Translate

Jumatano, 28 Novemba 2018

Sifa za Mke Mwema - Sehemu ya 2

                                                                ص فات ال زوج ة ال صال حة 

                                                                Sifa za Mke Mwema

                         Mwandishi : Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad.

                                                  Mfasiri: Abu Bakr Khatwiyb al-Atrush.




Tunaendeleaa.........


                                         Mke mwema anatakiwa kumfurahisha mume.



Katika sifa zingine za mke mwema ni kwamba anamfurahisha mume wake pindi anapomtazama sura yake, muonekano wake, sifa zake na mavazi yake yamfurahishe pindi mume wake anapomtazama. Anapaswa awe ni mwenye kujiandaa kwa kumtii na kutimiza maamrisho yake bila ya kuchukia na bila ya kuwa na kiburi. 


Zingatia Hadiyth katika “as-Sunan” ya an-Nasaa´iy Nambari. (3231). Imaam al-Albaaniy ameisahihisha katika ”as-Swahiyhah” (1738) imepokelewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhu) ambaye ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa juu ya mwanamke bora. Akajibu: 


“Ni yule mwenye kumfurahisha [mume wake] pindi anapomtazama, anamtii pale anapomuamrisha na haendi kinyume juu ya nafsi yake mwenyewe na mali yake dhidi ya anayoyachukia.al-Bukhaariy (5954) na Muslim (2107).


Namna hii ndivyo anavyotakiwa kuwa kwa njia ya sura na sifa. Anatakiwa kutilia uzito mkubwa juu ya sura na muonekano wake wakati anapokuwa mbele yake. Kadhalika anatakiwa kutilia uzito na kutilia umuhimu kwa kutimiza maamrisho yake, hamu yake na haja zake. 


Kwa masikitiko makubwa wanawake wengi wanatilia umuhimu kujipamba na kujipodoa tu wakati wanapotaka kutoka nyumbani kwenda katika mnasaba wa sikukuu, mkusanyiko na mfano wa hayo. Lakini wakati mume anapoingia nyumbani anamkuta katika mavazi mabaya na kunuka. 


Nywele zimevurugika na hazikutengenezwa. Anamkuta kwa sifa ambazo zinamkimbiza kwake. Halafu anakuwa ni mwenye kuumia kwa yeye kila siku kujipamba pindi anapotoka nyumbani bila hata kupata moja ya kumi. Vipi mwanaume atamtamani mwanamke kama huyu ambaye hizi ndizo sifa zake? 


Ni mahaba sampuli gani ambayo atakuwa nayo kwa mwanamke ambaye yuko namna hii? Hii ni dalili inayoonesha ujinga wa mwanamke na upungufu wa akili yake kwa kuhakikisha maisha ya ndoa na mafanikio yake. Aidha kuna wanawake wengi ambao ni waasi na wapekutevu. 


Wanawapuuza waume zao na kuwakasirikisha. Kunalalamikiwa sana juu ya tabia zao kwa waume zao na wengine. Mwanamke huyu anakuwa ni mwenye kuleta maisha magumu, maisha ya taabu na maisha ya udhaifu nyumbani kwake na anakuwa ni mwenye kuizika nafsi yake mwenyewe kwenye kaburi.

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh”Nambari. (715)  yake kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: 

“Mmoja wenu anapofika wakati wa usiku [kutoka safari] asiwajie familia yake.” 


Asimshtukizie mke usiku. Kwa nini? Anasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): 


“Ili mwanamke ambaye mume wake alikuwa hayupo aweze kujinyoa na mwanamke wa nywele zilizovurugika aweze kuchanua nywele zake".

Hapa kuna funzo tukufu kwa mwanamke. Nalo ni kwamba anatakiwa kumkaribisha mume wake kwa ukamilifu wa usafi, sura nzuri na mkutano mzuri. Hili khaswa pale ambapo mume wake alikuwa hayupo au amesafiri. Hili linahitajia kwa mwanamke kuweza kujiandaa na kujitayarisha. Hili linahusu hata kufanya utaratibu wa nyumba na muonekano wake. Mama wa waumini ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anha) ameelezea: 

Alikuja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutoka katika safari. Nikawa nimefunika mapazia yangu kwa kusahua na yalikuwa na picha. Wakati (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipiona akairarua na kusema: 


“Watu watakaokuwa na adhabu kali siku ya Qiyaamah ni wale wanaoigiza viumbe wa Allaah. Tukafanya mto mmoja au mito zaidi.”al-Bukhaariy, nambari. (5954), Muslim, nambari. (6107).


Kwa nini aliweka mapazia haya? Kwa kuwa alitaka atakapoingia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nyumbani akute nyumba na yeye mwenyewe katika sura nzuri. 


Katika Hadiyth hii tunapata faida kwamba mwanamke anatakiwa kutengeneza nyumba yake na kuipanga kama ambavyo vilevile inatakiwa kwake kujitayarisha maandalizi kwa njia ya kikamilifu na kukutana na mume wake kwa njia nzuri. Hizi zote ni sifa zilizokuja katika Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) za mwanamke na mke mwema.


Miongoni mwa hayo ni yale yaliyopokea at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Awsatw”Nambari. (1743). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika “Swahiyhah”, nambari. (3370) kupitia Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anhu) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: 


“Je, nisiwaeleze wanawake wenu Peponi?” 


Yaani mke mwenye sifa zinazosifika na kazi yenye kubarikiwa akawa ni mwenye kustahiki kuwa Peponi. Akaendelea na kusema: 


“Kila mwanamke mwenye mahaba na mwenye rutuba ambaye, pindi anapokasirika au akafanyiwa vibaya au mume wake akakasirika, anasema: “Naweka mkono wangu kwenye mkono wako. Sintosinzia mpaka utapofurahi.” 


Bi maana hatofumba macho, hatolala wala kufurahi mpaka awe radhi naye. 


Kwa masikitiko makubwa kuna wanawake wanaolala pasina kujali waume zao wamekasirika usiku wa kwanza, usiku wa pili, usiku wa tatu, usiku wa kumi au mwezi mzima. Kana kwamba jambo hili halimuhusu kabisa. Kana kwamba hatokuja kukutana na Allaah (Subhanaahu wa Ta´ala) na kumhesabu kwa matendo haya anayoyafanya.



                                                Mke mwema anatakiwa kumtii mume. 



Katika sifa za mke mwema ni yale yaliyopokelewa katika “as-Sunan” ya alBayhaqiy 7 7/82. Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”as-Swahiyhah” (3380). kupitia kwa Abu Udhaynah ambaye kaeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: 


“Wabora ya wanawake zenu ni wale wenye mahaba na wenye rutuba walio na maafikiano na wanausia kumcha Allaah. Waovu ya wanawake zenu ni wale wenye kuonyesha mapambo yao na wenye kiburi na ni wanafiki. Hakuna yeyote katika wao atakayeingia Peponi isipokuwa watakuwa ni mfano wa kiasi cha jogoo zilizo na madoa meupe kwenye mbawa na makucha.” 


Zitazame hizi sifa alizo nazo mke mwema. 


“...wenye rutuba... “ Bi maana azae watoto wengi. Ni sifa yenye kusifika kwa mwanamke. Mwanamke huyu ni katika wanawake bora. 


Ikiwa mwanamke yuko na ila yoyote au maradhi ni jambo ambalo halitomdhuru kwa kuwa sio jambo ambalo amezembea yeye au amefanya kwa khiyari yake. Allaah Hatomhesabu kwa hilo. Hili halimdhuru na wala haliathiri chochote katika wema wake.


 Ama ikiwa mwanamke ni mwenye rutuba lakini akawa ni mwenye kuzuia ujauzito na watoto, anadhurika kwa hili. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: 

“Oeni wanawake wenye mahaba na rutuba. Mimi nitajifakhari wingi wenu kwa Ummah zingine siku ya Qiyaamah.”Ahmad (12613), kupitia Anas (Radhiya Allaahu ´anhu). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika “Irwaa´-ul-Ghaliyl” (1784).


Linalotakikana kwa mwanamke ni kujitahidi kupata watoto na kutilia uzito katika kuwalea watoto na kuwaangalia. Vilevile ahesabu thawabu kutoka kwa Allaah kwa kupatikana katika jamii watoto wema na walinganiaji wanaotengeneza. Ahesabu hilo tokea siku ile ya kwanza anapoolewa. Azungumze baina yake yeye na Allaah Amkirimu wavulana watakaokuja kuwa maimamu wa uongofu, wanachuoni wa waislamu na walinganiaji katika kheri. Kwa hili aandikiwe thawabu kubwa kwa nia yake nzuri na kila kinachofanya hilo. 


“... walio na maafikiano... “ Bi maana asiwe ni mkali na mgumu. Anatakiwa kuwa msikivu na mtiifu. Hatakiwi kuwa ni mwenye kiburi na majivuno. Hatakiwi kumdharau mume. Hatakiwi kuwa muasi na mpekutevu. 


“...wanausia... “ Bi maana mwenye kumuusia na kumliwaza mume wake na kusimama karibu naye. Anatakiwa awe ni mwenye kumsaidia katika kheri na katika kumtii Allaah na kila kinachofanya kuleta furaha na mafanikio. 


“... kumcha Allaah... “ Bi maana sifa hizi zinakuwa ni zenye kunufaisha kwanza pindi mwanamke atakapomcha Allaah (´Azza wa Jalla). Lau atakuwa ni mwenye mahaba, rutuba, maafikiano na mwenye kuusia kwa kutafuta mambo ya kidunia na sio kwa ajili ya kumcha Allaah, sifa hizi hazitoleta manufaa yoyote wala hazitomfaa. Sifa hizi zitamnufaisha tu ikiwa anazifanya kwa kutafuta kupata Radhi za Allaah (´Azza wa Jalla) na akaishi juu ya uchaMungu. 


“Muovu ya wanawake zenu ni wale wenye kuonyesha mapambo yao... “ Bi maana wale wenye kuonyesha mapambo yao na kutoka nje kwa kujipodoa, msafi, mzuri, kwa kujiweka manukato na kujipodoa ili Shetani aweze kumfuata nyuma yake na kuharibu jamii. Mwanamke mwenye kutoka kwa sifa hizi anafanya hivyo ili apate kuwa mmoja katika askari wa Iblisi na kumsaidia kuiharibu jamii. Malengo ni kusambaza fitina na kueneza machafu kwa waumini. 


“... wenye kiburi... “ Bi maana walio na kiburi. Kuna mafungamano baina ya kuonyesha mapambo na kiburi. Mwanamke anayekwenda nje barabarani na kwenye masoko na ni mwenye kuonyesha mapambo, kajipodoa, kajitia manukato na kujipendezesha hawezi kwenda hivyo wakati huo huo akawa ni mwenye haya na mnyenyekevu kwa Allaah (Ta´ala). Anatoka hali ya kuwa ni mwenye kiburi, kujiweka juu na mwenye jeuri. Anakuwa ni mwenye kuzowea, katika muonekano wake na sura yake. Hivyo kuna mafungamano baina ya kuonyesha mapambo na kuwa na kiburi kama jinsi kuna mafungamano baina ya kuwa na heshima na haya.



Mwanamke mwenye heshima anakuwa na haya kamilifu. Moyo wake unakuwa ni wenye kujaa haya. Mwanamke mwenye kuonyesha mapambo yake anakuwa amevua Jilbaab ya haya na badala yake anavaa Jilbaab ya kiburi, kujiona na kiburi. Linamdhuru yeye, maisha yake ya ndoa na maisha yake yote. Ndio maana mwenye kuwa namna hiyo akasifiwa kuwa ni muovu katika wanawake. 


Kasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): 


“Muovu ya wanawake zenu ni wale wenye kuonyesha mapambo yao na wenye kiburi na ni wanafiki. Hakuna yeyote katika wao atakayeingia Peponi isipokuwa watakuwa ni mfano wa kiasi cha jogoo zilizo na madoa meupe kwenye mbawa na makucha.” 


Lini unaona jogoo ilio na madoa meupe kwenye mbawa zake na makucha yake? Ni zaidi ya mara kidogo sana kupata jogoo namna hiyo. Mara nyingi unaona jogoo yote huwa mweusi. Anasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): 


“Hakuna yeyote katika wao atakayeingia Peponi isipokuwa watakuwa ni mfano wa kiasi cha jogoo zilizo na madoa meupe kwenye mbawa na makucha.” 

bi maana ni idadi ndogo sana ya wanawake kama hawa watakaoingia Peponi. Kwa kuwa aina hii ya jogoo ni ndogo sana. 

Hadiyth hii inafanana na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): 

“Wanawake! Toeni Swadaqah kwa wingi na mumuombe Allaah mswamaha. Nimeona Moto nyinyi ndio wakazi wengi wa Motoni.”al-Bukhaariy (304) kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) na Muslim (79) kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa).


Kwa nini ameona wakazi wengi wa Motoni ni wanawake? Utakaposoma katika Sunnah kuhusu sifa hizi za wakazi wabaya wa Motoni utaona kuwa wanawake wengi wanapuuza na hawajali kabisa. Kana kwamba hatosimama mbele ya Allaah siku ya Qiyaamah na kumhesabu kwa hilo. Anaweza kufikiwa na Hadiyth na ujuzi juu ya suala hili, lakini anachojali tu yeye ni matamanio yake na matakwa yake.


Kuna Hadiyth nyingi zimekuja kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambazo zimetaja sifa za mwanamke anayelaumika. Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) anasema: 


“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemlaani mwanamke anayerefusha nywele na mwenye kurefushwa, mwanamke anayepiga chake (tattoo) na mwenye kupigwa chale.”al-Bukhaariy (5947) na Muslim (2124)


Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema: 


“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wanaume wanaojifananisha na wanawake na wanawake wanaojifananisha na wanaume.”al-Bukhaariy (5885).


Mbali na Hadiyth hizi na zingine zinazomlaani mwanamke kwa sifa mbalimbali utaona ni wanawake wangapi wanaosikia laana na kuwekwa mbali na Rahmah ya Allaah hata hivyo hawajali kabisa. Kana kwamba hawatosimama mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kuulizwa juu ya hayo. 


Kana kwamba haitokuja siku ambapo atawekwa ndani ya shimo na kufunikwa na mchanga na kusimama mbele ya Mola Wake kwa matendo yake. Anapuuza yote haya. Hafikirii lolote. Hamu yake kubwa anachojali ni kujipodoa na kujipamba hata kama kile anachokifanya ni kumuasi Allaah, kwenda kinyume na maamrisho ya Allaah na kujiweka mwenyewe katika Ghadhabu na Hasira za Allaah (Tabaaraka wa Ta´ala). 


Kuna sifa zenye kulaumika kumekuja ubainishaji wake katika Sunnah kwa wanawake ili mwanamke mwema aweze kuwa katika hadhari. Malengo la mwanamke kuzijua sifa hizi ni ili aweze kujiepusha nazo. Mshairi anasema: 

Nimejifunza shari sio kwa ajili [ya kuitaka hiyo] shari, kwa ajili nijitenge nayo Yule asiyetofautisha kati ya jema na shari hutumbukia ndani yake.



                                 Mke mwema anatakiwa kutofanya upungufu katika haki za mume




 Katika sifa za mke mwema ni kutofanya upungufu katika haki za mume wake. Anatakiwa kutilia uzito na juhudi katika kumtumikia. Zingatia juu ya hili ambalo an-Nasaa´iy amepokea katika “as-Sunan al-Kubraa”8913 na Ahmad (19003). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”as-Swahiyhah” (2612). kupitia kwa Huswayn bin Mihsan kutoka kwa shangazi yake ambaye ameeleza ya kwamba aliingia kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutekeleza haja. Baada ya kumaliza haja yake akamwambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): 


“Je, wewe una mume?” Akasema: “Ndio.” Akamuuliza: “Uko vipi kwake?” Akasema: “Ninamfanyia kila kitu.” Akamwambia: “Tazama ulivyo kwake. Kwani yeye ndio Pepo yako na Moto Wako.”8913 na Ahmad (19003). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”as-Swahiyhah” (2612).


Ni lini mume wa mke anakuwa ni Pepo yake na ni lini anakuwa ni Moto wake? Hapa ni lazima kwa mwanamke kufahamu uhakika huu na jambo hili kubwa. 

“Uko vipi kwake?” Una ya wajibu na wewe ni mja wa Allaah. Kuna Pepo na Moto. Allaah (´Azza wa Jalla) Amekuamrisha na kukuwajibishia kutimiza haki hizi za mume. Zitimize. Zitekeleze kwa njia nzuri kabisa na kikamilifu ili kumtii Allaah na kufikia Radhi Zake (Subhaanahu). Timiza wajibu wako na muombe Allaah haki zako: 


“Kwani yeye ndio Pepo yako na Moto Wako.” 



                                Mke mwema hamtii mume wake uzito katika matumizi. 



Katika sifa za mke mwema ni kutomtia mume uzito kwa matumizi na kutumia mali ya mume kwa israfu na ubadhirifu. Anatakiwa kuwa mkati na kati: 


: ً ام َ َو َك قـ ِ ل ٰ َْ َْي ذَ َن بـ َكا َ وا و ُ ُر تـ ْ ق َ يـ ْ ََل َ ُوا و ِرف ْ ُس ي ْ ُوا ََل َق ذَا أَنف ِ إ َ ين الَّذِ َ و 


“Na wale ambao wanapotoa huwa hawafanyi israfu na wala hawafanyi uchoyo na wanakuwa wastani baina ya hayo.” (25:67).


Wacha tuzingatie katika mlango huu yale ambayo Abu Sa´iyd na Jaabir wamepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba siku moja alisimama na kukhutubu kwa kirefusha na akataja mambo ya duniani na Aakhirah na akasema: 


“Wakati Wanawaisrael walipoangamia mara ya kwanza ilikuwa ni mwanamke wa fakiri mmoja alikuwa akimkalifisha [mume wake] mavazi na vipodozi yale anayokalifisha mwanamke wa tajiri. Kulikuwa mwanamke mmoja mfupi ambaye alikuwa akitumia mbao mbili za miguu na alikuwa na pete yenye kufungwa ambayo alikuwa akiijaza miski. Akatoka nje kati ya wanawake wawili warefu. Wakatuma mtu awafuate [hawa wanawake watatu]. Akawajua wale wanawake wawili warefu na akawa hakumjua yule mwanamke wa miguu ya mbao.”Ibn Khuzaymah katika ”Kitaab-ut-Tawhiyd” (487). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”as-Swahiyhah” (591).


Wakati wanaisrael walipoangamia ilianza kwa mwanamke wa fakiri mmoja kumkalifisha mume wake vipodozi na mapambo ambayo mwanamke wa tajiri anamkalifisha mume wake. Tazama huyu mwanamke mfupi amevyofanya israfu, ubadhirifu wa mali katika mambo yasiyokuwa na faida, udanganyifu na kutokinaika na yale Aliyomuandikia Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Mwanamke mwenye kuvaa viatu vya kisigino kirefu anakumbusha huyo mwanamke. al-Lajnah ad-Daaimah wametoa fatwa ifuatayo: 


“Kuvaa viatu vya kisigino kirefu haijuzu. Vinamtia mwanamke katika khatari. Shari´ah imemwamrisha mtu kujiepusha na madhara. Allaah (Ta´ala) Amesema:


كة ل ْ ََل التَّـه ِ إ ْ ي ُكم دِ ْ أَي ِ ُوا ب ُْلق ََل تـ َ و  


“Wala msijitupe kwa mikono yenu katika maangamizi." (02:195)

” ْ ُكم َ ُس ُوا أَنف ل ُ تـ ْ َق ََل تـ َ ۖ ا و ً يم َحِ ر ْ ُكم ِ َن ب َكا َ ـه َّن اللَّ ِ إ 


“Wala msijiue. Hakika Allaah kwenu ni Rahiymaa (Mwenye kurehemu).”  (04:29)


Vilevile vinamuonesha mwanamke kuwa mrefu na makalio zaidi ya alionayo. Ni udanganyifu na kuonyesha baadhi ya mapambo ambayo imeharamishwa kuyaonesha. 



                                    Mke mwema hatakiwi kukufuru neema kwa mume wake 



Katika sifa za mke mwema ni kuwa si mwenye kukufuru neema anazopewa. Kwa msemo mwingine ni kwamba hakufuru neema ambazo Allaah (Tabaaraka wa Ta´ala)Anazompa kupitia mume wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: 

“Yule asiyewashukuru watu hamshukuru Allaah.”Ahmad (7939) na Abu Daawuud (4811) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhu). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swhaiyh katika ”as-Swahiyhah” (416). 


al-Bukhaariy amepokea katika “al-Adab al-Mufrad” kupitia kwa Asmaa´ bint Yaziyd al-Answaariyyah ambaye amesema: 


“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinipitia wakati nilikuwa nimesimama na kundi la wanawake wenye umri mmoja nami. Akatusalimia na kusema: “Tahadharini na kukufuru neema.” Nikasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni nini maana ya kukufuru neema?” Akasema: “Huenda mmoja wenu ndoa yake ikaakhirishwa kisha baadaye Allaah Akamruzuku mume na akapata naye watoto. Wakati anapokuwa ni mwenye kukasirika siku moja anakufuru na kusema: “Sijawahi kamwe kuona kheri yoyote kutoka kwako.”1048. Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”as-Swahiyhah” (823).


an-Nasaa´iy amepokea katika “as-Sunan” al-Kubraa” kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Amr ambaye ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: 


“Allaah Hamtazami mwanamke ambaye hamshukuru mume wake wakati huo huo hawezi kujitosheleza naye [kukosa kuwa pamoja naye].” 9135. Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”as-Swahiyhah” (289).


NA  ALLAAH   ANAJUA   ZAIDI

Tutaendelea...Usikose Sehemu ya 3 In  Shaa  Allaah..............


from fisabilillaah.com https://ift.tt/2SbtxGk
via IFTTT

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...