Translate

Ijumaa, 28 Juni 2019

Ukihisi dalili hizi huenda damu imepungua

Huenda una upungufu wa damu bila kujijua kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha ya suala hili. Kwa lugha rahisi, upungufu wa damu hutokea chembe chembe nyekundu za damu zinapokuwa chache kiasi cha kushindwa kukidhi mahitaji ya mwili.

Mpendwa msomaji, fuatana nami katika makala ya leo ili kuzitambua sababu, dalili na dondoo za kufuata ili kuepukana na tatizo la upungufu wa damu.

Undani wa damu kwa ufupi

Katika mwili wa binadamu, mfumo wa damu umejengwa na moyo, mishipa ya damu na damu yenyewe. Tukiiangalia damu kiundani, tutaona kuwa, damu imejengwa na vitu viwili ambavyo ni maji yenye chumvi chumvi (plasma) na chembe chembe hai ambazo ni chembe nyekundu, chembe nyeupe na chembe za kugandisha damu.

Katika chembe zote hizi, upungufu wa chembe nyekundu ndiyo husababisha upungufu wa damu kwani dalili zote za upungufu wa damu hutokea endapo tu kiwango cha chembe hizi kitapungua.

Sababu za kupungua damu

Zipo sababu nyingi zinazoweza kupelekea upungufu wa damu. Upungufu huu pia, aghlabu, hutokea taratibu hadi mtu kuanza kupata dalili.

Kwa asilimia kubwa upungufu wa damu husababishwa na upungufu wa madini ya chuma na huwatokea zaidi wanawake wajawazito. Pia upungufu wa madini ya chuma huwapata zaidi wanawake wanaotoka damu nyingi wakati wa siku zao.

Mbali na upungufu wa madini ya chuma, upungufu wa damu pia unaweza kusababishwa na upungufu wa vitamini hasa vitamini B 12 ambayo inafanya kazi kubwa ya kuzalisha seli nyekundu za damu. Upungufu wa damu pia husababishwa na uwepo wa maradhi ya kudumu kama vile ukimwi au maradhi mengine ya muda mrefu kama vile figo na baadhi ya saratani. Upungufu wa damu huweza kusababishwa na maradhi ya mifupa na magonjwa mengine ya kurithi kama vile ugonjwa wa seli mundu (sickle cell).

Dalili zake

Tatizo la kupungua damu ni la kawaida kabisa kwa wanawake ambao wanapata siku zao kila mwezi, ila upungufu huu huitwa upungufu wa kawaida kwani hauleti dalili yoyote. Hali huwa tofauti ikiwa damu hii itapungua kwa kiasi cha kushindwa kuhudumia mwili ambapo dalili mbali mbali huanza kujitokeza kulingana na kiasi cha damu kilichopungua.

Miongoni mwa dalili za awali ambazo hujitokeza ikiwa damu itapungua ni pamoja na kizunguzungu, udhaifu na uchovu usio na sababu, maumivu ya kichwa, mapigo ya moyo kuenda mbio, maumivu ya kifua, mwili kuwa wabaridi hasa mikono na miguu, kukosa pumzi pamoja na ngozi kuwa na rangi ya njano au nyeupe.

Fanya haya kuongeza kiwango cha damu

Katika kipengele hiki tutaangazia zaidi kutibu maradhi ya kupungua damu ikiwa chanzo chake ni ukosefu wa madini ya chuma au vitamini. Upungufu huu unaweza kutibiwa kwa kuongeza matumizi ya vyakula vyenye virutubisho hivi kwa wingi.

Vyakula vyenye kiwango kikubwa cha madini ya chuma ni pamoja na nyama, maini, maharage na dengu na vile vyenye vitamini kwa wingi ni pamoja na mbogamboga, matunda, samaki na vyengine mfano wa hivyo.

 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...