Miongoni mwa habari zilizochapishwa inahusu funga (swaumu) ya siku sita za baada ya Ramadhan, yaani ‘Sittat Shawwal’.
Habari hiyo inaelezea umuhimu wa Muislamu kufunga siku hizi sita kama njia ya kujitakasa na upungufu au makosa mbalimbali yaliyojitokeza katika swaumu ya Ramadhan.
Pamoja na matarajio kuwa kila aliyefunga swaumu ya Ramadhan atapata ujira mwema Siku ya Kiyama, ukweli ni kwamba yapo makosa yanayofanywa na baadhi yetu ambayo kwa namna moja au nyingine hupunguza thawabu za swaumu.
Hivyo basi, ni muhimu sana kufunga siku hizi sita ili kufidia upungufu uliojitokeza katika swaumu ya Ramadhan.
Kisharia, funga hii ya siku sita za Shawwal [Mfungo Mosi] ni Sunna iliyosisitizwa sana (Sunnat Muaqqadah) na siyo faradhi. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesisitiza sana kufunga Sunna hii kwa sababu ina fadhila kubwa mbele ya Allah, kama alivyobainisha: “Yeyote afungae swaumu ya Ramadhan na akafuatisha na siku sita za mwezi Shawwal ni kama vile amefunga mwaka mzima,” [Muslim, Abu Daud, Nasai na Ibn Majah].
Ukilinganisha Hadithi hii na Aya inayozungumzia Usiku wa Cheo (Laylatul Qadr) kuwa ni bora kuliko miezi elfu moja (miaka 83 na miezi3), utaona jinsi fadhila za kufunga siku hizi ilivyo kubwa. Laylatul Qadr ni bora kuliko miezi elfu moja; na kufunga Sunna ya siku sita za Shawwal ni sawa na kufunga mwaka mzima. Subhanallah! Basi ni jambo gani litakalomfanya Muumini aliye mzima wa afya aache kufunga swaumu ya siku sita za mwezi Shawwal?
Kwa nini mwaka mzima? Mtume (rehema za Allahna amani zimshukie) amesema: “Allah amefanya kwa kila jema ni sawa na mema kumi. Hivyo kufunga mwezi mzima ni sawa na kufunga miezi kumi, na kufunga siku sita za Shawwal hukamilisha mwaka.” [Ibn Majah na Nasai].
Siku moja ya mwezi wa Ramadhan ni sawa na siku kumi. Hivyo basi, siku 30 za Ramadhan ni sawa na siku 300. Ukiongeza swaumu ya siku sita za Sunna ya Shawwal unatimiza siku 60, ambazo ukijumlisha na siku 300 unatimiza siku mia tatu na sitini (360), ambazo ukigawa kwa thelathini unapata miezi 12 (mwaka mmoja).
Hivyo ndivyo wanazuoni walivyoifafanua Hadithi hiyo ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie). Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba, faida ya ibada za Sunna kama swaumu hii ya siku sita za Shawwal, ambazo watu wengi huzipuuza ni kubwa Siku ya Hesabu [Kiyama] hasa linapokuja suala la kufidia upungufu uliojitokeza katika ibada za faradhi.
Katika Hadithi Sahihi, Mjumbe wa Allah amesema: “Kitu cha kwanza ambacho mja atahesabiwa kwacho ni sala. Allah atasema kuwaambia Malaika, ‘Angalieni sala ya mja wangu kama ipo kamili’ (Ingawa yeye anajua kila kitu). Kama iko kamili itahesabiwa kuwa kamili na kama ina upungufu, Allah atasema, ‘Angalieni iwapo mja wangu alikuwa na sala za sunna.’ Kama atakuwa na sala za Sunna, Allah ataikamilisha sala yake kwa sunna za mja wake. Kisha matendo yote yatapimwa vivyo hivyo,” (Abuu Daud).
Katika Hadithi hii, Mtume amesema: “…Kisha matendo yake yatapimwa vivyo hivyo,” Hii ina maana kwamba swaumu za faradhi zitakamilishwa na swaumu za Sunna ikiwamo hii ya siku sita za mwezi wa Shawwal.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni