Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:
1- Abu Shurayh ameeleza ya kwamba alikuwa akiitwa “Abul-Hakam”, baba wa wahakimu, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Allaah ndiye Hakimu na hukumu ni Yake.” Kisha Abu Shurayh akasema: “Hakika watu wangu wanapotofautiana katika kitu basi hunijia na nikahukumu baina yao na matokeo yake pande zote mbili huridhika.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ni uzuri ulioje wa jambo hilo! Kwani wewe huna mtoto?” Nikasema: “Shurayh, Muslim na ´Abdullaah.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ni nani mkubwa wao?” Nikasema: “Shurayh.” Ndipo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Basi wewe ni Abu Shurayh.”[1]
Ameipokea Abu Daawuud na wengineo.
MAELEZO
Anachotaka kubainisha mwandishi ni kwamba ni wajibu kuyaheshimu majina ya Allaah na kutahadhari juu ya kuyatweza, kuyadharau au kumwita nayo mwengine yale majina ambayo ni maalum Kwake Yeye. Kwa ajili hiyo ni jambo limesuniwa kuyabadilisha kwa ajili ya kuyaheshimu na kuyaadhimisha.
Majina yamegawanyika sehemu mbili:
1- Majina ambayo haifai kuwa nayo isipokuwa Allaah peke yake. Mfano wa majina hayo ni ar-Rahmaan, al-Khaaliq na Rabb-ul-´Aalamiyn.
2- Majina ambayo sio maalum kwa Allaah (Subhaanah) pekee. Katika hali hii majina haya ya Allaah yanalingana na utukufu na ukubwa wa Allaah na majina ya viumbe yanalingana na maumbile yao. Makusudio ya mlango huu ni hayo majina ya kwanza.
1- Abu Shurayh ameeleza ya kwamba alikuwa akiitwa “Abul-Hakam”, baba wa wahakimu, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Allaah ndiye Hakimu na hukumu ni Yake.” Kisha Abu Shurayh akasema: “Hakika watu wangu wanapotofautiana katika kitu basi hunijia na nikahukumu baina yao na matokeo yake pande zote mbili huridhika.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ni uzuri ulioje wa jambo hilo! Kwani wewe huna mtoto?” Nikasema: “Shurayh, Muslim na ´Abdullaah.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ni nani mkubwa wao?” Nikasema: “Shurayh.” Ndipo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Basi wewe ni Abu Shurayh.”
Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:
“Ni uzuri ulioje wa jambo hilo!”
Bi maana ni uzuri ulioje wa jambo hili wa kusuluhisha kati yao na kuwaombea hadi wakaridhika na wakaacha kuzozana. Hivi ndivo inavyotakikana kuwa.
Faida mbalimbali:
Ni wajibu kuyaheshimu majina ya Allaah na kubadilisha jina kwa ajili ya hilo. Ndio maana akambadilisha jina lake la Abul-Hakam na kumpa Abu Shurayh. Hadiyth inaonyesha pia kwamba kun-ya ya mtu inapaswa iwe ya yule mtoto wake mkubwa.
Hadiyth inatupa dalili nyingine kwamba imesuniwa kusuluhisha hali za watu na kwamba ni jambo linalotakikana na inapaswa kwa wale wakuu kuwaombea baina ya watu wakati wa magomvi ili wasiendelee kugombana na kufanyiana vifundo na chuki. Kusuluhisha kati ya watu ni bora kuliko kuwahukumu. Hukumu inapelekea katika mizozo. Wakipatana kwa kuridhiana na ikaondoka ile chuki yote iliyomo vifuani mwao na mapenzi na mahaba yakafunguka inakuwa bora.
Mwandishi amesema:
“Ameipokea Abu Daawuud na wengineo.”
Udhahiri ni kwamba mtunzi wa kitabu anaona kuwa Hadiyth ni hoja. Ndio maana ametosheka nayo. Ameitumia kama dalili kuonyesha kuwa haifai kuitwa kwa majina kama “al-Hakam” na “Abul-Hakam”. Kwa sababu hizi ni sifa za Allaah (Ta´ala). Yeye ndiye mwenye kuhukumu kati ya waja Wake. Katika dunia hii anahukumu kwa Shari´ah Yake na Aakhirah atahukumu Mwenyewe.
Lakini hata hivyo imekuja katika Hadiyth nyingi Swahiyh ambazo zinaonyesha kuwa kuna majina kama al-Hakam na al-Hakiym ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuyabadilisha. Hadiyth hizo ni Swahiyh zaidi kuliko Hadiyth hii katika mlango huu. Ni dalili inayoonyesha kuwa usahihi wa Hadiyth hii unahitaji kuangaliwa vizuri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyakubali majina kama Hakiym bin Hizaam, al-Hakam bin ´Amr al-Ghifaariy na majina mengineyo. Hakuyabadilisha. Lau ingelikuwa ni dhambi basi angeliyabadilisha. Jina “al-Hakam” kunalengwa yule anayewahukumu watu kwa Shari´ah ya Allaah. Ni jina lisilokuwa na neno. Vivyo hivyo inahusiana na jina “al-Haakim”, “al-Qaadhwiy” na mengineyo.
[1] Abu Daawuud (4955), an-Nasaa’iy (5387) na Ibn Hibbaan (504). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Mishkaat-ul-Maswaabiyh” (4766).
from Firqatu Nnajia https://ift.tt/2EVLvLk
via IFTTT
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni