Tukiitafakari funga kwa kina, tutabaini maana na malengo makuu ya funga ni pamoja na kumfanya mja asalimu amri na ajihisi ni mtumwa halisi wa Allah.
Kuwa mtumwa wa Allah, ndio kupata uhuru kamili, kama alivyosema Kadhi Iyadh: “Na kilichoniongezea fahari na utukufu na kukaribia kuikanyaga (nyota ya) Thuraya ni mimi kuingia kwenye neno lako, ‘Ewe mja wangu,’ na kumfanya Muhammad kuwa Nabii wangu.”
Hili la kuwa mtumwa wa Allah, ni tukufu mno, kwani limesemwa kwenye neno la Allah, ‘Enyi waja wangu.’ Pia, kuna mshairi mwingine anasema: “Nimeziendekeza tamaa zikanifanya mtumwa, lau kama nigelikinai, ningelikuwa huru.”
Kwa mantiki hii, uhuru wa kweli unapatikana kwa kuwa mtumwa wa Allah, na funga inamlea mtu katika hilo. Allah anasema:
“Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa Alfajiri katika weusi wa usiku.” [Qur’an, 2: 187]
Hii ni amri inayokutaka ule, na kwa mantiki hii, kula ni ibada. Na kama inavyofahamika, ni sunna kwa mwanadamu kula daku na kufuturu, na ni chukizo kuunganisha funga siku moja au siku mbili bila ya kula.
Hivyo basi, unatakiwa ule ili ukinaishe matanio yako ya kula na kunywa. Na katika wakati mwingine, Mola wako anakuamrisha kinyume chake (uache kula): “Kisha timizeni swaumu mpaka usiku.” [Qur’an, 2:187]. Mtu anajizuwia kula, kunywa na kila kinachofunguza tokea wakati wa alfajiri mpaka usiku kwa kumtii Allah Mtukufu, na huko ni kumtii Mola kiuhalisia. Allahb akikwambia: “Kula”, unakula; na akikwambia: “Kunywa”, unakunywa. Pia, akikwambia: “Funga”, unafunga.
Katika suala hili, mja anajifunza kuwa, suala si ladha anayoipata, tamaa, au hisia, bali ni kumtii Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu akituamrisha kula, tunakula; akituamrisha kufunga, tunafunga. Kwa mfano, kwenye sala, kuna wakati mtu anasimama, anarukuu, anasujudu, na kuna wakati anaketi kwa sababu hii ndiyo amri ya Mwenyezi Mungu, na hii ndiyo sababu hasa ya kufanya hivyo.
Mfano mwingine, katika Ihramu, mtu hakatazwi kula wala kunywa, isipokuwa hukatazwa kutenda jimai, na vinavyopelekea katika jimai. Pia, hukatazwa kufunika kichwa, kujitia manukato, kukata kucha, kupunguza nywele, na kila aina ya anasa.
Mtu hujikuta anajizuwia na yote hayo katika kipindi chote cha Ihramu kwa sababu Mwenyezi Mungu ndivyo alivyotaka tuwe. Lakini aliyehirimia, anaruhusiwa kula; na akiacha kula, atakuwa amezua jambo katika dini. Akimaliza Ihramu tu, mtu anatakiwa kwa lazima kufanya aliyokatazwa – kuanzia kunyoa nywele, kukata kucha, kujitia manukato na kukoga. Mwenyezi Mungu anasema: “Kisha wajisafishe taka zao, na waondoe nadhiri zao.” [Qur’an 22:29].
Haya ndiyo malezi halisi ya utumwa wa Allah. Allah anakuamrisha kutenda jambo unatekeleza; na unakatazwa unaacha. Wala hakuna lazima ya kujua sababu au hekima ya hiyo amri au katazo. Kifupi, hekima inapatikana kwenye eneo la kwamba: Allah ameamuru nawe umetekeleza, amekukataza nawe umeacha. Hii ndio maana halisi ya utumwa. Miongoni mwa maana za swaumu/funga ni kuipa mafunzo jamii kwani huenda kuna wengi katika jamii wamefunga sunna aidha Siku Nyeupe, Ashura, au Arafa nk.
Je, kuna tofauti gani kati ya funga ya sunna na funga ya faradhi?
Kwenye funga ya sunna, mtu hupata tabu na usumbufu wa aina fulani, lakini kwenye funga ya faradhi mtu husema, “Sub-haana llah! Yashangaza funga ilivyo nyepesi, ni kama hatujafunga.” Na hivi ndivyo isemwavyo na watu wote.
Unaweza ukajiuliza, hali hii inasababishwa na kitu gani? Wala hakuna shaka kuwa Allah huwasaidia waja wake katika funga za sunna na zile za faradhi, japo msaada katika funga za faradhi huwa mkubwa zaidi. Msaada upo kwenye funga zote, lakini kwa mtazamo wangu, kwa sababu Allah ameifanya funga ya Ramadhan kuwa faradhi kwa wote; na kwamba kila uendapo sokoni, skuli, kazini na hata ukirejea nyumbani, kila mahali unakutana na watu wamefunga; basi hali hii hufanya usihisi uzito. Hutohisi uzito kwa sababu unahisi hili ni jambo la wote.
Ni kwa sababu hii wale wenzetu wanaoishi kwenye nchi za watu wanaokula mchana, mfano nchi za Ulaya, hupata tabu sana katika kufunga mwezi wa Ramadhan.
Ni kwamba, katika maeneo hayo watu wanaonekana wanakula kila mahali mchana, huyu mfungaji hatizamwi kama amefunga. Kama ni kazini, mtu huyo anatakiwa afanye kazi kama wafanyavyo watu wengine, na aingie kama waingiavyo watu wengine, na atoke kama watokavyo watu wengine, bila kujali kama amefunga. Mtu huyu (anayeishi nchi wanazokula mchana), hujikuta anapata tabu mno, kama tunavyosimuliwa na jamaa zetu wanaoishi Ulaya katika mwezi wa Ramadhan. Lakini, unapo-
ziangalia jamii za Kiislamu zinazofunga, watu hawapati tabu za funga, na hivi ndivyo inavyolelewa jamii.
http://bit.ly/2w9jNU8
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni