Translate

Ijumaa, 31 Mei 2019

Ni Sunnah kuswali Rak´ah mbili baada ya ´Aswr

Ni Sunnah kuswali Rak´ah mbili baada ya ´Aswr



Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) haachi Rak´ah mbili kabla ya Fajr na Rak´ah mbili baada ya ´Aswr.

Ameipokea Ibn Abiy Shaybah katika ”al-Muswannaf” (2/352): ´Affaan ametuhadithia: Abu ´Awaanah ametuhadithia: Ibraahiym bin Muhammad bin al-Muntashir ametuhadithia, kutoka kwa baba yangu ambaye alikuwa akiswali Rak´ah mbili baada ya ´Aswr. Wakati alipoulizwa akasema:

”Nisingeziswali isipokuwa ni kwa sababu nilimuona Masruuq akiziswali, pamoja na kwamba alikuwa ni mtu mwaminifu. Lakini nikamuuliza ´Aaishah kuhusu jambo hilo ambapo akasema:

”Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) haachi Rak´ah mbili kabla ya Fajr na Rak´ah mbili baada ya ´Aswr.”

Miongoni mwa makosa yaliyoenea katika vitabu vya Fiqh ni pale wanapokataza Rak´ah mbili hizi bali na kutozitaja miongoni mwa jumla ya Sunnah za Rawaatib, pamoja na kwamba zimethibiti kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akidumu kwazo kama ambavyo alikuwa akidumu kuswali Rak´ah mbili za kabla ya Fajr. Hakuna dalili yoyote inayoonyesha kuwa zimefutwa au kwamba ni mambo maalum kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pekee. Ni vipi iwe hivyo ilihali mjuzi zaidi wa watu alikuwa akizihifadhi, naye si mwengine ni mama wa waumini ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa), na Maswahabah na Salaf wengine walioafikiana naye?

Aidha inatakiwa kutambulika kwamba zile Hadiyth zilizokuja kwa jumla zinazokataza kuswali baada ya ´Aswr zimekuja kwa njia iliyofungamana kwa Hadiyth zengine Swahiyh ambazo zimesema wazi kwamba inafaa kuswali midhali jua bado halijakuwa manjano. Moja katika Hadiyth hizo ni ile ya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) inayosema:

”Msiswali baada ya ´Aswr isipokuwa mkiswali jua liwe limeshainuka.”

Hadiyth ni Swahiyh na imepokelewa kwa njia nyingi.



Rejea Kitab Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (7/1/528)



Jumanne, 28 Mei 2019

Siku Kumi Za Mwisho Za Ramadhwaan


عَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ : "كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا دَخَلَ الْعَشْرُ أَحْيَا اللَّيْلَ وَأَيْقَظَ أَهْلَهُ وَجَدَّ وَشَدَّ الْمِئْزَرَ" رواه البخاري (2024) ومسلم (1174)
Imepokelewa kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa pindi zilipoinga kumi za mwisho, akikesha usiku na akiamsha ahli zake na akijitahidi na kukaza shuka yake." [Al-Bukhaariy, Muslim]
     
Hadiyth hii ni uthibitisho kuwa siku kumi za mwisho za Ramadhwaan zina fadhila mahsusi na adhimu kuliko siku nyenginezo ambazo Muislamu inampasa aongeze utiifu na kutekeleza ‘ibaadah kama kuswali, kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kusoma Qur-aan.

‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amtuelezea hali ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inavyokuwa kama ni mfano bora kabisa kwa sifa nne zifuatazo:

1-Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikesha katika ‘ibaadah.

Alikuwa halali usiku. Kwa hiyo yeye Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikesha usiku mzima kufanya ‘ibaadah na akihuisha nafsi yake kwa kutumia usiku wake kukaa macho na kuachakulala. Hii ni kwa vile kulala usingizi ni mauti madogo. Maana ya "akihuisha (akikesha usiku)" ni kwamba yeye Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitumia wakati huo katika hali ya Qiyaam (kusimama kuswali usiku) na kufanya ‘ibaadah ambazo zinatendwa kwa ajili ya Allaah, Rabb wa walimwengu. Inatupasa tukumbuke kuwa siku kumi za mwisho za Ramadhwaan ni chache zilizokadariwa kwa idadi.

Ama kuhusu ilivyonukuliwa katika Hadiyth ya 'Abdullaah Ibn ‘Amr, imekatazwa kukesha usiku mzima katika Swalaah, hii inahusu mtu anayefanya hivyo kwa mfululizo wa siku zote za mwaka.

  
2-Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiamsha ahli zake.

Ni wake zake waliotakasika ambao ni Mama wa Waumini, ili nao wanufaike katika ‘ibaadah hizo za kumdhukuru Allaah na ‘ibaadah nyenginezo katika siku hizo zenye baraka nyingi.


3-Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya bidii.

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akijizuia na akijitahidi sana katika ‘ibaadah, akiongeza ‘amali njema zaidi kuliko alivyokuwa akifanya siku ishirini za mwanzo (wa Ramadhwaan). Akifanya hivi kwa sababu Laylatul-Qadr inatokea katika usiku mmoja wa siku hizo kumi.  


4-Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikaza shuka yake.

Alikuwa akijihimiza na kufanya bidii kubwa katika ‘ibaadah nzito. Inasemekeana vile vile Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akijitenga na wake zake. Hii ni kauli iliyo sahihi zaidi kwa vile inakubaliana na ilivyotajwa kabla katika Hadiyth ya Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikunja kitanda chake na akijitenga na wake zake" [Latwaaif-ul-Ma'aarif, Uk. 219]

Vile vile Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya I'tikaaf katika siku za mwisho za Ramadhwaan na watu wenye kuwa katika hali ya I'itikaafhujizuia kujamii na wake zao.

Kwa hiyo enyi ndugu Waislamu, jitahidini kujizoesha na kuwa katika sifa na khulka hizi. Na tekelezeni Swalaah za usiku pamoja na Imaam hata baada ya kuswali Taraawiyh ili jitihada zenu katika siku hizi kumi za mwisho zipindukie siku ishirini za mwanzo na ili mpate kufaulu kupata sifa ya "kuuhuisha usikukwa ’ibaadah" kwa kuswali. 

Na ni lazima muwe na subira katika utiifu wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na ‘ibaadah za usiku kwani hakika Tahajjud ni ngumu lakini thawabu zake ni kubwa sana. Naapa kwa Allaah, ni fursa kubwa katika maisha ya Muislamu na vile vile ni faida kubwa kuitumia fursa hii kwa yule aliyejaaliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Kwani mwana Aadam hawezi kujua kama ataweza kuchuma tena thawabu nyingi kama hizi, ambazo zitamfaa katika maisha yake ya dunia na ya Aakhirah. 

Salafus-Swaalih (Wema waliotangulia) wa Ummah huu walikuwa wakijitahidi katika ‘ibaadah za masiku haya kwa kuzirefusha Swalaah za usiku. As-Swaa'ib bin Yaziyd amesema, "'Umar bin Al-Khattwaab alimuamrisha Ubay bin Ka'ab na Tamiym Ad-Daariy kuimamisha watu katika Swalaah kwa Raka'ah kumi na moja. Imaam alikuwa akisoma Aayah mia moja hadi ilibidi tuegemee mkongojo kwa sababu ya kisimamo kirefu, natulikuwa hatupumziki hadi inapoanza kuingia Alfajiri".  [Al-Muwattwa, Mjalada 1, Uk. 154]

'Abdulllaah Bin Abiy Bakr amesema "Nimemsikia baba yangu akisema, wakati wa Ramadhwaan, tulikuwa tukichelewa  kumaliza Swalaah za usiku hata tukiwahimiza watumishi kutuwekea suhuwur (daku) kwa kuogopa Alfajiri isitufikie"  [Muwattwa ya Imaam Maalik, Mjalada 1, Ukurasa 156]

Nafsi ya Muumini inapambana na jitihada mbili katika Ramadhwaan; Jitihada ya mchana kwa swiyaam na jitihada ya usiku kwa Qiyaam. Kwa hiyo yeyote atakayejumuisha jitihada mbili hizi na akatimiza haki zake, basi yeye atakuwa miongoni mwa wenye subira kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ﴿١٠﴾
  Hakika wanaosubiri watalipwa kikamilifu ujira wao bila ya hesabu. [Az-Zumar: 10]

Siku kumi hizi ni za mwisho katika mwezi mtukufu huu, na ‘amali za Muislamu zinazohesabika zaidi ni zile za mwisho, kwa sababu huenda akafaulu kukutana na usiku wa Laylatul-Qadr wakati akiwa amesimama katika Swalaah ikawa ni fursa nzuri ya kufutiwa madhambiyake yote na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

Ni wajibu wa kila mtu kuamsha na kuhimiza na kushurutisha familiayake kutekeleza ‘ibaadah khasa nyakati hizi tukufu, kwani hakuna atakayedharau kufanya hivi ila yule aliyenyimwa fadhila hizi.  Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba wakati wengine wako katika ‘ibaadah khasa za masiku haya kumi, wengine wanatumia wakati wao katika vikao vya maasi. Hakika hii ni khasara kubwa.

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atuhifadhi na Atuhidi. 

Kwa hiyo Muislamu atakayejishughulisha na ‘ibaadah katika siku kumi hizi za mwisho atakuwa amejiingiza katika milango ya kuchuma mema yaliyobakia katika mwezi huu mtukufu. Ni khasara kwa mtu aliyeanza mwezi wa Ramadhwaan kusimama kwa nguvu kuswali, kusoma Qur-aan na dhikru-Allaah kisha siku za mwisho akawa na mzito na mvivu katika kufanya ‘ibaadah na hali hizi siku za mwisho ndio siku muhimu na zenye uzito wa thawabu za kusimama kuswali na kadhaalika kuliko zote. Hivyo kila mmoja inampasa aongeze bidii zaidi na kujitahidi kwa kadiri awezavyo kuongeza ‘ibaadah katika kumalizia mwezi mtukufu huu. Na kukumbuka kuwa ‘amali za mtu zinahesabika zile za mwisho.

Du’aa ya Laylatul-Qadr:

Katika siku hizi kumi za mwisho ni vizuri sana kuisoma du'aa hii kila mara khasa katika usiku wa Laylatul-Qadr kama ilivyothibiti katikaHadiyth ifuatayo:

عَنْ عَائِشَةَ أَنَّهَا قَالَتْ : يَا رَسُولَ اللَّهِ  أَرَأَيْتَ إِنْ وَافَقْتُ لَيْلَةَ الْقَدْرِ مَا أَدْعُو؟ , قَالَ : ((تَقُولِينَ : اللَّهُمَّ إِنَّكَ عَفُوٌّ تُحِبُّ الْعَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي))  ابن ماجه و صححه الألباني
Imepekelewa kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema: “Ee Rasuli wa Allaah! Je nitakapojaaliwa kufikia Laylatul-Qadrniombe nini?" Akasema, ((Sema: Allaahumma Innaka 'Afuwwun Tuhibbul-'Afwa fa'fu 'anniy - Ee Allaah Hakika Wewe Ndiye Mwenye Kusamehe Unapenda Kusamehe basi Nisamehe)) [Ibn Maajah na kaisahihisha Al-Albaaniy]     

Na  Allaah  anajua  zaidi


Swalah ya Uzushi katika Kumi la Mwisho Wa Ramadhaan

SWALI

Assalam allaykum warahmatullahi
Kwanza napenda kuwapongeza wote wanaoshiriki katika kazi hii ya kuelimisha umma wa kiislam hasa kwa sisi ambao tuko kwenye nchi hizi za kimagharibi . Ahsanteni sana na allah atawajaza majazo mema leo duniani na kesho akhera. Suali langu ni hili tokea kukaribia kumi la mwisho la mwezi huu mtukufu wa ramadhan nimekuwa napokea email kutoka watu mbali mbali zinazoelezea kuhusu sala ya laylatul Qadri ambayo husaliwa  kwa rakaa zaidi ya kumi na moja pamoja sura zake maalum  kwa kila siku (yaani kila siku na sura zake maalum) kwa mfano kuna siku usome sura zinazoanza na haa mim na nyenginezo pia ikiwemo salatul tasbihi. hivyo naomba nasaha zenu watu wa alhidaaya kwani tumo ndani utata mkubwa waislam. Assalam alaykum warahmatullhi
Barua yenyewe ni hii:
ASSALAM ALAYKUM,
NDUGU ZANGU WAISLAM NAWAOMBA TUFANYE BIDII NA JITIHADA NA KUHAKIKISHA
KILA MMOJA WETU ANATEKELEZA SALA HII PINDI HALI IKIMRUHUSU, INSHAALLAH.
TAREHE 21 USIKU - MWEZI WA RAMADHANI
a) USIKU WA TAREHE 21 SALI RAKAA 4, TOA SALAM KILA BAADA YA RAKAA 2. KILA RAKAA SOMA SURAT FAT-HA x 1, AL-QADIR x 1 NA IKHLAS x 1 UKIMALIZA MSALIE MTUME (S.A.W) x 70.
b) USIKU HUO HUO - SALI RAKAA 2, KILA RAKAA SOMA SURAT FAT-HA x 1,
AL-QADIR x 1 NA IKHLAS x 3. BAADA YA SALAM VUTA URADI
UFUATAO:
"ASTAGHGIRULLAHI LLADHI LAILAHA ILLA HUWA
WAATUBU ILAYHI" x 70.
c) VILE VILE USIKU HUO HUO WA TAREHE 21 SOMA SURAT QADR x 21.
 USIKU WA TAREHE 23 - MWEZI WA RAMADHANI
a) SALI RAKAA 4(MBILI MBILI), KILA RAKAA SOMA SURAT FAT-HA x 1,
AL-QADIR x 1 NA IKHLAS x 1. BAADA YA SALAM MSALIE MTUME (S.A.W) x 70.
b) USIKU HUO HUO - SALI RAKAA 8 (MBILI MBILI), KILA RAKAA SOMA SURAT FAT-HA x 1, AL- QADIR x 1 NA IKHLAS x 1. UKIMALIZA VUTA URADI UFUATAO:
"SUB-HANA LLAHA WALHAMDULLILLAHI WALAILAHA ILLALLAHU WALLAHU AKBARU" x 70.
c) VILE VILE USIKU HUO HUO WA TAREHE 21 SOMA SURAT YASEEN x 1 NA ARRAHMAN x 1.

USIKU WA TAREHE 25 - MWEZI WA RAMADHANI
a) SALI RAKAA 4 (MBILI MBILI), KILA RAKAA SOMA SURAT FAT-HA x 1,
AL-QADIR x 3 NA IKHLAS x 3. BAADA YA SALAM LETE ISTIGHFARA
"ASTAGHFIRULLAHI LLADHI LAILAHA ILLA HUWA WAATUBU ILAYHI" x 70.
(Sala hii ni nzuri kwa kusamehewa dhambi zako).
b) USIKU HUO HUO - SALI RAKAA 2, KILA RAKAA SOMA SURAT FAT-HA x 1,
AL- QADIR x 1 NA IKHLAS x 15. UKIMALIZA SOMA "LAILAHA ILLALLAH MUHAMMAD RASULULLAH"
c) VILE VILE USIKU HUO HUO WA TAREHE 25 SOMA SURAT DUKHAN x 7
UNAEPUSHWA NA ADHABU YA KABURINI. VILE VILE SOMA SURAT FAT-HA x 7.
 USIKU WA TAREHE 27 - MWEZI WA RAMADHANI
 a) SALI RAKAA 4 (MBILI MBILI), KILA RAKAA SOMA SURAT FAT-HA x 1,
AL-QADIR x 3 NA IKHLAS x 50. BAADA YA KUTOA SALAM SUJUDU NA USOME:
 SUB-HANA LLAHA WALHAMDULLILLAHI WALAILAHA ILLALLAHU WALLAHU AKBARU.
Kisha omba haja zako kwa Mola wako (yeye ndie mtoaji).
 b) USIKU HUO HUO SOMA SURA SABA (7) ZENYE KUANZA NA "HAAMMIIM". PIA
SOMA SURAT "MULK"x 7.
SALAT TAS-BIHI.
VIZURI KUSALIWA MWEZI WA RAMADHAN NA HASA TAREHE 26.
KUMI LA MWISHO LA RAMADHAN:
a) KILA SIKU SOMA "LAILAHA ILLA-LLAH SADIQAN LAILATUL QADR".
b) VILE VILE KATIKA KUMI HILI KILA SIKU BAADA YA SALA YA ISHAA SOMA
SURAT
QADR x 7.

IJUMAA LA MWISHO WA MWEZI WA RAMADHANI KABLA YA SALA YA ADHUHURI SOMA
SURAT QADR x 3.
 1. BAADA YA SALA YA ADHUHURI/IJUMAA SALI RAKAA 2:
RAKAA YA KWANZA SOMA SURAT FAT-HA x 1, IKHLAS x 10,
ZULZILAT x 1.
RAKAA YA PILI SOMA SURAT FAT-HA x 1, ALKAFIRUN x 3. BAADA YA SALAM
MSALIE MTUME (SAW) x 10, BAADAE
 2. SALI RAKAA 2 NYENGINE:
RAKAA YA KWANZA SOMA SURAT FAT-HA x 1, TAKATHUR x 1, IKHLAS x 10.
RAKAA YA PILI SOMA SURAT FAT-HA x 1, AYATUL KURSIYYU x 3, IKHLAS x 25
(Thawabu za sala hii zinaendelea
mpaka siku ya kiama).

NDUGU MUISLAM, TUPATE NINI TENA KUTOKA KWA MOLA WETU, KILA YA NJIA YA KUJJIPATIA MEMA AMETUWEKEA.

MTUMIE NA MUISLAM MWENZIO IKIWA NI MWENYE KUAMINI NA MWENYE IMANI YA
KWELI.WAALAYKUM SSALAAM.


JIBU



Naam kwa Hakika ndugu Waislamu, kutokana mitandao ya jamii siku hizi uzushi mwingi umekuwa unarushwa na kuwafikia Waislamu wengi ambao nao bila ya kujua wanapata mafunzo yasiyo sahihi, nao wanawatumia wenzao, hivyo hivyo inaendelea hadi kuwafikia maelfu wa Waislamu.

Yafutayo ni maelezo tunayowatahadhirsha ndugu zetu wote kuhusu ujumbe huu:


1-Si Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) bali ni maneno yaliyopangwa na baadhi ya watu.  

2-Ibada yoyote ile kwa mpangilio wa idadi na namba, inahitaji ushahidi na dalili. Zikikosekana basi inatupasa kuziacha na kutozifanyia kazi.

3-Ujumbe kama huo unaorushwa hakika unwashughulisha sana Waislam na wengi wakihadaika wakidhani ni mambo ya Dini na hali ni mambo yasiyokuwepo na yaliyotungwa tu na watu.

4-Inawasababisha pia Waislam kukosa kheri na fadhila za kufanya ibada zilizothibiti zenye dalili ambazo zingewaongezea ujira mkubwa haswa katika masiku haya matukufu ambayo tumesisitizwa sana kuongeza juhudi katika ibada.

Tunatoa nasaha kwa ndugu zetu katika Iymaan musiwe na haraka ya kueneza mambo ambayo yanadhaniwa ni Hadiyth au mafunzo ya Dini na hali ni utungo tu kutoka kwa wasio na kazi ila kuwashughulisha watu na kuwapotezea muda wao kwa mambo ambayo hayawezi kuwapatia ujira bali watarudishiwa wao na kutopata kitu zaidi ya kupoteza muda. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kapinga hilo sana na kalikemea vikali pale aliposema:
(Mwenye Kuzusha jambo katika DINI yetu hii, basi litarejeshwa kwake) [Al-Bukhaariy na Muslim]. Yaani hatopata kitu zaidi ya kuua muda wake na kujichosha bure!

Tujihadhari na ujumbe tupatazo kwenye mitandao ya kijamii kwani nyingi huwa ni za kutungwa jambo ambalo ametukaza nalo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((من كذب علي متعمدا فليتبوأ مقعده من النار)) متفق عليه
((Atakayeniongopea makusudi basi ajitayarishie makazi yake motoni))  [Al-Bukhaariy Na Muslim]

Tambueni kuwa ujumbe wowote unaoonekana wa kidini kama huo ni kujiepusha nao kwa sababu  hauna dalili, wala ushahidi kuliposemwa maneno hayo, nani kasema? Wapi kasema? Nani kapokea, Vitabu gani n.k!

Madhara makubwa huwafikia Waislamu kuupokea ujumbe kama huo kwani utakuwa wangapi wameshaanza kuuhifadhi na kuusoma na kuufanyia kazi kwa kuswali Swalah hizo na kuacha kuswali Swalah zilizothibiti, au kusoma Qur-aan na mengine yenye ushahidi.

Na Allaah Anajua zaidi


Je,Inafaa Kufanya Adhkaar Nyumbani Kumi La Mwisho Ramadhwaan Ikiwa Siruhusiki Kwenda Msikitini?

SWALI

Mimi huwa nakaa macho na kusoma kuran na kuswali tahjud, kuomba dua, kumtaja Allah kwa adkhaar katita kumi la mwisho wa mwezi wa ramadhani nikiwa nyumbani je ninafanya makosa? Nimesoma kwenye alhidaaya kuwa itikafu haikaliwi nyumbani je nifanye nini nami nataka kupata dhawabu zake na msikiti wetu hawaruhusiwi wanawake kukesha.


JIBU


Naam kwa Hakika ni kuwa adhkaar unaweza kuleta mahali popote na wakati wowote ule isipokuwa chooni lakini I‘tikaaf haifanywi isipokuwa katika Msikiti. 

Jambo linalotakiwa kutoka kwenu ni kuweza kuzungumza na Imaam kuhusu kuruhusiwa kwa wanawake kufanya I’tikaaf kama walivyofanya Maswahaba wa kike (Radhwiya Allaahu ‘anhunna) wakati wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakiwemo wakeze.

Ikiwa wameshindwa kuwapa ruhusa nyinyi hamna haja kuhuzunika kwani ‘amali zote hutazamwa na kutegemea Niyyah. 

Niyyah yako au yenu ikiwa nzuri basi mtapata thawabu kamili japokuwa hamkukaa I’tikaaf hiyo ndani ya Msikiti. 

Hata hivyo, nyumbani huko unaweza kuleta adhkaar, kusoma Qur-aan na kufanya mengineo ya kukupatia thawabu nyingi mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).


Na Allaah Anajua zaidi


Mwanamke Mwenye Hedhi Afanye Nini Masiku ya Mwisho Kupata Laylatul-Qadr?

SWALI

Nilikuwa nawaza mwanamke mwenye hedhi afanye nini usiku wa Laylatul-Qadr ili aweze kupata thawabu zaidi kwa kujishughulisha na ibada? Na kama inafaa, ibada ya aina gani inaruhusiwa afanye usiku huo?


JIBU


Naam,Mwanamke mwenye hedhi anaweza kufanya vitendo vyote vya ibada isipokuwa kuswali, kufunga, kuzunguka Ka'bah na kukaa I'tikaaf Msiktini.

Imesimuliwa kwamba Mtume  صلى الله عليه وآله وسلم  alikuwa akikesha usiku katika siku kumi za mwisho za Ramadhaan.

(Al-Bukhaariy 2401) na (Muslim 1174) wamesimulia kwamba Mama wa Waumini 'Aaishah رضي الله عنهاamesema ((Zinapoingia siku kumi za mwisho katika Ramadhaan, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم hujiepusha na wake zake, na hukesha usiku na kuwaamsha 'aila (familia) yake))

Kukesha usiku haina maana kwamba ni kwa kuswali pekee, bali ni kwa kila aina ya vitendo vya ibada, na hivi ndivyo walivyofasiri 'Ulamaa.

Al-Haafidh kasema: "Kukesha usiku ina maana kwamba kufanya aina za vitendo vya ibada"

An-Nawawy kasema:  "Kukesha usiku kwa kusimama kuswali na kadhalika",  akasema katika 'Awn al-Ma'abuud' kwamba ni kuswali, kufanya dhikr na kusoma Qur-aan.

Kuswali kwa kusimama ni kitendo bora kabisa Muislamu anaweza kufanya usiku wa Laylatul-Qadr kutokana na kauli ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :((Yeyote atakayesimama  kuswali  usiku wa Laylatul-Qadr kwa imani na kutaraji malipo atafutiwa madhambi yake ya nyuma)) Al-Bukhaariy 1901 na Muslim 760

Kwa sababu mwanamke mwenye hedhi haruhusiwi kuswali, ila anaweza kukesha usiku kwa kufanya aina ya vitendo vya 'Ibaadah zingine mbalimbali kama vile:

1) Kusoma Qur-aan

2) Kumdhukuru Allaah  kama kusema Subhaan-Allaah, La ilaaha illa Allaah, al-Hamdu Lillaah, anaweza kurudia kusema Subhaana-Allaah wal-Hamdu Lillaah, wa laa ilaaha illa Allaah, wa Allaahu Akbar na vile vile Subhaana Allaah wa bihamdihi, Subhaana Allaahul-‘Adhiym.

3) Istighfaar kwa kurudia kusema "Astaghfiru-Allaah"

4) Kuomba Du'aa.  Anaweza kumuomba Allaah anayohitaji ya duniani na Akhera kwani Du'aa ni kitendo bora kabisa cha 'Ibaadah. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema ((Du'aa ni 'Ibaadah))  At-Tirmidhiy, 2895; na imesemwa kuwa ni  Swahiyh na Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy, 2370

Mwanamke mwenye hedhi anaweza kufanya vitendo vyote hivi usiku wa Laylatul-Qadr. 

 Na Allaah Anajua zaidi


Ramadhwaan Inaaga Chukua Fursa Masiku Yaliyobakia Kutenda Mazuri

Enyi waja wa Allaah! Hakika mwezi wa Ramadhwaan unaaga na hakuna kilichokabakia isipokuwa masiku machache. Basi aliyetenda mazuri katika mwezi aendelee kufanya na ambaye amekasiri, ajitahidi kumaliza mwezi kwa vizuri, kwani hakika matendo yanahesabika mwishoni mwake.

Kwa hiyo  chukua fursa kwa (masiku) yaliyobakika ya mwezi, na uage mwezi kwa mazuri kabisa na amani. 




Usiku wa Laylatul-Qadr Hubadilika Kila Mwaka

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah):


Layaltul-Qadr hubadilika katika masiku ya kumi na si kwamba kuna siku maalumu katika nyusiku hizo. Huenda ikawa ni usiku wa 21 au 23 au 25 au 27 ambazo ni aghlabu zinategemewa na huenda pia ikwa usiku wa 29, au hata pia unaweza kuangukia masiku ya shafawiy (20, 22, 24, 26, 28).

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akihusisha nyusiku hizi kwa kuongezea na kujitahidi (katika ‘ibaadah) ambazo hakuwa hakizitekeleza katika masiku ya 20 ya mwanzo (ya Ramadhwaan) na Maswahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na Salaf walikuwa nao wakihuisha nyusku hizi na kujitahidi mno katika aina mbali mbali za ‘amali njema.”


[Al-Ikhtiyaraat Al-Fiqhiyyah, uk. 243]



Sharh Thawabu Za Kumfuturisha Mwenye Swawm


Kuhusu Hadiyth Ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((Atakayemfuturisha Aliye Na Swawm Atapata Thawabu Kama Zake Bila Ya Mwenye Swawm Kupungukiwa Na Kitu)).

Wamekhitilafiana ‘Ulamaa katika maana ya “Atakayemfuturisha mwenye swawm.” Ikasemwa: Lilokusudiwa kumfuturisha ni chochote kidogo anochofuturu japo kama ni tende. 

Na wengine wakasema: Imekusudiwa amfuturishe kwa kumshibisha kwa sababu ndio itakayomsaidia mwenye swawm usiku wake wote na huenda ikamtosheleza na sahuwr (daku). Lakini iliyo dhahiri katika Hadiyth ni kwamba mtu akimfuturisha mwenye swawm japo kwa tende moja basi atapata thawabu sawa na thawabu zake.  Kwa hiyo basi inampasa mtu atilie himma kufuturisha wenye swawm kwa kadiri ya uwezo wao khasa kwa vile wenye swawm wanahitaji kusaidiwa kutokana na umasikini wao na kuhitaji kwao kwa vile hawapati wenye kuwaandalia futari na kama hayo.


[Imaam Ibn 'Uthaymiyn – Sharh Riyaadhw Asw-Swaalihiyn]


Kuichelewesha Zakaatul-Fitwr

SWALI

Nilikuwa katika safari na nikasahau kutoa Zakaatul-Fitwr. Nikuwa nasafiri usiku wa 27 Ramadhwaan na hatukutoa Zakaatul-Fitwr hadi leo.

JIBU



Ikiwa mtu amechelewesha Zakaatul-Fitwr japokuwa alikumbukua kuitoa, basi atakuwa ni mtenda dhambi na itampasa atubie kwa Allaah na kuilipa kwa sababu ni kitendo cha ibada ambacho kinabakia kuwajibika japokuwa muda wa kutoa umepita kama mfano wa Swalaah. Lakini kama muulizaji huyu alivyotaja kuwa alisahau kuilipa kwa wakati wake, hivyo hakuna dhambi juu yake lakini lazima ailipe.
Kusema kuwa hakuna dhambi juu yake ni maana kwa ujumla kutokana na dalili inayoonyesha kuwa hakuna dhambi kwa mtu anayesahau lakini bado atakuwa amewajibika kuilipa kutokana na sababu zilizotolewa juu.


Wa biLLaahi At-Tawfiyq wa Swalla Allaahu ‘alaa Nabiyyina Muhammad wa aalihi wa Swahbihi wa sallam.


[Fataawaa Al-Lajnah Ad-Daaimah  (2867)]



Kuwalipia Zakaatul-Fitwr Wafanyakazi

SWALI

Tuna kiwanda na shamba ambamo kuna wafanyakazi wanaolipwa mishahara. Je tuwalipe Zakaatul-Fitwr au wajilipe wenyewe?



JIBU

Wafanyakazi ambao wanalipwa mishahara kwa kibarua chao katika kiwanda au shamba wanapaswa kujilipia wenyewe Zakaatul-Fitwr kwa sababu hukmu ya asili ni kwamba imewajibika kwako. (Hivyo hupasi wewe kuwalipia)

Wa biLLaahi At-Tawfiyq wa Swalla Allaahu ‘alaa Nabiyyina Muhammad wa aalihi wa Swahbihi wa sallam.

[Fataawaa Al-Lajnah Ad-Daaimah (9/372)]




Inaruhusiwa Kumpa Zakaatul-Fitwr Mama Wakubwa Na Wadogo?

 SWALI


Je, inafaa kutoa Zakaatul-Fitwr kwa mama mkubwa na mama mdogo   ambaye ameachwa, hana watoto wa kiume bali ana watoto wa kike ambao wameolewa na anamiliki 500 mita mraba ya ardhi.  Hana chanzo cha kipato. Je inaruhusiwa kumpa Zakaah hii au wapewe maskini wengine?


JIBU


Sifa Zote Ni Za Allaah

Kwanza:

‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu watu wa kuwapa Zakaatul-Fitwr. Rai ya wengi wao ni kwamba wapewe aina nane ya watu ambao wametajwa kupewa (katika Suwrah At-Tawbah Aayah ya 60). Rai ya wengineo ni kwamba wapewe wote waliomo katika aina nane ya watu na wengineo wameona kwamba itolewe kwa masikini na wenye kuhitaji pekee.

Inasema katika al-Mawsu’ah al-Fiqhiyyah (23/344): “Mafuqahaa wamekhitilafiana kuhusu nani apewe Zakaatul-Fitwr na kuna rai tatu:

1- Rai ya wengi wao ni kwamba inaruhusiwa kuigawa baina ya aina nane ya watu ambao Zakaah ya mali inapasa kuwapa. – Rai ya Maalik.
2- Rai ya Imaam Ahmad ambayo imependekezwa na Ibn Taymiyyah kwamba wapewe masikini na wanaohitaji pekee.

3- Rai ya Shaafi'y igaiwe kwa aina nane ya watu au yeyote aliyekuweko. [mwisho wa kunukuu]

Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah amekanusha rai ya kwanza na ya tatu katika Majmuw' al-Fataawa (25/73-78). Ameelezea kwamba Zakaatul-Fitwr inategemea idadi ya watu, sio mali. Baadhi ya aliyoyataja ni yafuatayo:

"Hivyo Allaah Ameamrisha itolewe kwa mfumo wa chakula kama Alivyoamrisha kafara iwe pia katika mfumo wa chakula.

Kutokana na rai hii, haipasi kuitoa Zakaatul-Fitwr ila wale wanostahiki kupokea chakula kama ni kafara. Nao ni wale wanaopokea kwa sababu wanakihitaji. Hivyo isitolewe kwa wale wa kutiwa nguvu nyoyo zao, au watumwa n.k. Hii ni rai iliyo na nguvu kabisa, kutokana na dalili.

Rai dhaifu kabisa ni ile wanaosema kwamba ni fardhi kwa kila Muislamu kutoa Zakaatul-Fitwr kwa (watu) kumi na mbili, au kumi na nane, au ishirini na nne, au ishirini na nane, au thelathini na mbili n.k. kwa sababu hii ni kinyume na desturi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Makhalifa Waliongoka na Maswahaba wote.

Hakuna Muislamu aliyefanya hivi zama hizo bali Muislamu alijitolea Zakaatul-Fitwr na Zakaatul-Fitwr ya familia yake kwa Muislam mmoja. Walipomuona mtu anagawana swaa’ baina ya watu wakigawana kitanga cha mkono, walikataza kwa nguvu na ilionekana kama ni bid'ah na kitendo kisichokubaliwa. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwamba kuamrishwa kwa swaa’ ya tende, au swaa’ ya shayiri, au nusu swaa’ au swaa’ ya ngano imepimwa kuwa inamtosheleza maskini mmoja. Pia ameelezea kwamba iwe katika mfumo wa chakula wapewe siku ya 'Iyd ili wawe wenye kujitegemea. Ikiwa mtu maskini atachukua kitanga cha chakula haitamnufaisha na haitamtosheleza. Hali kadhalika ni hali ya mwenye deni na msafiri. Wakichukua kitanga cha mkono cha ngano haitawatosheleza. Uislamu umezingatia kitendo hiki ambacho hakuna mtu mwenye busara angelikubali na ambacho hakuna Salaf au Maimaam wa Ummah walifanya" 
Juu ya hivyo, maneno ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Kama ni chakula cha masikini)) inaonyesha kwamba hii ni haki ya maskini kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Aayah za Dhwihaar (kafara ya Dhwihaar):
((basi awalishe masikini sitini)) [Al-Mujaadilah: 58:4]

Hivyo ikiwa hairuhusiwi kuitoa kuwapa hao aina nane ya watu basi inahusu hapa pia" [mwisho wa kunukuu]

Kutokana na  hii, rai iliyo sahihi kabisa miongoni mwa hizo rai tatu ni ya pili ambayo Zakaatul-Fitwr itolewe kwa masikini na wenye kuhitaji na sio mtu mwingine. Hivyo ndivyo iliyochukuliwa kuwa ni rai iliyo sahihi kabisa na Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) kama inavyosema katika ash-Sharh al-Mumtii' (6/17)
Pili:

Ikiwa Zakaatul-Fitwr na Zakaah ya mali watapewa jamaa ambao wanastahiki, ni bora zaidi kuliko kuwapa wengineo wanaostahiki kwa sababu katika hali hii Zakaah zote mbili zinaunganisha ukoo. Lakini inategemea na hali ya huyo jamaa kama anastahiki kupewa (yaani kama ni maskini na mwenye kuhitaji)  
Shaykh Muhammad Swaalih bin 'Uthaymiyn (Rahimahu  Allaah) alipoulizwa kuhusu hukmu ya Zakaatul-Fitwr kupewa jamaa walio masikini.

Alijibu:
Inaruhusiwa kutoa Zakaatul-Fitwr na Zakaah ya mali kuwapa jamaa walio masikini. Na hakika kuwapa jamaa ni bora kuliko kuwapa watu wageni kwa sababu kuwapa jamaa huwa ni sadaka na pia kuunga ukoo. Lakini sharti isiwe kwa ajili ya kuhifadhi mali yake ambayo ndivyo itakavyokuwa hali ikiwa jamaa yenyewe aliye maskini ni ambaye mwenye jukumu naye kumhudumia. Kwa hali hiyo hairuhusiwi kumtimizia mtu haja kwa chochote katika Zakaah yake kwa sababu akifanya hivyo atakuwa anahifadhi mali yake kutokana na anachokitoa (kwa maana atakuwa anataoa Zakaah yake kwa kumpa mtu ambaye ni wajibu wake kumhudumia) Nayo haipasi wala kuruhusiwa.
Lakini ikiwa hana majukumu naye basi anaweza kumpa Zakaah bali kutoa Zakaah yake kwa jamaa ni bora kuliko kumpa mtu mgeni kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   amesema: ((Swadaqah zenu kwa jamaa ni swadaqah na pia ni kuunga ukoo))[mwisho wa kunukuu- Majmuu' Fataawa Shaykh Ibn 'Uthaymiyn (18/Swali Namba 301]

Hitimisho:
Ikiwa mama mkubwa na mama mdogo wako ni maskini anastahiki Zakaah, japo kuwa anamiliki mita mraba 500 ya ardhi. Lakini ni bora kwake aiuze ili awe ni mwenye kujitegemea mwenyewe ili asitegemee zawadi kutoka kwa watu.
Waislamu wasiwaache jamaa zao hadi mwezi wa Ramadhwaan unamalizika ndio waanze kuwafikiria na kuwapa swaa’ ya chakula, bali Waislamu wanapaswa daima kuwahudumia maskini na wanaohitaji na kukimbilia kuwapa wanayohitaji ya chakula, pesa na nguo na hivi inapaswa ifanyike zaidi na zaidi ili walio matajiri wawe wanawafikiria na kuwahudumia jamaa zao walio maskini.

Na Allaah Anajua zaidi 


Je,Ni Kweli Swawm Inanin'ginia Baina ya Mbingu na Ardhi hadi Mtu atoe Zakaatul-Fitwr?

SWALI


Je, Hadiyth inayosema kuwa Swawm ya Ramadhaan inaning'inia baina ya mbinu na ardhi na haipandishwi juu hadi ilipwe Zakaatul-Fitwr ni Sahihi? 



JIBU


Naam kwanza kabisa Hadiyth hiyo ni dhaifu.

Katika Al-Jaami' as-Swaghiyr, as-Suyuwtwiy ameihusisha kwa Ibn Shaahiyn katika Targhiyb yake: "Imesimuliwa katika Adhw-Dhwiyaa' kutoka kwa Jariyr bin 'Abdillaah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: Mwezi wa Ramadhaan unaning'inia baina ya mbingu na ardhi na (Swawm) haipelekwi juu kwa Allaah isipokuwa kwa (kutolewa) Zakaatul-Fitwr"

Imechambuliwa kuwa ni dhaifu na as-Suyuwtwiy. Al-Manaawiy ameeleza sababu yake katika Faydhw Al-Qadiyr ambako amesema: "Imesimuliwa na Ibn Al-Jawziy katika Al-Waahiyaat na kasema: Sio Swahiyh, isnaad yake inajumuisha Muhammad bin 'Ubayd al-Baswriy ambaye ni majhuwl (asiyejulikana).

Imechambuliwa pia kuwa ni dhaifu na Imaam al-Albaaniy katika as-Silsilatul-Ahaadiyth ad-Dhwa'iyfah (43). Kasema: "Hata kama ingekuwa ni Hadiyth Swahiyh, basi maana iliyodhihiri ni kukubaliwa kwa Swawm ya Ramadhwaan inategemea baada ya kulipa Zakaatul-Fitwr tu, na ikiwa mtu hakulipa, basi Swawm  yake haitokubaliwa. Lakini simjui Mwanachuoni yeyote aliyesema hivyo na Hadiyth sio Swahiyh" [mwisho wa kunukuu]

Kwa vile Hadiyth sio Swahiyh, hakuna atakayeweza kusema kwamba Swawm ya Ramadhwaan inakubalika tu baada ya kutoa Zakaatul-Fitwr kwa saabu hakuna atakayejua hivyo isipokuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Imethibitika katika Sunan Abi Daawuwd kwamba Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amefaridhisha Zakaatul-Fitwr kuwalisha masikini kama ni kutakasa swiyaam za aliyefunga kutokana na maneno ya upuuzi na kauli chafu" [Imepewa daraja ya Hasan na Shaykh al-Albaaniy katika Swahiyh Sunan Abi Daawuwd] 

Hadiyth hii inaelezea hikma ya Zakaatul-Fitwr ambayo kufidia kasoro yoyote iliyotokea katika Swawm. Haisemi kuwa Swawm haitokubaliwa ila tu baada ya kutoa Zakaatul-Fitwr.

Na Allaah Anajua zaidi



20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...