Shari’ah ya Kiislamu imeasisi na kulingania ustaarabu mbali mbali wa jamii. Wakati huo huo, imetahadharisha kuwepo adhabu siku ya Qiyaamah pindipo mtu atakaposhindwa kushikamana na Shari’ah hizo. Imaam Muslim amepokea kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Je munamjua nani muflisi?)) Walijibu: ((Muflisi miongoni mwetu ni yule ambaye hana pesa wala mali.)) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Muflisi ndani ya ummah wangu ni yule anayekuja siku ya Qiyaamah akiwa na Swalah, Zakaah na Swawm, hata hivyo alikuwa akivunjia heshima, kusengenya, kutukana na kuwapiga wengine. Hivyo wenye kumdai wanalipwa kutokana na matendo yake mazuri. Iwapo mema yake yamemalizika, anaadhibiwa kwa matendo yao maovu hadi pale anapotupwa Motoni.))
1. Adabu za Kula:
a. Anza kula kwa jina la Allaah (BismiLlaahir Rahmaanir Rahiym) na malizia kwa kumhimidi na kumshukuru Allaah (Al-Hamdul Lillaahi Rabbil-‘Aalamiyn). Kula kile kilichopo mbele yako kwenye chombo chako na tumia mkono wako wa kulia, kwa sababu mkono wa kushoto kawaida yake unatumika kwa kusafishia uchafu.
Al-Bukhaariy na Musim wamepokea kutokana na simulizi ya ‘Umar bin Abi Salaam (Radhiya Allaahu ‘anhu), kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemwambia:((Litaje jina la Allaah, kula kwa mkono wako wa kulia na kula kile kilichopo mbele yako kwenye chombo.))
b. Katu usilalamike au kukataa chakula kwa namna yoyote.Al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutokana na simulizi ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu), kwamba:((Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hakupatapo kuona kasoro kwenye chakula chochote. Iwapo amekipenda, atakila, iwapo hakukipenda atakiacha tu.))
c. Jiepushe na kula au kunywa kupita mpaka kwa mujibu wa muongozo wa maneno ya Qur-aan:
[Suraatul-‘Aaraaf, 7:31]
Na kwa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):((Mtoto wa Aadam (mwanaadamu) hakupatapo kujaza chombo zaidi ya tumbo lake. Iwapo hakuna njia yoyote, basi iwepo thuluthi kwa chakula, nyengine kwa kinywaji na nyengine kwa pumzi zake.)) [Imesimuliwa na Ahmad].
d. Usishushie pumzi wala usipulizie ndani ya vyombo. Kutokana na Ibn ‘Abbaas Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:((Jihadharini na kurudushia pumzi au kupulizia ndani ya chombo.))[Imepokewa na At-Tirmidhidy].
e. Kula pamoja na wengine, usiwe peke yako, kwani Mjumbe wa Allaah amesema: ((Kusanyikeni kwenye chakula chenu ili kibarikiwe.))[Imepokewa na Abu Daawuud na Tirmidhiy].
f. Iwapo umealikwa kwenye chakula na umemchukua mtu pamoja na wewe, ni lazima uombe ruhusa kutoka kwa mwalikaji. Kutokana na Abu Mas’uud Al-Badriy (Radhiya Allaahu ‘anhu), mtu mmoja alimualika Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye chakula pamoja na watu wengine wanne. Kuna mtu mmoja alimfuata Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alipofika mlangoni, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia mwalikaji (mwenyeji):
((Mtu huyu amekuja pamoja nasi: Iwapo utaruhusu ataingia ndani, na iwapo hutamruhusu atarudi zake.))Mwalikaji akasema: Ninampa ruhusa, Ewe Mjumbe wa Allaah. [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim].
2. Adabu za Kuomba Ruhusa:
Kuna aina mbili za ustaarabu:
a. Zile ambazo zipo nje ya mlango wa nyumba:
[Suratun-Nnuur, 24: 27].
b. Zile ambazo zimo ndani ya nyumba:
[Suratun-Nnuur, 24: 59].
Haya yote yanaazimia kuzilinda siri za nyumba na kuzipa nyumba faragha, kama ilivyooneshwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Kuomba idhini kunakusudia kulinda stara.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim].
Inashauriwa kutong’ang’ania kuomba ruhusa ya kuingia kwa mtu (kupiga hodi): ((Ni lazima uombe ruhusa (kuingia kwa mtu) mara tatu. Iwapo hujaruhusiwa kuingia ndani, rudi zako.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim].
3. Adabu za Kuamkia (Salaam):
Uislamu umehimiza sana mila ya kusalimiana miongoni mwa wana jamii kwa sababu inapelekea kwenye mahabba na urafiki. Hili linaenda sambamba na Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Hautaingia Peponi hadi muwe Waumini, na wala hautakuwa Waumini hadi mpendane. Je, nikuelekezeni kwenye jambo ambalo linawafanya mpendane mmoja kwa mwengine? Kithirisheni maamkizi kwa amani miongoni mwenu.)) [Imepokewa na Muslim] – Kuitikia maamkizi ni lazima: [Suratun-Nisaa, 4: 86].
Uislamu pia umetoa maelezo ya daraja kuhusu mwenye kuwajibika kutoa salamu juu ya mwengine. Kwa mujibu wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mpandaji amsalimie mwenye kwenda kwa miguu, mwenye kwenda kwa miguu amsalimie aliyeketi, na kikundi kidogo cha watu kwa idadi kiwasalimie kikundi kilicho kikubwa kwa idadi.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]. Kwenye mapokezi moja kutoka Al-Bukhaariy, imeongezwa: ((Mtoto au kijana amsalimie mtu mzima.))
4. Adabu za Kikao:
a. Toa salamu juu ya waliohudhuria kwenye kikao au mjumuiko. Imesimuliwa kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Iwapo atakuja mmoja kwenye kikao basi na aseme: Assalaamu ‘Alaykum (yaani Amani Iwe Juu Yenu) Na anapoondoka afanye hivyo hivyo, kwani maamkizi ya mwanzo hayana umuhimu sana kuliko ya mwisho.)) [Imepokewa na Abu Daawuud na At-Tirmidhiy].
b. Haifai kumtaka mtu mmoja kuondoka (kumpisha) kwenye kikao chake kwa ajili ya mtu mwengine:((Wala asimfanye (asimtake) yeyote kati yenu mmoja wenu kunyanyuka kwenye sehemu yake na (yeye) kukalia sehemu yake; isipokuwa, tengenezeni nafasi (toeni nafasi, zitanue) zaidi kwa ajili ya wengine kuweza kukaa.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim].
c. ((Iwapo mtu ataondoka kwenye sehemu yake kisha akarejea, atakuwa na haki zaidi na ile sehemu aliyoiacha.))kama ilivyosimuliwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). [Imepokewa na Muslim].
d. Wala usiwatenganishe watu wawili waliokaa: ((Hairuhusiwi kwa mtu kuwatenganisha watu wawili (kwa kujiingiza kukaa kati baina yao) isipokuwa watakapompa ruhusa.))[Abu Daawuud na At-Tirmidhiy].
e. Usizungumze faragha na rafiki mbele ya mtu wa tatu: ((Kama mupo watu watatu, haipasi watu wawili peke yao kuzungumza bila ya kumshirikisha wa tatu hadi mutakapojumuika pamoja na watu wengine, kwani hili litamsikitisha wa tatu.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy].
f. Wala usikae katikati ya duara au kundi la watu: ((Amelaanika yule mwenye kukaa katikati ya watu waliokaa kikundi.)) [Imepokewa na Abu Daawuud].
g. Acha nafasi kwa wengine kuweza kukaa: [Suratul-Mujaadalah, 58: 11].
h. Inapendekezwa kuzuia miayo kwa kadiri itakavyowezekana kwani ni alama ya uvivu: ((Miayo unatokana na Shaytwaan, hivyo pale mmoja wenu anapokwenda miayo basi na ajitahidi kuuzuia kwa kadiri atakavyoweza, kwani iwapo mtu atalalama ‘Aaah!’ (pale anapokwenda miayo) Shaytwaan atamcheka.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim].
i. Ama kuhusu kwenda chafya, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Pindipo mmoja wenu anapokwenda chafya, basi na aseme: Shukrani zote ni za Allaah! Na ndugu yake Muislamu amwambie: Allaah Akurehemu! Ambapo naye atajibu: Allaah Akuongoze na Akutengenezee mambo yako vizuri.))[Imepokewa na Al-Bukhaariy]. Pia inahimizwa kwa mtu, kama vile ilivyosimuliwa na Mjumbe wa Allaah kutokana na simulizi ya Abu Hurayrah:((pale anapokwenda chafya, kufunika mdomo wake kwa mkono wake au guo na kuizuia sauti yake.)) [Imepokewa na Abu Daawuud na At-Tirmidhiy].
j. Acha kwenda mbweu pale unapokaa mbele ya wengine. Kutokana na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma), mtu mmoja alienda mbweu mbele ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ambapo Mtume alimwambia: ((Acha kwenda mbweu, walaji wakuu humu duniani ndio watakuwa wenye njaa kali zaidi siku ya Qiyaamah.)) [Imepokewa na At-Tirmidhiy na Ibn Maajah].
k. Mkusanyiko wa watu usiwe na mashughuliko ya mambo yasiyo na maana au yaliyo batili katika kumkumbuka Allaah na kufanya mazungumzo yenye manufaa duniani na katika Diyn. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuhusiana na hili:((Mtu yeyote anayeinuka kutoka kwenye mkusanyiko ambapo jina la Allaah halitajwi ni sawaswa na wale wanaoinuka kutoka katika mzoga wa punda, na mkusanyiko huo (ambao ndani yake hatajwi Allaah) utakuwa ni chanzo cha huzuni kwao.)) [Imepokewa na Abu Daawuud].
l. Mtu asiwaelekee wale wanaokaa pamoja naye kwa kile kinachowachukiza.
5. Adabu za Mikusanyiko:
Uislamu unaheshimu hisia za watu wanaokusanyika kwenye sehemu kufanya mikusanyiko yenye kupendeza na kupiga marufuku mikusanyiko yote yenye kusababisha watu kuchukiana. Hivyo, Uislamu unatoa muongozo kwa wafuasi wake kuwa ni wenye mwili msafi, usio na harufu mbaya, na nguo zilizovaliwa ziwe safi, zisizo na muonekano wa kuchukiza. Pia Uislamu unawaelekeza kumsikiliza mzungumzaji bila ya kumkatisha na pia kukaa pale ambapo watakuta nafasi bila ya kukanyaga shingo (unapopita na kuwapangua watu waliokaa kwenye Swafu Msikitini) za watu au kuwasababibishia usumbufu kwa kuwabana bana. Hili linaenda sambamba na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale alipowahutubia Waislamu khutbah ya Ijumaa: ((Yeyote anayeoga siku ya Ijumaa, akavaa nguo yake iliyo bora kuliko zengine, akaitia manukato, kisha akahudhuria Swalah ya Ijumaa bila ya kuwapita pita (kuwapangua waliokaa) watu na akaswali rakaa anazoweza kuswali, kisha akakaa kimya pale Imaam anapowahutubia watu hadi akahitimisha Swalah yake, basi Swalah yake itakuwa ni malipo kwa wiki nzima hadi wiki nyengine.)) [Imepokewa na Abu Daawuud].
6. Adabu za Majadiliano:
a. Msikilize mzungumzaji bila ya kumkatisha hadi amalize kuzungumza. Katika khutbah yake ya kuaga wakati wa Hajj, Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((Waombe watu wakae kimya.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim].
b. Zungumza kwa ufasaha ili kwamba wasililizaji waweze kukuelewa. Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha), mke wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yalikuwa ni yenye ufasaha hadi kwamba watu wote wakiweza kuyafahamu.)) [Imepokewa na Abu Daawuud].
c. Kuwa mchangamfu na zungumza kwa furaha. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):((Usidogoshe aina yoyote ya matendo, hata kumpokea ndugu yako kwa uchangamfu.)) [Imepokewa na Muslim], na Hadiyth yake nyengine: ((Neno zuri ni tendo jema.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]. Al-Hussayn (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema:((Nilimuuliza Baba yangu kuhusu adabu za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) miongoni mwa wafuasi wake.)) ambapo alijibu:((Daima alikuwa mchangamfu, mwenye tabia nzuri na laini. Alikuwa sio mbughudhi, mwenye kelele, mtukanaji, mvunjaji heshima wala mdhurifu. Alikuwa ni mwenye kuliangalia kwa matarajio ya juu jambo asilolipenda bila ya kuwazuia watu wengine matumaini au kuwajibu kwa mtindo wa kuwakatisha tamaa. Alijizuia katika mijadala, kung’ang’ania hoja na kufanya makelele. Alijihadharisha na mambo matatu: Alikuwa sio mwenye kufanya fujo, kuona kosa au kuwafuatilia. Alizungumza pale tu anapotarajia kuwepo malipo. Pale anapozungumza, wasikilizaji wake waliinamisha vichwa vyao kimya kabisa na pale anapokuwa kimya wao wanazungumza. Walikuwa hawazungumzi kwa fujo mbele yake. Iwapo mmoja wao atazungumza mbele yake, watamsikiliza hadi amalize. Alikuwa akicheka na kushangaa pale wanapocheka au kushangaa. Alikuwa ni mwenye subira kwa watu wasioeleweka ambao walikuwa ni wabughudhi kwenye mazungumzo na maombi yao.))
7. Adabu za Mzaha:
a. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kwa Swahaabah wake aitwaye Hanzalah, ambaye alidhani kwamba maisha yapo mbali na michezo na starehe ambaye alicheza na kupumbazana kwa unafiki pamoja na mkewe na watoto wake: ((Lakini, Hanzalah, ufanye upya moyo wako muda hadi muda.)) [Imepokewa na Muslim]. Hapa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuelezea mtu huyo kwamba furaha zilizoruhusiwa na kujiliwaza mwenyewe ni yenye kukubalika kwa roho ya mwanaadamu ili kurudisha tena uhai na mishughuliko yake tena. Yeye, (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), pia aliwafunza kanuni za tabia njema kwa mnasaba wa mzaha, pale alipoulizwa kuhusiana na mzaha wake pamoja nao, kwa kusema: ((Ndio, lakini ninazungumza ukweli.))[Imepokewa na At-Tirmidhiy].
b. Mara moja alikuja bibi mzee na kusema: Ewe Mjumbe wa Allaah, niombee du’aa juu yangu ili niingie Peponi. Alimwambia: ((Hakuna bibi kizee atakayeingia Peponi. Aliposikia hivi (bibi yule), alikwenda zake huku akilia. Akasema (Mtume): Mwambie kwamba hatokuwa bibi kizee pale atakapoingia Peponi. Allaah, Mtukufu Anasema: [Al-Waaqi’ah, 56: 35-37]
c. Mizaha ya Mjumbe wa Allaah haikuwa tu kwenye maneno, bali pia yalikuwa kwenye matendo. Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu), amesema: Bedui mmoja akiitwa Zaahir alikuwa akileta zawadi kutoka jangwani kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa pia akimpatia vitu anapoondoka. Alisema kuhusiana naye:((Zaahir ni ‘jangwa’ letu na sisi ni ‘mji’ wake.)) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimpenda, ingawa alikuwa na sura ambayo kwa wanaadam inaonekana haivutii. Siku moja, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimjia akiwa anauza bidhaa fulani, alimkumbatia kwa nyuma bila ya (Zaahir) kutambua. Zaahir akasema: “Niachie” Kisha akaangalia kwa nyuma na kumgundua Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hivyo akaegemeza mgongo wake dhidi ya kifua cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatangazia: ((Nani atamnunua huyu mtumwa?)) Zaahir akasema: “Ewe Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), utatambua kwamba mimi siuziki”. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu: ((Lakini mbele ya Allaah, wewe sio mwenye kutouzika)), ama alisema: ((Mbele ya Allaah, wewe ni mpenzi mno.)) [Imepokewa na At-Tirmidhiy].
d. Mzaha usiwe ni wenye kunasibiana na kumuumiza au kumtusi Muislamu yeyote. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hapana ruhusa kwa Muislamu kumtisha Muislamu mwengine.)) [Imepokewa na Abu Daawuud]. Pia amesema: ((Asichukue(Muislamu) yeyote mali za ndugu yake.)) [Imepokewa na Abu Daawuud na At-Tirmidhiy].
e. Mzaha usiwe ni wenye kumpelekea Muislamu kusema uongo kwa ajili ya kuwafanya wengine wacheke; hili linafahamika kutokana na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Ole wake yule anayesema uongo pale anapozungumza ili kuwafanya watu wacheke. Ole wake! Ole wake!))
8. Adabu za Kuomboleza:
a. Kitendo cha kuomboleza kinaelezwa kwamba kina lengo la kuifariji familia ya mfiwa, kuwapatia afueni na kupunguza majonzi. Mjumbe wa Allaah amesema: ((Muumini ambaye anamuomboleza ndugu yake kwa kufariki kwake atavishwa na Allaah nguo bora kabisa kwa heshima na hadhi ya juu Siku ya Qiyaamah.))
b. Hakuna mfumo maalumu wa kuomboleza. Hata hivyo, Imaam Ash-Shafi’iy amependekeza kauli ya:((Allaah Akujaalie kuongezeka malipo yako, Akupatie faraja na kumsamehe maiti wako.))
c. Inapendekezwa kutayarisha chakula kwa familia ya mfiwa kama inavyooneshwa wazi kutokana na Hadiyth ifuatayo: ((Tayarisheni chakula kwa familia ya Ja’afar kwani wamepatwa na [jambo kubwa] lisilotegemewa.))
9. Adabu za Kulala:
a. Litaje neno la Allaah: “BismiLlaahir Rahmaanir Rahiym” na lalia ubavu wako wa kulia kwa mujibu wa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yaliyosimuliwa na Al-Baraa bin ‘Aazib: ((Unapokwenda kitandani, chukua Wudhuu kama wa Swalah, kisha lalia ubavu wako wa kulia, na sema: Ee Allaah! Ninajisalimisha Kwako, na kuelekeza uso wangu Kwako, na nina matumaini ya jambo lolote juu Yako, na kimbilio langu ni Kwako, kwa mapenzi na khofu Kwako. Hakuna hifadhi wala kimbilio kutoka Kwako isipokuwa Kwako. Ninaamini Kitabu Chako, ambacho Umekiteremsha kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ambaye Umemtuma kama ni Mjumbe.))[Imepokewa na Bukhariy na Muslim].
b. Usichelewe kulala hadi usiku (wa manane) na jitahidi kadiri uwezavyo kulala mapema isipokuwa pale panapo na udhuru au haja maalumu. Imesimuliwa kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akichukizwa kulala kabla ya Swalah ya ‘Isha (jioni) na (kukaa na) kuzungumza baada yake. [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim].
c. Usilalie tumbo lako, kwani hili limekatazwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mtindo huo wa ulalaji unachukizwa na Allaah.))[Imesimuliwa na Abu Daawud].
d. Hakikisha kwamba hakuna chochote ambacho kinakuumiza kitandani mwako, kama ilivyopendekezwa na Mtume wetu Mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Pindipo mmoja wenu anapokwenda kitandani, asafishe kitanda chake kwa pande la kitambaa chake kwani hajui nini kimelala ndani yake baada ya yeye kuondoka, na aseme: “Allaahumma bika wadhwa’tu janbiy, wabika afra’uh. Allahumma in amsakta nafsiy faghfir laha, wa in arsaltaha fahfadh-ha bima tahfadhu bihi ‘ibaadas-Swaalihiyn.” – “Ee Allaah! Kwa jina Lako nimejilaza ubavu, na kwa jina Lako ninainuka. Ee Allaah! Iwapo utaikamata roho yangu (yaani kuchukua maisha yangu), basi [nakuomba] unifanyie huruma, na iwapo utairudisha, basi ilinde kwa kile Unachowalindia waja wako Wacha Mungu.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim].
e. Kuwa muangalifu na ondosha kitu chochote kinachoweza kusababisha hatari. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Moto huu ni adui kwenu, hivyo munapotaka kulala uzimeni.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy].
10. Adabu za Tendo la Ndoa:
a. Inapendekezwa, kabla ya kuingiliana na mkewe au mumewe kulitaja jina la Allaah. ((Pale mmoja wenu anapomuingilia mkewe, iwapo atasema: “Kwa jina la Allaah! Tuepushe mbali kutokana na Shaytwaan, na muweke mbali Shaytwaan na (mtoto) utakayeturuzuku.” na iwapo mtoto atazaliwa kutokana na mjumuiko huu, Shaytwaan hatakuwa na mlango wa kumuumiza mtoto huyo.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim].
b. Mahusiano ya kifaragha baina ya mume na mke ni lazima yawekwe siri, kama ilivyosimuliwa katika Hadiyth ifuatayo: ((Ambaye atakuwa na hadhi mbovu kulizo za watu wote mbele ya hesabu ya Allaah Siku ya Qiyaamah atakuwa ni mtu ambaye anaingiliana na mkewe au mwanamke ambaye anaingiliana na mumewe, kisha aidha yeyote kati ya hao anatoboa siri za (kitandani) za mwenza wake.))[Imesimuliwa na Muslim].
c. Mjumbe wa Allaah amehimiza kuchezeana kimapenzi, ubembe wa mazungumzo na kubusiana kabla ya tendo la ndoa kama ilivyothibitishwa na maneno yake kwa Swahaabah wake:((Usifanye tendo la ndoa na yeye isipokuwa pale anapokuwa na hamu/hali sawa sawa ya kufanya tendo la ndoa ili usimalize kabla yake yeye.))Akauliza: Je nifanye hivi? Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Ndio, mbusu, mkumbatie na mtomase hadi uone kwamba ana hali ya shauku na hamu kama ulivyo wewe, kisha fanya naye tendo la ndoa pamoja naye.))[Imepokewa na Imaam Ahmad].
d. Mume asiichopoe dhakari yake kutoka kwenye utupu wake hadi pale (mke) anapomaliza.
11. Adabu za Kusafiri:
a. Rejesha amana kwa wenyewe, sawazisha malalamiko na madeni, na iache familia yako ikiwa na mahitaji ya kutosha. Usisafiri peke yako isipokuwa kwa haja ya dharura ambapo hujapata Swahiba. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:((Abiria mmoja ni Shaytwaan, abiria wawili ni Mashaytwaan wawili, lakini abiria watatu wanafanya kuwa ni msafara.)) [Imesimuliwa na Abu Daawuud, An-Nasaaiy na At-Tirmidhiy].
b. Unaposafiri, chagua Swahiba mwema na teuni mmoja wenu kuwa ni kiongozi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:((Pindipo watu wawili wanapokwenda safarini, ni lazima wateue mmoja wao kama ni kiongozi.)) [Imesimuliwa na Abu Daawuud].
c. Ni lazima uwaarifu familia yako wakati unaporudi kwao. Usirejee nyumbani kwako usiku kwani hili halipendezi ili kwamba usione vitu ambavyo utavichukia. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Iwapo mmoja wenu hayupo nyumbani kwa muda mrefu, asirejee kwa familia yake usiku.)) Katika tamko jengine la Hadiyth, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimzuia mtu kurejea nyumbani usiku. [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim].
d. Awaage kwa heri familia yake, marafiki na watu wake wa karibu kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Iwapo mmoja wenu anadhamiria kwenda safarini, basi na aseme kwaheri kwa ndugu zake, kwani Allaah Mtukufu Atafanya ndani ya du’aa zao baraka kwake.))
e. Arejee nyumbani kwake haraka baada ya kufanikisha lengo la safari yake. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Safari ni kipande cha masumbuko kwani inazuia kila msafiri (kwako wewe) kwenye huduma za kula, kunywa na kulala. Hivyo, pindipo mmoja wenu anapotimiza lengo la safari yake arejee nyumbani kwake haraka.)) [Al-Bukhaariy na Muslim].
12. Adabu za Sokoni
a. Miongoni mwa sharti za adabu (njema) sokoni ni zile ambazo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Acheni kukaa mitaani [mabarazani])). Maswahaabah wakasema: ((Ewe Mjumbe wa Allaah, hatuna (njia) mbadala, hakuna sehemu nyengine yoyote ambapo tutakaa na kujadili masuala.)) Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Iwapo ni hivyo, basi kwa suala hilo, tekelezeni majukumu yenu (kwa haki) ya njia [mabarazani].))
b. Maswahaabah waliuliza ni jambo gani linalohitajika kutelekezwa mtaani [majiani, mabarazani]. Alisema:((Kuangusha macho chini, kuondosha vikwazo mitaani, kuitikia maamkizi ya salaam, kuamrishana mema na kukatazama maovu.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]. Katika simulizi nyengine, aliongezea:((Kuwasaidia wenye matatizo na kuwaongoza walemavu.)) [Imepokewa na Abu Daawuud].Pia amesema:((Jihadharini na matendo mawili yaliyolaaniwa)) Maswahaabah wake wakasema: ((Ni yepi hayo matendo mawili yaliyolaaniwa?)) Yeye, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akajibu: ((Mtu kwenda haja mbele za watu anapoonekana au kwenye sehemu za vivuli (sehemu ambazo watu wanapumzika).))[Imepokewa na Muslim].
c. Mpitaji njia aache kubeba zana au vyombo vya hatari kama ilivyoamrishwa na Mtume Mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye amesema: ((Pindipo mmoja wenu yeyote atatokezea kuingia Misikitini mwetu au sokoni (madukani) akiwa na mshale (mkononi) ni lazima aukamate ncha yake mkononi mwake, ili kwamba hakuna yeyote miongoni mwa Waislamu atakayepata jeraha kutokana nao.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim].
13. Adabu za Kununua na Kuuza
a. Kishari’ah, kuuza ni halali ndani ya Uislamu kwa sababu kumeegemezwa kutokana na kubadilishana manufaa baina ya muuzaji na mnunuzi. Hata hivyo, iwapo kuna dhara yoyote iliyojitokeza kwa upande wowote, makubaliano hayo yanakuwa ni haramu kwa mujibu wa Aayah ifuatayo: [Suratun-Nisaa, 4: 29].
b. Pia kwa mujibu wa Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), pale alipotokezea kupita rundi la kinacholiwa (mahindi). Alipenyeza mkono wake ndani ya rundi hilo na mikono yake ikatokeza kuwa na majimaji. Alisema kumwambia mmiliki wa rundi lile: ((Ni nini hichi)) Akajibu: “Ewe Mjumbe wa Allaah, hizi zimeharibika kutokana na kuanguka kwa mvua”. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatanabahisha: ((Kwanini usiliweke hili (rundi la mahindi zilizorowana) juu ili kwamba watu waone? Yeyote anayetudanganya sisi sio miongoni mwangu (yaani mfuasi wangu).))[Imepokewa na Muslim].
c. Ukweli na maelezo yaliyo wazi (ya kasoro, kama ipo) inahitajika kwa mujibu wa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyesema: ((Pande zote mbili ndani ya mauziano ya biashara ina haki ya kubatilisha alimuradi hawajatawanyika. Hivyo, iwapo watazungumza ukweli na kufanya kila kitu dhahiri watabarikiwa ndani ya mauziano yao; lakini iwapo wataambizana uongo na kuficha chochote, baraka za mauziano yao zitazuiliwa.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim].
d. Huruma na makubaliano yaliyo haki yanahimizwa ndani ya biashara, kwani inamaanisha kujenga mahusiano mazuri ya muuzaji-mnunuzi kama ilivyotanabahishwa na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Allaah Amjaalie rahma juu ya mtu ambaye ni mwepesi na makini anapouza, kununua au kuulizia malipo ya haki zake.)) [Imepokewa na Al-Bukhariy]. Hii ni kwa sababu Uislamu unahitaji huu wepesi wa makubaliano na kuvumiliana ndani ya masuala ya kuuza na kununua kuwaokoa watu kutokana na kuweka mbele maslahi ya dunia ambayo yanaharibu udugu na mahusiano ya kibinaadamu.
e. Jiepushe na kula kiapo unapouza, kwa mujibu wa maelekezo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Jiepushe na kula kiapo sana pindipo unapouza (bidhaa zako), kwani mwanzoni inashajiisha biashara na baadaye inaleta hasara zote.))[Imepokewa na Muslim].
Hizo juu ni baadhi ya tabia za mwenendo wa Kiislamu na adabu zake, na zipo nyengine zaidi ambazo zitahitaji muda zaidi wa kuzielezea. Juu ya hivyo, inatosheleza hapa kukumbushia kwamba hakuna tendo la binaadamu, la faragha au dhahiri, lisiloendana na maelezo na muongozo wa Qur-aan au Hadiyth za Mtume ambazo zinatafsiri na kushurutisha.
from fisabilillaah.com https://ift.tt/2Qr4kus
via IFTTT
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni