Katazo la Wanawake kuunganisha Nywele
Tendo hili kwa huzuni kubwa limekuwa ni katika yenye kuonekana kuwa ni miongoni mwa mapambo, bali ni pambo lisiloepukika kwa kila mwenye kutaka kujiremba hasa kwa wenye kutaka kuolewa; wawe hawana nywele au wenye nywele ngumu/fupi au hata wenye nywele za singa; yote kutaka kuiga na kujifananisha na kudanganya, kwa kuwa tuko mbali na yaliyopokelewa kutoka kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu kuunganisha nywele.
Kutoka kwa Asmaa (Radhiya Allaahu 'anhaa) amesema: Alikuja mwanamke kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:"Ee Mjumbe wa Allaah! Hakika mimi nina binti ambae ni bibi harusi, amepatwa na maradhi –surua- hivyo nywele zake zimenyonyoka; je, niziunganishe?" Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: "Allaah Amemlaani mwanamke mwenye kuunganisha nywele na mwanamke mwenye kutaka kuunganishwa nywele" [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Al-Libaas, mlango wa mwenye kuunganishwa nywele, Hadiyth namba 5515].
Na kutoka kwa bibi 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa) kuwa palikuwa na mjakazi aliyeolewa miongoni mwa wanawake wa ki-Answaar, na huyo mjakazi alipatwa na maradhi yaliyopelekea kunyonyoka nywele zake, basi watu wake wakataka kuziunganisha nywele zake, wakamuuliza Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na kuunganisha nywele? Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:"Amelaaniwa mwanamke mwenye kuunganisha nywele na mwanamke mwenye kutaka kuunganishwa nywele". [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Al-Libaas, mlango wa kuunganisha katika nywele, Hadiyth namba 5508 na 5509 na 5510].
Kwa hakika hichi kitendo cha kuunganisha nywele si miongoni mwa matendo yanayostahiki kutendwa na wenye kuamini Allaah na Siku ya Qiyaamah; kwani ni katika matendo na mitindo yenye kufanya na wasioamini Allaah na Siku ya Mwisho –wake kwa waume-, na hili liko dhahiri katika ulimwengu wetu; hivyo kwa mwanamke mwenye kuamini Allaah na Siku ya Qiyaamah kuunganisha nywele au kutaka kuunganishwa huwa anajifananisha na makafiri, na hilo limekatazwa kama ilivyopokewa kuwa Sa’iyd bin Musayyib amesema kuwa: “Alikuja Mu’aawiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) Madiynah mara ya mwisho aliyokuja Madiynah akatuhutubia, basi akatoa donge la nywele [za bandia]akasema: Sikuwahi kumuona mtu yeyote anafanya haya isipokuwa Mayahudi; kwa hakika Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekiita kitendo hichi Az-Zuura: yaani mwenye kuunganisha nywele” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Al-Libaas, mlango wa kuunganisha katika nywele, hadiyth namba 5512; na Muslim, katika Kitabu cha Mavazi na Mapambo, mlango uharamu wa kitendo cha mwenye kuunganisha nywele na mwenye kutaka kuunganishwa, Hadiyth namba 3976].
Hadiyth hizi ziko wazi kabisa katika kuharamishwa kuunganisha nywele kama alivyosema al-Imaam An-Nawawiy na kulaaniwa kwa muunganishaji na mwenye kutaka kuunganishwa.
Tendo hili -la kuunganisha nywele- ni katika madhambi makubwa kwa kumthibitikia Laana ya Allaah mwenye kufanya au kufanyiwa tendo hili; lakini kwa masikitiko makubwa kabisa juu ya kuthibiti Laana ya Allaah kwa watu hao [muunganishaji na mwenye kutaka kuunganishwa nywele] bado kuna wanawake wengi kabisa wenye kufanya tendo hili la kuunganisha nywele za wanawake wenzao au wenye kutafuta wa kuwaunganisha nywele kwa kisingizio cha kujiremba na kujipamba huku wakidai kuwa wao pia ni miongoni mwa wenye kumfuata na kumpenda Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Ni vyema ieleweke kuwa mwanamke akijipamba ikiwa si kwa ajili ya mumewe basi huwa haramu; na ikiwa atajipamba kwa ajili ya mumewe haitakiwi kujipamba au kujiremba isipokuwa kwa kilichohalalishwa na kukubaliwa na Shariy’ah ya Allaah; kwani haijuzu kwa mwanamke kujipamba kwa ajili ya mumewe kwa kitu Alichoharamisha au Alichokikataza Allaah.
Na Allaah anajua zaidi
https://ift.tt/2IeNI4P i live islam
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni