SWALI
Sababu gani ya kisheria inayopelekea mwanamke kutoa mimba na asipate madhambi...?
MAJIBU
Kutoa mimba ikiwa ni kabla ya kupuliziwa roho au baada ya kupuliziwa roho kisheria ni haraam. Wakati unaokubalika kutoa mimba ni pale tu itakapokuwa kuna dharura za kisheria ndipo panaweza kukubalika tena kwa masharti yake.
Dharura hizo, ni kama kumehakikishika kuwa kuna uwezekana wa mama kufariki kwa kuwa na kiumbe hicho, au kuendelea kwake kuwa na mimba hiyo kutamletea mauti. Na isitoshe kukubalika huko, bali kumetakiwa uthibitisho huo utolewe na daktari mwenye kuaminika kabisa.
Na muhimu kwanza atafutwe daktari Muislamu mwenye kuaminika, ikishindikana, basi daktari yeyote ambaye ni muaminifu sana.
Ama kuitoa mimba tu kwa sababu ya kutotaka mtoto, au kukhofia riziki yake, au malezi yake, au kuchelea gharama za maisha kama kumsomesha, kumvisha, au kumlisha n.k. hayo yote hayaruhusiwi kisheria kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:
“Wala msiwaue wana wenu kwa kuogopa umasikini. Sisi Tunawaruzuku wao na nyinyi. Hakika kuwaua hao ni khatia kubwa” [Al-Israa: 31]
“Wala msiwaue watoto wenu kwa sababu ya umasikini. Sisi Tunakuruzukuni nyinyi na wao” [Al-An'aam: 151]
Ingawa kuna baadhi ya Maulamaa wanaonelea kuwa inafaa kutoa mimba katika siku za arobaini za mwanzo, lakini iliyo sahihi zaidi ni kutokufaa kutoa katika hali zote ila kwa dharura kubwa kabisa inayokubalika katika sheria.
Ama katika hatua ya pili ya siku arobaini nyingine ambayo ni 'alaqah (kipande cha damu), au hatua ya tatu ya siku arobaini nyingine ambayo inajulikana kama ni 'mudhwgah' (kipande cha nyama), haitoruhusiwa kutolewa hiyo mimba hadi jopo la madaktari wenye kuaminika wathibitishe kuwa kweli kuendelea kuwepo mimba hiyo kutasababisha mama kufariki au ikiwa kumeonekana na kujulikana kuwa kiumbe (kijusi) hicho kimeshakufa tumboni ndipo katika hali hiyo kutaruhusika kutolewa baada ya kila njia kutumika kuondosha hatari hiyo kufeli.
Baada ya hatua hiyo ya tatu, na kufika miezi minne (siku mia na ishirini, yaani arobaini tatu) ambapo ndio roho itakuwa ishapuliziwa hicho kiumbe, hapo patakuwa haparuhusiki kabisa na ni madhambi makubwa kabisa ila kwa dharura kuu kabisa kama ilivyotajwa hapo nyuma, na tena kuwe kumefanyika juhudi kubwa za kuokoa hali sababishi (chenye kusababisha) na kwa hali hiyo kutakuwa kumetumika maslahi ya 'unafuu kati ya madhara mawili'.
Na unafuu hapo ni uhai wa mama ambao ndio bora zaidi na wa msingi zaidi kuliko wa huyo kiumbe. Kwa sababu mama tayari kamili na anaishi na kuwepo kwake bado kuna matumaini ya kupatikana vizazi vingine, pia ni mwenye majukumu na wajibu katika maisha, na msimamizi wa nyumba, mlezi, n.k., hali hicho kiumbe kilichopo tumboni, hakina uhakika wa kuishi hadi kitakapozaliwa na haijulikani kama kitakapozaliwa kitakuwa hai au la, na pia kisicho na majukumu yoyote kwa wakati huo. Kwa hali hiyo, kati ya kulinda na kuokoa hali moja kati ya mbili, basi kumuokoa na kumlinda mama ni bora zaidi kuliko kile kilichoko tumboni.
Hali hiyo uliyoieleza, inaonyesha hakukuwa na dharura hiyo, na hivyo huyo mwanamke katenda kitendo kiovu ambacho sheria haikikubali kabisa. Tendo hilo la dhambi, linahitaji toba kwa mtendaji; toba ya dhati kabisa.
Ama kafara ya kitendo hicho, wametofautiana Maulamaa wakati wake na hata aina ya kafara yenyewe.
Baada ya kutazama pande zote, lililo lenye nguvu ni kuwa, kabla ya kupuliziwa roho kiumbe (kijusi), hakulazimiki kutoa kafara (fidia), pamoja na kuwa kuna wanaoona kuwa inapaswa kutolewa.
Lakini aliyefanya kitendo hicho anatakiwa atubu toba ya kweli na azidishe kufanya 'amali nyingi za kheri na kutoa sadaka sana kulipa maovu yake, kwani mema hufuta maovu.
Ama baada ya kupuliziwa roho, hakuna tofauti kukubaliwa kwake kuwepo na kafara au kutolewa fidia 'Diyah' (blood money).
Baadhi ya Maulamaa wamesema kuwa kunatolewa fidia ya pesa kwa wale wenye kuhusiana na kiumbe hicho kwa kiasi cha gramu 213 za dhahabu, na wanalipwa wale wanaomrithi kile kiumbe (yaani kaka, dada au babu, bibi n.k. kulingana na sheria ya Mirathi), hatopewa yule aliyeshiriki kukitoa (kukiua) japo anaweza kumrithi. Na ikiwa wanaomrithi wakasamehe basi hakuna malipo.
Kisha anatakiwa aache huru mtumwa (ikiwa inawezekana hilo), ikiwa haiwezekani au hakuna hali hiyo, basi anatakiwa afunge miezi miwili mfululizo ambayo ni kafara kwa ajili kuua.
Kama Asemavyo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
“Na haiwi Muumini kumuua Muumini ila kwa kukosea. Na mwenye kumuua Muumini kwa kukosea basi amkomboe mtumwa aliye Muumini, na atoe diya kuwapa jamaa za maiti, isipokuwa waache wenyewe kuwa ni sadaka. Na akiwa ni jamaa wa maadui zenu, hali yeye ni Muumini, basi ni kumkomboa mtumwa aliye Muumini. Na akiwa ni miongoni wa watu ambao pana ahadi baina yenu na wao basi wapewe diya watu wake na akombolewe mtumwa Muumini. Na asiye pata, basi afunge miezi miwili mfululizo, kuwa ni toba kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hekima” [An-Nisaa: 92]
Hivyo, utaratibu wa kufanya kwa yule aliyetoa mimba baada ya siku mia na ishirini (miezi minne) yaani baada ya kupuliziwa roho, ni huu:
Kufanya toba ya kweli, na milango ya toba iko wazi hadi wakati karibu jua litakapochomoza upande wa magharibi (kabla halijachomoza), au wakati wa gharghar (roho itakapokuwa imefika kooni wakati wa kutolewa ‘mkoromo wa mauti’).
Na masharti ya toba ni haya yafuatayo:
Kulipa fidia 'Diyah' (blood money);
Kafara kwa kukiua kiumbe, nayo ni kuacha huru mtumwa, au kufunga miezi miwili mfululizo.
Pia kutoa mimba kwa sababu imetokana na kitendo cha zinaa, ni jambo lisilokubalika kabisa.
Kiumbe hakina makosa na tunajua kuwa habebi kiumbe madhambi ya mwengine.
Allaah Anasema:
"Wala habebi mbebaji mzigo wa mwengine" [Al-An’aam: 164]
Na Amesema tena:
Na mbebaji habebi mzigo wa mwingine.)) [Faatwir 35:18]
Pia tukitazama kisa cha mwanamke wa ki-Ghaamidy aliyezini na akaenda kwa Mtue kutaka apewe adhabu ya mzinifu, na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamtaka aende hadi atakapozaa, na kasha akamrudisha tena hadi amnyonyeshe huyo mtoto na kisha mtoto alipokuwa mkubwa ndipo akatekeleza adhabu kwake. (Swahiyh Muslim).
Tukio hilo linatuonyesha kuwa mtoto japo wa kitendo cha zinaa hairuhusiwi kabisa kuuliwa anapokuwa tumboni.
Na tufahamu kuwa kila kiumbe kinachozaliwa kinakuwa ni Muislam, na huenda huyo mtoto wa tendo la zinaa akawa Muislam bora sana kuliko wengi. Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aallihi wa sallam) anasema: "Kila mtoto anazaliwa katika hali ya fitwrah (maumbile ya asli; Uislam)..." Imepokewa na Imaam Al-Bukhaariy
Vilevile mwanamke ambaye amebakwa, haruhusiwi kutoa mimba yake kwa kauli yenye nguvu, ingawa baadhi ya Maulamaa wanasema anaweza kutoa katika siku zile arobaini za mwanzo ikiwa kuwa kwake na hiyo mimba kutamsababishia madhara katika jamii yake au kwa watu wake ima kwa kumtenga, kumsusa au hata kumuua kwa kigezo cha ‘kulinda hadhi’ ya familia au ukoo.
Lakini, pamoja na sababu hizo, utakuta hazitoshi kuhalalisha kutoa mimba kwani kufanya hivyo, ni kutenda dhambi nyingine na inajulikana kuwa hicho kilichopo tumboni hakihusiki kwa njia moja au nyingine na jarima ile ya kubakwa mwanamke huyo, na maadam haikuwa ridhaa ya mwanamke kufanywa hivyo na alijitahidi kupambana na mbakaji/wabakaji akazidiwa.
Ni wajibu wake kukihifadhi hicho kiumbe na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atakilinda na kukijaalia kuwa ni chema na poza kwa mama yake. Na ikiwa mwanamke huyo hajaolewa, basi ni jambo jema kwa wanaume wa Kiislam kumsitiri na kumsaidia kumtoa katika mitihani hiyo iliyomkumba. Ama kama ana mume, basi mume wake ajitahidi japo ni vigumu sana, kusubiri na kukikubali kiumbe hicho ambacho hakina hatia yoyote ile. Na malipo makubwa yanawasubiri watu aina hiyo.
Wa Allaahu A’alam