Wanaostahiki kupewa Zakaah
Swadaqah ya kawaida, anapewa mtu yeyote hata akiwa si Muislam, ama Zakaatul Fitwr wanapewa watu wa aina mbili tu, nao ni masikini na mafakiri Waislam.
Zakaatul Maal (Zakaah ya mali), hii wanapewa aina 8 tu ya Waislamu waliowataja na Allaah katika kitabu chake kitukufu Aliposema:
إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاء وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِّنَ اللّهِ وَاللّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ
"Swadaqah hupewa (watu hawa):-
1. Mafakiri na
2. Masikini na
3. Wanaozitumikia na
4. Wanaotiwa nguvu nyoyo zao (juu ya Uislam) na
5. Katika kuwapa uungwana watumwa na
6. Katika kuwasaidia Wenye deni na
7. Katika (kutengeneza) Mambo aliyoamrisha Allaah na
8. Katika (kupewa) Wasafiri (walioharibikiwa).
Ni faradhi inayotoka kwa Allaah, na Allaah ni Mjuzi (na) Mwenye hikima".
At-Tawbah: 60.
Ayakayeichunguza aya hii ataona kuwa Allaah ametumia neno 'Lil' katika kuwataja watu aina nne wa mwanzo wanaostahiki kupewa Zakaah. Na hii inaitwa Laam ya tamliyk, na maana yake ni kuwa lazima kuwamilikisha watu wa aina nne wa mwanzo (yaani kuwapa mikononi mwao) Zakaah yao.
Allaah Anasema:
إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاء وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ
Ama katika aina nne waliobaki, Allaah ametumia neno 'Fiy'. Na kwa kutumia neno hilo Allaah hatulazimishi, kuwamilikisha kwa kuwapa Zakaah yao mikononi mwao.
Allaah Anasema:
وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ
Kwa hivyo katika aina nne za mwisho, kwa mfano kama unataka kumsaidia mwenye deni, hulazimiki kumpa pesa hizo mkononi mwake, bali unaweza kwenda kumlipia deni hilo moja kwa moja bila ya kumkabidhi mdaiwa huyo pesa hizo mkononi mwake. Hata hivyo, ukitaka unaweza pia kumkabidhi mweyewe mkononi mwake.
Ukitaka kuzitumia pesa za Zakaah katika njia ya Allaah, unaweza kununua kwa mfano silaha na kuwakabidhi wapiganaji 'Mujaahidiyn' au unaweza kuzitumia katika njia ya Allaah bila ya kumkabidhi mtu pesa hizo mkononi mwake, wakati huo huo unaweza ukitaka kuwakabidhi wanaohusika au wajuzi ili ipate kutumika kwa usahihi zaidi.
Mafakiri Masikini
Juu ya kuwa watu wamehitalifiana juu ya nani masikini na nani fakiri, lakini kwa ujumla hawa ni watu ambao wanachokipata hakiwatoshi katika matumizi yao ya kila siku.
Mtu anaweza kuwa masikini hata kama anapata mshahara mkubwa lakini wakati huo huo ana watoto wengi au wazee na ndugu wanaomtegemea anaowajibika kuwatizama, au ana madeni kiasi ambapo juu ya kuwa anapata mshahara mkubwa, pesa hizo hazimtoshi kuwalisha watu wake hao.
Kwa ajili hiyo juu ya tofauti iliyopo baina ya masikini na fakiri katika sharhi yake, lakini katika kuhitajia kwao msaada, wote wawili wapo katika hali moja.
Zipo Hadiyth zinazotujulisha kuwa wapo baadhi ya masikini wenye kustahi kuombaomba juu ya shida kubwa walokuwa nazo. Waislam wanatakiwa wawachunguze watu wa aina hii na kuwasaidia na wasiwaache mpaka hali zao zikawa mbaya.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"Masikini si yule anayeomba akapewa tende moja au mbili akaondoka, au tonge moja au mbili, lakini masikini wa kweli ni yule anayejizuwia. Someni mkitaka (kauli ya Allaah isemayo):
التَّعَفُّفِ تَعْرِفُهُم بِسِيمَاهُمْ لاَ يَسْأَلُونَ النَّاسَ إِلْحَافًا
"Utawafahamu kwa alama zao hawawaombi watu wakafanya ung'ang'anizi".
Anayepewa Zakaah ni Masikini au Fakiri Muislam tu, ama Masikini au Fakiri asiyekuwa Muislam hapewi katika mali ya Zakaah, na kama Fakiri asiyekuwa Muislam atahitajia msaada, basi atapewa katika mali ya Swadaqah na si ya Zakaah.
Wenye Kuzitumikia
Wanaozitumikia Zakaah ni wale waliopewa jukumu la kuipokea, kuikusanya kutoka kwa matajiri na wenye kazi ya kuihifadhi, waandishi, na wenye kuigawa, wakiwemo wachungaji wa wanyama wa Zakaah.
Ili waweze kupewa katika Mali ya Zakaah, watu hao lazima wawe Waislam, na wasiwe katika wale walioharamishwa kupokea Zakaah katika watu wa Ahlul Bayt ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Banu 'Abdil-Muttalib ambao tutawataja baadaye.
Katika wanaoitumikia Zakaah, hata akiwa mtu tajiri basi anastahiki kupewa katika mali hiyo, na ikiwa mtu wa aina hiyo amepewa na wakubwa wanaohusika na akawa hana haja nayo mali hiyo, basi aichukuwe na kuwagawia anaowataka au kumnunulia zawadi anayemtaka.
Imepokelewa kuwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipokuwa akifanya kazi ya kukusanya mali ya Zakaah, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa katika mali hiyo.
‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:
"Mimi najitolea tu na sina haja ya kulipwa, mpe mwenye kuzihitajia zaidi kuliko mimi".
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
"Alichokupa Allaah katika mali hii bila ya wewe mwenyewe kuiomba, uichukue na uitumie au itolee Swadaqah."
[Al-Bukhaariy na An-Nasaaiy]
Wenye Kutiwa Nguvu
Hawa ni watu wanaopewa katika mali ya Zakaah kwa ajili ya kulainishwa nyoyo zao na kutiwa nguvu kutokana na udhaifu wa nyoyo hizo, na wengine hupewa kwa ajili ya kuwaepusha Waislam na shari zao, au kuwavutia katika kuupenda Uislam na kuupa nguvu.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwapa wakubwa wa makabila ya kiarabu na hasa makabila ya kibedui kwa ajili ya kuwapendekeza katika Uislam.
Imepokelewa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa mtu mmoja aitwae Swafwaan bin Umayyah ngamia wengi sana katika ngamia wa ngawira waliopatikana katika vita vya Hunain, na Safwan huyu alikuwa mkubwa wa kabila lake.
Safwaan alikuwa wakati huo bado hajasilimu, na alipopewa mali hiyo, akarudi kwa watu wake na kuwaambia:
"Enyi watu wangu, ingieni katika dini ya Kiislam, kwani Muhammad anatoa utoaji wa mtu asiyeogopa ufakiri".
(Mwenye kuchunguza, ataona kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwatendea makabila ya Kibedui tofauti na anavyowatendea watu wa mijini. Alikuwa akiwachukulia kwa akili zao. Na hii ni kwa sababu Mabedui ni watu wagumu sana kufahamu. Hata katika kuuliza masuali, Mabedui walikuwa wakimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) masuali na kujibiwa, wakati masuali hayo hayo wangeuliza Maswahaba wanaokaa mjini (Radhwiya Allaahu ‘anhum), basi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angekasirika nayo masuali hayo).
Wakati wa ukhalifa wake Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akiendelea kuwapa watu wa aina hii, lakini ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) siku moja alikataa kutoa, akawaambia:
"Hii Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikupeni kwa ajili ya kuzizowesha nyoyo zenu na kuzilainisha, lakini sasa Allaah amekwishautukuza Uislam na hatuna haja nanyi tena, mkitaka ingieni katika Uislam, na kama hamtaki basi baina yetu na baina yenu ni panga. Allaah Amesema:
وَقُلِ الْحَقُّ مِن رَّبِّكُمْ فَمَن شَاء فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاء فَلْيَكْفُرْ
"Na sema; 'Huu ni ukweli ulotoka kwa Mola wenu, basi anayetaka na aamini na anayetaka na akufuru.”
Al-Kahf: 29
Anasema Sayyid Saabiq katika Fiqhis Sunnah:
"Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikubaliana na ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) katika uamuzi wake huo, na hapana hata Sahaba mmoja (Radhwiya Allaahu ‘anhum) aliyepinga. Na hii ni katika Ijtihadi zake ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na hata makhalifa waliokuja baada yake, Uthmaan na Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhum) hawakuwapa tena watu wa aina hii katika mali ya Zakaah.
Hata hivyo," anaendela kusema Shaykh Saabiq, "hii haimaanishi kuwa watu wa aina hii wasipewe, na Imaam yeyote yule atakayetawala na akaona kuwa ipo haja ya kuwapa watu wa aina hii, basi atawapa kwa sababu dalili ipo katika Qur-aan na Sunnah.”
Katika Kugomboa
Uislam umeijaalia ‘Ibaadah hii ya kuwagomboa mateka na watumwa kuwa ni kitendo kinachompatia mtu thawabu nyingi sana na kumuingiza katika Pepo za Allaah Subhanaahu wa Ta’ala.
Kutoka kwa Al-Barra-a (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:
"Mtu mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia:
"Nijulishe juu ya amali (njema) itakayonikurubisha na Pepo na kunibaidisha na Moto".
Akasema:
"Waachie huru watu na wagomboe watumwa".
Akauliza (tena):
"Ewe Mtume wa Allaah, si yote hayo yanabeba maana moja tu?"
Akasema:
"La, (sivyo), 'kuwaachia huru' ni kujihusisha peke yako katika kuwaacha huru, na 'kuwagomboa' ni kusaidia katika kulipa thamani ya kuwagomboa".
[Ahmad na Ad-Daaraqutniy].
Wakati ule ilikuwa mtumwa anaweza kuandikiana na kukubaliana kuwa atakapoweza kulipa malipo fulani katika muda fulani, ataachwa huru. Kwa hivyo Waislam walitakiwa wawasaidie watu wa aina hiyo kwa kuwalipia kiasi hicho ili waweze kujigomboa.
Kumsaidia Mwenye Deni
Hawa ni wale wenye madeni makubwa wakashindwa kuyalipa kutokana na kula hasara katika biashara zao nk. Sharti madeni hayo yawe katika mambo ya halali au yatokane na maasi aliyotubu nayo mtu huyo.
Imepokelewa kutoka kwa MaImaam Ahmad na Abuu Daawuwd na Ibn Maajah na At-Tirmidhiy, kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:
"Mas-alah (ya kuwasaidia wenye madeni), hayawi halali isipokuwa katika mambo matatu; aliye fakiri sana, au mwenye deni zito sana, au mwenye kudaiwa damu (ya diya - fidiya).”
(Huyu ni mtu aliyejikuta amebebeshwa deni la diya kutokana na ndugu yake au jamaa yake aliyeuwa kwa bahati mbaya. Ikiwa hajalipa diya hiyo, basi ndugu yake huyo au jamaa yake atauliwa kwa ajili ya kulipa kisasi)
Katika Kutengeneza
(Fiy sabiyli-LLaah), Maulamaa wengi wanasema kuwa haya ni mambo yanayohusiana na vita vya Jihadi tu pamoja na watu wanaopigana vita hivyo.
Hawa wana sehemu yao katika mali ya Zakaah wanayopewa hata kama askari mpiganaji Jihadi ni tajiri anayejiweza.
Vitu vinavyonunuliwa kutokana na pesa za Zakaah kwa ajili ya vita, kama vile farasi, panga, n.k. lazima virudishwe katika nyumba ya hazina ya Waislam (Baytul maal) baada ya kumalizika kwa vita.
Kadhaalika, Maulamaa wengi wanaonelea kuwa kusaidia mtafutaji elimu ya Dini "Twaalibul-'Ilm" inaingia katika "Fiy sabiylil-LLaah". Na utafutaji elimu ya Dini ni katika jambo tukufu sana.
Katika Kupewa Wasafiri
Msafiri aliyeishiwa na pesa akawa hana njia nyingine ya kupata pesa za matumizi, huyu anapewa katika mali ya Zakaah, sharti safari yake hiyo iwe katika mambo ya twa'a na si katika kumuasi Mola wake, hata akiwa msafiri huyo huko kwao alikotoka ni mtu tajiri mwenye mali nyingi.
http://bit.ly/2VwtRkw i live islam
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni