Translate

Jumapili, 25 Novemba 2018

Risaalah fiy Sujuudus-Sahw (Sijda ya kusahau) - 5

                                             Risaalah fiy Sujuudus-Sahw (Sijda ya kusahau) 


                                   Mwandishi: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn 

                                                      Mfasiri: Abu Bakr Khatwiyb al-Atrush



Tunaendelea na Sehemu ya 5




                                                                Sujuud-us-Sahuw kwa maamuma 


Pale atakaposahau Imamu inakuwa ni wajibu kwa maamuma kumfuata Imamu katika Sujuud-us-Sahuw. 


Kutokana na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): 

“Hakika Imamu amewekwa ili afuatwe. Hivyo asiende kinyume na Imamu” mpaka pale aliposema “... na iwapo atasujudu basi nanyi sujudini.” (al-Bukhaariy na Muslim, kutoka katika Hadiyth ya Abu Hurayrah)


Sawa ikiwa Imamu atasujud Sujuud-us-Sahuw kabla ya kutoa Salaam au baada ya kutoa Salaam, itakuwa ni wajibu kwa maamuma kumfuata. 


Isipokuwa tu ikiwa huyo maamuma amepitwa na baadhi ya Rakaa. Hapo hawezi kumfuata katika Sujuud-us-Sahuw kutokana na udhuru utakaokuwa umetokea kwa yule ambaye amepitwa na Rakaa kwa kuwa haiwezekani kwake kutoa Salaam na Imamu wake. Kwa ajili hiyo yule maamuma atakamilisha yaliyompita kisha atoe Salaam, halafu atasujudu Sujuud-usSahuw na kutoa Salaam.


Mfano wa hilo


>>Mtu ameingia na Imamu katika Rakaa ya mwisho na Imamu juu yake ana Sujuu-us-Sahuw baada ya kutoa Salaam. Hivyo pale ambapo Imamu atatoa Salaam, huyu ambaye amepitwa na Rakaa atasimama ili kukamilisha (kulipa) yaliyompita na wala hatosujudu pamoja na Imamu. 


>>Pale atakapokamilisha Swalah yake, atasujudu Sujuud-us-Sahuw baada ya kutoa Salaam. Pale atakaposahau maamuma isiyokuwa Imamu, hali ya kuwa hakupitwa na kitu chochote katika Swalah, katika hali hii hana Sujuud-us-Sahuw juu yake. Kwa kuwa kusujudu kwake katika hali hii inapelekea katika kwenda kwake kinyume na Imamu na kutakuwa kumepatikana upungufu katika kumfuata. Kwa kuwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) waliacha Tashahhud ya kwanza pale ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ameisahau na hawakukaa chini. Wakasimama pamoja na yeye na hawakukaa katika Tashahhud kwa sababu ya kuchunga kule kumfuata Imamu na kutoenda naye kinyume. 



>>Ikiwa amepitwa na kitu katika Swalah na akawa amesahau kitu pamoja na Imamu wake wakati anaswali pamoja naye (bila ya yeye Imamu kusahau) au kwa zile Rakaa ambazo alikidhi (alilipa) baada yake. Katika hali hii haitombomokea (yaani ni lazima kwake) Sujuud-us-Sahuw. Itamlazimu kusujudu Sujuud-us-Sahuw baada ya yeye kukidhi (kulipa) zile Rakaa ambazo zitakuwa zimempita aidha kabla ya kutoa Salaam au baada ya kutoa Salaam kutokana na ufafanuzi uliyotangulia.


Mfano wa hilo


Maamuma amesahau kusema “Subhaana Rabbi al-´Adhwiym” katika Rukuu na hakupitwa na kitu chochote katika Swalah, sio lazima kwake kusujudu Sujuud-us-Sahuw. Endapo atakuwa amepitwa na Rakaa moja au zaidi, atailipa halafu atasujudu Sujuud-us-Sahuw kabla ya kutoa Salaam.


Mfano mwingine


Maamuma anaswali Dhuhr na Imamu wake. Wakati Imamu aliposimama katika Rakaa ya nne, yule maamuma alikaa akifikiria ya kwamba ile ni Rakaa ya mwisho. 

>>Lakini pale alipojua ya kwamba Imamu amesimama na yeye akasimama. 


>>Ikiwa hakupitwa na kitu chochote katika Swalah, itakuwa sio lazima kwake Sujuud-us-Sahuw. Na ikiwa alikuwa amepitwa na Rakaa moja au zaidi, ataikidhi (atazilipa) na kutoa Salaam, kisha atasujudu Sujuud-usSahuw kisha atatoa Salaam.



                                                                            Hitimisho


Inatubainikia sisi kutokana na yaliyotangulia: 

Kwamba Sujuud-us-Sahuw wakati mwingine inakuwa kabla ya kutoa Salaam na wakati mwingine inakuwa baada ya kutoa Salaam. 


Inakuwa kabla ya kutoa Salaam katika sehemu mbili;


Ya kwanza: 


Ikiwa kumetokea upungufu katika Swalah. Hili ni kutokana na Hadiyth ya ´Abdullaah bin Buhaynah (Radhiya Allaahu ´anhu) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisujudu Sujuud-us-Sahuw kabla ya Salaam wakati alipoacha Tashahhud ya kwanza. Hadiyth hii imeshatajwa hapo juu kwa lafdhi yake. 


Ya pili: 


Ikiwa mtu atakuwa na shaka na wala asibainikiwe na moja kati ya mambo mawili. Hili ni kutokana na Hadiyth ya Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anhu) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)aliamrisha yule ambaye amepatwa na shaka katika Swalah yake na akawa hajui ameswali Rakaa ngani, tatu au nne, atachukua ile idadi ya uchache na kusujudu Sujuud-us-Sahuw kabla ya kutoa Salaam. Hadiyth hii imeshatajwa hapo juu kwa lafdhi yake.



Inakuwa baada ya kutoa Salaam katika sehemu mbili;


Ya kwanza: 


Ikiwa mtu amezidisha katika Swalah yake. Hili ni kutokana na Hadiyth ya ´Abdullaah Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anhu) pale ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali Dhuhr Rakaa tano. Walipomkumbusha hili baada ya kutoa Salaam akasujudu Sujuud-us-Sahuw kisha akatoa Salaam. 

>>Wala hakubainisha ya kwamba Sujuud ni baada ya kutoa Salaam kwa kuwa hakujua kwamba amezidisha isipokuwa baada ya kutoa Salaam. Hili linaonesha dalili juu ya kuenea kwa hukmu vilevile. 


>>Inaonesha vilevile ya kwamba kule mtu kusujudu kwa sababu ya kuzidisha inakuwa baada ya kutoa Salaam, sawa ikiwa alijua kule kuzidisha kabla ya kutoa Salaam au baada ya kutoa Salaam.


Na katika mambo yanayohusu hilo 


Pale ambapo mtu atatoa Salaam kabla ya kumaliza Swalah yake kwa kusahau, kisha baadaye akakumbuka na akaikamilisha Swalah yake. 


>>Hapo atakuwa amezidisha Salaam katikati ya Swalah. Atatakikana kusujudu Sujuud-usSahuw baada ya kutoa Salaam. Hili ni kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhu) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoa Salaam katika Swalah ya Dhuhr au ´Aswr baada ya Rakaa mbili. Wakati walipomkumbusha  akakamilisha Swalah yake kisha akatoa Salaam. Halafu akasujudu Sujuud-usSahuw kisha akatoa Salaam.


Ya pili: 


Ikiwa mtu amepatwa na shaka halafu ikambainikia moja kati ya mambo mawili. Hili ni kutokana na Hadiyth ya Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anhu) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliamrisha kwa yule aliyepatwa na shaka katika Swalah yake atafute (ajengee) juu ya la usawa na aendelee kwa hilo kisha atoe Salaam halafu asujudu Sujuud-us-Sahuw kisha atoe Salaam. Hadiyth hii imeshatajwa hapo juu kwa lafdhi yake.


Pale ambapo mtu atakosea kwa kusahau mara mbili katika Swalah, ikamlazimikia yeye sehemu moja kusujudu Sujuud-us-Sahuw kabla ya kutoa Salaam na sehemu ya pili ikamlazimikia yeye kusujudu Sujuud-us-Sahuw baada ya kutoa Salaam. Wanachuoni wanasema ile ya kabla ya kutoa Salaam ndio itatangulizwa, hivyo atasujudu Sujuud-us-Sahuw kabla yake.



Mfano wa hilo


Mtu anaswali Dhuhr, akasimama katika Rakaa ya tatu. Lakini hakukaa katika Tashahhud ya kwanza, akakaa katika Tashahhud katika Rakaa ya tatu, akifikiria ya kwamba ndio Rakaa ya pili. Kisha akakumbuka ya kwamba ni Rakaa ya tatu, hivyo atasimama na kuswali Rakaa moja. Kisha atasujudu Sujuud-us-Sahuw halafu atatoa Salaam. 


Mtu huyu ameacha Tashahhud ya kwanza, ambapo hukumu yake Sujuud inakuwa kabla ya kutoa Salaam. Akazidisha kukaa katika Rakaa ya tatu, ambapo Sujuud inakuwa baada ya kutoa Salaam. Hivyo ile Sujuud-us-Sahuw kabla ya kutoa Salaam ndio itatangulizwa juu ya ile ya baada ya Salaam na Allaah ndiye Anajua zaidi. 



Ninamuomba Allaah Atuwafikishe sisi na ndugu zetu Waislamu kufahamu Kitabu Chake na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuvifanyia kazi, kwa nje na kwa ndani, katika ´Aqiydah, ´Ibaadah, mua´alama na Atupe mwisho mwema sote. Hakika Yeye Allaah ni Mkarimu.


from fisabilillaah.com https://ift.tt/2PSYu5L
via IFTTT

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...