Miongoni mwa majukumu hayo, la awali kabisa ni kwanza, kumtambua Yeye, Mwenyezi Mungu, kwa dhati. Kwa vile Allah hana sifa ya kuonekana katika maisha ya dunia, pia hashikiki, hagusiki na wala hadirikiwi kupitia milango ya fahamu, ndio maana ameweka utaratibu wa kujitambulisha kwa waja wake kwa sifa na ishara mbali mbali.
Kisha Allah Aliyetukuka alimpa mwanadamu nyenzo na uwezo wa kuzigundua ishara hizo na kuzifanya kuwa kielelezo cha kuthibitisha uwepo wa Mola anayestahiki kuabudiwa peke yake. Kwa hivyo, milango ya fahamu aliyotunukiwa mwanadamu si kwa ajili ya kuitafuta dhati ya Allah Muumba, bali ni kwa ajili ya kumsaidia kuzizingatia sifa, dalili na ishara za uwepo, ukubwa, nguvu na utawala wake, kisha wajisalimishe kwake kwa ibada na utiifu.
Msiba mkubwa uko kwa wale wajitiao upofu, uziwi na umajununi wakaenda kupinga uwepo wa nguvu inayoyatawala maumbile, yenye elimu isiyo na ukomo na hekima, yaani wanaopinga uwepo wa Allah. Wanakana licha ya kushuhudia dalili nyingi zinayothibitisha hayo!?
Aidha, hasara kubwa ni kwa wale wanaoamini katika wingi wa waungu (washirikina): “Na Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu, hakuna anayestahiki kuabudiwa ila Yeye, Yeye ni Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.” [Qur’an, 2:161].
Makala yetu ina nia ya kuzipitia dalili mbali mbali katika Qur’an zinazobainishana kuthibitisha uwepo wa Allah na Upweke wake, ukubwa wa huruma na neema kwa waja wake. Nakusudia makala hii kuwa ni nyenzo muhimu ya kuzijenga imani zetu juu ya Mola wetu na kuyastawisha matendo yetu ya kila siku.
Hoja juu ya Upweke wa Allah
Kimantiki, akili haikubali imani ya kuwepo zaidi ya mungu mmoja katika ulimwengu huu ulioumbwa kwa umakini, ufundi na ustadi wa ajabu, na ambao una nidhamu ya hali ya juu ya uendeshaji, kama ambavyo haiwezekani nchi moja kuwa na watawala wawili katika nafasi moja ya juu kabisa ya utawala bila mambo kwenda harijojo!
Hoja hii ya kifalsafa imeelezwa kati- ka Qur’an: “Mwenyezi Mungu hakujifanyia mtoto, wala hakuna pamoja naye mungu mwengine, ingekuwa hivyo basi kila mungu angelivichukua alivyoviumba, na baadhi yao wangeliwashinda wengine, Mwenyezi Mungu ameepukana na sifa wanazomsifu.” [21:91]
Hoja hii imewekwa wazi zaidi katika aya ya 22 sura ya 21 aya inayosema: “Lau kama wangelikuwemo humo (mbinguni na ardhini) waungu zaidi ya Mwenyezi Mungu (Muumba) bila shaka zingeliharibika, na ametakasika Allah yu mbali na yale (mapungufu) wanayomsifia.”
Aya hizi licha ya kuthibitisha upweke wa Allah, zinawashangaa wanaodai kuwepo waungu wengi wanavyoshindwa kutumia akili zao katika kuufikia ukweli halisi.
Tunajifunza kutokana na aya hizi kwamba, upweke wa Allah ni kitu kinacholazimishwa na akili iliyo salama; na akili hiyo inakataa kinyume. Aya hizi zinatufahamisha kwamba, utulivu wa viumbe vikubwa vinavyomzunguka binadamu ni kielezo tosha cha upweke wa Muumba, na kwamba pangelikuwa na miungu wengi pasingelibaki salama kwani wangegombea katika umiliki na madaraka hayo na kufikia maamuzi ya kuvunja ushirika huu wa kuumba na kuviendesha viumbe. Matokeo yake, kila mmoja angehamisha alichokiumba. Aya zinatupa picha kwamba, licha ya kila mungu kuamua kuondoka na alichokimiliki, lakini angelitaka kuvichukua hata vile vilivyoumbwa na waungu wenzake.
Kwa mfano, kama kuna mungu aliumba jua, bahari na miti, mwenzake aliumba mwezi, watu na wanyama, yule wa kwanza angehamisha vya kwake kisha akataka kumdhulumu mwenzake kwa kumuibia wanyama wake. Vurugu inglianza hapo. Ndio Allah Aliyetukuka anatuambia kwamba, mparaganyiko wa viumbe hivi vizito ungelitokea na kuangamiza hata viumbe vidogo vidogo na hapo maisha yasingewezekana.
Huu ugekuwa ni mparaganyiko uliosababishwa na ugomvi wa waungu (watawala) wengi wanaogombania madaraka. Lakini kwa vile ukweli hasa Mungu ni mmoja, ndio tunaona maumbile haya jinsi yanavyokwenda kwa utulivu na kwa hekima isiyo kifani.
Hapa yanathibitika maneno ya Allah Aliyetukuka: …لَوْ كَانَ فِيهِمَا آلِهَةٌ إِلَّا اللَّهُ لَفَسَدَتَا
Lau kaana fiihimaa aalihatun illla llaahu lafasadataa.” (lau kungelikuwa waungu wengi katika mbingu na ardhi zaidi ya Allah basi vingeliharibika).
Chukulia mfano mwengine. Allah Muumba wa dhati alishahukumu kwa elimu na hekima zake kulitoa jua Mashariki na kuzama Magharibi tokea mwanzo wa dunia mpaka karibu na kumalizika siku zake. Kama kungelikuwa na miungu mwengine kwa madaraka ama kwa uchokozi wake, siku moja angelitaka kuibadilisha nidhamu hii kwa kulitoa jua Magharibi na kwenda Mashariki!
Aibu na fedheha ilimpata kafiri aliyekumbana na Mtume Ibrahim (amani ya Allah imshukie) pale walipohojiana kuhusu maswala ya Imani. Huu ni moja ya ushahidi kuwa muumba na muendeshaji viumbe ni mmoja tu, hataki kuingiliwa katika mambo ya uumbaji, umiliki na uendeshaji viumbe.
Kisa kile cha Ibrahim kinasimuliwa kwa ufasaha katika Qur’an: “Hukusikia yule aliyehojiana na Ibrahim juu ya Mola wake kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa ufalme hamuongozi? Ibrahim aliposema, ‘Mola wangu ni Yule ambaye huhuisha na kufisha.’ Akasema, ‘Mimi pia huhuisha na kufisha.’ Ibrahim akasema,‘Mola wangu hulitoa jua Mashariki basi wewe litowe Magharibi.’ Akafedheheka Yule aliyekufuru, na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.” [Qur’an, 2:258].
Ishara za kuwepo Allah Ta’ala
Mwanadamu amezungukwa na miujiza na maajabu kila upande inayomtaka amtambue Allah na ukubwa wake. Jua, mwezi, miti mifupi na miefu, mimea, maziwa, mabwawa, bahari, milima na mabonde nk, vyote hivi kwa ajili hiyo.
Hata hivyo, vikwazo kadhaa vinamtenga mwanadamu na Imani ya kweli na kuathiri matendo yake. Vikwazo hivyo ni pamoja na maumbile yake ya kukizoea kitu kisha kukidharau, upotofu wa shetani, anasa zinazomvuta. Vyote hivi vinazidi kuilemaza akili ya mwanadamu na hata kumpelekea kukumbatia dhana ya ukoministi inayodai kila kitu kimejiumba chenyewe, na kwamba binadamu hana lengo lolote la kuwepo katika uhai huu zaidi ya kustarehe kwa kula sana, kunywa na kujamiiana.
Dhana ya ukomunisti inawataka wanadamu waamini kuwa, hatohojiwa na yoyote kuhusu maisha yake hapa duniani. Allah Aliyetukuka anasema: “Na ishara ngapi na ngapi katika mbingu na ardhi wanazozipitia na hali yakuwa wanazipuuza, na wengi katika wao hawamuamini Allah isipokuwa huku wanatia ushirikina.” [Qur’an, 12: 105- 106].
Allah Aliyetukuka anasema pia: “Na katika ishara zake ni usiku na mchana na Jua na Mwezi basi msilisujudie Jua wala Mwezi msujudieni aliyeviumba ikiwa nyinyi mwataka kumuabudu.”
Katika kuwakumbusha waja wake kwenye aya nyingine anasema: “Je hawaangalii katika ufalme wa mbinguni na ardhini na (hawafikiri) kuwa pengine ajali yao iko karibu, basi baada ya maneno haya hadithi gani watakayoiamini?” [Qu’an, 7: 185].
Basi ndio hivi walimwengu tunaishi kwa mghafala mkubwa na maumbile haya katika makazi yetu na tukisafiri tunakwenda kushuhudia maajabu mengi na makubwa zaidi, lakini si wengi miongoni mwetu wanaokumbuka kuweka ufahamu wa kweli na kuona utukufu wa Mola Muumba na kumnyenyekea.
Allah anasema: “Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kutofautiana usiku na mchana na vyombo vipitavyo katika bahari kwa (kuchukua vitu) vifaavyo watu, na maji ayateremshayo Allah kutoka mawinguni na kwa maji hayo akaifufua ardhi baada ya kufa kwake, na akaeneza humo, kila aina ya wanyama, na katika mabadiliko ya pepo na mawingu yaamrishwayo kupita baina ya mbingu na ardhi, bila shaka (katika yote hayo) zimo ishara (za kuwepo Mwenyezi Mungu) kwa watu wenye akili.” [Qur’an 2:164].
Aya hizi na zinazofanana nazo zinatutaka tutumie akili na vipawa vyetu kwa kuyazingatia maumbile na mazingira tunayoyashuhudia kila siku, na hilo litupelekee kuipata imani ya kweli juu ya Muumba.
Mabadiliko ya upepo kutoka mashariki kwenda magharibi, kutoka kusini kwenda kaskazini, vyombo vya baharini vikiwa vimebeba mizigo na bidhaa kwa maslahi ya watu, mvua inayotegemewa kuingiza unyevuunyevu katika ardhi, uoteshaji wa miti mirefu, mifupi na mimea kwa maisha ya watu na wanyama, hizi zote ni ishara za wazi zinazomtambulisha mja kumjua Mola wake, hekima na uwezo wake usio na mipaka ambazo waja wanazidi kuzipuuza.
“Na katika ishara zake ni usiku na mchana na jua na Mwezi basi msilisujudie Jua wala Mwezi msujudieni aliyeviumba ikiwa nyinyi mwataka kumuabudu.”
“Je hawaangalii katika ufalme wa mbinguni na ardhini na (hawafikiri) kuwa pengine ajali yao iko karibu, basi baada ya maneno haya hadithi gani watakayoiamini? [Qu’an, 7: 185]
from TIF https://ift.tt/2P12z2v
via IFTTT


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni