Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:
1- Allaah (Ta´ala) amesema:
وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ
“Ukiwauliza bila shaka watasema: “Hakika sisi tulikuwa tunaporoja na tunacheza.“(at-Tawbah 09:65)
2- Ibn ´Umar, Muhammad bin Ka´b, Zayd bin Aslam na Qadaatah wamesimulia:
“Wakati wa vita vya Tabuk kuna mtu aliyesema: “Hatujapata kuona watu kama wasomi wetu hawa, matumbo yao yanapenda kula sana, ndimi zao zinasema uongo na ni waoga wakati wa mapambano”. Akimaanisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake waliokuwa wasomi. ´Awf bin Maalik akamwambia: “Hakika umesema uongo, lakini wewe ni mnafiki! Nitamweleza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” ´Awf akaenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumweleza ambapo akakuta Qur-aan imekwishamtangulia. Mtu yule akaja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akakuta Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio anaanza kuondoka mahali hapo na kishampanda ngamia wake. Yule mtu akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Hakika sisi tulikuwa tunafanya mzaha na tukipiga masoga ili muda uweze kwenda.”
Ibn ´Umar amesema:
“Kama kwamba hivi sasa namuona mtu huyo akining´inia kamba za ngamia wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na huku mawe yakikwaruza miguu yake na huku akisema: ”Hakika tulikuwa tunaporoja na tunacheza.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia:
أَبِاللّهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِؤُونَ
“Je, mlikuwa mkimfanyia mzaha Allaah na Aayah Zake na Mtume wake?”
Hamgeukii na wala hazidishi jengine zaidi ya hayo.”[1]
MAELEZO
Mlango huu unazungumzia kwamba wale waislamu ambao wanafanya istihzai na Allaah, Qur-aan na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanaritadi. Mlango unazungumzia kwamba kufanya mzaha ni kuritadi na kufuru, kama inavyopata kufahamika kutoka katika kichwa cha mlango. Ni jambo linalotambulika kutokana na maneno ya Allaah (Ta´ala):
وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ قُلْ أَبِاللّهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِؤُونَ
“Ukiwauliza bila shaka watasema: “Hakika sisi tulikuwa tunaporoja na tunacheza. Sema: “Je, mlikuwa mkimfanyia mzaha Allaah na Aayah Zake na Mtume wake?”
2- Ibn ´Umar, Muhammad bin Ka´b, Zayd bin Aslam na Qadaatah wamesimulia:
“Wakati wa vita vya Tabuk kuna mtu aliyesema: “Hatujapata kuona watu kama wasomi wetu hawa, matumbo yao yanapenda kula sana, ndimi zao zinasema uongo na ni waoga wakati wa mapambano”. Akimaanisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake waliokuwa wasomi. ´Awf bin Maalik akamwambia: “Hakika umesema uongo, lakini wewe ni mnafiki! Nitamweleza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” ´Awf akaenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumweleza ambapo akakuta Qur-aan imekwishamtangulia. Mtu yule akaja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akakuta Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio anaanza kuondoka mahali hapo na kishampanda ngamia wake. Yule mtu akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Hakika sisi tulikuwa tunafanya mzaha na tukipiga masoga ili muda uweze kwenda.”
Mtu yule alisema:
“Matumbo yao yanapenda kula sana… “
Bi maana wanapenda kula sana.
Vilevile amesema:
“… na ni waoga wakati wa mapambano.”
Bi maana sio mashujaa.
´Awf bin Maalik amesema:
“Hakika umesema uongo, lakini wewe ni mnafiki!”
Hapa ndani yake kuna kukemea maovu kwa yule aliyeyasikia. Ni wajibu kwa yule aliyeyasikia kuyakaripia na khaswakhaswa ikiwa inahusiana na maovu kama haya makubwa na ya khatari ambapo Allaah, Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na dini yake vinatukanwa.
Imekuja katika Hadiyth:
“… ambapo akakuta Qur-aan imekwishamtangulia.”
Bi maana akakuta kumekwishateremshwa Aayah juu yao, nazo ni maneno Yake Allaah (Ta´ala):
وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ قُلْ أَبِاللّهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِؤُونَ
“Ukiwauliza bila shaka watasema: “Hakika sisi tulikuwa tunaporoja na tunacheza. Sema: “Je, mlikuwa mkimfanyia mzaha Allaah na Aayah Zake na Mtume wake?”
Hapa kuna dalili inayoonyesha kwamba yule mwenye kufanya istihzai na Qur-aan, Sunnah au Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi ni kafiri. Haijalishi kitu hata kama atasema kuwa anafanya hivo ili muda uweze kwenda haraka safarini na kwamba hakuwa ni mwenye kumaanisha hivo; ni kafiri kwa hali zote. Kwa sababu kufanya mzaha kama huu haufai safarini wala kwenginepo. Mwenendo kama huu unaonyesha unafiki uliyomo moyoni mwake, ubaya na chuki zake dhidi ya waislamu. Muislamu hawezi kusema maneno yaliyosemwa na mtu huyu na khaswa anapowatuhumu uongo. Huku ni kumkadhibisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake. Amewatuhumu kwamba ni waoga na waroho, jambo ambalo linaonyesha kuipupia kwao dunia. Wakati alipokuja akitoa nyudhuru mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akampuuza. Hakuna jengine alichomwambia isipokuwa:
أَبِاللّهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِؤُونَ
“Je, mlikuwa mkimfanyia mzaha Allaah na Aayah Zake na Mtume wake?”
Ni dalili inayothibitisha kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumkubalia udhuru wake huu na akambainishia kwamba ni kafiri kwa kitendo hichi. Hapa tunapata kubainikiwa kwamba yule mwenye kufanya mzaha na Shari´ah ni kafiri baada ya kuamini kwake. Kadhalika ikiwa atamponda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au akasema kuwa ni mwoga, mwongo, kwamba hakufikisha ujumbe au mapungufu mengine kama hayo. Vivyo hivyo inahusiana na yule mwenye kusema kwamba Qur-aan ni yenye kujigonga, kwamba Qur-aan au Shari´ah si vyenye kukamilisha yale wanayohitajia watu au mfano wa ukosoaji au upungufu mwingine kama huo. Hata hivyo akisema kuwa Qur-aan imekuja kubainisha baadhi ya mambo ambayo hayakutajwa katika Qur-aan ni kweli. Ama ikiwa anazungumza hivo kwa njia ya kejeli na kwamba watu wanahitajia sheria zilizotungwa na watu na kwamba Qur-aan na Sunnah si venye kutosheleza ni kufuru kubwa na kuritadi. Kadhalika inahusiana na anayesema kwamba Pepo ni mambo ya ndoto tu na sio mambo ya kweli.
[1] Ibn Jariyr (10/172) na Ibn Abiy Haatim (10047). Nzuri kwa mujibu wa al-Waadi´iy katika ” as-Swahiyh al-Musnad min Asbab-in-Nuzuul”, uk. 122.
from Firqatu Nnajia https://ift.tt/2PCIpQF
via IFTTT
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni