Ni kwa sababu hii Allah Ta’ala alitutumia Mitume na miongozo ya vitabu ili tuweze kumtambua na kisha kumuamudu. Mtume Muhammad (rehema na amani zimshukie) alitumwa kufikisha dini ya haki kwa watu wote. Naye akafikisha ujumbe, akatekeleza amana, akanasihi umma na baada ya kufa kwake aliuacha umma katika njia nyoofu na bila upotofu.
Kwa kuzingatia hayo, Uislamu ukateua madrasa na kuifanya kuwa taasisi muhimu katika kustawisha misingi ya kupata jamii ya watu wanaojitambua katika kuitumikia dini na jamii. Hata hivyo inasikitisha kuona Waislamu wenyewe ndio ambao wanahusika katika kuidhoofisha taasisi hii (madrasa).
Tunasema hivyo kwa sababu, tuna ushahidi juu ya wazazi wengi wa Kiislamu wanaolipa mamilioni ya pesa za ada za watoto wao katika shule zinazotoa elimu ya mazingira lakini wanashindwa kufanya hivyo kwa walimu wa madrasa.
Baadhi ya wazazi wamekuwa wagumu na wabahili kiasi cha kushindwa kuchangia ada ya mwalimu wa madrasa kwa kiasi kidogo tena wakati mwingine cha shilingi 3,000 za kitanzania kwa mwezi mmoja. Hicho ni kiasi kidogo sana ukilinganisha na gharama za kila siku za mwanafunzishuleni. Kwa hili, Waislamu tusitafute mchawi wa kuwalea watoto wetu kwani kama tunashindwa kuwathamini walimu wa madrasa, ni kipi tunachotegemea katika suala zima la malezi na maadili ya dini kwa vijana wetu?
Tatizo ni kwamba, jamii yetu inawatazama walimu wa madrasa kama watu wa daraja la chini sana kimaisha. Kwa hakika, huu si mtazamo sahihi kwani ukweli ni kwamba walimu ni watu wa tabaka la juu, na ambao Mwenyezi Mungu amewatukuza na kuwathamini kama anavyofahamisha: “…Mwenyezi Mungu atawainua walioamini miongoni mwenu na waliopewa elimu ya daraja za juu…,” (Qur’ an, 58:11).
Hivyo, ni jukumu letu kuwaangalia walimu wa madrasa kwa jicho la tatu kwani hata wao wanaweza kuwa na shughuli nyingine za kujitafutia riziki lakini wanaziacha na kufanya kazi ya madrasa wakitafuta radhi za Muumba wao. Waislamu watambue kuwa elimu ndio zawadi na urithi bora kwa watoto wao katika kuwajengea moyo wa imani na uchamungu, kujua utu sambamba na kumtukuza Mola wao mlezi, jambo ambalo kama watoto wakishikamana nalo watakuwa watu wema katika jamii.
Hivyo, ni muhimu tujenge ustawi mzuri wa walimu wa madrasa na wale wanaofundisha masomo ya dini shuleni kwa kuboresha mazingira ya kazi na maisha yao kwa ujumla.
Kimsingi walimu wa madrasa hapa nchini wamesahauliwa kabisa na wameachwa katika hali ya upweke kiasi cha kuona ugumu wa kuendelea na kazi hiyo. Na hali ikiendelea kuwa hivyo madrasa tutaziua kwa mikono yetu sisi wenyewe. Ni vigumu kumaliza changamoto za walimu wa madrasa kwa kutegemea nguvu ya kundi moja la watu (Masheikh na wazazi) lakini tukiwahusisha Waislamu wote tunaweza kufikia lengo.
Hivyo, tunapendekeza suala la kulipa mishahara ya walimu wa madrasa liwe la Waislamu wote na si kutegemea matajiri kwani hata tukirejea historia ya Uislamu na Maswahaba wa Mtume (Allah awe radhi nao), walijitolea kwa hali na mali katika kuitumikia dini na hatimaye kutufikia sisi hii leo.
from TIF https://ift.tt/2AwkeJX
via IFTTT
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni