Translate

Jumanne, 27 Novemba 2018

Umuhimu wa kuwatembelea na kuwalingania wagonjwa

Imepokewa hadithi kutoka kwa Anas bin Maliki (Allah amridhie) amesema kijana wa Kiyahudi aliyekuwa akimtumikia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliugua. Mtume akaenda kumtembelea, akakaa karibu na kichwa chake akamwambia “Silimu.” Yule kijana alimtazama baba yake ambaye naye alikuwepo mahala pale. Baba yake akamwambia: “Mtii Baba wa Kasimu (Mtume).” Yule kijana akasilimu. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akatoka huku akisema: “Namshukuru Allah ambaye amemuokoa na moto.” [Bukhari]

 

Tukio hili linatufundisha umuhimu wa kuwatembelea wagonjwa na kuwalingania katika kheri hasa wanapokuwa katika hatua ya mwisho ya maisha yao kwani huenda kwa taufiq ya Allah wakapata mwisho mwema. Si hilo tu, kuna mengi mengine tunayojifunza kutoka katika tukio hiili, ambayo tutayajadili katika makala hii.

Kuwa na watumishi wasiokuwa Waislamu

Inafaa kuwafanya wasiokuwa Waislamu kuwa watumishi kwa sharti la kujiaminisha na vitimbi na tabia zao, kwani Mayahudi walikuwa hawatekelezi ahadi, si waaminifu na vilevile walikuwa na vitimbi, hadaa na khiyana nyingi. Lakini kama ilivyothibiti katika baadhi ya riwaya, kuwa kijana huyu alimtumikia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) isichukuliwe kuwa ni  kigezo cha kuwafanya wawe watumishi hasa wa ndani bila kuzingatia tabia maadili na kuchunga mwenendo wake na dhamira yake.

Ukichukua tu ruhusa hii kijumlajumla bila kuzingatia tabia ya mtumishi huyo asiyekuwa Muislamu inaweza kuleta tatizo kwa jamii ya Kiislamu na matokeo yake watoto wakakosa malezi yenye taathira ya kidini hasa katika kipindi hiki ambacho wanawake wamejisahau katika suala la ulezi na kukimbilia katika maeneo ya kazi kwa ajili ya kujipatia kipato hata kama hamna haja ya kufanya hivyo.

Kuwatembelea wagonjwa hata wasiokuwa Waislamu

Pia inafaa kumzuru mgonjwa ambaye ni Myahudi au Mnaswara kwa ushahidi tuliouona katika tukio hili ambapo Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alimtembelea kijana huyu. Kwa upande mwingine inatajwa kuwa kwa sababu huyu alikuwa ni mtumishi wake, haichukuliwi moja kwa moja kuwa ruhusa hii inawahusu wengine wote. Pia inashukiwa kuwa alifanya hivyo ili akamlinganie Uislamu.

Kwa hiyo, kumtembelea mgonjwa wa namna hii itakuwa ni Sunna ikiwa mtu amekusudia kumlingania katika Uislamu ili mgonjwa huyo aokoke na adhabu ya moto. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie] mesema: “Allah akimuongoza mtu mmoja kupitia wewe ni bora kuliko kupata ngamia wekundu,” akimaanisha kuwa kama utamlingania mtu katika Uislamu na Allah akamuongoza kuukubali, basi hilo ni bora kwako kuliko kupata ngamia wekundu ambao walikuwa na thamani kubwa kwa Waarabu katika zama hizo.

Kumkumbusha mgonjwa 

Inatakikana kwa mtu yoyote atakayemtembelea mgonjwa, amuongoze katika mambo ya kheri na kumhamasisha, hasa ikiwa anajua kuwa mgonjwa huyo ni mtu mwenye kuzembea.

Mtu atakayemtembelea mgonjwa ni muhimu amwelekeze kufanya toba na istighfaar kwa wingi, kwani zawadi iliyo bora kwa mgonjwa ni lile jambo litakalomnufaisha katika dini yake. Ama kumchekesha tu na kumsimulia yanayojiri mitaani hayatamnufaisha kwa lolote.

Taathira ya mzazi kwa mtoto

Mzazi anaweza kuwa na taathira kwa mtoto wake akawa ni mwenye kufanya kheri hata kama yeye mwenyewe haifanyi kheri hiyo. Baba wa huyu kijana wa Kiyahudi alimuamuru mwanawe amtii Mtume kwa kusilimu ingawa yeye mwenyewe hakusilimu.

Wazazi wanatakiwa wawe mfano bora kwa watoto wao kimatendo na kwa mazungumzo; na ikitokea kutofanya hivyo, basi walau mzazi asisite kumhimiza mtoto katika njia bora.

Mtume wa haki

Kuna dalili inayothibitisha kuwa Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) Mtume wa haki. Dalili yenyewe ni yule Myahudi kumuamuru mwanawe amtii Mtume. Ni wazi kuwa, Myahudi yule anajua kuwa Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) ni Mtume wa haki. Ijulikane wazi kuwa, haki iliyowazi ni ile inayoshuhudiwa na maadui, jambo ambalo linashuhudiwa na Qur’an, Pale ilipoelezwa kwamba, Mayahudi na Manaswara wanamjua vizuri Mtume kama wanavyowajua watoto wao.

Mwenyezi Mungu aliyetukuka anasema: “Wale tuliowapa Kitabu wanayajua haya kama wanavyowajua watoto wao; na kuna kikundi katika wao huificha haki na hali wanajua.”[Qur’an, 2:146].

Katika Qur’an 7:157, Mwenyezi Mungu anasema: “Ambao kwamba wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiye soma wala kuandika, wanayemkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili, anaye waamrisha mema na anawakanya maovu, na anawahalalishia vizuri, na anawaharimishia viovu, na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyo kuwa juu yao. Basi wale waliomuamini yeye, na wakamhishimu, na wakamsaidia, na wakaifuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye – hao ndio wenye kufanikiwa.”

Lakini kiburi na husda kiliwazuia kumwamini kama Allah alivyosema: “Wengi miongoni mwa watu wa Kitabu wanatamani lau wangekurudisheni nyinyi muwe makafiri baada ya kuamini kwenu, kwa ajili ya uhasidi uliomo ndani ya nafsi zao, baada ya kwisha wapambanukia haki.” [Qur’an, 2:109].

Umuhimu wa kutembelea wagonjwa

Abu Huraira (Allah amridhie) amesema: “Hakika Allah Aliyetukuka atasema Siku ya Kiyama, ‘Ewe mwana wa Adam, niliumwa na usije kunitembelea.’ Atasema, ‘Ewe Mola, vipi nije kukutembelea nawe ni Mola Mlezi wa ulimwengu?’ Atasema, ‘Kwani ulijua kuwa mja wangu fulani alikuwa mgonjwa na hukwenda kumtembelea! hukujua kuwa ungekwenda ungalinikuta niko pamoja naye?’

“Ewe mwana wa Adam, nilikuomba chakula na hukunipa.’ Atasema, ‘Ewe Mola, vipi nitakupa chakula na wewe ni Mola Mlezi wa ulimwengu?’ Atasema, ‘Kwani hukujua kuwa mja wangu fulani alikuomba chakula na hukumpa? Hukujua kuwa ungalimpa chakula ungalikuta hayo kwangu?’

“Ewe mwanadamu, nilikuomba maji na hukunipa.’ Atasema, ‘Ewe Mola, vipi nitakupa maji na Wewe ni Mola wa ulimwengu?’ Atasema, ‘Mja wangu fulani alikuomba maji na hukumpa. Hukujua kwamba ungalimpa maji ungalikuta hayo kwangu.’” [Muslim].

Kwa hiyo akiugua mtu ambaye si Muislamu unaweza kumtembelea kama utakuwa na mategemeo kuwa katika kumtembelea kutakuwa na kheri, kama vile kumlingania huenda atasilimu.

Jengo la watoto, Hospital ya taifa ya Muhimbili

Vijana wa kujitolea wa The Islamic foundation wakiwatembelea watoto katika hospitali ya taifa ya Muhimbili



from TIF https://ift.tt/2Q2anGz
via IFTTT

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...