Translate

Jumatano, 3 Aprili 2019

Katazo la Wanawake Kujichora [Tattoo], Kunyoa Nyusi na Kuchonga Meno

                  Katazo la Wanawake Kujichora [Tattoo], Kunyoa Nyusi na Kuchonga Meno


Matendo haya matatu yote yamekatazwa; kwa kuthibiti laana kwa mwenye kuyafanya kwa kuwa ndani yake kuna kubadilisha maumbile ya Allaah.  Matendo haya pia ni katika yenye kuonekana kuwa ni miongoni mwa mapambo na ni mtu kujitengeneza kwa namna atakavyo, kwa kuwa Muumba –wal –‘iyyaadhu bilLaahi- hakuwa na ufanisi wa kuwaweka vile watakavyo wenyewe katika kuwaremba kwa rangi na chapa tofauti iwe kwa mapicha zikiwemo za wanyama na kadhalika; huku wakisahau kuwa Muumba amesema:Bila ya shaka tumemuumba mtu kwa umbo lilio bora kabisa” [At-Tiyn 95: 4].

Mambo haya kwa baadhi ya ndugu zetu hasa waliobahatika kupata fursa ya kukutana au kuwaona makafiri yamekuwa ni uthibitisho wao wa kuwathibitishia wengine kuwa wao waliwahi kufika Ulaya na katika waliyoyaona ni huku kujichora, kujipiga chapa na kadhalika.
Msiba huu wa kujiremba na kujichapa kwa kijichora umewasibu pia baadhi ya waliojaaliwa kuwa wanaume, yote kwa kuwa hawana shukurani kwa kuumbwa waume wala hawaelewi thamani yake; hivyo kwa kupenda kuiga na kujifananisha mtu hujisahau mpaka akafikia kutojikumbuka kuwa umbile lake lilikuwa namna ipi.

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhumaa) amesema kuwa:Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemlaani mwanamke mwenye kuunganisha nywele na mwanamke mwenye kutaka kuunganishwa nywele, na mwanamke mchanjaji[mwenye kuwachanja wanawake wenzake kwenye sehemu yoyote ile ya mwili] na mwanamke mwenye kutaka kuchanjwa.”  [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Al-Libaas, mlango wa mwenye kutaka kuchanjwa, Hadiyth namba 5511, 5514,5516 na 5521].

Ama kunyoa au kunyolewa nyusi ni janga jengine; kwani imekuwa ni katika mapambo kwa kila mwenye kutaka kujiremba hasa kwa wenye kutaka kuolewa.
Na kutokana na 'AbdullAah bin Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema kwamba: “Allaah Amewalaani wanawake wenye kuwachanja wenzao [tattoo], na wanawake wenye kuchanjwa, na wanawake wenye kuwanyoa wenzao nyusi na wanawake wenye kunyolewa nyusi; na wanawake wenye kuchonga meno kwa urembo [kutengeneza mwanya wapate kuonekana kama ni wasichana, kwa kuwa mwanya hupendeza kwa wasichana]  kwa ajili ya kujipamba; wanawake wenye kubadilisha maumbile ya Allaah”; akasema: Hadiyth hii ikamfikia mwanamke kutoka Bani Asad aliyekuwa akiitwa kwa jina la Ummu Ya’quub, mwanamke huyu alikuwa msomaji wa Qur-aan, aliposikia Hadiyth hii alikuja kwa Ibn Mas'uud(Radhiya Allaahu 'anhu) nakumwambia kuwa: “Kilichonileta kwako ni Hadiyth niliyofikishiwa kuwa wewe umewalaaani wanawake wenye kuwachanja wenzao na wanawake wenye kuchanjwa; na wanawake wenye kuwanyoa wenzao nyusi na wanawake wenye kunyolewa nyusi; na wanawake wenye kuchonga meno kwa ajili ya urembo; na wanawake wenye kubadilisha maumbile ya Allaah”; yule mwanamke akamuuliza kuhusu jambo hili? Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) akamwambia:"Kwa nini nisimlaani yule aliyelaaniwa na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na aliyelaaniwa katika Kitabu cha Allaah!. Yule mwanamke akasema: “Kwa hakika nimesoma baina ya magamba mawili ya msahafu [Kitabu cha Allaah chote kwa ukamilifu] mbona sijakutana na hilo?!” Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) akamwambia: “Kama ulikisoma kwa ukamilifu basi bila ya shaka yoyote ile ulikutana na hilo; Allaah Aliyetukuka Amesema:“Na anachokupeni Mjumbe chukueni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho” [Al Hash-r 59:7]. Yule mwanamke akasema: “Hakika mimi naona kuna jambo kama hili kwa mkeo hivi sasa; Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) akamwambia: “Nenda ukaangalie vyema”, Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) akasema: “Yule mwanamke aliingia ndani kwa mke wa 'Abdullah lakini hakuona kitu alichodai kuwa anacho huyo mke wa Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu)”;yule mwanamke akasema: “Sikuona kitu”; Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) akasema: “Na kama angekuwaanacho hicho ulichodai kuwa anacho basi nisingelimuingilia” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Tafsiyr Qur-aan, Suuratul Hashr, Hadiyth namba 4534; na katika kitabu cha al-Libaas, mlango wa mwanamke mwenye kutaka kuchanjwa, Hadiyth namba 5522; na mlango wa wanawake wenye kunyoa nyusi, Hadiyth namba 5506, 5513 na 5517; na Muslim, katika Kitabu cha Mavazi na Mapambo, mlango uharamu wa kitendo cha mwenye kuunganisha nywele na mwenye kutaka kuunganishwa, Hadiyth namba 3973].

Na kutoka kwa Abu Juhayfah (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema:Amekataza Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) [Kutumia]thamani ya damu, thamani ya mbwa, pato la mhasharati; na amemlaani mwanamke mwenye kuwachanja wenzake na mwanamke mwenye kutaka kuchanjwa; na mla ribaa nawakala wake; na mchora picha”[Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Hajj, milango ya Muhswar na jaza ya Swayd [kuwinda], Hadiyth namba 2095; na katika kitabu cha Al-Libaas, mlango wa mwenye kuchanja,Hadiyth namba 5519.; na katika Kitabu cha Tafsiyr Qur-aan, Suurat Qul A’uwdhu birabbil Falaq, Hadiyth namba 5535].

Matendo haya yote –kujipiga chapa, kunyoa nyusi na kuchonga meno- ni haramu kwa mtendaji na mwenye kutaka kutendewa kutokana na Hadiyth hizo, na pia matendo hayo yote ni katika yenye kueleweka kuwa ni kubadilisha maumbile ya Allaah, na ni udanganyifu.

Kuthibiti Laana ya Allaah kwa mwenye kufanya au kufanyiwa matendo haya inathibitisha kuwa matendo hayo ni katika madhambi makubwa pia, lakini kwa masikitiko makubwa kabisa bado kuna wanawake tena wengi sana wenye kutaka kuolewa hufanya matendo haya au hufanyiwa; ili wadhaniwe kuwa ni wasichana wadogo au wadhaniwe kuwa ni wenye nyuso nzuri na za kuvutia; la kusikitisha na kuhuzunisha zaidi ni kule kwa baadhi ya kina mama kuwapeleka wasichana wao wadogo kufanyiwa matendo haya.

Huenda likazuka suala hapa; je wale wanawake wenye kuota ndevu au masharubu inaruhusiwa kwao kuzinyoa au kuyanyoa?
Jawabu: Naam, inajuzu kwa wanawake kama hawa kuzinyoa ndevu zenye kuota katika nyuso zao au masharubu; na wala hawaingii katika laana; bali kwa kuzinyoa hizo ndevu na hayo masharubu watakuwa wanatekeleza agizo la Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) la kuwataka wanawake wasijifananishe na wanaume, na kwa wanawake kama hawa hawana njia ya kutojifananisha na wanaume isipokuwa kunyoa hizo ndevu au hayo masharubu; na watakapoziacha hizo ndevu au hayo masharubu watakuwa wamejifananisha na wanaume na huko ndiko kwenda kinyume na agizo laMjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Pia ikiwa mwanamke atahitaji kuchonga meno yake kwa sababu za kimatibabu au kuondosha aibu katika meno; mwanamke huyu haingii katika laana wala kufanya hivyo haitokuwa haramu kwake kwa kuwa neno “...kuchonga meno kwa urembo”lililotumika katika Hadiyth linaonyesha wazi kuwa uharamu uko kwa mwenye kuchonga kwa ajili ya kutafuta urembo na uzuri, hivyo wakati wowote ule atapohitajia mwanamke kuchonga meno yake kwa ajili ya kimatibabu huwa hana dhambi, Allaahu A‘alam.



https://ift.tt/2HVf0h0 i live islam

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

20-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aadhah Kwa Asiyekuwa Allaah

  إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم   Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!   20 - Isti’aadhah  (Kuomba Kinga) Kwa Asiyekuwa Allaah   ...