Translate

Alhamisi, 21 Februari 2019

Mambo ya Haramu yanayofanyika Saloon - 1

Mambo ya Haramu yanayofanyika Saloon katika kazi ya Unyozi


Assallaam  Aleykum  WarahmatulLaah Wabarakatuh

1. Kukata Nywele kwa Mitindo ya Kikafiri

Mitindo kama inayojulikana kama “Marines” au “panki” au “denge” na majina mengine mfano wa hayo. Mitindo kama hiyo ya kukata nywele sehemu ya kichwa na kuacha sehemu nyingine. Ima kwa kunyoa kipara kwa maeneo ya pembeni kote na kuacha sehemu ya juu ya kichwa, au kupunguza sana sehemu za chini na kuacha nyingi sehemu ya juu.

Unyoaji huo ujulikanao Kiislamu kama Al-Qaza’ umeharamishwa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye anasema kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza (unyoaji wa) Al-Qaza’. [Al-Bukhaariy na Muslim]

Mitindo hiyo ya kunyoa au kupunguza nywele na kuziacha baadhi yake kama mitindo iliyopo sasa watu hunyoa kama kunguru kichwa chote hunyolewa na kuachwa nywele nyingi sehemu moja kama vile utosini na kadhalika, ni mitindo isiyofaa, bali ni mitindo haramu. 

Hiyo ni katika mtindo inayopendezeshwa na washirikina kwa Waislamu haswa waliofitinishwa na mchezo mpira na muziki; huwa wanawaiga wachezaji na wanamuziki katika kila kitu likiwemo hili la mitindo ya kunyoa nywele zao, hivyo ieleweke kuwa haifai kwani unyoaji huo umekatazwa na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama tulivyoeleza hapo juu katika Hadiyth ya Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ambayo kwa kirefu ni kama ifuatavyo:
“Kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza Al-Qaza’; akasema: nikamuuliza Naafi’ ni nini Al-Qaza’? Akasema: kunyoa baadhi ya kichwa cha mtoto na na kuacha baadhi yake (panki)”Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Mavazi na mapambo, mlango kuchukiwa kwa Al-Qaza' (kunyoa panki)’.

Ole wake yule anayependa kufufuliwa akiwa pamoja na aliyempenda katika makafiri wacheza mpira au wasanii.


2. Kunyoa Ndevu

Unyoaji ndevu kwa vinyozi wengi ni jambo la kawaida sana –ila wale wachache sana waliorehemewa na Allaah- hadi inaonekana ajabu mtu anapowafikishia na kuwajulisha kuwa kazi hiyo ni haramu na inapingana na mafundisho ya dini.

Vinyozi kunyoa wateja wao ndevu au kuzichonga kama ramani fulani au kuzinyoa zote na kubakisha mduara kidevuni ujulikanao kama alama ya "o" kwa kuiga makafiri na wasio na maadili, ni jambo limezoeleka na hata kuwepo picha za mitindo hiyo kwa vinyozi ni kitu kilichoenea sana. Yote hayo ni haramu na yanapingana na mafunzo ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mwenendo wa Mtume Muhammad (‘Alayhimus-Salaam) waliotangulia na pia mwenendo wa Maswahaba na wema waliotangulia.

Ndevu ni pambo la mwanamme ambalo limeamrishwa kuliweka na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth nyingi.

Na Wanachuoni wakiwemo ma-Imaam wakubwa wanne wote wamekubaliana kuwa ni haramu kunyoa ndevu.

Baadhi za Hadiyth zenye kuthibitisha uwajibu wa kufuga ndevu kwa wanaume ni hizi zifuatazo:

a- Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuru kuziachilia. Amri hii ni ya lazima, kwani hakuna kiashirio chochote kinachoigeuza na kuipeleka katika usunnah. Na kati ya amri hizo ni neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
“Kuweni kinyume na washirikina; fugeni ndevu kwa wingi na punguzeni masharubu.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

Na neno lake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
“Kateni masharubu na ziachilieni ndevu; nendeni kinyume na wanaoabudu moto.” [Muslim]

b- Ni kwamba kuzinyoa ni sawa na kujifananisha na makafiri kama inavyoonekana katika Hadiyth mbili zilizotangulia.

c- Ni kwamba kuzinyoa ni sawa na kuubadilisha Uumbaji wa Allaah na kumtii Shaytwaan asemaye:

“...na hakika nitawaamrisha, basi watabadili Aliyoyaumba Allaah” [An-Nisaa: 119]

d- Ni kwamba kuzinyoa ni sawa na kujifananisha na wanawake. Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani wanaume wanaojifananisha na wanawake. [Al-Bukhaariy na At-Tirmidhiy]

Na kwa ajili hiyo, Shaykh Al-Islaam amesema:
“Na inaharamishwa kunyoa ndevu zake.” [“Al-Ikhtiyaaraat Al-Fiqhiyyah” cha ‘Alaaud-Diyn Al-Ba’aly, uk.10, na “Al-Furuw’” cha Ibn Muflih (1/291).]
Ibn Hazm na wengineo, wamenukuu Ijmaa’ ya Wanachuoni juu ya uharamu wa kunyoa ndevu.
Amesema Ibn ‘Abdil-Barri (Allaah Amrehemu) katika kitabu chake At-Tamhiyd:“Na ni haramu kunyoa ndevu, na hawanyoi isipokuwa Makhanithi katika wanaume.”
Khanithi ni nani?
Ni yule mwenye tabia za kike, anapenda mambo ya kike kike.

Amesema Al-Imaam Ash-Shanqiytwiy (Allaah Amrehemu) katika Tafsiyr yake Adhw-waau Al-Bayaan:

"Vitofautisho vilivyo wazi mno baina ya mwanamme na mwanamke ni ndevu.”
Amesema Shaykh Muqbil Al-Waadi'iy (Allaah Amrehemu) katika Ijaabat As-Saail:
"Kunyoa ndevu (jambo hilo) huzingatiwa kuwa ni kujifananisha na wanawake.”
Uharamu wa unyoaji ndevu uko wazi na hauna shaka kwa mwenye kutafuta haki na mwenye kutaka kuifuata Dini yake na mafunzo sahihi yaliyothibiti kutoka kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). 

Ama kwa yule mwenye matamanio yake na mpenda dunia, huyo hana la kufanywa ikiwa hataki kukubali haki.

Kadhaalika Wanachuoni wengi wameonelea hata kupunguza ndevu pia ni jambo lisilokubalika, isipokuwa baadhi yao wanaonelea ni makruuh na wengine wanaonelea kuzipunguza kunaruhusiwa pindi zinapozidi mshiko wa kiganja cha mkono. ‘Alaa kulli haal, kwa kifupi kuzipunguza vilevile ni jambo lenye utata na linapaswa kuepukwa.

Mwanachuoni Shaykh ‘Abdul-Muhsin Al-‘Abbaad (Hafidhwahu Allaah) anasema:
“Na mwanaume akinyoa ndevu zake anafanana na mwanamke. Mwanamke ndiye asiyekuwa na ndevu. Mwanaume akinyoa ndevu zake anakuwa kama mwanamke.”
Na akanukuu Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:
“Allaah Kamlaani mwanamme mwenye kujifananisha na wanawake. Na mwanamke mwenye kujifananisha na wanaume.”[Al-Bukhaariy]
Mwisho wa kumnukuu.

Na kujifananisha mwanamme na wanawake, ni pamoja na kunyoa ndevu alizoamrishwa na shariy’ah azifuge, kuvaa hereni, kuvaa mikufu, kutoboa masikio, kusuka nywele na kuvaa mabangili na mfano wa hayo yafanywayo na wanawake.

Na katika mitihani mingine iliyopo vilevile katika saluni zingine za Waislamu, ni kusuka wanaume nywele.

Kunyoa ndevu haifai kabisa, mwanamme Muislamu anatakiwa awe anafuga ndevu na kupunguza masharubu na si kinyume chake; hivyo basi kwa kuwa wewe ni kinyozi bila shaka yoyote wako wanaokuja kutaka uwanyoe ndevu na haya yamekatazwa na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alichoamrisha ni kufuga na kuzikuza ndevu na si kuzinyoa kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliposema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Wakhalifuni washirikina (muwe tofauti na wanavyofanya) wacheni ndevu zenu na punguzeni masharubu yenu – na katika riwaya nyingine: kupunguza masharubu ni katika fitwrah (maumbile ya asli – Uislamu -)” [Al-Bukhaariy]

Na Ahaadiyth za kuamrishwa kufuga ndevu ni nyingi mno.

Inaendelea....USIKOSE TOLEO  LINALOFUATA  MUDA  SI MREFU....


https://ift.tt/2DYciTC i live islam

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...