Hijabu
Assallaaam Aleykum WarahmatulLaah Wabarakatuh
Nataka kulenga shabaha kwenye mojawapo ya vifaa vya stara. Kitu muhimu katika maisha ya mwanamke ni Hijaab. Nitaanza na Hijaab ya wanawake.
Ingelikuwa kaka zetu na dada zetu wa kiislamu wana haya, basi jamii yetu ingeongoka katika njia ya haki. Lengo langu sio kushambulia au kuhukumu wanawake. Namuomba Allaah سبحانه وتعالى Awape thawabu kwa kuchukua wakati kusoma maneno haya. Nitaanza na mojawapo ya rangi za stara, nayo ni stara ya mwanamke.
Kwanini naanza na mwanamke? Nataka kumshambulia au kumhukumu? Labda sitaki kuwaudhi wanaume? La hasha! Allaah سبحانه وتعالى Asijaaliye. Lakini mwanamke akiongoka na akihifadhi stara yake, basi jamii yote pia itaongoka na itahifadhi stara yake.
Hivyo basi , maadui wa waislamu wanapotaka kuangamiza kitu, kitu cha kwanza wanacho athiri ni mwanamke! Kwasababu mwanamke akipoteza stara yake, ni rahisi kwa vijana pia kupotea, hivyo basi ni rahisi kwa jamii nzima kupoteza stara yao. Kwahivyo tukisema stara kwa mwanamume ni wajib, basi kwa mwanamke pia ni wajib, na ni mujibu. Kwa ajili ya tabia ya mwanamke ya kuwa na haya, ni rahisi kwake kuwa karibu na stara. Na kitu muhimu kabisa kwa mwanamke ni nini?
Ni kujihifadhi na kujifunika mwili wake. Kitu kikubwa anachomiliki mwanamke, ni Hijaab yake. Kwa kaka na dada wanaosoma haya, someni na muwafahamishe dada zenu na jamaa zenu. Na dada yangu katika Uislamu, ikiwa unasoma haya, ilihali wewe ni muhajjaba (mwenye kuvaa Hijaab), basi eneza risala hii kwa dada zako wa kiislamu, na ikiwa wewe sio muhajjaba, basi jaribu upate faida kutokana na haya.
Kitu kilichotukuka kabisa ambacho mwanamke anamiliki, ni stara. Na kitu cha thamani katika stara ni Hijaab. Nikikuuliza kitu gani cha thamani unachomiliki, itakuwa ni nini? Ukiwa na kitu cha thamani, utakitunza na kukihifadhi? Utakificha au la? Ukiwa na lulu au johari, je, utaihifadhi mahali pazuri au la? Kila thamani yake ikizidi, basi utazidi kutaka kuihifadhi. Hivyo basi, utaificha watu wasiione. Au utaionyesha na kuiweka wazi mbele ya kila mtu aione na achukue atakacho kutokana nayo?
Hakika utaihifadhi! Vile vile, mwanamke ni kiumbe mwenye thamani kubwa kwa hivyo inampasa ajihifadhi.
Ndugu na dada, je, unajua kama lulu inahifadhiwa na kaka (ganda) lake? Kweli au si kweli. Kwa hivyo huwezi kuwa bila ya Hijaab kwani Hijaab inakuhifadhi na fitna nyingi.
Mwanamke ni lazima ajistiri kwa kuvaa Hijaab kwasababu ni rahisi sana mwanamume kumtongoza yeye kwa uzuri wake.
Kabla ya Uislamu kutujia, mataifa mengi yaliamini kuwa uzuri wenye thamani unapatikana katika mwili wa mwanamke peke yake. Uislamu ulipokuja ulibadili fikra hizo kwa kufundisha watu kuwa uzuri wa mwanamke sio wa mwili peke yake, bali ni wa tabia, fikra na mengineyo mengi.
Haijaandikwa kabisa sheria ya kuwa mwanamke lazima ajioneshe uzuri wake. Hakuna apasae kuuona wala kuufaidi uzuri wake ispokuwa mumewe. Watu aina gani wanampa mwanamke heshima anayostahiki? Watu ambao wanamfanya mwanake ajioneshe uzuri wake, au wenye kumfundisha ajistiri uzuri wake ila kwa wale wanaostahiki kumuona uzuri wake? Wengine wanadai kuwa Hijaab sio wajibu. Tuangalie Qur-aan inasema nini kuhusu Hijaab.
{Ee Mtume waambie wake zako, na binti zako, na wanawake wa Kiislamu wajiteremshe uzuri nguo zao. Kufanya hivyo kutapeleka upesi wajulikane (kuwa ni watu wa heshima) wasiudhiwe. Na Allaah ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu} [Al-Ahzaab 33: 59].
Tuzingatie kuwa Allaah anapozungumzia kuhusu Hijaab kuwa wajibu, Amejumuisha wanawake wenye kuamini pia, sio wake za Mtume صلى الله عليه وسلم peke yake, kwa hivyo ni wazi kuwa aya hii haikuteremshwa kwa jamii ya Mtume صلى الله عليه وسلم pekee, imeteremshwa kwa ajili ya kuhifadhi wanawake wote. Kwa hivyo wanawake wote wenye kuamini ni lazima wavae Hijaab ili waheshimiwe na wajulikane kuwa ni wenye haya. Hakuna atakaemdhuru kwa ajili ya heshima aliyojiwekea juu ya mavazi yake.
Hijaab ni lazima! Allaah سبحانه وتعالى Anasema:
{Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yaliyo khusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajuulikane mapambo waliyo yaficha. Na tubuni nyote kwa Allaah, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa} [An-Nuwr 24: 31].
Wataalamu wengi wanasema kuwa ni lazima wanawake wajifunike mwili wote ispokuwa viganja vya mkono na uso.
Allaah سبحانه وتعالى Aliposema wanawake wavae Khimaar, Hakumaanisha kuwa wavae leso kubwa tu, bali ni kuwa mwanamke akivaa hiyo Khimaar, itamfunika mapambo yake muhimu, nayo ni masikio, shingo na kifua. Kwa hivyo, mwanamke akivaa kitambaa kidogo ambacho hakimsitiri mapambo yake hayo tuloyataja, basi hiyo sio Hijaab
Baada ya kuona katika Qur-aan kuwa Hijaab ni wajibu, inampasa mume kumhimiza mkewe na kumshawishi avae Hijaab ili aheshimiwe na athaminiwe kuwa ni mchaji Allaah. Katika aya nyengine Allaah سبحانه وتعالى anawahutubia wanawake wa Kiislamu wasioneshe mapambo yao kama walivyokuwa wakifanya wanawake wakati wa jahilia (kabla Uislamu). Wanawake wa jahilia walikuwa wakivaa nguo ndefu lakini mapambo yao yote yalikuwa yakionekana, kama vile shingo, masikio, nywele na kadhalika.
Aayah ya Hijaab ilipoteremka tu, wanawake wote walitoka huku wamevaa Hijaab. Wanaume waliposikia aya hiyo waliwaeleza wanawake maana yake, basi wanawake walikuwa tayari Kufuata shari'ah ya Allaah سبحانه وتعالى kama alivyoieleza katika Qur-aan. Madhali walikuwa hawana uwezo wa kununua nguo mpya, walinyanyua nguo zao kwa sehemu mbili ili watumie kama Hijaab.
Hiyo ni kinyume na vile wanawake wakisasa walivyo. Wao hutoa visingizio kwa kutovaa Hijaab inayotakikana. Mtume صلى الله عليه وسلم alisema:
“Kikundi cha wanawake hawatoingia peponi. Hao ni miongoni mwa wale wanaovaa nguo za kubana, za kuonyesha mwili na hawafuati amri ya Allaahسبحانه وتعالى ya kuvaa Hijaab. Hawataingia tu peponi bali hata hawatasikia harufu ya pepo ambayo harufu yake husikilizana masafa ya mwendo wa miaka 500.” [Muslim].
Kutilia mkazo umuhimu wa kujifunika, Ilimbidi Mtume صلى الله عليه وسلم alipige vita kabila moja la Kiyahudi ambalo lilimchezea shere mwanamke wa Kiislamu sokoni. Walimfanyia hila huyo mwanamke kwa kuifunga nguo yake ili akitembea aanguke na nguo yake ipasuke kisha awe uchi. Basi mwanamume mmoja aliyeshuhudia hayo, alipigana na kumuuwa yule Yahudi aliyefanya mambo hayo. Mtume صلى الله عليه وسلم aliamrisha jeshi lake liwafukuze kabila hilo la Kiyahudi nje ya Madinah.
Ni Ipi Sababu Yako Ya Kutovaa Hijaab?
1. Sijasadikika Na Hijaab
Sasa nitakuuliza wewe ni nani? Utajibu wewe ni Muislamu. Uislamu unaamanisha nini? Uislamu ni kumtii Allaah سبحانه وتعالى kabisa kwa mambo yote aliyotuamrisha. Na kuvaa Hijaab ni mojawapo ya maamrisho ya Allaah سبحانه وتعالى. Mwanamke ambae hataki kuvaa Hijaab basi hajamtii Allaah سبحانه وتعالى.
2. Sababu Ya Pili
Mwanamke ambae anadai kuwa kitu muhimu ni nia yake, na kuwa dhamira yake sio mbaya na kuwa yeye ni mtu mzuri, na kuwa Hijaab ni ya moyo. Mwanamke huyo huyo anadai kuwa anaswali swala tano, sunna na swala za usiku na anatoa sadaka. Kweli anafanya yote hayo, lakini kisha anasema ibada hizo zinatosha. Subhana Allaah! Kasema Allaah سبحانه وتعالى:
{Je! Mnaamini baadhi ya Kitabu na mnakataa baadhi yake? Basi hana malipo mwenye kutenda hayo miongoni mwenu ila hizaya katika maisha ya duniani, na Siku ya Qiyaamah watapelekwa kwenye adhabu kali kabisa. Na Allaah si mwenye kughafilika na yale mnayo yatenda}. [Al-Baqarah 2: 85].
Kwa hivyo tufanye hisabu, unasema unafanya mengi mema, kuwa nia yako ni nzuri na moyo wako ni msafi. Sawa, lakini kila siku unapotoka, wanaume wangapi wanakuangalia nywele zako, na uzuri wako wote, je unakusanya madhambi tele au la? Hakika unakusanya madhambi kwasababu hukufuata amri ya Allaah سبحانه وتعالى. Na huyu mwanamke atashindana kuwa sio makosa yake wanaume wakimuangalia kwasababu nia yake sio mbaya, bali atasema kuwa wanaume ndio watakao pata madhambi. La hasha! Wewe ndio chanzo cha hao wanaume kukuangalia kwasababu hujavaa Hijaab na unavutia.
Mwanamke ambae havai Hijaab bila shaka anakusanya madahmbi mengi, kwasababu, wanaume wana nyoyo zenye matamanio na macho yenye kutaka. Hebu fikiria madhambi kiasi gani anayakusanya mwanamke huyu. Je, yale mema yote yanamtosha yakilinganishwa na madhambi yake? Fikiria akitoka, ndani ya mabasi, ndani ya treni, kazini, barabarani, na kila pahali, madhambi mangapi atapata kwa kila mwanamume anaemuangalia uzuri wake akamtamani?
Allaah سبحانه وتعالى Hakukuamrisha uvae Hijaab? Nakuogopea kuwa mema yako yana anguka kutoka kwenye mfuko uliopasuka. Yale mema yanaingia kwa juu na kutoka kwa chini.
3. Hijaab Na Joto
Mwanamke anaweza akalalamika kuwa nywele zake zinadondoka akivaa Hijaab kwa ajili ya joto, na akakuuliza, “unataka niwe kipara sasa?” Ewe dada, Allaah سبحانه وتعالى anasema kuwa moto wa jahannam ni mkali kuliko moto wa duniani.
Mtume صلى الله عليه وسلم amesema:
“Moto umezungukwa na matamanio yetu, na pepo imezungukwa na juhudi zetu.”
Bado unaona tabu kuvaa Hijaab, unaona tabu kufuata maamrisho ya Allaah سبحانه وتعالى .
4. Si Hoja Kuvaa Hijaab Kuwa Ndio Heshima
Wengine husema kuwa wanajua wanawake ambao wanavaa Hijaab lakini wana tabia mbaya kabisa. Kwa hivyo hawataki kuvaa Hijaab wakaonekana kama hao.Sasa basi kwa yule mwanamke anaedai hayo: Tunajua watu tele wanaoswali lakini wanafanya maaswia, hiyo inamaanisha sisi pia tusiswali? Wengine ni muhujjaj na wanafanya mambo yasiokuwa, inamaana tusende hajj? Kwa hivyo dada yangu Hijaab sio mbaya, bali mwenye kuivaa na kuiharibia sifa zake ndio mbaya.
5. Allaah سبحانه وتعالى Hajaniongoza Bado
Nitavaa Hijaab baadae lakini sio sasa kwasababu Allaah سبحانه وتعالى hajaniongoza bado.Kwa hivyo nikifika miaka hamsini baada ya kufaidi ujana wangu, ndio nitavaa Hijaab. La, dada yangu! Hiyo ni makosa kabisa. Allaah سبحانه وتعالى anasema kuwa Habadili hali ya watu mpaka wale watu wabidili yaliyomo mwao. Huwezi kuvaa Hijaab mpaka ujitahidi. Haikubaliki kusema kuwa Allaahسبحانه وتعالى hajakuongoza, la, Allaah سبحانه وتعالىamekuongoza kiasi ya kuwa unasoma makala haya. Sibabu ya wewe kusoma haya ni kuwa Allaah سبحانه وتعالى anakufungulia njia ya kuongoka, Nae Hamuachi mja Wake ispokuwa Anamuonesha uongofu, sasa ni uu ya yule mja kufuata au kukanusha.
6. Nikiolewa Nitavaa Hijaab.
Wanaume wengi wanapotaka kuoa, hutafuta wanawake wacha Mngu walio na heshima wanaovaa Hijaab. Munapotaka kuolewa, oleweni na wanaume ambao watakupendeni kwa ajili ya dini yenu na watakao waheshimu. Kwa hivyo Allaah سبحانه وتعالى Atakupeni waume walioshika dini.
Yuko mtu alikwenda kwa ulamaa akamuuliza,” nikitaka kumuozesha dada yangu, nimuozeshe mtu aina gani?” ‘Aalim akamjibu, “Muozeshe mwanamume ambae ni rafiki wa Uislamu, hivyo basi, akimpenda, atamheshimu, na akimchukia hatomfanyia ubaya.
Kwa hivyo dada zangu, oleweni na wanaume ambao watakao wakinga na kuwaheshimu na kufurahikia kuwa nyinyi ni Muhjaba.
7. Mimi Bado Kijana
Unajua lini utaiaga hii dunia dada yangu? Vifo vya vijana vimeenea! Nitawapa mfano. Kisa hichi kilitendeka kikweli huko Misri(Egypt, Alexandria) wakati wa Ramadhani
Yuko mtu na mkewe ambae ni muhajaba na majirani zao ambao ndani yake yumo msichana ambae sio muhajaba. Huyo msichana kama wasichana wengi wakiislamu alikuwa na moyo mzuri, lakini hakufahamu maana ya Hijaab katika Uislamu. Huyo mwanamke muhajaba alikuwa na uhusiano mzuri na yule msichana. Hakumpuuza kwa ajili havai Hijaab, la, alikuwa rafiki yake. Siku moja yule msichana alimuomba yule mwanamke ampeleke madukani akanunue ya patashika ( jeans). Yule mwanamke muhajaba alikuwa na hikma na alijua kuwa ni lazima ampe yule msichana mawaidha, basi akakubali kumpeleka lakini kwa shuruti moja. Akamwambia amfuate kwenye muhadhara. Basi yule msichana akakubali.
Walipokwenda kwenye muhadhara, mada ilikuwa kuhusu kutubia kwa Allaah سبحانه وتعالى Basi yule msichana aliingiwa na imani nyingi kwa yale yaliyokuwa yakisemwa, mpaka akaanza kulia na huku akirudia maneno haya,”nimetubu Mola wangu, nifunikeni”. Wale waliohudhuria wakamwambia watampeleka nyumbani ili akavae Hijaab, lakini yule msichana alikataa, alitaka avae Hijaab pale pale, kasema hawezi kutoka hapo bila ya kuvaa Hijaab. Basi akatafutiwa Hijaab akavishwa, akitoka tu na kutaka kudakia barabara, gari likamgonga, hapo hapo akafariki. MashaAllaah! Msichana huyo alikufa baada tu ya kutubia, Subhana Allaah! Kwa hivyo wasichana, musitoe sibabu ya kuwa bado nyinyi ni wadogo, hakuna anaejua ataondoka duniani saa ngapi.
8. Nataka Kufuata Fesheni, Nikivaa Hijaab Nitaachwa Nyuma
Mola wako mlezi sio bora kuliko fesheni? Nakuhakikishia, ukivaa Hijaab utakuwa una nuruitokayo kwako.
9. Nataka Kuiga Watu Wa Magharibi (Westerners).
Nani anaemheshimu mwanamke zaidi? Uislamu au wale ambao hawawezi kuuza kitu bila ya kuweka picha ya mwanamke aliye kuwa tupu? Wao ndio wamempa mwanamke heshima au wamemdhulumu? Au Uislamu uliomheshimu mwanamke na kumpa daraja za juu na kumstiri kutokana na kudhulumiwa?
10. Sitaki Kuvaa Hijaab Kwa Sababu Naogopa Nitaivua
Subhaana Allaah! Dada, kwanini huvai Hijaab na nia madhubuti huku unamuomba Allaah سبحانه وتعالى Akuhifadhi na kuitoa. Kuitoa Hijaab ni madhambi makubwa, usifanye hivyo, utakuwa unatoa mfano gani?
Vaa Hijaab kisha ufanye mambo haya ili uhakikishe kuwa hutoitoa Hijaab yako.
1. Kuwa na marafiki wema walioshika dini.
2. Hudhuria na sikiliza mawaidha ya Kiislamu.
3. Omba dua kwa Allaah سبحانه وتعالى Akuzidishie Imani ya dini yako na Akupe guvu ili uvae Hijaab yako kila siku.
11. Naona Hayaa
Naona haya na aibu kutokana na yale watakayoyasema marafiki zangu nikivaa Hijaab. Dada, hutaona haya mbele ya Allaah سبحانه وتعالىsiku ya kiama? Hutotahayuri mbele ya Mtume Muhammad صلى الله عليه وسلم? Hakuna kutahayuri wala kuona haya mbele ya waja ikiwa unamuasi Mola wako.
Siku ya kiama utakuwa na kiu cha ajabu, na Mtume صلى الله عليه وسلم atakuwa anawapa watu maji. Utamkimbilia Mtume صلى الله عليه وسلم ili na wewe upate maji, lakini Malaika wawili watakuzuia ili usimfikie Mtume صلى الله عليه وسلم. Nae Mtumeصلى الله عليه وسلم atawaambia wale Malaika wakuache kwasababu wewe ni katika umma wake. Wale Malaika watamwambia Mtume صلى الله عليه وسلم kuwa huyu ni katika wale ambao hawakufuata maamrisho ya Allaah سبحانه وتعالى. Basi Mtume صلى الله عليه وسلم ataondoka na kwenda mbali nawe huku anasema hataki uhusiano wowote na wewe kwa ajili hukufuata maamrisho ya Allaah سبحانه وتعالى.
Nani atatahayuri wakati huo? Yule ambae anaonesha mapambo yake kwa kila mtu au yule anaejistiri na kujiheshimu?
Mtume صلى الله عليه وسلم amesema: “Ukamateni Uislamu na mikono yenu na meno yenu”.
Nawasisitiza dada zangu katika Uislamu, mukitaka kuvaa Hijaab, vaeni sasa musisubiri baadae, kwani hamujui kama mutafika wakati huo munaoutarajia. Ukivaa Hijaab sasa, Mshukuru Allaah سبحانه وتعالى, swali kwa saa zake, tafuta marafiki wema na soma Qur-aan kila siku hata kama ni kidogo.
Mukifanya mambo hayo, basi inshaAllaah Hijaab yako itakwenda sambamba na kuabudu kwako, tabia yako njema, na pia utakuwa mfano mzuri kwa wanawake Waislamu na wasiokuwa Waislamu.
Ukiwa umeamua kuwa muhajaba, basi usifikirie kuwa kuvaa Hijaab ndio kumekamilisha ibada zako na utaingia peponi, la, kuvaa Hijaab ndio miongoni mwa njia za kuelekea kwa Allaah سبحانه وتعالى.
Kumbuka kuwa wewe ni mfano kwa wanawake Waislamu na wasiokuwa Waislamu, kwa tabia yako njema, kuabudu kwako, mavazi yako, na kadhalika. Bila shaka utamuathiri kila anaekuona hata bila ya kusema chochote. Utakuwa umeisafisha jamii, na matendo yako mema yako katika daraja ya juu mbele ya Allaah سبحانه وتعالى. Utawaongoza dada zako katika Uislamu kwasababu wewe ndio mfano na waziri wa Waislamu.
Yafuatayo ni machache tu kuhusu namna gani kuvaa Hijaab. Ikiwa hufuati haya, basi ina maana kuwa huvai Hijaab sawa sawa.
1- Sio-lazima uvae Khimaar au ‘Abaayah. Unaweza ukavaa chochote, alimradi iwe ndefu na sio ya kushika mwili, na ifunike mwili wote. Ukivaa chochote ambacho kinaonesha umbile la miguu, kiuno, mabega, kifua, na kadhalika, basi hujavaa Hijaab sawa sawa.
2- Kutovaa nguo nyembamba zinazoonyesha mwili.
3- Kujifunika mwili mzima.
4- Kutovaa nguo zinazofanana na nguo za kiume.
5- Kutotia manukato unapotoka nje.
Ukifuata hoja hizi wakati wote, basi umekamilisha Hijaab na umekuwa Muhajjabah In shaa Allaah.
from fisabilillaah.com https://ift.tt/2DkWIDF
via IFTTT
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni