Translate

Jumatano, 15 Mei 2019

Mambo mengine yasiyoharibu swawm

                                        Mambo yasiyoharibu swawm


1- Wanja
Kwa mujibu wa maoni sahihi ya wanachuoni wanja hauharibu swawm ya mwanamke wala ya mwanaume. Lakini hata hivyo lililo bora kwa mfungaji autumie usiku. Hali kadhalika hukumu hiyo hiyo ina vipodozi vingine vyote kama sabuni, mafuta na vinginevyo vinavyopakwa mwilini. Mfano wa vitu hivyo ni hina, vipodozi na kadhalika. Ni sawa kwa mfungaji kutumia vyote hivyo. Lakini haifai kutumia vipodozi ikiwa vinaudhuru uso.


2- Dawa ya mswaki

Swawm haiharibiki kwa kuswaki kwa dawa ya mswaki. Ni kama Siwaak. Lakini mtu anatakiwa kuhakikisha hakumeza kitu katika dawa hiyo. Ikimteleza akameza kitu katika dawa sio wajibu kwake kulipa siku hiyo.

3- Dawa za matone ya macho na masikio

Dawa za matone ya macho na masikio haziharibu swawm kwa mujibu wa maoni sahihi ya wanachuoni. Ikiwa mtu atahisi ladha yake shingoni lililo salama zaidi ni kulipa siku hiyo. Lakini hata hivyo sio wajibu kwa sababu macho na masikio havina njia za kupitisha chakula na kinywaji.
Kuhusu dawa za matone ya pua hazijuzu kwa sababu kuna njia ya kupitisha chakula na kinywaji. Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayh wia sallam) amesema:
“Yapandishe maji vizuri wakati wa kusukutua isipokuwa ikiwa kama utakuwa mfungaji.”[1]
Kujengea juu ya Hadiyth hii ni wajibu kwa mwenye kutumia dawa za matone ya pua kulipa siku hiyo.


4- Kuota na fikira za kimapenzi

Kuota na fikira za mapenzi haziharibu swawm hata kama zitamfanya mtu kumwaga. Mtu akiona manii ni wajibu kwake kuoga janaba. Akiota na kumwaga baada ya Fajr na akachelewesha mpaka Dhuhr hakuna neno. 


Hali kadhalika ikiwa atamwingilia mke wake usiku na akaoga baada ya kupambazuka alfajiri. Ni sawa. Imethibiti ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anafanya jimaa usiku, anaamka asubuhi hali ya kuwa na janaba, akioga na kuendelea na swawm. 


Hali kadhalika mwenye hedhi na mwenye nifasi. Endapo watatwaharika usiku na wakaoga baada ya kuwa alfajiri imeshaingia hakuna neno na swawm zao ni sahihi. 

Lakini haijuzu kwa wanawake hawa, wala kwa yule aliye na janaba, kuchelewesha kuoga au swalah mpaka jua likachomoza. Bali ni wajibu kwao wote kuoga kabla ya jua kuchomoza ili waweze kuswali kwa wakati wake.


5- Kucheza na mke

Inafaa kwa mwanaume aliefunga kucheza na mke wake, kumbusu na kumkumbatia maadamu hawakufanya jimaa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwabusu na akiwakumbatia wakeze ilihali amefunga. Lakini mtu akichelea kutumbukia katika yale aliyoharamisha Allaah itakuwa yaliyotajwa ni haramu kwake. Endapo atamwaga anatakiwa kuendelea kufunga na ailipe siku hiyo. Hata hivyo kwa mujibu wa wanachuoni wengi hana juu yake kafara.

Kuhusu madhii, hayaharibu swawm kwa mujibu wa maoni sahihi ya wanachuoni. Asli ni kuwepo kwa swawm na madhii ni vigumu kuyaepuka.


6- Kumeza mate

Mate hayadhuru swawm kabisa. Ni sawa kumeza mate na ni sawa vilevile kuyatema.

Kuhusu makohozi yanayotoka kifuani au mapuani, ni wajibu kwa mwanaume na mwanamke kuyatema na asiyameze.

Ee waislamu! Swawm ni kitendo chema na kikubwa na thawabu zake ni tele na khaswa khaswa swawm ya Ramadhaan. Uadhimisheni – Allaah akurehemuni – kwa kuwa na nia njema na kujitahidi kuhifadhi swawm yake, kusimama nyusiku zake na kukimbilia matendo mema na kutubia madhambi na makosa yote. Tahadharini na yale Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walokataza na mtiini katika Ramadhaan na wakati mwingine. Usianeni na saidianeni juu ya hayo. Amrisheni mema na katazeni maovu ili muweze kupata Pepo, furaha, utukufu na kufuzu duniani na Aakhirah.

Tunamuomba Allaah atuhifadhi sisi na nyinyi kutokamana na yale yote yenye kusababisha ghadhabu Zake, atukubalie swawm zetu na visimamo vyetu, azitengeneze hali za watawala wa waislamu na ainusuru dini Yake kupitia wao na awakoseshe nusura maadui Wake kupitia wao na awawafikishe wote waweze kuifahamu dini na kuwa na msimamo juu yake na kuhukumu na kuhukumiwa kwayo katika mambo yote. Hakika Yeye ni muweza juu ya hayo.

Swalah na salaam zimwendee mja na Mtume Wake, Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na wale wote wataofuata njia yake hadi siku hiyo ya Qiyaamah.


[1] Abu Daawuud (2366), at-Tirmidhiy (788), an-Nasaa’iy (78), Ibn Maajah (407) na Ahmad (16430). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (930).


http://bit.ly/30jGCT0 i live islam

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...