Translate

Alhamisi, 28 Februari 2019

Madhambi Makubwa Na Madogo

Madhambi Makubwa:


Madhambi makubwa ni yale ambayo yametajwa katika Qur-aan na Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nayo ni yale ambayo mja anapoyafanya huwa na hukmu zifuatazo:


1-Madhambi ambayo Allaah Anaalaani kitendo chake.


2-Madhambi ambayo yamewekewa adhabu kali kama mfano mwenye kuzini na hali ameoa au ameolewa kupigwa mawe hadi kufa au kupigwa bakora 100 kwa asiyeoa au asiyeolewa.


3-Madhambi ambayo Anaghadhibika nayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala).


4-Madhambi ambayo Allaah Anamnyima Rahmah Yake mwenye kuyatenda.


Hadiyth ifuatayo imeyaelezea baadhi ya madhambi hayo makubwa ambayo yanajulikana  Sab'ul-Muwbiqaat (saba yenye kuangamiza).

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  عن النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((اجْتَنِبُوا السَّبْعَ الْمُوبِقَاتِ)) قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ وَمَا هُنَّ؟  قَالَ: ((الشِّرْكُ بِاللَّهِ وَالسِّحْرُ وَقَتْلُ النَّفْسِ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلاَّ بِالْحَقِّ وَأَكْلُ الرِّبَا وَأَكْلُ مَالِ الْيَتِيمِ وَالتَّوَلِّي يَوْمَ الزَّحْفِ وَقَذْفُ الْمُحْصَنَاتِ الْمُؤْمِنَاتِ الْغَافلاَتِ)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Jiepusheni na mambo saba yanayoangamiza!)) Wakauliza: Ni yepi hayo ee Rasuli wa Allaah? Akasema: ((Ni kumshirikisha Allaah, sihri [uchawi], kuua nafsi Aliyoiharamisha Allaah isipokuwa kwa haki, kula ribaa, kula mali ya yatima, kukimbia wakati wa kupambana na adui na kuwatuhumu uzinifu wanawake Waumini waliohifadhika walioghafilika)).  [Al-Bukhaariy, Muslim, An-Nasaaiy, Abu Daawuud]


Madhambi hayo makubwa ni haya yafuatayo ambayo yametajwa katika Hadiyth hiyo juu na mengine mengi ambayo baadhi ya ‘Ulamaa wamejaribu kuyaorodhesha kwa kuyanyambua kutoka katika Qur-aan na Sunnah kulingana na makatazo, makemeo, laana, na adhabu zake, kama vile madhambi 70 aliyoyaorodhesha mwanachuoni mkubwa Imaam Muhammad bin ‘Uthmaan Adh-Dhahabiy kwenye kitabu chake Al-Kabaair:


1-Kumshikirika Allaah


2-Kuua


3-Uchawi


4-Kuacha Swalaah


6-Kuacha kufunga Swawm ya Ramadhwaan bila udhuru


7-Kutokuhiji kwa mwenye uwezo


8-Kutokuwatii wazazi


9-Kuwahama na kuwakata jamaa na ndugu; kutengana nao


10-Uzinzi (kufanya zinaa)


11-Liwati (matendo ya kaumu Luwt; watu kuingiliana nyuma) mwenye kufanya na kufanywa wote wanaingia


12-Kula ribaa


13-Kula mali ya yatima na kumdhulumu


14-Kumsingizia Allaah na Rasuli Wake uongo


15-Kukimbia vitani


16-Kiongozi kuwa mdanganyifu kwa raia wake na kutokuwa muadilifu


17-Kiburi, majivuno na kujitukuza


18-Kutoa ushuhuda wa uongo 


19-Kunywa pombe


20-Kamari


21-Kumsingizia mwanamke mtwaharifu tuhuma ya uzinifu


22-Kuiba ngawira za vita

23-Wizi


24-Ujambazi


25-Kutoa kiapo cha uongo


26-Dhulma (Kudhulumu)


27-Chumo la haramu


28-Kupata utajiri kwa njia za haramu


29-Kujiua


30-Kusema uongo (kila mara)


31-Kutohukumu kwa uadilifu


32-Kutoa na kupokea rushwa


33-Mwanamke kujifananisha na mwanamme na mwanamme kujifananisha na mwanamke kimavazi, kutembea, kuzungumza na mengineyo


34-Udayuthi, ukuwadi, na kutokuwa mwaminifu katika ndoa


35-Kumuoa mwanamke aliyeachika kwa talaka tatu ili awe halali kwa mume aliyemuacha kumrudia


36-Kutojilinda kurukiwa na mikojo


37-Riyaa (kujionyesha matendo mema)


38-Kutafuta elimu kwa maslahi ya dunia, na kuificha elimu uliyonayo


39-Kufanya khiyana


40-Kutangazia na kuhesabu mema uliyoyatenda


41-Kupinga Qadar


42-Kusikiliza siri za watu


43-Kuhamisha maneno (umbea)


44-Kulaani wengine


45-Kuvunja ahadi


46-Kuwaamini makuhani, watabiri, wapiga ramli (watazamiaji)


47-Mke kutomtii mumewe


48-Kutengeneza masanamu, vinyago, na picha


49-Kupiga mayowe, kuchana nguo, kujipiga na kujikatakata wakati wa msiba


50-Kutokuwa muadilifu kwa watu


51-Kutokuwa na huruma na kuwafanyia ujeuri mke, wafanyakazi, madhaifu na wanyama


52-Kumuudhi jirani


53-Kuwaudhi na kuwatukuna Waislamu


54-Kuwaudhi na kuwafanyia ujeuri watu


55-Isbaal (mwanamme kuvaa nguo ndefu inayovuka viwiko vya miguu kwa kiburi au ufakhari)


56-Mwanaume kuvaa hariri


57-Mtumwa kumkimbia bwana wake


58-Kutokuchinja mnyama kwa ajili ya Allaah


59-Kumwita mtu kwa ubini wa baba asiyekuwa wake huku unajua (kwa makusudi)


60-Kugombana na kupigana


61-Kuzuilia (watu) maji


62-Kupunja kipimo


63-Kujilinda na Aliyoyapanga Allaah


64-Kuwaudhi waja wema vipenzi vya Allaah


65-Mwanaume kuacha kuswali Swalaah ya jama’aah (Msikitini) na kuswali pekee bila udhuru


66-Kuacha kuswali Ijumaa kwa makusudi au kutotilia umuhimu na kupuuzia


68-Kupanga njama na kufanya hila


69-Kuwapeleleza Waislamu kwa ajili ya makafiri na maadui


70-Kuwatukana Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum)


Hayo ni madhambi 70 aliyojaaliwa Imaam Adh-Dhahabiy (Rahimahu Allaah) kuyakusanya kutoka katika Qur-aan na Sunnah.


Madhambi makubwa mengineyo:

71-Kusherehekea sikukuu za makafiri

72-Kunyoa nyusi

73-Kuunga nywele za bandia

74-Kujichora tattoo          

75-Kuvunja mkataba (bila sababu ya ki-shariy’ah)
 
76-Kula nguruwe, nyamafu na damu

77-Kutoa kiapo cha uongo kwenye biashara

78-Kudharau na kuzikebehi Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ndevu, mswaki wa mti, kupunguza nguo isiburuze kwa wanaume n.k.

79-Kuwakebehi na wakuwapa majina mabaya wale wanaozifuata Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

80-An-Namiymah (Kufitinisha watu)

81-Ghiybah (kusengenya)

82-Kuamini nuksi (superstition), na kutabiri kwa nyota (horoscope), kutundika vitu na kuvaa kwa kuitakidi kuwa vinamlinda mtu na shari

83-Bid-ah za aina zote katika Dini

84-Kudanganya watu kupata maslahi ya kidunia

85-Kufanya israfu ya chakula na israfu katika sherehe ambayo inadhihirisha riyaa (kujionyesha kwa watu)

86-Kukufuru neema za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)

87-Kuisoma Qur-aan kimakosa kwa kubadilisha maana za Maneno ya Allaah

88-Kuapa uongo kama kuapia kwa ajili ya kumvutia mteja biashara

89-Kughushi katika biashara kama kupunja au kuuza bidhaa mbovu

90-Mwanamke kutokujisitiri vizuri kwa hijaab ya ki-shariy’ah



Madhambi Madogo:

Madhambi madogo ni yale ambayo hayamo katika fungu hilo hapo juu nayo ni yale ambayo yamekusudiwa katika kauli ya Allaah (Subhanaahu wa Ta'aalaa): 

 الَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ إِلَّا اللَّمَمَ ۚ  
Wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na machafu isipokuwa makosa madogo-madogo. [An-Najm: 32]

Madhambi hayo ambayo Allaah Humghfuruia mja maadam mja hatoendelea kuyatenda kila mara kwani kuyaendeleza husababisha kugeuka kuwa ni madhambi makubwa. Mfano kuchanganyika wanawake na wanaume, mtu kuzungumza na asiye Mahram wake bila ya sababu ya ki-shariy’ah, husababisha kukaribia zinaa na huenda yakampeleka mja kutumbukia katika maasi hayo makubwa.

Madhambi madogo kama ilivyo dalili katika Qur-aan na Sunnah kwamba kila jema alifanyalo mja hufuta ovu lake kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَأَقِمِ الصَّلَاةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِّنَ اللَّيْلِ ۚ إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ ۚ ذَٰلِكَ ذِكْرَىٰ لِلذَّاكِرِينَ﴿١١٤﴾
Na simamisha Swalaah katika ncha mbili za mchana na sehemu ya kwanza ya usiku; hakika mema yanaondosha maovu. Hivyo ni ukumbusho kwa wanaokumbuka.  [Huwd: 114]

Mfano kufanya wudhuu vizuri, madhambi madogo hupuputika.

Madhambi hayo pia yanaweza kuwa ni kama, kutazama picha na sinema chafu zisizofaa, kusikiliza maovu, kusikiliza na kuimba muziki, kutamka maneno maovu kama kutukana, kuwa na ghadhabu, na mengi mengineyo ambayo hayakuwekewa adhabu kali au laana, au ghadhabu ya Allaah.


from Uislamu Wangu https://ift.tt/2XDI6pY
via IFTTT

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...