Translate

Jumanne, 27 Novemba 2018

Sifa Za Mke Mwema - Sehemu ya 1

                                                              ص فات ال زوج ة ال صال حة 

                                                                Sifa za Mke Mwema

                         Mwandishi : Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad.

                                                  Mfasiri: Abu Bakr Khatwiyb al-Atrush.




UTANGULIZI


Assallaam   Aleykum  WarahmatulLaah  Wabarakatuh


Himidi zote ni Zake Allaah. Tunamhimidi na kumtaka msaada na kumuomba mswamaha na tunatubu Kwake. Tunajikinga kwake kutokana na shari ya nafsi zetu na matendo yetu maovu. Mwenye Kuongozwa na Allaah hakuna wa kumpoteza. Mwenye Kupotezwa na Allaah hakuna wa kumwongoza.

Nashuhudia ya kwamba hapana mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah Mmoja asiyekuwa na mshirika. Nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja Wake na Mtume Wake, Swalah na salaam zimwendee yeye, ahli zake na Maswahabaha zake wote.

Amma ba´ad... 


Maudhui ya Risaalah hii iliyo na anuani ”Sifa za mke mwema” hayamuhusu tu msichana mdogo ambaye yuko katika njia ya kutaka kuolewa na anataka kujua sifa ambazo mke anatakiwa kuwa nazo ili ajiandae nazo, kuishi nazo na kuzitimiza.


Vilevile hayamuhusu tu mwanamke ambaye ameolewa ambaye anataka kuwa na sifa za mke mwema ili aweze kuzidhibiti na kuishi nazo katika maisha yake.


Vilevile hayamuhusu tu mwanamke mwenye upungufu ili aweze kutibu upungufu wake na kujisahihisha mwenyewe na ndoa yake tukufu. Ni wito na ukumbusho ulio jumla kuliko hivyo.


Ni ukumbusho kwa baba ambaye anataka wasichana zake na wanawake ambao wako katika usimamizi wake wapate kukuwa vizuri na malezi mazuri na ndoa ambayo inaafikiana na Matakwa ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).


Kwa kupitia kalima hii itakuwa ni usaidizi kwake kuweza kuwakumbusha vidhibiti vya Shari´ah na sifa ambazo inatakikana kwa msichana kukuwa juu yake.

Kadhalika ni ukumbusho kwa mama ambaye ni mchungaji katika nyumba yake na wasichana wake na kuwatengeneza. Wasichana wengi wanakuwa kwa tabia na sifa mbalimbali ambazo wamepata kutoka kwa wamama zao.

Kadhalika ni ukumbusho kwa walinganiaji ili waweze kuliwekea uzito hili, kutiliia umuhimu na kufanya juhudi katika kueneza sifa hizi tukufu, tabia zilizosifiwa na kazi iliyobarikiwa ili ziweze kupatikana kwa wasichana na wanawake katika jamii ya imani na majumbani.


Hili ni khaswa hivi leo wakati mwanamke ameshambuliwa kwa njia ambayo kamwe haijawahi kuonekana hapo kabla. Inafanyika kwa kutumia namna na njia mbalimbali. Malengo ni kutaka kumpotezea mwanamke heshima yake, utukufu wake, ukamilifu wake, fadhila zake, uzuri wake, imani yake, tabia yake na wema wake.

Hapo kabla ilikuwa ni vigumu sana kwa mwanamke kufikiwa na propaganda zinazoharibu, matamanio ya udanganyifu na maoni yaliyofungamana. Hilo lilikuwa likitendeka ima kwa kupitia rafiki mbaya au mfano wa hayo.

Ama leo mwanamke anafikiwa na uchafu na uharibifu wote wa duniani nyumbani kwake.


Hahitaji kutoka nje kwa ajili ya hilo. Sasa mwanamke anaweza kukaa chumbani mwake mbele ya TV, intaneti au magazeti machafu na akapata uchafu na shari zote katika moyo wake na fikra zake.

Mwanamke Ili aweze kuwa mwema, mtwaharifu, mwenye Dini na mwenye kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) analazimika kufunga madirisha, njia na mwanya wa kila shari na uharibifu.

Mwanamke ana majukumu makubwa kwa wale watu ambao anawasimamia. Suala hili linahitajia kuliwekea umuhimi mkubwa kabisa.

Katika kivuli cha hali hii na upungufu wa ukumbusho na ukumbusho wa imani, tabia nzuri na maelezo mazuri ambayo mwanamke anatakiwa kuwa nayo, wanawake wengi wamekuwa wadhaifu. Wametumbukia katika kuwa na upungufu katika haya na Dini na kuanguka katika upungufu mwingi na kuathirika.

Kalima hii ni kama tulivyosema ni kuhusu sifa za mke mwema. Ninamuomba Allaah Mtukufu, Mola wa ´Arshi kubwa, afanye iwe ya kheri na manufaa na afanye iwe ni ufunguo wa kheri ufunge shari na uongoze nyoyo, uzitengeneze nafsi na ufanye kuwepo mawasiliano na Mola wa walimwengu ili Radhi Zake na Mapenzi Yake viwezi kufikiwa na kuepuka yale yanayomkasirikisha na kumghadhibikisha (Jalla wa ´Alaa).



                                                        Kanuni ya sifa za mke mwema


Wakati tunapozungumzia kuhusu sifa za mke mwema na wema hatutakiwi kupuuza kanuni kubwa ambayo ni kanuni ya msingi ya kufikia wema, nayo ni kwamba wema hauwezi kufikiwa isipokuwa kwa mambo mawili:

Jambo la kwanza ni uafikishaji wa Allaah (Jalla wa ´Alaa), uongofu Wake, msaada Wake, usahali Wake na uafikishaji. Mwenye Kuongoza ni Allaah. Ndiye Muwafikishaji. Mambo yote yako Mikononi Mwake (Jalla wa ´Alaa).

Allaah (Ta´ala) Kasema:

 َدِ ت ْ ه ُ الْم َ و ُ َه فـ ُ ـه اللَّ ْدِ ه َ ن يـ َ ۖ ا ً م د شِ ْ ُّمر ًّا ي ِ ل َ و ُ لَه َ د َن ََتِ ل َ فـ ْ ل ِ ُ ْضل ن ي َ م َ و

“Ambaye Allaah Amemhidi, basi yeye ndiye aliyehidika. Na Anayempotoa (kwa vile mwenyewe ametaka kupotoka), basi hutompatia mlinzi wa kumuongoza.” (18:17)

 يٍم ِ ق َ ت ْ ٍط ُّمس ا َ ََٰل ِصر ِ إ ُ َ َشاء ن ي َ ي م ْدِ ه َ يـ َ و َّسََلمِ ا ِر ال َ ََٰل د ِ و إ ُ ْدع َ ي ُ ـه اللَّ َ و

“Na Allaah Anaitia kwenye Daarus-Salaam (nyumba ya amani, Peponi), na Anamhidi Amtakaye kwenye njia iliyonyooka.”(10:25)

Uongofu uko Mikono Mwake, wema uko Mikononi Mwake na uafikishaji uko Mikononi Mwake. Anayotaka huwa. Asiyotaka hayawi.


Jambo la pili ni kwamba mtu mwenyewe ajitahidi kufanya juhudi kufikia wema na kufuata sababu zake zinazopelekea katika hilo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekusanya kati ya mambo haya mawili wakati aliposema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth Swahiyh:

“Pupia katika yale yanayokunufaisha na umuombe msaada Allaah.”Muslim (2664)


Maana ya “Pupia katika yale yanayokunufaisha... “ ni kwa kufanya sababu zinazonufaisha na njia za kunufaisha ambazo hufikiwa kwazo wema na kupitia hayo unafikiwa uongofu.

Maana ya “... na umuombe msaada Allaah” ni kwa kumtegemea, kumuomba msaada Wake na kutaraji kutoka Kwake (Subhaanahu wa Ta´ala) kuwa Atakuwafikisha, kukupa ustawi na kukusaidia kufikia wema na msimamo. Hii ni kanuni kubwa ambayo ni pamoja na viumbe wote.

Kanuni nyingine ambayo ni lazima kuitanabahisha, nayo ni kuwa asli ya wema, elimu yake na njia ya kuuendea ni Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa ajili hiyo ni wajibu kwa kila ambaye anakumbusha na analingania katika wema na mtengenezaji kujengea kila kitu juu ya Kitabu cha Allaah (´Azza wa Jalla) na Sunnah za Mtume Wake Mtukufu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Allaah (Ta´ala) Anasema:

 م َ ْو أَقـ َ ي ِ لَِِّت ه ِ ي ل ْدِ ه َ َن يـ آ ْ ُر َٰذا الْق ـ َ َّن ه ِ إ

“Hakika hii Qur-aan inaongoza katika yaliyonyooka kabisa.”(17:09)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu ya Sunnah na uongofu wake:

“Nimewaachia mambo mawili ambayo mkishikamana nayo hamtopotea; Kitabu cha Allaah na Sunnah zangu.”al-Haakim (1/172). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´” (2937).




                                                  Mke mwema uhusiano wake na Allaah 


Kitu cha kwanza nitachoanza nacho ni yaliyotajwa kuhusu sifa za mke mwema katika Suurat an-Nisaa´:

 ُ ـه َظ اللَّ ِ ف َ ا ح َ ِ ِب ِب ْ ي َ ْلغ ٌت لِّ ظَا ِ اف َ ٌت ح ا َ ت ِ ان َ ُت ق ا َ ال َّصاِلِ َ ف

“Basi wanawake wema watiifu [kwa Allaah], wenye kuhifadhi (hata) wanapokuwa hawapo (waume zao) kwa Aliyoyahifadhi Allaah.”(04:34)


Katika sehemu hii ya Aayah Allaah Ameleta maelezo na sifa zote ambazo mwanamke mwema anatakiwa kuwa nazo. Andiko hili tukufu linatuonesha kwamba mke mwema ni yule mwenye sifa mbili:

Sifa ya kwanza inahusiana na uhusiano wake kwa Mola Wake.

Sifa ya pili inahusiana na uhusiano wake kwa mume wake. Uhusiano wake kwa Mola Wake ni katika Kauli Yake (Subhaanahu):

 ٌت ا َ ت ِ ان َ ق “... watiifu [kwa Allaah]... “

Ina maana ni mwenye kudumu katika kumtii Allaah, anahifadhi ´ibaadah na utiifu kwa Allaah, kutilia umuhimu faradhi za Uislamu na kuacha kuyaapuza. Yote hayo yanaingia chini ya Kauli Yake (Subhaanahu wa Ta´ala):

 ٌت ا َ ت ِ ان َ ق

“... watiifu [kwa Allaah]...

“ Sehemu ya pili katika Kauli Yake (Subhaanahu wa Ta´ala):ُ


 ـه َظ اللَّ ِ ف َ ا ح َ ِ ِب ِب ْ ي َ ْلغ ٌت لِّ ظَا ِ اف َ ح

“... wenye kuhifadhi (hata) wanapokuwa hawapo (waume zao) kwa Aliyoyahifadhi Allaah... ”


Ina maana anahifadhi haki za mume wake pindi anapokuwa hayupo na ushuhuda. Anamhifadhi katika mali zake, rafiki wa kitandani, haki zake wajibu wake:

 ُ ـه َظ اللَّ ِ ف َ ا ح َ ِ ِب ِب ْ ي َ ْلغ ٌت لِّ ظَا ِ اف َ ح

“... wenye kuhifadhi (hata) wanapokuwa hawapo (waume zao) kwa Aliyoyahifadhi Allaah... ”


Ina maana hawezi kufanikiwa kufanya hilo kwa sababu yeye ni mtu wa sawasawa, mwenye akili, fahamu na mwerevu, isipokuwa ni kutokana na uafikishaji wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kumrahisishia hilo. Hili linatukumbusha yale niliyotaja karibuni, nayo ni kwamba uzuri na wema ni kutokana na uafikishaji wa Allaah, usahilishaji Wake na Msaada Wake.


Katika Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

ٌت ا َ ت ِ ان َ ق

“... watiifu [kwa Allaah]... “

kunaingia ndani yake mwanamke ambaye anahifadhi faradhi za Uislamu. Kuna Hadiyth nyingi ambazo zimepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusiana na maana hii.

Miongoni mwazo ni yale aliyopokea Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh nambari. (3163).” yake kupitia Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Mwanamke akiswali [Swalah zake] tano, akafunga mwezi wake, akahifadhi tupu yake na akamtii mume wake, ataingia mlango wowote wa Peponi autakao.”


Imaam Ahmad amepokea katika “al-Musnad nambari. (1661)” yake kupitia kwa ´AbdurRahmaan bin ´Awf (Radhiya Allaahu ´anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanamke akiswali [Swalah zake] tano, akafunga mwezi wake, akahifadhi tupu yake na akamtii mume wake, ataambiwa: “Ingia Peponi kwenye mlango wowote wa Pepo uutakao.” 


Tunampa hongera mwanamke wa Kiislamu kwa ahadi hii tukufu na fadhila kubwa na kheri ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Amemuahidi nayo. Inahusiana na mambo mane tu ambayo anaweza kuyahesabu kwa kutumia mkono wake mmoja kwa vidole vyake na si kwa kutumia [mikono] miwili. Akiishi kwa kuyahifadhi mambo mane ataambiwa siku ya Qiyaamah:


 “Ingia Peponi kwa mlango wowote wa Pepo uutakao.”


Hivi kweli mwanamke ambaye anajitamania kheri juu ya nafsi yake si awekee uzito na kutilia umuhimu sifa hizi na kudhibiti matendo haya? Anatakiwa kuhifadhi Swalah zake, Swawm, tupu na haki za mume wake ili aweze kushinda ahadi hii tukufu na fadhila na kheri hii kubwa ili aweze kuambiwa siku ya Qiyaamah:

“Ingia Peponi kwa mlango wowote wa Pepo uutakao.” 


Msingi wa wema wa mwanamke uko katika wema wake kwa Mola Wake kwa kumtii, kujikurubisha Kwake na kudhibiti ´ibaadah Zake. Wema na msimamao huu ndio siri ya mafanikio yake, kushinda kwake na uafikishaji katika maisha yake kukiwemo na maisha yake ya ndoa, watoto wake kuwa wema na kizazi chake na kuishi kwake maisha ya baraka na mazuri.


Kwa ajili hiyo ndio maana ikawa ni jambo lililosisitizwa kwa yule mwenye kuitakia nafsi yake kheri na kwa wasimamizi ambao wanawatakia wasichana wao kuwalea wanawake juu ya wema, msimamo, kuhifadhi ´ibaadah, faradhi za Uislamu na khaswa Swalah tano na kufunga mwezi wa Ramadhaan na kujitenga mbali na mambo yote yanayoathiri utwaharifu wa mwanamke na utukufu wake.

Ni hayo ndio yamebainishwa katika Hadiyth hii:

“... Akahifadhi tupu yake... “


Mwanamke kuhifadhi tupu yake ni jambo linalohitajia kutoka kwake na kwa walii wake kufunga milango na njia zote kwa yale yanayoharibu, yanayopelekea katika shari na kusababisha madhambi. Hili ni jambo kubwa ambalo kwa kila yule mwenye kuitakia nafsi yake kheri anatakiwa kuilea nafsi yake juu ya hilo.


Mwanamke anatakiwa kuihifadhi nafsi yake daima katika kumtii Allaah, kumuabudu Allaah na kujikurubisha Kwake (Subhaaahu wa Ta´ala) kwa yale yanayomridhisha katika maneno mema na matendo mazuri. Allaah Akimneemesha mume mzuri na wa sawa, ni juu yake kumcha Allaah kwa kuhakikisha anachunga haki za mume wake tokea ile siku ya kwanza ya ndoa.


Hili linawajibisha kukumbusha juu ya suala ambalo kosa lake limekuwa ni lenye kuenea na kusambaa. Nalo linahusiana na israfu na ubadhirifu unaokuwa katika usiku ule wa ndoa na katika matumizi ya ndoa. Hili ni jambo ambalo khatari yake ni kubwa na madhara yake ni makubwa mno. Wanawake wengi wanapoelekea katika kutaka kuolewa wanachozingatia ni yale ya nje na wanawake wa rika sawa naye.


Wanatazama ni nini walichofanya wanawake wengine katika ndoa mbalimbali. Wanafikiria kwa njia hiyo na hivyo kunakuwa israfu na ubadhirifu. Wanapoteza vingi na pesa nyingi katika visivyokuwa na maana. Aidha kunaweza kuwepo hata maovu na mambo ya haramu. Kwa ajili hiyo mwanzo huu unakuwa na utangulizi wa ndoa ni sababu ya ukosefu wa baraka na kheri.


Hali huwa sivyo ikiwa mwanamke na familia yake watajitenga mbali na hayo, kujiepusha na israfu, mambo ya maasi na madhambi na wakafanya matumizi kuwa rahisi na pasina israfu wala ubadhirifu. Katika hali hii huja kheri na kufikiwa baraka. Imekuja katika Hadiyth Swahiyh katika “as-Sunan” Abu Daawuud Nambari. (2117). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika “as-Swahiyhah” (1842). imepokelewa na ´Uqbah bin ´Aamir (Radhiya Allaahu ´anhu) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:


“Bora ya ndoa ni ile iliyo rahisi.” 

Katika Hadiyth nyingine imesemwa: “Wanawake walio na baraka zaidi ni wale wenye matumizi rahisi.”Ameipokea Ahmad katika “al-Musnad”, nambari. (25120), an-Nasaa´iy katika “al-Kubraa”, nambari. (9274) kupitia Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anha)

Wanawake bora ni wale walio rahisi. Kwa ajili hii ndio maana inatakikana kwa mwanamke na kwa wazazi wake wahakikishe ndoa iwe rahisi na isiwe na ugumu, unyenyekevu na sio kiburi, nzuri na yenye utulivu na kusiwe israfu na ubadhirifu. Mambo yote haya yana taathirika katika maisha ya ndoa kwa uzuri na ubaya.


Ikiwa ndoa ni rahisi na ikafanywa kuwa sahali na kujiepusha na mamabo ya israfu, hukabiliwa na baraka na kheri. Kama ndoa iko na israfu, ubadhirifu, maasi na aina mbalimbali ya dhambi, ni baadhi ya sababu kubwa ya kukosekana baraka na tunaomba Allaah Atukinge.



                                                   Mke mwema uhusiano wake na Shetani 



Sifa nyingine ambayo mke mwema anapaswa kuwa nayo ni kwamba atahadhari na Shetani aliyefukuzwa. Kazi ya Shetani katika maisha haya ni kuharibu. Anaharibu Dini, tabia, mu´amala, mshikamano, udugu na lililo la kheri. Kila siku anatuma wajumbe na askari kutimiza kazi hii.


Zingatia Hatiyth hii katika “as-Swahiyh” ya Muslim imepokelewa na Jaabir bin ´Abdillaah(Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:


“Iblisi hukiweka kiti chake katika maji. Kisha anatuma vikosi vyake. Yule mwenye nafasi kubwa kwake ni yule mwenye fitina kubwa. Pindi mmoja wao anamjia anamuuliza aliyofanya. Wakati anaposema aliyofanya, anamwambia: “Hujafanya kitu.” Wakati mwingine anamjia na kusema: “Sikumuacha mpaka nimehakikisha nimemfarikanisha yeye na mke wake” hivyo anamchukua na kumwambia: “Wewe ni mzuri ulioje!” Muslim (2813).


Anawatuma askari na wajumbe ili waende kuharibu. Anayekuwa karibu na yeye ni yule ambaye anasababisha matatizo kati ya watu. al-A´mash amesema kwamba Shetani anamkumbatia na kuchukua askari ambao wanafarikanisha kati mwanamke na mume wake.


Mwanamke mwema anatakiwa kufahamu na kuelewa uhakika huu. Hali kadhalika mume. Wote wanapaswa kufahamu kwamba kuna adui aliyejificha. Anakuona, lakini wewe huwezi kumuona. Anapita ndani ya mwili wako kama damu inavyopita kwenye mishipa.


Anapuliza na kutia wasiwasi. Anapanga hila na njama. Anafanya yote hayo bila ya wewe kumuona. Anauzungumzisha moyo wako wewe mume na moyo wa mke. Anakuja na mashaka yanayopelekea katika uadui. Ana njia nyingi za ufanya kazi wake.


Kwa ajili hii imekuja katika Sunnah jinsi ya mtu atakavyojikinga kutokana na Shetani wakati mtu anapoingia nyumbani kwake, wakati wa maingiliano, wakati wa chakula, wakati anapokuwa na hasira na mambo mengine yote ambayo mtu anahitajia kujikinga kutokana na Shetani ili Shetani asiweze kuwa na ushirikiano wowote na watu wa nyumbani kwake, nyumba yake na watoto wake.


Hivyo anahitajia mtu kuikinga nafsi yake na Adhkaar zilizobarikiwa, Qur-aan Tukufu, Du´aa zilizopokelewa na kuhifadhi utiifu na ´ibaadah za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).


Mke mwema anapaswa kujihadhari na kampeni za Shetani na wasiwasi wake autiao katika nasfi na ambao unaharibu uhusiano na maisha ya ndoa.


Ni familia ngapi na nyumba ambazo amefarikanisha daima kwa kumtii Shetani na kufuata wasiwasi wa Shetani? Lau kila mmoja angeliomba kinga kwa Allaah kutokana na Shetani aliyefukuzwa na kujiweka na kujitenga mbali na uchochezi wake na wasiwasi wake kusingelitokea mambo hayo na mfarakano huo.


Ni majumba mangapi kumetokea mfarakano kwa sababu ya kumtii Shetani? Kisha baadaye huyu muharibifu – askari wa Shetani – anaenda kwa Iblisi ili aweze kupata nafasi ya kuwa karibu naye pindi atakapomuhadithia alivyofarikanisha kati ya muma na mke.


Kuna kitu cha manufaa ambacho ni lazima kukumbuka. Huyu adui aliyejificha ambaye anakuona na ambaye wewe huwezi kumuona na uzowefu mkubwa. Leo wakati kunapozungumziwa baadhi ya waajiriwa wa kampuni na uzowefu wao mara nyingi huwa ni uzowefu wa miaka khamsini au sitini. Lakini uzowefu wa Iblisi wa kupotosha, kuzuia watu na njia ya Allaah na kueneza uadui kati ya watu? Ni uzowefu wa maelfu ya miaka.


Ni watu wangapi wamekufa na kuzikwa baada ya kuwa ni wafungwa wa Shetani na kutumbukia katika uharibifu na upotoshaji wake? Kwa ajili hii ndio maana ni lazima nyumba ya Muislamu ajikinge yeye mwenyewe na kuiweka mbali na Shetani aliyefukuzwa.



Tutaendelea.......Usikose  Sehemu ya 2  In  Shaa Allaah..................

from fisabilillaah.com https://ift.tt/2E1BATl
via IFTTT

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...