Katika mambo yenye kupendeza mbele ya Allah ni namna tunavyoinua mikono yetu kumuomba atutatulie shida na kutupa mahitajio yetu. Dua pia ni ibada kama ilivyokuja katika Hadithi aliyoipokea Imamu Ahmad: “Dua ni ibada.”
Kadhalika, yatupasa tufahamu kuwa, hakuna bahati mbaya katika dua ambayo unamuomba Allah, kama alivyothibitisha Allah alipomzungumzia Nabii wake Zakariya: “Akasema, ‘Mola wangu Mlezi! Mafupa yangu yamedhoofika, na kichwa kinameremeta kwa mvi; wala, Mola wangu Mlezi, sikuwa mwenye bahati mbaya kwa kukuomba Wewe.” [Qur’an, 19:4].
Kuwafikishwa na Allah katika kumuomba Yeye ni neema kubwa kabisa kwani siku zote hakuna ugumu katika kupokelewa dua bali ugumu ni katika sisi kuwafikishwa na Allah katika dua tuombazo na kujaalia ziwe zenye kufika kwake. Tunaweza kugawa kipengele hiki cha dua katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza ni mpokeaji (Istiqbaal), ambaye ni Allah na sehemu ya pili ni muombaji (Irsaaal).
Na kama tulivyosema, hakuna tatizo katika upokewaji wa dua kwani Allah ametutaka tumuombe na akaahidi kuwa atatuitikia dua zetu. Allah anasema: “Na Mola wenu Mlezi anasema, ‘Niombeni nitakuitikieni.’” Ama kuhusu muombaji wa dua (Irsaal), huyu ni binadamu ambaye pia ndiye mtendaji mkuu. Jambo muhimu hapa ni namna gani anatuma au kuomba dua zake ili zifike kwa Allah. Na hapa ndiyo penye tatizo.
Kwanini dua za baadhi yetu hazijibiwi?
Sababu kuu ya kutojibiwa dua zetu ni matatizo katika njia ya maombi (dua) kwani Mtume wa Allah alitubainishia masharti ili maombi yawe salama na yaepukane na mapungufu.
Alipata kuuliza Saad bin Abii Waqqas namna gani atakuwa ni mwenye kujibiwa dua zake? Mtume alimjibu: “Fanya uzuri katika chakula chako utakuwa ni mwenye kujibiwa dua….” [Twabraaniy]. Maana ya kauli hii ni, ajitahidi chumo lake chakula liwe la halali. Hili ndiyo sharti la msingi katika kujibiwa kwa dua.
Je, ni mahusiano gani yaliyopo baina ya utafutaji mzuri wa chakula na kujibiwa dua? Tunafahamu kuwa, chakula ndiyo hutengeneza seli za miili yetu. Pia, viungo tunavyotumia kuomba dua – ulimi, akili, moyo na mikono – vinategemea chakula.
Ikiwa viungo hivi tunavyotumia kuomba dua vimejengwa kwa haramu, ni kwa namna gani basi maombi yatafika kwa mpokeaji? Au yawaje viungio hivi vitume maombi halafu yawe sahihi? Ukweli ni kwamba, viungo vya namna hii haviwezi kutuma kwa usahihi maombi hayo na wala hayatapokelewa kwa sababu njia hiyo ina mapungufu.
Katika Hadithi nyingine aliyoipokea Muslim, inaelezea juu ya msafiri aliyepigwa na vumbi akawa ni mwenye kuinua mikono yake juu lakini chakula, kinywaji, mavazi – vyote ni vya haramu. Basi, ikahojiwa, ni kwa namna gani atajibiwa dua yake huyu?
Saad alipofahamu sharti hili la dua kujibiwa, alianza kujichunguza katika chumo lake na chakula chake; na hivi ndivyo walivyokuwa Maswahaba wa Mtume. Wao walitekeleza yale waliyoambiwa bila ya kusita. Katika moja ya majibu ya dua ya Saad, imekuja Hadithi katika Bukhari iliyoeleza tukio ambapo siku moja, bwana mmoja aliyeitwa Abuu Sa’adah alimshtaki kwa kumzulia uongo Saad bin Abii Waqqas kwa Khalifa wa wakati huo Umar bin Khattwaab. Wakati huo, Saad alikuwa ni mmoja wa viongozi katika mji wa Kufa.
Abuu Sa’adah alisema: “Saad siyo mtu mwenye kuwaangalia watu wake, hana uadilifu na usawa katika mambo na wala haendi vitani.” Saad akasema: “Ewe Allah, ikiwa anasema uongo mpe upofu, uurefushe umri wake na mdhihirishie fitna.”
Hakika, yalipita masiku na miaka, mtu yule akazeeka hadi kuwa kikongwe, anayesimama barabarani akiangalia wanawake wapitao. Akaambiwa: “Hivi huoni aibu hali ya kuwa wewe ni mzee na unafanya haya?” Akasema: “Nifanye nini Hakika imenipata dua ya Saad.” Hivi ndivyo athari ya dua ya Saad ilimpata Abuu Sa’adah kwa sababu ya aliyomzushia. Kadhalika, Umar Khattwaab (Allah amridhie) alipata kuomba katika hijja yake ya mwisho na Allah alimjibu. Aliomba: “Ewe Allah umedhoofika mwili wangu na wamezidi watu wangu. Ewe Allah, nijaalie Shahada katika njia yako na kuzikwa katika mji wa Mtume wako.”
Hakika, alifariki Umar katika sala ya Alfajiri akiwasalisha Waumini, na alizikwa siyo tu ndani ya mji wa Mtume bali ndani ya chumba cha Mtume. Hii yote inaonesha namna gani Maswahaba walivyojichunga katika machumo yao ili zijibiwe dua zao.
Baada ya kufahamu sharti muhimu ya kujibiwa dua zetu, tujiulize ni kwa kitu gani tumuombe Allah? Ili kuomba dua bora na zenye fadhila, inatakiwa kujua maneno muhimu ya kuombea, au kama umesahau maneno hayo kama alivyoandikwa, basi utumie maneno yako mwenyewe ukiunganisha na maneno yale muhimu.
Tuangalie kipengele hiki katika sehemu kuu tatu.
Dua zilizokuja ndani ya Qur’an
Hii ndiyo daraja ya kwanza kabisa na bora zaidi. Ipo mifano mingi ya dua hizi, miongoni mwa walizoomba Mitume wa Allah. Mfano, ukitaka kumuomba Allah msamaha, angalia namna Allah alivyomfundisha Nabii Adam. Anasema Allah Aliyetukuka: “Wakasema, ‘Mola wetu Mlezi! tumejidhulumu nafsi zetu, na kama hutatusamehe na kuturehemu, hakika tutakuwa katika wenye kukhasirika.” [Qur’an, 7:23].
Kama wewe ni mgonjwa, angalia dua aliyoiomba Nabii Ayub [Quran, 21:83]. Aliyepatwa na balaa na matatizo angalia namna gani Yunus alivyoomba [Qur’an, 21:87] na mfano wa hayo.
Dua zilizokuja katika Sunna.
Hizi ni dua alizotufundisha Mtume wa Allah, ikiwemo nyingi alizotufundisha tuombe ndani ya mwezi huu. Miongoni mwa dua hizo ni hii fupi lakini yenye maana pana, aliyofundishwa Mama Aisha alipomuuliza Mtume katika Hadithi iliyopokewa na Imamu Tirmidhy.
Dua inasema: “Allahuma innaka afuwwun tuhibbul afwaa fa -af annaa.”
Maana ya ‘Afuwwu’ ni ufutaji kabisa wa dhambi bila ya kubakia athari ya aina yoyote nayo ni daraja ya juu kuliko Maghfira. Maghfira ni kusitiri. Athari imebakia, lakini umesamehewa.
Dua katika tunachohitaji
Kisha tuombe katika kile tunachohitaji sisi kwa Allah, baada ya kufuatiliza daraja hizo mbili. Wengi katika
sisi tunatamani majibu ya dua zetu yawe haraka au hapo kwa hapo lakini siyo hivyo tunavyofikiria.
http://bit.ly/2HwzHi5
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni