Zakaah Ya Biashara
Hukmu Yake
Wapo baadhi ya Wanachuoni ambao ni wachache sana wanaosema kuwa hapana dalili ya kuwa mali ya biashara inatolewa Zakaah, lakini dalili zilizomo ndani ya Qur-aan na Sunnah zinaleta maana kinyume na rai zao.
Allaah Anasema:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ إِنَّ صَلاَتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ
"Chukua (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika mali zao Swadaqah, uwatwaharishe na uwatakase kwazo na waombee (du’aa na maghfirah). Hakika du’aa yako ni utulivu kwao. Allaah ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote."
[At-Tawbah - 103]
Aayah hii inaleta maana ya ujumla kuwa Zakaah inatakiwa itolewe kutoka katika mali zao (Matajiri), mali ya aina yoyote ile ikiwemo mali ya biashara, bila kufafanua aina ya mali hiyo.
Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Ichukuliwe kutoka kwa matajiri wao na kurudishiwa mafakiri wao".
Kwa hivyo dalili hizi zinatujulisha kuwa mali yoyote ile, ikiwemo mali ya biashara, lazima itolewe Zakaah, na kwamba Zakaah hiyo ichukuliwe kutoka kwa matajiri, na bila shaka wafanya biashara ni matajiri, na kwamba irudishwe kwa masikini. Muhimu mali hiyo iwe imekifikia kile kiwango cha kutolewa Zakaah (Niswaab) na imekamilisha muda wa mwaka.
Namna Ya Kutoa Zakaah Ya Biashara
Mwenye kumiliki mali ya biashara iliyofikia Niswaab, akishakamilisha mwaka anatakiwa ahesabu mali yake yote aliyokuwa nayo kwa ajili ya biashara. Kama ni mfaya biashara wa nyumba, basi azihesabu nyumba zake (zile tu alizozitayarisha kwa ajili ya biashara), au ardhi au vyombo vya nyumbani, magari au nguo au biashara ya aina yoyote ile. Atavihesabu vitu alivyokuwa navyo kwa ajili ya biashara pamoja na kuzihesabu pesa zote alizonazo kwa ajili ya biashara kisha atazitolea Zakaah yake, nayo ni mbili unusu katika mia au moja katika arubaini.
Atafanya hesabu hiyo bila kujali kama wakati wowote ule ndani ya mwaka ule pesa hizo zilipungua au kuongezeka.
Kumbuka
Ikumbukwe kuwa vitakavyohesabiwa (katika Zakaah ya Biashara) ni vitu vilivyotayarishwa kwa ajili ya biashara tu.
Kwa mfano mtu anamiliki magari hata yakifikia idadi ya magari kumi au zaidi, au atataka kuuza gari lake mwenyewe kwa ajili ya kulibadilisha tu na kununua gari jengine au ardhi au nyumba au chochote kile, ikiwa anataka kuuza kwa ajili ya kutaka kununua kingine badala yake au kwa ajili ya mahitajio mengine yasiyokuwa ya kibiashara, basi mali hiyo haitolei Zakaah ya biashara, na hii ni kwa sababu Niyah ya kuviuza vitu hivyo si kwa ajili ya biashara.
Kumbuka pia kuwa Zakaah inatolewa kutokana na asili ya chochote kilichoongezeka kutokana mali hiyo wakati wowote ule katika mwaka. Ama kile kilichoongezeka kutokana na asili nyingine, basi mwaka wake unaanza kuhesabiwa kuanzia siku ile iliyoongezeka mali hiyo.
Kwa mfano;
Mfanya biashara alikuwa akiendela kupata faida katika biashara yake na kufikia kiasi cha Shilingi laki kumi, kisha katika mwezi wa mwisho au hata katika siku ya mwisho kabla ya kutimia mwaka, akapata faida kiasi cha Shilingi laki saba, pesa zote hizozitahesabiwa pamoja na Zakaah ya biashara ya mwaka huo, kwa sababu asili yake (faida iliyopatikana) inatokana na biashara hiyo anayoitolea Zakaah.
Mfano mwingine:
Mfanya biashara alikuwa akiendelea kupata faida katika biashara yake na kufikia kiasi cha shilingi laki kumi, kisha katika mwezi wa kumi na mbili au katika siku ya mwisho au siku yoyote ile ndani ya mwaka huo kabla ya kuingia muda wa kulipa Zakaah ya mwaka ule, mtu huyo akarithi mali au pesa kutoka kwa jamaa yake aliyefariki kiasi cha Shilingi milioni moja.
Pesa hizo alizorithihazitohesabiwa katika Zakaah ya mwaka huo, bali ataanza kuzihesabia mwaka wake mpya kuanzia siku ile alizozipata pesa hizo. Kwa sababu asili ya pesa hizo hazitokani na biashara ile anayoitolea Zakaah, bali inatokana na asili nyingine, ambayo ni urithi.
Wenye Kupokea Mishahara
Kwa kawaida mwenye kupokea mshahara pesa zake huongezeka na kupungua katika miezi mbali mbali. Kwa vile itakuwa vigumu kwake kuweka hesabu ya kila mwezi pale zinapokamilisha Niswaab au kuongezeka pale zinapopungua, wanavyuoni wakasema kuwa mtu huyo ataanza kuuhesabu mwaka wake kuanzia siku ile aliyoweza kutimiza Niswaab, na kuanzia mwezi huo, atakuwa akiitolea Zakaah mali yake kila anapotimiza mwaka.
http://bit.ly/30vLuom i live islam
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni