Zakaah Ya Deni (Mwenye Kudai)
Wanachuoni wameigawa deni katika hali mbili.
1. Ikiwa anayedaiwa ni mtu tajiri au mtu muaminifu, deni hilo litachukuliwa mfano wa pesa zilizowekwa dhamana katika benki ambapo wakati wowote mtu anaweza kuzipata au ana uhakika wa kulipwa deni lake.
Katika hali hii zipo rai tatu.
a) Ya kwanza ni kuwa mwenye kudai anatakiwa ailipie mali hiyo Zakaah yake, juu ya kuwa halazimiki kuilipia mpaka pale atakapozipata na wakati huo atailipia pamoja na Zakaah ya siku zote za nyuma.
b) Ya pili ni kuwa analazimika kuilipia Zakaah yake kila unapotimia mwaka, kwa sababu pesa hizo zitahesabiwa mfano wa pesa zilizowekwa benki, na hii ni kwa sababu aliyekopeshwa ni mtu tajiri au muaminifu kiasi cha kuwa ana uhakika wa kulipwa au wa kuzipata pesa zake hizo wakati wowote ule anapozitaka.
c) Rai ya tatu ni kuwa hazilipii mpaka pale atakapolipwa deni hilo, na hapo atazilipia Zakaah ya mwaka ule mmoja tu.
Anasema Imaam Muhammad bin Uthaymiyn (Rahimahu Allaah):
"Rai ya mwanzo, nayo ni kuilipia Zakaah ya miaka yote pale atakapozipata pesa zake ni bora zaidi na inakubalika zaidi".
2. Ikiwa anayedaiwa ni mtu masikini au mtu asiyekuwa muaminifu, haimuwajibikii mwenye kudai kuzitolea Zakaah pesa hizo mpaka atakapozipata na kubaki nazo muda wa mwaka mzima kisha atazilipia Zakaah ya mwaka huo tu, ambao mali yake hiyo ilibaki kwake kama kawaida ya utoaji wa Zakaah.
Anasema Imaam Muhammad bin Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)::
"Haijuzu kumdai au kumlazimisha mtu masikini au kumshitaki na hatimaye kumuingiza jela na kumtenganisha na watu wake ikiwa mtu huyo kweli hana uwezo wa kulipa deni, na ikiwa mtu huyo hafanyi ujanja wa kuchelewesha makusudi, na badala yake tunatakiwa tumsitahamilie mpaka pale Allaah Atakapomfariji.
Allaah Anasema:
وَإِن كَانَ ذُو عُسْرَةٍ فَنَظِرَةٌ إِلَى مَيْسَرَةٍ وَأَن تَصَدَّقُواْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ وَاتَّقُواْ يَوْمًا تُرْجَعُونَ فِيهِ إِلَى اللّهِ ثُمَّ تُوَفَّى كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لاَ يُظْلَمُونَ
"Na kama (mkopi) ana dhiki, basi (mdai) angoje mpaka afarijike, na kama nyinyi (mnaodai mkizisamehe deni zenu) mkazifanya Swadaqah, basi ni bora kwenu. Ikiwa mnajua haya (basi fanyeni).
Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Allaah, kisha viumbe wote watalipwa kwa ukamiliyote waliyoyachuma, nao hawatadhulumiwa".
[Al-Baqarah: 280-281]
Mtu akisema:
"Pesa zangu kwanini nisizidai?", Anaendelea kusema Imaam Ibn ‘Uthaymiyn,
"Tunamwambia:
Ni kweli pesa zako, lakini wewe mwenyewe ndiye uliyemkopesha pesa hizo. Pale alipokujia kutaka kukukopa ungelimtafutia udhuru wowote ule, kisha ukampa kiasi chochote cha mali ikiwa kama ni msaada (Swadaqah) tu kutoka kwako, basi yasingekukuta haya. Lakini umkopeshe na hali unajuwa kuwa mtu huyu ni masikini, kisha akishindwa kukulipa ukamshitaki, umtie jela na kumtenganisha na mke na watoto wake, jambo hilo ni haramu kabisa na haijuzu kwa Muislam kulitenda".
[Mwisho wa maneno ya Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)].
http://bit.ly/30vyG0X i live islam
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni