Translate

Alhamisi, 29 Novemba 2018

Kuwa makini na utapeli: upotoshaji katika ‘tiba ya Kisunna’

Kitambo sasa tangu iingie tiba dhidi ya majini na mashetani ijulikanayo kama ‘tiba ya kisunna’ na wengine wakiita ‘tiba mbadala.’ Lakini, je tiba hii kweli inakidhi viwango vya kuitwa tiba ya Kisunna?

Ni jambo la kushukuriwa kwamba wanaojishughulisha na tiba hii ya Kisunna wamerejesha imani ya watu kuhusu Qur’an na Sunna kwani kuna kipindi, waliokumbwa na mashetani walikimbilia katika mahubiri ya Wakristo na huko waliombewa ‘Kwa jina la Yesu’!!

Ilifikia hatua waathirika hao kuvalishwa misalaba na kuambiwa wachome Qur’an na vitabu vyote vya dini ya Kiislamu na hata waachane na dini hii tukufu. Ni baada ya kufanya hivyo, waliahidiwa ndiyo wangetolewa hayo mapepo.

Kwa hiyo, tiba ya waathirika hao kwa Qur’an na Sunna kupitia aya za Ruqyah na dua mbali mbali [adhkaari] za kinga ni hatua muhimu sana katika kuwanusuru Waislamu dhidi ya njama za kuwaritadisha.

Wapo walioingilia fani

Pamoja na kuingia kwa tiba ya Sunna nchini Tanzania, kwa bahati mbaya wapo watu waliongilia fani hii ambayo si fani yao na hivi sasa wanaitia dosari kubwa tiba nzuri ya Kisunna kutokana na jinsi wanavyoifanya tiba hiyo.

Baadhi ya vijana wanaofanya tiba za Kisunna hawafanyi kwa mujibu wa Uislamu. Wameingia katika fani hii pasina ujuzi wa A’qida/itikadi sahihi, na wakaanza kutibu watu kwa Qur’an, ambayo baadhi yao hawajui hata kuisoma vizuri kwa hukumu zake wala kujua tafsiri yake.

Wengine wanajinasibu kwa majina yanayoonesha wana elimu kubwa kuhusu majini na mashetani kiasi cha kuitwa ‘Kiboko ya majini,’ pengine wengine hawajui hata Nawaaqidhu Al islam [vinavyotoa mtu katika Uislamu]. Wengine hawajui hata hukumu za udhu na Swala ipasavyo.

Kikubwa walichojifunza ni jinsi ya kuzisoma aya za ruqya tu au kusoma kitabu fulani juu ya jinsi ya kufanya ruqya kisha nao kuanza kutibu watu! Tahamaki! Wameangukia katika mambo mengi yaliyoharamishwa pasina kujua. Matokeo yake, kwa sasa, kwa kiasi kikubwa umeenea uzushi juu ya tiba za Kisunna kiasi cha kuanza tena kuwatoa l imani watu walioanza kujenga imani juu ya uwezo wa Qur’an na Sunna kutibu watu waliokumbwa na mashetani.

Sababu mambo kwenda harijojo

Sababu ya tiba za Kisunna kwenda harijojo ni mambo mawili, la kwanza ni mfanyatiba ya Kisunna kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu mambo ya dini, na la pili ni kuamini kila kisemwacho na shetani akishapanda kichwani kwa mgonjwa na hatimaye kuleta ugombanishi.

Kuna wakati, jini aliyepanda kichwani kwa mgonjwa huanza kumpa maelekezo au nasaha yule anayemtibu mgonjwa na kusema, kwa mfano, huyu mgonjwa hali yake ni hii kwa hiyo msomee sura fulani. Wakati mwingine, jini husema, huyu anayo majini kadhaa na unatakiwa umwandikie Qur’an kwenye mwili wake. Basi mwenye kumtibia mgonjwa hushika maelekezo hayo na wakati mwingine kuyatekeleza kama yalivyo na kuingia katika mtego wa shetani.

Wapo wanaotibia watu kwa tiba za Kisunna waliojikuta wakiandika aya za Qur’an kwenye sehemu za siri za wagonjwa jambo ambalo ni haramu kabisa kwani Qur’an haitumiki hivyo katika tiba.

Yaliyo haramu katika tiba kwa Qur’an

Kuna mambo ambayo ni haramu kufanywa katika tiba kwa kutumia Qur’an. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuandika herufi zisizoeleweka maana yake katika mwili wa mgonjwa, kuandika herufi fupifupi au zilizogeuzwa kwenye paji la uso au vidole vya mgonjwa.

Mengine yaliyo haramu ni kuandika jina la Allah Aliyetukuka kwenye kitambaa kisha kukichoma halafu mgonjwa anavuta moshi wake, kuchoma ubani au udi wakati wa kumtibu mgonjwa, kung’amua aina ya jini kwa kumuangalia mgonjwa kwenye paji la uso [kupima mgonjwa], mwanaume kubaki faragha na mgonjwa wa kike, kusoma aya za ruqya kwenye maji ya chumvi kisha kunyunyizia kuzunguka nyumba na mfano wa hayo.

Ni muhimu kwa wanaojishughulisha na tiba za Kisunna kuchunga sana wasitie doa Sunna ya Mtume kwani kupitia tiba zao aidha Waislamu watapata heshima au watajidhalilisha mbele ya wanadamu.

Siku hizi wamezuka wafanya tiba za Kisunna wengi na haijulikani wamesomea wapi. Mtu anaibuka tu na kuanza kutibu watu. Ukiongeza na matumizi ya njia ya mawasiliano kama runinga na simu za kiganjani, wengine wameshakuwa maarufu huku na hawajui kitu, kuhusu tiba za Kisunna, hususan maadili yake.

Ni vema Waislamu wakafanya juhudi kupambanua kati ya tiba za kisuna, tiba mbadala, wachawi, na matapeli wanaotumia jina la tiba za Kisunna kwa maslahi yao kupitia jina la kufanya ruqya ya kisharia ambao ni lazima wawe ni watu wenye kushikama na kikweli kweli na Sunna za Mtume kwa maneno yao na vitendo vyao vya kila siku.

 



from TIF https://ift.tt/2DRUjQi
via IFTTT

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...