua na wa kwenda atakapo na kujiandalia atakavyo.
Pili, kule kuamrishwa kufanya mema na kukatazwa kufanya mabaya ni dalili kuwa mwanaadamu anao uwezo wa kufanya atakalo, maana kama asingekuwa na uwezo huo kule kukatazwa na kuamrishwa kusingekuwa na maana yoyote.
Allaah Anasema:
لاَ يُكَلِّفُ اللّهُ نَفْسًا إِلاَّ وُسْعَهَا
"Allaah Haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri iwezavyo."
Al-Baqarah - 286
Tatu, Allaah Anamsifia Atendaye mema kwa wema wake, na Anamlaumu atendaye ovu kwa ovu lake. Mwanaadamu asingekuwa na uwezo wa kutenda atakalo basi pasingekuwa na haja ya kumsifia mwema wala kumlaumu muovu kwa sababu huko ni kumpa mtu sifa asiyoistahiki.
Nne, Allaah Ameleta Mitume.
Allaah Anasema:
رُّسُلاً مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلاَّ يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللّهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ
"Mitume hao ni wabashiri na waonyaji, ili watu wasiwe na hoja juu ya Allaah baada ya kuletewa Mitume."
An-Nisaa – 165
Yangelikuwa matendo ya watu hayafanyiki kwa uwezo wao na uchaguzi wao, hoja yao isingebatilika kwa kuletewa Mitume.
Tano, kila mtu anapotenda jambo huhisi kuwa ametenda au ameacha kutenda. Utamuona anaposimama, anapokaa, anapoingia, anapotoka, anaposafiri, anapolala. Anapotenda lolote katika haya hufanya kama anavyotaka na wala hahisi kama yupo yeyote anayemlazimisha kufanya hayo, bali anaiona tofauti iliyopo anapofanya jambo kwa hiari yake mwenywe na anapolazimishwa, na hata shari’ah inatofautisha pale mtu anapofanya jambo kwa hiari yake na anapolazimishwa wakati Allaah Hamuhesabii kuwa ametenda kosa mtu anayefanya jambo kwa kulazimishwa.
Wakati huo huo anayefanya maasi kwa hiari yake huyo anahesabiwa kama ni mkosa, kwa sababu amechagua kufanya hayo kwa hiari yake mwenyewe bila kuelewa kuwa Allaah Keshamuandikia. Kwa hivyo hapana anayejua nini alichoandikiwa ila baada ya kutenda.
Allaah Anasema:
وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا
"Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho."
Luqmaan – 34
Na Akasema:
سَيَقُولُ الَّذِينَ أَشْرَكُواْ لَوْ شَاء اللّهُ مَا أَشْرَكْنَا وَلاَ آبَاؤُنَا وَلاَ حَرَّمْنَا مِن شَيْءٍ كَذَلِكَ كَذَّبَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِم حَتَّى ذَاقُواْ بَأْسَنَا قُلْ هَلْ عِندَكُم مِّنْ عِلْمٍ فَتُخْرِجُوهُ لَنَا إِن تَتَّبِعُونَ إِلاَّ الظَّنَّ وَإِنْ أَنتُمْ إَلاَّ تَخْرُصُونَ
"Watasema walioshirikisha: Lau kuwa Allaah Angetaka tusingelishiriki sisi, wala baba zetu; wala tusingeliharimisha kitu chochote. Vivi hivi walikanusha waliokuwa kabla yao mpaka walipoonja adhabu yetu. Sema: Je, nyinyi mnayo ilimu mtutolee? Nyinyi hamfuati ila dhana. Wala hamsemi ila uongo tu."
Al-An’aam – 148
Kwa hivyo tunamuambia mwenye kufanya maasi; 'Kwa nini usitende mema huku ukitegemea kuwa Allaah ndiye Alokuandikia uyatende? Kwa sababu hapana tofauti kwako baina ya mema na maovu kwa vile hujui nini ulichoandikiwa kabla ya kukitenda.'
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipowaambia Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum);
"Kila mmoja keshaandikiwa makao yake ya Peponi na ya Motoni." Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wakamuuliza: "Si bora tuache kufanya ‘amali na tuyategemee tuliyokwishaandikiwa?" Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akawaambia: "Hapana! Bali fanyeni, kwani kila mtu amewepesishiwa yale ambayo kwa ajili yake ameumbiwa."
Na tunamuuliza mwenye kutenda maasi: 'Kwa mfano wewe unasafiri kwa gari kuelekea Makkah, ukakuta mbele yako njia mbili, mtu mkweli akakuambia kuwa ukipita njia ya mwanzo utakutana na vitisho vingi na utapambana na tabu, ama njia ya pili ni nyepesi na haina matatizo yoyote. Bila shaka utapita njia ya pili, na haiwezekani ukapita ya mwanzo ukasema; 'Nishaandikiwa', na kama utafanya hivyo, watu watakuona mwendawazimu.
Mfano mwengine; Ukifanikiwa kupata kazi mbili, mojawapo ina mshahara mkubwa sana na nyengine mshahara mdogo, ukaambiwa uchague, bila shaka utachagua ile yenye mshahara mkubwa. Basi vipi unajichagulia nafsi yako katika ‘amali za Aakhirah zile zilizo duni kisha unasema kuwa 'Hivi ndivyo nilivyokadiriwa (nishaandikiwa)?
Unapoumwa kwa mfano, utawatafuta madaktari bora na utakubali kustahamili kupigwa sindano zenye kuuma au kufanyiwa operesheni na kustahamili kunywa dawa chungu, unafanya yote hayo ili upate kupona. Kwa nini basi huachi kujitibia na kusema; 'Nishaandikiwa?'
Baadhi Ya Faida
Itikadi hii tukufu yenye mizizi mitukufu ina matunda mengi yenye faida nyingi ndani yake, na zifuatazo ni baadhi tu ya faida hizo:
Imani ya kumuamini Allaah na majina Yake na sifa Zake vinaongeza mapenzi yetu kwa Allaah na kumtukuza. Mambo ambayo kupatikana kwake kunasababisha kuzidisha hima ya kuisimamia dini na kujiepusha na makatazo ya Allaah na kufuata maamrisho Yake Subhaanahu wa Ta’ala kwa ajili ya kupata furaha ya duniani na ya Aakhirah.
Allaah Anasema:
مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَى وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُواْ يَعْمَلُونَ
"Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda."
An-Nahl – 97
Matunda Ya Kuamini Malaika
Kwanza: Tunapata kujua utukufu wa Aliyewaumba Subhaanahu wa Ta’ala na kuzijua nguvu Zake na Ufalme wake.
Pili: Kumshukuru Allaah kwa kuwalinda waja Wake, kwani Malaika hawa wamo miongoni mwao wenye kazi ya kuwalinda Waislamu na kuandika ‘amali zao n.k.
Tatu; Kuwapenda Malaika kwa kumuabudu kwao Allaah kwa ukamilifu, na kwa kuwaombea kwao maghfira Waislamu.
Matunda Ya Kuviamini Vitabu
Kwanza: Tanapata kuielewa rehma ya Allaah juu ya waja Wake, kwa vile Amewateremshia Kitabu kila umati kwa ajili ya kuwaongoza.
Pili: Tunaiona hekima ya Allaah Aliyeweka ndani ya Vitabu hivi shari’ah zenye kunasibiana na kila umati, na akakifanya Kitabu cha mwisho kuwa Qur-aan tukufu ili kiwe kwa umati wote uliobaki katika zama zote na wakati wote mpaka Siku ya Qiyaamah.
Tatu: Tunapata kumshukuru Allaah kwa neema Yake hiyo.
Matunda Ya Kuamini Mitume
Kwanza: Tunaijua rehma ya Allaah kwa waja wake Aliyewapelekea Mitume kwa ajili ya kuwaongoza.
Pili: Tunapata kumshukuru Allaah kwa neema Yake hiyo.
Tatu: Kuwapenda Mitume na kuwaheshimu na kuwapa sifa wanazozistahiki, kwani wao ni Mitume wa Allaah waliochaguliwa miongoni mwa watu wote, wakamuabudu Allaah kama Anavyostahiki kuabudiwa, wakaifanya kazi ya kuwalingania watu huku wakisubiri na kustahamili udhia.
Matunda Ya Kuiamini Siku Ya Qiyaamah
Kwanza: Kumtii Allaah kwa kutegemea kupata thawabu zitakazokufaa Siku ya Qiyaamah, na kuepukana na kufanya madhambi kwa kuihofia adhabu ya Siku hiyo.
Pili: Kumliwaza Muislamu kwa yale anayoyakosa katika neema za hapa duniani na anasa zake, akitegemea neema na anasa za Siku ya Aakhirah.
Matunda Ya Kuamini Qadar
Kwanza: Kumtegemea Allaah katika kila jambo, kwa vile vyote ni kwa uwezo Wake Allaah.
Pili: Starehe ya nafsi na utulivu wa moyo, maana mtu anapotambua kuwa hapana kinachoweza kutokea bila Allaah kutaka, moyo hutulia na nafsi huingiwa na matumaini akaridhika na kile alichomuandikia Mola wake. Na hapana mtu anayeishi maisha mazuri na mwenye nafsi iliyotulia kupita yule mwenye kuamini juu ya Qadar.
Tatu: Kuondoa majisifu pale mtu anapofanikiwa kupata analolitaka, kwani kupata chochote ni neema itokayo kwa Allaah na kwa kuwa keshaandikiwa (keshajaaliwa) mtu huyo kuyapata mafaniko yale au kheri ile, kwa hivyo mtu huyo anatakiwa amshukuru Allaah badala ya kujisifu.
Nne; Kuondosha hofu na uoga pale mtu anapokikosa anachokitaka au anapopata msiba kwani yote hayo yanatokana na Allaah.
Allaah Anasema:
مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الأَرْضِ وَلا فِي أَنفُسِكُمْ إِلا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا إِنَّ ذَلِكَ عَلَى اللَّهِ يَسِيرٌ
"Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwishaandikwa katika Kitabu kabla hatujauumba. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi."
Al-Hadiyd – 22
Tunamuomba Allaah Subhaanahu wa Ta’ala Atuthibitishe katika itikadi hii na Atuonjeshe matunda yake na atuongezee katika fadhila Zake na asizipoteze nyoyo zetu baada ya kuziongoza, na atumiminie rehma kutoka Kwake kwani Yeye ndiye Mpaji.
WalhamduliLlaahi Rabbil ‘aalamin – Mola wetu mswalie na msalimie Mtume wako Muhammad pamoja na Maswahaba wake na ‘Aali zake wema, na kila atakayemfuata kwa wema na uongofu mpaka Siku ya Qiyaamah.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni