Sufyaan bin ´Abdillaah ath-Thaqafiy amesema:
“Nilisema: “Ee Mtume wa Allaah! Nambie katika Uislamu kitu ambacho sintomuuliza yeyote baada yako.” Akasema: “Sema: “Nimemwamini Allaah” kisha kuwa na msimamo.”[1]
Mtu huyu alimuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) maneno ya kheri yaliyokusanya kheri na manufaa yote na yenye kumfikisha mwenye nayo katika mafanikio yote. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwamrisha kumwamini Allaah ambapo kumekusanya yale yote ambayo ni wajibu kuyaamini, katika I´tiqaad na misingi ya imani na yale yote yanayopelekea katika hilo katika matendo ya moyo, unyenyekevu na kujisalimisha kwa Allaah, kwa undani na kwa uinje. Kisha mtu adumu juu ya hilo na ashikamane nayo mpaka wakati wa kufa. Hayo yanafanana na maneno Yake (Ta´ala):
إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْتُوعَدُونَ
“Hakika wale waliosema: “Mola wetu ni Allaah” kisha wakanyooka barabara, basi Malaika huwateremkia [wakiwaambia]: “Msikhofu na wala msihuzunike na pateni bishara njema ya Pepo ambayo mlikuwa mkiahidiwa.” (41:30)
Ameeleza kwamba kuamini na kuwa na msimamo kunapelekea mtu kusalimika kutokamana na sharti zote na kufikia Peponi na yale yote yanayopendwa. Kuna maandiko mengi katika Qur-aan na Sunnah ambayo yamefahamisha kuwa imani imekusanya zile I´tiqaad sahihi zilizomo ndani ya moyo, matendo yake (kukiwemo kuwa na shauku juu ya kheri, kuwa na woga juu ya shari, kutaka kheri na kuchukia shari) na matendo ya viungo – na hayo hayatimii isipokuwa mpaka mtu ashikamane nayo barabara.
[1] Muslim (38), at-Tirmidhiy (2410), Ibn Maajah (3972) na Ahmad (14990).
from Firqatu Nnajia https://ift.tt/2BWAci6
via IFTTT
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni