Mwandishi: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
Mfasiri: Abu Bakr Khatwiyb al-Atrush
Tunaendelea na Sehemu ya 4
Sababu ya tatu
Ash-Shakk
Ash-Shakk Maana yake ni kuwa na shaka ni kutokuwa na uhakika kati ya mambo mawili ni lipi lililotokea.
Shaka haizingatiwi katika ´Ibaadah katika hali tatu:
1- Ikiwa ni dhana tu na hana hakika ya jambo hilo, kama wasiwasi.
2- Ikiwa shaka hiyo itakuwa kwa mtu sana kwa kiasi ambacho hawezi kufanya ´Ibaadah yoyote isipokuwa anapatwa na shaka.
3- Ikiwa shaka hiyo inamjia baada ya kumaliza ile ´Ibaadah, shaka hiyo haizingatiwi, maadamu hajakuwa na yakini juu ya hilo. Hivyo mtu atafanya kwa Muqtadhwa wa yakini yake.
Mfano wa hilo
Ni mtu ameswali Dhuhr.
>>Wakati amepomaliza kuswali Swalah yake akapatwa na shaka, je, ameswali Rakaa tatu au nne.
>>Katika hali hii asizingatie shaka hii isipokuwa ikiwa atakuwa na yakini ya kwamba hakuswali kweli isipokuwa Rakaa tatu, hapo ataikamilisha Swalah yake ikiwa (amekumbuka) kwa wakati wa karibu, kisha atatoa Salaam, halafu atasujudu Sujuud-us-Sahuw na kutoa Salaam. Endapo hakukumbuka isipokuwa baada ya muda mrefu kupita, hapo atarudi kuswali Swalah yake upya.
Ama shaka, mahapa pengine pasipokuwepo mahala patatu hapa, shaka hiyo itakuwa ni yenye kuzingatiwa. Shaka inaweza kuwa tu katika hali mbili:
Hali ya kwanza
Ikambainikia yeye moja katika mambo mawili.
>>Hapa atafanyia kazi lile ambalo limembainikia.
>>Atatakiwa kujengea Swalah yake juu ya hilo, halafu atatoa Salaam, kisha atasujudu Sujuud-us-Sahuw na kutoa Salaam.
Mfano wa hilo
Mtu anaswali Swalah ya Dhuhr na akawa na shaka juu ya Rakaa aliyomo, je, ni Rakaa ya pili au ni ya tatu.
>>Lakini ikambainikia (akaegemea zaidi) ya kwamba ile Rakaa ni ya tatu, basi ataifanya kuwa ni ya tatu.
>>Baada ya hapo ataswali Rakaa nyingine moja – ambayo inatimiza nne – amalize Swalah yake halafu atasujudu Sujuud-us-Sahuw kisha ndio atoe Salaam.
Dalili ya hilo
Yaliyothibiti katika Swahiyh al-Bukhaariy na Muslim kutoka katika Hadiyth ya ´Abdullaah Ibn Mas´uud ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Atakapokuwa na shaka mmoja wenu katika Swalah yake, atafute (ajengee) juu ya la usawa na aendelee kwa hilo. Baadaye atoe Salaam kisha asujudu Sijda mbili (Sujuudus-Sahuw).”
Hali ya pili
Isibainike kwake moja kati ya mambo mawili.
>>Atafanyia kazi lile ambalo ni yakini, nalo ni (kuchukua) kwa idadi ya uchache (kati ya hayo mawili).
>>Atakamilisha Swalah yake kujengea kwa hilo halafu atasujudu Sujuud-usSahuw kabla ya kutoa Salaam kisha ndio atoe Salaam.
Mfano wa hilo
Mtu anaswali ´Aswr na akawa na shaka ni Rakaa ngapi ameswali, ni mbili au tatu. Isibainike kitu kwake ya kwamba hii ni Rakaa ya pili au ya tatu, atajaalia kuwa ni Rakaa ya pili (atajengea juu ya ile idadi ya uchache).
>>Atakaa Tashahhud ya kwanza kisha baada ya hapo aswali Rakaa zingine mbili, halafu atasujudu Sujuud-us-Sahuw kisha atoe Salaam.
Dalili ya hilo
Yale aliyopokea Muslim kutoka kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anhu) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Atakapokuwa na shaka mmoja wenu katika Swalah yake, na asijue (Rakaa) ngapi ameswali, tatu au nne, aondoe ile shaka na ajengee kwa lile aliloyakinisha katika moyo wake kisha asujudu Sijda mbili (Sujuud-us-Sahuw) kabla ya kutoa Salaam. Ikiwa atakuwa ameswali Rakaa tano, Swalah yake itamshufaia (itamuombea). Na ikiwa atakuwa ameswali Swalah kikamilifu, basi hio itakuwa ni fedheha kwa Shaytwaan.”
Mfano wa shaka
Ni Mtu anapokuja na Imamu amerukuu. Mtu huyo atapiga Takbiyrat-ul-Ihraam hali ya kuwa amesimama wima kisha arukuu. Na wakati atakapofanya hivyo, hatotoka katika hali tatu:
1- Awe na yakini ya kwamba amemuwahi Imamu kwenye Rukuu kabla ya kuinuka kutoka katika Rukuu. Hapo atakuwa amewahi ile Rakaa na itambomokea yeye kusoma al-Faatihah.
2- Awe na yakini ya kwamba Imamu aliinuka kutoka kwenye Rukuu kabla ya kumuwahi katika Rukuu hiyo. Hapo atakuwa amekosa ile Rakaa.
3- Awe na shaka, je alimuwahi Imamu kwenye Rukuu akawa ni mwenye kuwahi ile Rakaa au yule Imamu aliinuka kutoka kwenye Rukuu kabla ya kumuwahi akawa ni mwenye kukosa ile Rakaa. Iwapo itambainikia yeye (ataegemea zaidi) moja kati ya hayo mawili, atafanyia kazi lile lililombainikia halafu atakamilisha Swalah yake kisha atatoa Salaam, halafu atasujudu Sujuud-us-Sahuw na kutoa Salaam. Ikiwa hakupitwa na kitu chochote katika Swalah, hapo hatakiwi kuleta Sujuud-us-Sahuw.
Lakini ikiwa haitombainikia yeye moja kati ya mambo mawili, atatakiwa kukamilisha Swalah yake na kusujudu Sujuud-us-Sahuw kabla ya kutoa Salaam kisha atoe Salaam.
Faida
Ikiwa mtu atakuwa na shaka katika Swalah yake akafanyia kazi yakini au kulingana na itakavyokuwa imembainikia (alipoegemea zaidi), kutokana na ufafanuzi tuliyoutaja. Baadaye ikambainikia ya kwamba alilofanya ndio sawa na kwamba yeye hakuzidisha katika Swalah yake na wala hakupunguza.
Basi hapo itambomokea yeye (hatohitajia) kusujudu Sujuud-us-Sahuw kutokana na kauli inayojulikana kutoka katika madhehebu (ya Hanbaliy). Hili ni kwa kule kuondoka lile jambo linalowajibisha kusujudu, ambalo ni shaka. Inasemekana vilevile ya kwamba haitombomokea – yaani bado itakuwa ni wajibu kwake kusujudu Sujuud-us-Sahuw – ili amfedheheshe Shaytwaan.
Hili ni kutokana na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Na ikiwa ameswali kikamilifu Rakaa nne, inakuwa ni fedheha kwa Shaytwaan” na kwa sababu atakuwa ameswali sehemu katika Swalah hali ya kuwa ni mwenye shaka, na hii ndio kauli sahihi zaidi.
Mfano wa hilo
Mtu anaswali, kisha akawa na shaka katika Rakaa kama ni ya pili au ya tatu, na asibainikiwe na kitu kati ya hayo mawili.
>>Hivyo ataifanya hiyo Rakaa kuwa ya pili na atajengea Swalah yake juu yake. Kisha (katikati ya Swalah kabla hajatoa Salaam) ikambainikia ya kwamba kweli ilikuwa ni Rakaa ya pili, basi hana Sujuud-us-Sahuw juu yake.
>>Hili linajulikana katika madhehebu (ya Hanbaliy).
>>Na kauli ya pili tuliyotaja ni kwamba inamlazimu yeye kusujudu Sujuud-us-Sahuw kabla ya kutoa Salaam.
Itaendelea, Usikose sehemu ya 5 In Shaa Allaah..................................
from fisabilillaah.com https://ift.tt/2RdaTOn
via IFTTT
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni