Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 21
Kumpendelea Kheri Ndugu Yako Muislamu Kama Unavyojipendelea Nafsi Yako
عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قَالَ: ((لاَ يُؤْمِنُ أَحَدُكُمْ حَتَّى يُحِبَّ لإِخِيهِ مَا يُحِبُّ لِنَفْسِهِ)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa Anas (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hatoamini mmoja wenu mpaka ampendelee nduguye anayojipendelea nafsi yake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Uislamu unasisitiza Waumini kupendana na kuungana, na unapendelea ummah uwe mmoja wenye nguvu.
Rejea: Aal-‘Imraan (3: 200).
2. Iymaan zinatofautiana kwa daraja, Waumini wengineo iymaan zao ni kubwa kabisa kiasi cha kumpendelea mwenziwe anayojipendelea nafsi yake. Nayo si sifa nyepesi kuimiliki. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
لَن تَنَالُوا الْبِرَّ حَتَّىٰ تُنفِقُوا مِمَّا تُحِبُّونَ ۚ وَمَا تُنفِقُوا مِن شَيْءٍ فَإِنَّ اللَّـهَ بِهِ عَلِيمٌ ﴿٩٢﴾
Hamtoweza kuufikia wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda. Na kitu chochote mnachotoa basi hakika Allaah kwacho ni Mjuzi. [Aal-’Imraan 92]
3. Waumini wapendeleane kheri daima, wakirimiane na waoneane huruma. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ ۚ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ ۖ
Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ni Rasuli wa Allaah. Na wale walio pamoja naye ni wakali zaidi dhidi ya makafiri; wanahurumiana baina yao. [Muhammad: 29]
4. Muumin daima awe ni mwenye kumnufaisha mwenziwe na jambo lao liwe moja katika kumtii Allaah (سبحانه وتعالى).
Rejea: At-Tawbah (9: 71).
Rejea pia Hadiyth namba (22), (23).
5. Muumin ayachukie maovu kumfikia mwenziwe kama anavyochukia kumfikia mwenyewe.
6. Muumin asiwe na sifa ya uchoyo, bali ajikhini nafsi yake kwa ajili ya nduguye. Kisa cha familia ya Abuu Twalha Al-Answaariy na mkewe Ummu Sulaym (رضي الله عنهما) ambacho ni sababu ya kuteremshwa Aayah ya Suwrah Al-Hashr (59: 9).
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، . أَنَّ رَجُلاً، مِنَ الأَنْصَارِ بَاتَ بِهِ ضَيْفٌ فَلَمْ يَكُنْ عِنْدَهُ إِلاَّ قُوتُهُ وَقُوتُ صِبْيَانِهِ فَقَالَ لاِمْرَأَتِهِ نَوِّمِي الصِّبْيَةَ وَأَطْفِئِي السِّرَاجَ وَقَرِّبِي لِلضَّيْفِ مَا عِنْدَكِ - قَالَ - فَنَزَلَتْ هَذِهِ
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba mtu alilala usiku kama mgeni kwa mtu mmoja katika Answaariy ambaye hakuwa na chakula isipokuwa chakula cha watoto wake akamwambia mkewe: “Laza watoto na zima taa karibisha wageni kwa (chakula) ulichonacho.” Ikateremka kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):
وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ﴿٩﴾
…na wanawapendelea kuliko nafsi zao japokuwa wao wenyewe wanahitaji. Na yeyote anayeepushwa na ubakhili na tamaa ya uchu wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu. [Al-Hashr: 9]
7. Sifa ya kumpendelea mwenzio imesawazishwa na iymaan kwa maana kuwa ikiwa Muislamu hatompendelea nduguye anachokipendelea yeye, basi iymaan yake itakuwa na utata.
http://bit.ly/2HTD0P1
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni